'Walimuua binti yangu': Majonzi yalivyomgeuza mama kuwa mpinzani wa Iran

Onyo: Taarifa hii ina maelezo ambayo huenda ikawaathiri baadhi ya wasoma
Kabla ya yote haya, Samira hakuwa mtu wa kufuatilia siasa.
Akizungumza na BBC Panorama, Samira alisema: "Nilikuwa nafanya kazi ya kuuza vipodozi nchini Iran." Hayo yalikuwa maisha yake kabla ya siku ambayo binti yake wa pekee aliuawa mbele ya macho yake na vikosi vya usalama vya Iran. Tangu wakati huo, maisha yake yalibadilika kabisa.
Sevda, mwenye umri wa miaka 16, alikuwa miongoni mwa waliojiunga na maandamano dhidi ya utawala wa Iran yaliyosambaa nchini humo mapema mwaka huu. Maandamano hayo yalitokea kabla ya mashambulizi makubwa ya anga yaliyozidisha mvutano kati ya Iran, Marekani na Israel.
Samira anasema majonzi yake yaligeuka kuwa hasira kali baada ya mamlaka za Iran kuzuia jitihada zake za kumtafuta na kuupata mwili wa binti yake, badala ya kumpa msaada.
Samira alisema:"Niligundua wakati huo kwamba kumpata Sevda hakukuwa mwisho wa mateso yangu, bali mwanzo wa msururu wa manyanyaso niliyokumbana nayo kutoka kwao."
Kutokana na hali hiyo, Samira alikimbia Iran kupitia safari hatari, akitembea kwa miguu katika maeneo ya milimani yenye mazingira magumu. Kwa sasa anaishi mafichoni nje ya nchi na anajieleza kama "jeshi la mtu mmoja katika mapambano dhidi ya utawala."
Katika harakati zake za kutafuta haki na uwajibikaji kufuatia kuuawa kwa binti yake, Samira aliazimia kuweka hadharani majina ya maafisa wa vikosi vya usalama na viongozi ambao anaamini walihusika katika tukio la kupigwa risasi kwa binti yake wakati wa maandamano hayo.
"Wanaweza kufanya kila wawezalo kunidhuru, lakini kunitafuta na kunipata haitakuwa rahisi. Siwezi tena kurejea maisha ya kawaida. Hakuna njia ya kurudi nyuma," alisema.
Samira ni mmoja wa Wairan wengi ambao BBC imezungumza nao tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Baadhi yao, hasa wale wanaoishi nchini Iran, walisema waliamua kuzungumza licha ya hatari zinazowakabili. Wanasema imekuwa vigumu kuendelea kuwa na matumaini baada ya ukandamizaji mkali uliofuatia maandamano makubwa yaliyoitikisa nchi hiyo.
Ubalozi wa Iran mjini London uliiambia BBC Panorama kwamba maandamano hayo, ambayo yalianza kwa amani, yaliingiliwa na mataifa ya kigeni, hasa Marekani. Ubalozi huo uliituhumu Marekani kwa kuchochea vurugu, kusambaza silaha na vifaa, na kuhatarisha usalama wa umma.
"Sikuweza hata kupiga kelele."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sevda aliuawa Januari 9 akiwa pamoja na mama yake, Samira, katika maandamano makubwa yaliyokuwa yanafanyika nje ya mji mkuu wa Iran, Tehran. Maandamano hayo yalikuwa yameanza mwezi uliotangulia.
Mwanzoni, waandamanaji walikuwa wakilalamikia hali ngumu ya maisha na uchumi, lakini baadaye madai yao yakapanuka na kuwa wito wa kuondolewa kwa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu nchini humo.
Samira anasema wakati huo hakuwa na shauku kubwa ya siasa, lakini binti yake alikuwa tofauti.
Sevda aliwaona Mahsa Amini na Nika Shakarami kama mashujaa wake. Mahsa alifariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kutuhumiwa kukiuka sheria za hijabu, jambo lililochochea maandamano makubwa nchini Iran. Nika, kwa upande wake, aliuawa wakati wa maandamano yaliyofuata dhidi ya sheria kali za mavazi kwa wanawake.
Samira alisema:"Aliendelea kuwaenzi na hakuwahi kuwasahau. Kila mara alitaka kuendeleza mapambano yao."
Anakumbuka kuwa siku moja kabla ya Sevda kuuawa, idadi ya waandamanaji ilikuwa kubwa sana. Yeye na binti yake waliitikia wito wa Reza Pahlavi, mwana wa Shah wa mwisho wa Iran ambaye anaishi uhamishoni, wa kushiriki maandamano hayo.
"Vikosi vya usalama vilikuwa vimepoteza udhibiti," alisema.
Kwa mujibu wa Samira, ongezeko kubwa la waandamanaji liliitia hofu serikali ya Iran. Anasema siku iliyofuata mamlaka zilitoa amri ya kuwapiga risasi waandamanaji kwa nia ya kuwaua.
Hata hivyo, wakati huo yeye na wengine hawakuamini kuwa tishio hilo lingetekelezwa.
"Nchini Iran wamezoea kutoa vitisho vingi. Hatukuwahi kufikiria kwamba mauaji ya kiwango hiki yangeweza kutokea."
Samira alisema waandamanaji wengi walipata matumaini kutokana na ahadi ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba angewaunga mkono.
Januari 8, Trump aliliambia vyombo vya habari vya Marekani:
"Niliwaambia viongozi wa Iran kwamba wakianza kuwaua watu, jambo walilowahi kufanya wakati wa machafuko yaliyopita, tutajibu kwa nguvu kubwa."
Hata hivyo, Samira anakumbuka kuwa siku iliyofuata idadi ya waandamanaji ilionekana kuwa ndogo zaidi.
Anaamini Sevda alitambua hatari iliyokuwa mbele yake. Kabla ya kuondoka nyumbani, alivua hereni zake na kumpa bibi yake, na pia alimpa Samira nambari ya siri ya simu yake.
Mama na binti walijiunga na waandamanaji wengine kabla ya Sevda kupanda juu ya pipa la taka na kuanza kuongoza kauli za maandamano.
Akikumbuka hali ya eneo walilokuwapo, Samira alisema:
"Ilionekana kana kwamba maafisa wa usalama walikuwa wengi kuliko raia. Sijui waliwezaje kuwakusanya wanachama wengi kiasi hicho wa Basij na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kwa siku moja tu."
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi lina jukumu la kulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, huku Basij, kikosi cha kujitolea chenye silaha, kikifanya kazi chini ya uongozi wake.
Samira alisema mpiga risasi aliyekuwa juu ya jengo lililokuwa upande wao wa kulia ndiye aliyefyatua risasi iliyomuua binti yake.
"Kulikuwa na mlenga shabaha juu ya paa la jengo upande wetu wa kulia. Risasi ilitoka huko na kumpiga moja kwa moja moyoni. Sikuweza hata kupiga kelele. Nilibaki nimesimama nikimtazama tu Sevda. Mwili wake haukusogea. Damu zilikuwa zikimtoka mdomoni na puani. Sikuamini kilichokuwa kinatokea. Sikuamini kwamba alikuwa akivuta pumzi zake za mwisho. Macho yake yalikuwa yamenitazama moja kwa moja."
Samira alifanikiwa kumfikisha Sevda hospitalini, ambako aliambiwa madaktari walikuwa wakimfanyia upasuaji. Lakini baadaye mlango ulipofunguliwa, alishtuka kukuta mwili wa binti yake ukiwa tayari umewekwa kwenye mfuko wa kuhifadhia maiti.

Chanzo cha picha, Sisu Pictures Ltd
Mwili wa Sevda uliondolewa katika eneo la tukio na kupelekwa kwengine, na Samira anasema ilimchukua siku kadhaa kumpata tena binti yake. Kama familia nyingine nyingi zilizokuwa zikitafuta wapendwa wao, alijikuta akizunguka katika moja ya vyumba vikubwa vya kuhifadhia maiti mjini Tehran.
"Walikuwa vijana tu, wasichana na wavulana. Wengi wao walikuwa wameuawa," alisema huku akitokwa na machozi.
Alisema kila mfuko wa maiti alioufungua ulimwongezea maumivu na uchungu.
"Kila mara nilipofungua mfuko wa maiti, nilihisi kama sehemu yangu inakufa. Sijawahi kuona miili mingi kiasi hicho maishani mwangu, lakini sikuweza kukata tamaa," alisema.
Hatimaye, alimkuta Sevda.
"Miili mitatu ilikuwa imerundikwa juu ya mwili wa Sevda. Hivyo ndivyo tulivyompata," alisema.
Wakati huo, mamlaka za Iran zilikiri kuwa zaidi ya watu 3,000 waliuawa wakati wa maandamano hayo, lakini zilisema baadhi yao walikuwa wanachama wa vikosi vya usalama. Hata hivyo, shirika la kutetea haki za binadamu la HRANA linakadiria kuwa zaidi ya watu 7,000 waliuawa, wengi wao wakiwa waandamanaji.
Kwa Samira, kumpata binti yake hakukuwa mwisho wa mateso yake, bali mwanzo wa mgogoro mwingine na mamlaka za Iran.
Anasema ili aruhusiwe kuuchukua na kuuzika mwili wa Sevda, alilazimika kusaini hati iliyodai kuwa "magaidi", na si vikosi vya usalama, ndio waliohusika na kifo chake.
"Walitaka kuficha kilichotokea Januari 8 na 9 na kuficha idadi halisi ya waliouawa. Familia zililazimishwa kusema kwamba wapendwa wao waliuawa na magaidi wa Israel au Marekani."
Anasema hata baada ya mazishi hakuruhusiwa kutembelea kaburi la binti yake, wala kuweka jiwe la kumbukumbu.
Manyanyaso hayo yaliendelea. Siku chache kabla ya kumbukumbu ya siku 40 tangu kifo cha Sevda, tukio lenye umuhimu mkubwa katika utamaduni wa Iran, Samira alipokea wito kutoka tawi la Wizara ya Ujasusi katika eneo alikokuwa akiishi.
Anasema maafisa walimwambia:
"Lazima ufanye mahojiano na useme kwamba Sevda alikuwa mwanachama wa Basij na kwamba aliuawa na waandamanaji. Tukifanya hivyo tutamtangaza kuwa shahidi, na wewe utapata marupurupu, nyumba au chochote utakachoomba."
Samira anaamini mamlaka zilichukua hatua hiyo kwa sababu aliwasilisha taarifa za kuuawa kwa Sevda kwa chombo cha habari cha Iran kinachofanya kazi kutoka London mara tu huduma za intaneti ziliporejeshwa nchini humo.
"Walikuwa na hofu kubwa kwamba nilikuwa nikiwasiliana na vyombo vya habari na taasisi zilizoko nje ya Iran."
Ili kuepuka kufanya mahojiano hayo, Samira aliondoka Iran mara tu baada ya kumbukumbu ya siku 40 ya kifo cha binti yake.
"Sikutaka kunufaika kutokana na damu ya mwanangu."
Anasema alisaidiwa na watu waliowatorosha wahamiaji kuvuka mpaka kutoroka Iran, akipitia mito na milima hadi alipofika salama. Wakati wa safari hiyo, alirekodi video iliyomuonyesha akiwa na hasira na maumivu makubwa.
"Utawala huu umenitesa sana. Watu hawa wamenipa mateso makubwa," alisema akiwa anatembea kwenye njia nyembamba ya mlimani, kandokando ya korongo.

Samira anasema kuwa baada ya kuendelea kutoa mahojiano kwa vyombo vya habari vya kigeni akiwa uhamishoni, alishtakiwa akiwa hayupo nchini kwa makosa mbalimbali, yakiwemo ya hirabah au "kupigana vita dhidi ya Mungu", shtaka ambalo linaweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo.
Katika siku ambayo Sevda angeadhimisha miaka 17 ya kuzaliwa, ndugu na marafiki waliandaa mkesha wa kumbukumbu. Samira alifuatilia tukio hilo kwa matangazo ya moja kwa moja akiwa uhamishoni.
"Ghafla matangazo yakakatika," alisema.
Baadaye aligundua kuwa vikosi vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi vilivamia mkusanyiko huo na kuwakamata baadhi ya ndugu na marafiki zake.
Anasema mamlaka pia ziliionya familia yake kuwa ikiwa ingeendelea kukusanyika katika kaburi la Sevda, kaburi hilo lingefukuliwa na mabaki ya mwili wake kuhamishwa sehemu nyingine.
Sasa Samira anafanya kampeni ya kuweka hadharani majina ya wanachama wa vikosi vya usalama na maafisa wa Iran ambao anaamini walihusika katika mauaji yaliyotokea wakati wa maandamano ya Januari 8 na 9.
"Ninataka haki itendeke kwa kila mtu ninayemtaja. Wamewaua vijana wengi. Lengo langu ni kufichua utambulisho wao ili hatimaye wafikishwe mahakamani."
Baada ya mmoja wa watu ambao Samira alikuwa amewataja mtandaoni kupatikana ameuawa, mfuasi wa serikali alitangaza zawadi ya dola 5,000 kwa yeyote ambaye angeweza kutoa taarifa za mahali alipo, akiamini kuwa alikuwa na uhusiano na kifo hicho. Vyombo vya habari vya serikali baadaye viliripoti kuwa watu tisa walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Licha ya hatari hizo, Samira anasema hataacha kuzungumza.
"Kila siku na kila sekunde inayopita bila Sevda ni ngumu sana kwangu. Ni kama mama aliyepoteza moyo wake, roho yake na hata maisha yake."
Hata hivyo, anaamini kwamba kumpoteza binti yake ndiko kulikompa nguvu ya kuendelea kupigania kile anachoamini.
"Lakini kifo cha Sevda kilinibadilisha kabisa. Kilinipa nguvu ya kusimama imara na kutafakari jinsi ya kuheshimu maisha na ndoto zake. Miili niliyoiona na kila mfuko wa maiti nilioufungua nikimtafuta Sevda ndiyo inayonipa nguvu ya kuendelea kupambana na Jamhuri ya Kiislamu hadi pumzi yangu ya mwisho,"
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi































