Moja kwa moja , Marekani yaonya 'wanaoendelea kuiunga mkono Iran'

Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, ametoa onyo kwa wale wanaoendelea kuiunga mkono serikali ya Iran, kufuatia tangazo la vikwazo vipya dhidi ya mtandao mkubwa wa uhalifu.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Bodi ya Dawa Kenya yaonya dhidi ya matumizi ya cetirizine kukaza au kukausha uke

    f

    Bodi ya Dawa na Sumu Kenya (PPB) imewaonya Wakenya dhidi ya matumizi yasiyo sahihi ya vidonge vya cetirizine kwa lengo la kukaza au kukausha uke, ikisema tabia hiyo inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inaweza kusababisha madhara ya kiafya.

    Katika tahadhari yake ya usalama, bodi hiyo imekanusha madai yanayoashiria kuwa cetirizine, dawa inayotumika kupunguza dalili za mzio, inaweza kutumiwa kwa madhumuni yanayohusiana na uke.

    Bodi hiyo imesema hakuna ushahidi wa kisayansi uliothibitishwa unaounga mkono madai hayo na kusisitiza kuwa cetirizine haijaidhinishwa kutumiwa ukeni.

    Cetirizine ni dawa ya kumeza inayotumika kutibu hali mbalimbali za mzio, zikiwemo mzio wa njia ya pua, hali inayosababisha vipele vinavyowasha kwenye ngozi. Dawa hiyo inapaswa kumezwa tu kwa kufuata kipimo kilichopendekezwa na maelekezo ya mtaalamu wa afya.

    Bodi hiyo imeonya kuwa kuingiza vidonge vya cetirizine ukeni kunaweza kusababisha muwasho, hisia ya kuungua, maumivu na usumbufu.

    Imewataka wananchi kutoweka ukeni cetirizine au dawa nyingine yoyote iliyotengenezwa kwa ajili ya kumezwa. Pia imeonya dhidi ya kutegemea madai yasiyothibitishwa yanayosambazwa mitandaoni kuhusu afya ya uzazi na afya ya tendo la ndoa.

    Aidha, imewashauri watumiaji wa dawa hiyo kutozidisha kipimo kilichopendekezwa na kuitumia kwa madhumuni yaliyoidhinishwa pekee, kwa njia iliyoelekezwa na wataalamu wa afya.

    Watu wanaokabiliwa na ukavu wa uke au changamoto nyingine zinazohusiana na afya ya uzazi na tendo la ndoa wameshauriwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya wenye sifa badala ya kujaribu njia za matibabu ambazo hazijaidhinishwa.

    Bodi hiyo pia imewataka wananchi kuripoti madhara yanayoshukiwa kusababishwa na dawa pamoja na changamoto nyingine za usalama wa dawa kupitia mifumo yake ya kuripoti matukio hayo.

    Taarifa hiyo ya tahadhari imesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Dawa na Sumu, Dkt Ahmed I. Mohamed, Novemba 4, 2026.

    Onyo hilo limetolewa wakati ambapo kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu taarifa potofu za kiafya zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, hususan madai yanayohamasisha matumizi ya dawa kwa madhumuni ambayo hayajaidhinishwa katika afya ya uzazi na maeneo nyeti ya mwili.

    Soma Pia:

  2. Tanzania na Kenya zashindana kuongoza mustakabali wa AI Afrika Mashariki

    x

    Tanzania inaongeza juhudi za kuimarisha uwezo wake katika teknolojia za kidijitali, wakati utafiti mpya wa Jumuiya ya Madola ukibainisha fursa kubwa za kiuchumi zinazoweza kupatikana kutokana na matumizi ya Akili Unde (AI) katika Afrika Mashariki.

    Ripoti hiyo, iliyotolewa na taasisi ya Ayre Think Tank wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi na serikali za Jumuiya ya Madola, inaonyesha kuwa Kenya inaongoza kwa utayari wa kutumia teknolojia ya AI miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa nafasi ya 22 duniani kwa alama 48.7 kati ya 100.

    Uganda inafuatia katika nafasi ya 23 kwa alama 47, Tanzania ikiwa nafasi ya 25 kwa alama 45.5, huku Rwanda ikishika nafasi ya 47 kwa alama 38.1.

    Ingawa nchi zote nne za Afrika Mashariki bado ziko chini ya wastani wa utayari wa kimataifa wa alama 53, fursa za kiuchumi zinazoweza kupatikana ni kubwa.

    Kwa kutumia makadirio ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), utafiti huo unaonyesha kuwa matumizi yenye mafanikio ya teknolojia ya AI yanaweza kuongeza pato la taifa la Kenya kwa dola bilioni 1.971 za Marekani ndani ya miaka 10. Kiasi hicho ni miongoni mwa ongezeko kubwa zaidi linaloweza kupatikana katika nchi zinazoendelea duniani.

    Kwa Tanzania na nchi jirani, ripoti hiyo inaeleza kuwa mafanikio yatategemea kuimarisha upatikanaji wa teknolojia kwa uhakika, kutengeneza mifumo inayozingatia lugha za wenyeji na kuhakikisha vijana hawabaki kuwa watumiaji wa teknolojia pekee, bali wanashiriki pia katika kuibuni na kuiendeleza.

    Katika orodha ya kimataifa inayojumuisha nchi 56, Singapore inaongoza, huku Mauritius ikiwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa kushika nafasi ya nane duniani.

    Huku eneo hilo likiendelea kuwekeza katika teknolojia, changamoto kubwa ni kuwaandaa vijana kwa ujuzi wa kidijitali utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa baadaye.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Mahakama Kuu Tanzania yapiga marufuku adhabu ya viboko shuleni

    N

    Mahakama Kuu Tanzania imetangaza kuwa kanuni zilizokuwa zikiwaruhusu walimu kuwaadhibu wanafunzi kwa kuwachapa ni kinyume cha Katiba, ikisema zinakiuka haki ya utu wa binadamu na uhuru dhidi ya adhabu au vitendo vya kikatili, visivyo vya kibinadamu au vinavyodhalilisha.

    Katika uamuzi uliotolewa Novemba 3, 2026, kupitia usajili wake wa Dodoma, mahakama hiyo ilibatilisha Kanuni za 2, 3 na 6 za Kanuni za Elimu kuhusu Adhabu ya Viboko za mwaka 2002, zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 294.

    Jopo la majaji watatu, likijumuisha Majaji Amir Mruma, Hassan na Irene Musokwa, lilibaini kuwa kanuni hizo zinakiuka Ibara ya 12(2) na 13(6)(e) ya Katiba, zinazohakikisha heshima na utu wa binadamu na kupiga marufuku vitendo au adhabu za kikatili, zisizo za kibinadamu au zinazodhalilisha.

    Uamuzi huo umetokana na ombi la kikatiba lililowasilishwa mwaka 2025 na Samweli Maduhu Mangu dhidi ya Waziri wa Elimu, kwa msaada wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

    Kesi hiyo iliwasilishwa kwa niaba ya mlezi wa Mhoja Maduhu, mwanafunzi wa kidato cha pili aliyefariki baada ya tukio la madai ya kuchapwa viboko shuleni, kifo chake kikichochea upya wito wa kukomesha adhabu ya viboko katika taasisi za elimu.

    Mhoja alifariki Februari 26, 2025, katika Shule ya Sekondari Mwasamba, wilayani Busega, mkoani Simiyu, baada ya kudaiwa kuchapwa na mwalimu kwa kushindwa kukamilisha kazi ya kikundi ya somo la Jiografia.

    Wanafunzi wengine ambao pia walikuwa hawajakamilisha kazi hiyo waliripotiwa kuadhibiwa. Hata hivyo, inadaiwa kuwa Mhoja alipigwa sehemu kadhaa za mwili wake, ikiwemo kichwani, alipokuwa akijaribu kujikinga.

    Soma Pia:

  4. Kenya yapoteza mabilioni ya shilingi kutokana na ufisadi - Ripoti

    n

    Ripoti mpya ya Benki ya Dunia kuhusu hali ya uchumi wa Kenya imebainisha kuwa ufisadi ni mojawapo ya vikwazo vikuu vinavyoizuia nchi hiyo kutumia kikamilifu uwezo wake wa kiuchumi.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kenya inapoteza mabilioni ya shilingi kutokana na udhaifu katika mifumo ya utawala na usimamizi wa umma.

    Ripoti inaeleza kuwa utawala dhaifu unaathiri uchumi kwa kuongeza shinikizo kwenye fedha za umma na kupanua nakisi ya bajeti.

    Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa ufisadi pekee unachangia kuongezeka kwa nakisi ya bajeti kwa kiwango kinachokadiriwa kuwa asilimia mbili ya pato la taifa.

    Mbali na kuongeza nakisi hiyo, ufisadi pia unapandisha gharama za huduma muhimu, ikiwemo umeme na usafirishaji wa bidhaa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, gharama hizo nchini Kenya ni zaidi ya mara mbili ya zile zinazorekodiwa katika maeneo mengine duniani.

    Ufisadi pia umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kuu zinazokabili wafanyabiashara, huku asilimia 39 ya kampuni zilizoshiriki katika utafiti zikiutaja kuwa kikwazo kikuu kwa shughuli zao.

    Athari hizo pia zinagusa kaya za wananchi.

    Benki ya Dunia inasema kushughulikia changamoto za utawala bora kutakuwa muhimu katika kuharakisha ukuaji wa uchumi wa Kenya.

    “Mafanikio ya kiuchumi yanayoweza kupatikana kutokana na kuimarisha utawala bora yanaweza kuwa makubwa sana. Ripoti inaonyesha kuwa iwapo mwaka 2025 ungekuwa na mageuzi katika utawala bora, pato la taifa lingeweza kuongezeka kwa karibu asilimia tisa ikilinganishwa na mwenendo wa sasa. Mageuzi makubwa zaidi yangeweza kuongeza pato la taifa kwa zaidi ya asilimia 20,” amesema Qimiao Fan, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Afrika Mashariki.

    Ripoti hiyo imekuja wakati ambapo ufisadi unaendelea kuwa mojawapo ya masuala yanayowatia wasiwasi Wakenya. Hata hivyo, matokeo yake yanaweka wazi zaidi gharama halisi za ufisadi kwa uchumi wa nchi.

    Mtaalamu mkuu wa utawala bora wa Benki ya Dunia amesema wananchi wanahofia zaidi athari za kiuchumi za ufisadi, kuliko athari zake katika utoaji wa huduma pekee na namna unavyozuia kuboreka kwa hali zao za maisha.

  5. JD Vance amkosoa Trump kwa tahadhari, alaumu vita vya Iran kwa kushindwa kwa uchaguzi

    n

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amekitaka chama cha Republican kuimarisha uungwaji mkono wa wananchi na kushinda mjadala wa kisiasa badala ya kukata tamaa kutokana na kushindwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

    Ujumbe wake wa hivi karibuni unatazamwa pia kama hatua za awali za kujiandaa kwa uwezekano wa kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2028.

    Katika ujumbe wake mrefu, Vance alisema chama cha Republican kilishindwa kwa sababu kilijitenga na ahadi kuu kilizowapa wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2024. Ahadi hizo zilijumuisha kupunguza mfumuko wa bei na gharama za bidhaa muhimu, pamoja na kuiepusha Marekani na vita vya nje.

    Hata hivyo, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, tofauti zimejitokeza kuhusu masuala hayo hata ndani ya vuguvugu la kisiasa linalomuunga mkono Rais Donald Trump.

    Mivutano kati ya viongozi wakuu wa vuguvugu hilo na watu wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii imeongezeka, hasa kuhusu vita dhidi ya Iran na uungwaji mkono wa Marekani kwa Israel.

    Vance amekuwa akipinga vita dhidi ya Iran. Kauli zake za hivi karibuni pia zinaashiria kukubaliana na mitazamo ya watu kama Tucker Carlson, wanaoamini kuwa vita dhidi ya Iran vinaweza kuwa na madhara ya kisiasa kwa utawala wa Trump.

    Kwa mujibu wa wachunguzi wa masuala ya kisiasa, msimamo wa Vance unaweza kuwa sehemu ya jitihada za kujijengea utambulisho wa kisiasa unaojitegemea kwa kiasi fulani na Rais Trump, huku akiimarisha ushawishi wake miongoni mwa wafuasi wa sera ya America First, inayotanguliza maslahi ya Marekani.

    Uchambuzi huo unaashiria kuwa Vance ameanza hatua za awali za kuimarisha nafasi yake kisiasa kuelekea uchaguzi wa urais wa mwaka 2028, wakati suala la nani atamrithi Trump katika uongozi wa chama cha Republican litakapokuwa muhimu.

    Hata hivyo, safari hiyo haitakuwa rahisi. Rais Trump bado ana ushawishi mkubwa ndani ya chama cha Republican, huku vita na mzozo unaoendelea na Iran katika Mashariki ya Kati vikiendelea kuwa changamoto kubwa kwa utawala wake.

    Soma Pia:

  6. Tetesi za soka Alhamisi: Emery kuongezewa mkataba Aston Villa

    d

    Aston Villa iko katika mazungumzo ya hatua za mwisho na kocha wake Unai Emery kuhusu mkataba mpya, kufuatia tetesi zilizomhusisha na Manchester United. (Telegraph)

    Kiungo wa Liverpool, Trey Nyoni, mwenye umri wa miaka 19, anatarajiwa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo baada ya ofa ya pauni milioni 30 kutoka Nottingham Forest kukataliwa wakati wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi. (The Athletic)

    Leeds United inaweza kumsajili kiungo wa Liverpool, Harvey Elliott, mwenye umri wa miaka 23, kwa mkataba wa kudumu katika dirisha la usajili la Januari, huku Valencia ikijiandaa kuvunja mkataba wake wa mkopo. (Football Insider)

    Everton inamuwania mshambuliaji wa Palmeiras ya Brazil, Vitor Roque, mwenye umri wa miaka 21, ambaye anatarajiwa kuuzwa kwa takriban pauni milioni 42. (Sport)

    Manchester United, Arsenal na Chelsea zote zinafuatilia maendeleo ya kiungo wa Galatasaray na timu ya taifa ya Urusi, Aleksey Batrakov, mwenye umri wa miaka 21. (Teamtalk)

    Beki wa Como, Jacobo Ramon, mwenye umri wa miaka 21, pia yuko kwenye rada ya Manchester United, ingawa Chelsea inaweza kuwa mpinzani wake katika kinyang'anyiro cha kumsajili Mhispania huyo. (Teamtalk)

    Aliyekuwa kocha wa Liverpool na Chelsea, Rafa Benitez, anataka kurejea katika ukocha wa Ligi Kuu ya England. (Talksport)

    Kipa wa Liverpool, Alisson Becker, mwenye umri wa miaka 34, anavutia vilabu vya Flamengo, huku mkataba wake na Liverpool ukitarajiwa kumalizika Juni. (Sport Witness)

    Barcelona haina uwezekano mkubwa wa kumsajili beki wa Inter Milan, Federico Dimarco, mwenye umri wa miaka 28, baada ya klabu hiyo kutumia kipengele cha kuongeza mwaka mmoja katika mkataba wa Muitaliano huyo. (Sport)

    Wachezaji wa Newcastle wanadaiwa kuchanganyikiwa kuhusu kile ambacho kocha Matthias Jaissle anataka kutoka kwao. (Daily Mail)

    Soma Pia:

  7. Republicans watumia mamilioni kunadi sera, lakini washindwa kuvuna ushindi

    D

    Kampeni za matangazo zilizogharimu mamilioni ya dola za Marekani za wagombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani hazikuzaa matunda yaliyotarajiwa.

    Wagombea wa Republican walitumia zaidi ya dola milioni 280 za ziada katika matangazo ya kampeni ikilinganishwa na wapinzani wao wa chama cha Democratic katika majimbo matano muhimu yanayowania viti vya Seneti. Hata hivyo, wagombea hao sasa wanakabiliwa na uwezekano wa kushindwa katika majimbo hayo.

    Kwa mujibu wa kampuni ya AdImpact inayofuatilia matumizi ya matangazo ya kisiasa, majimbo matano yaliyotumia fedha nyingi zaidi katika kampeni za kuwania viti vya Seneti hadi mwisho wa mwezi Oktoba ni Ohio, Texas, Michigan, Iowa na Maine.

    Katika majimbo hayo matano, wagombea wa Republican walitumia jumla ya takriban dola milioni 960 katika matangazo, lakini wagombea wa Democratic wanaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi.

    Tofauti kubwa zaidi ya matumizi ilirekodiwa Texas, ambako mgombea wa Republican, Ken Paxton, alitumia zaidi ya dola milioni 140 zaidi katika matangazo kuliko mpinzani wake wa Democratic, James Talarico. Hata hivyo, Talarico anatabiriwa kuwa mbele kwa zaidi ya asilimia 10 ya kura.

    Iowa ndilo jimbo pekee kati ya hayo matano ambako mgombea wa Democratic, Josh Turek, alitumia fedha kidogo zaidi katika matangazo kuliko mpinzani wake wa Republican, licha ya kuwa katika nafasi ya kushinda kwa tofauti ya takriban asilimia tano.

    Matokeo hayo yanaonesha kuwa matumizi makubwa ya fedha katika matangazo ya kampeni si lazima yahakikishe wagombea wanapata uungwaji mkono wa wapiga kura.

    Soma Pia:

  8. Muingereza aliyeambukizwa Ebola DRC kurejeshwa nchini Uingereza kwa matibabu

    x

    Raia mmoja wa Uingereza aliyethibitishwa kuambukizwa virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anatarajiwa kurejeshwa nchini humo kwa matibabu.

    Hiki ni kisa cha kwanza kuthibitishwa cha raia wa Uingereza kuambukizwa Ebola katika mlipuko wa sasa wa ugonjwa huo nchini DRC, ambao hadi sasa umesababisha vifo vya zaidi ya watu 5,000.

    Hata hivyo, bado haijafahamika ni lini ndege itakayomsafirisha mgonjwa huyo itaondoka.

    Awali, msemaji wa serikali ya Uingereza alisema nchi hiyo ina taratibu zilizowekwa za kushughulikia visa vya aina hiyo na kwamba taratibu hizo tayari zimeanza kutekelezwa. Aliongeza kuwa hatari ya maambukizi kwa umma nchini humo bado ni ndogo.

    Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa mwanamume huyo ni mfanyakazi wa sekta ya afya, likinukuu waraka wa ndani ambao BBC News haijaweza kuupata.

    Visa vya watu kuingiza virusi vya Ebola nchini Uingereza ni nadra sana na havijawahi kusababisha vifo.

    Tangu ugonjwa huo utambuliwe, ni visa vinne pekee vilivyothibitishwa nchini Uingereza. Kesi moja ilirekodiwa mwaka 1976 kutokana na ajali ya maabara, huku nyingine tatu zikihusisha wahudumu wa afya waliokuwa wakikabiliana na mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2015.

    Msemaji wa serikali ya Uingereza alisema:

    "Uingereza ina taratibu zilizowekwa vizuri za kushughulikia visa vya aina hii, na taratibu hizo tayari zimeanza kutekelezwa. Taarifa zaidi zitatolewa kwa wakati unaofaa. Hatari ya Ebola kwa umma nchini Uingereza bado ni ndogo."

    Tangu mlipuko wa sasa ulipoanza nchini DRC mwezi Mei, zaidi ya visa 10,000 vya maambukizi vimethibitishwa, na kuufanya kuwa mlipuko wa pili kwa kusababisha vifo vingi zaidi kuwahi kurekodiwa duniani, baada ya ule wa Afrika Magharibi.

    Hata hivyo, mlipuko huo sasa umegeuka kuwa mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia ya DRC, huku kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa huo kikiripotiwa kufikia asilimia 48.6 mwishoni mwa mwezi uliopita.

    Soma zaidi:

  9. Majaribio ya chanjo mpya za Ebola kuanza DRC

    .

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatarajia kuanza majaribio ya chanjo mbili mpya dhidi ya Ebola, baada ya wataalamu kupendekeza ziongezwe kwenye utafiti unaoendelea wa kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.

    Chanjo hizo, moja iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford kwa ushirikiano na Serum Institute of India na nyingine na kampuni ya Moderna, zitajumuishwa katika majaribio hayo baada ya kuidhinishwa na mamlaka za afya za Congo.

    Hii itakuwa mara ya kwanza chanjo zilizobuniwa mahsusi kutoa kinga dhidi ya virusi vya Ebola vya aina ya Bundibugyo kufanyiwa majaribio wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo.

    Majaribio hayo yalianza mwezi uliopita kwa kutumia chanjo inayotoa kinga dhidi ya aina ya Zaire, ambayo ndiyo aina ya Ebola iliyoenea zaidi, lakini haitoi kinga dhidi ya aina ya Bundibugyo inayosababisha maambukizi ya sasa.

    Utafiti huo utahusisha majaribio ya chanjo mbalimbali kwa watu waliougua ugonjwa huo au waliokutana na wagonjwa.

    Watafiti pia wanajaribu matibabu yanayoweza kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo, wakati wahudumu wa afya wakipambana na mlipuko uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 5,000, wengi wao wakiwa mashariki mwa Congo, ambako majimbo manane yameathirika.

    .

    Soma zaidi:

  10. Masoko ya fedha duniani yapaa baada ya ushindi wa Democrats Marekani

    x

    Masoko ya fedha duniani yameshuhudia ongezeko kubwa la thamani kufuatia ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, huku bei ya mafuta ghafi ikishuka chini ya dola 100 kwa pipa.

    Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent katika soko la dunia ilishuka kwa zaidi ya asilimia nane Jumatano alasiri, na kufikia takriban dola 95 kwa pipa. Hiyo ni bei ya chini zaidi kurekodiwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

    Kushuka kwa bei ya mafuta kunahusishwa kwa kiasi kikubwa na kauli ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, aliyesema kuwa vita dhidi ya Iran ni miongoni mwa sababu zilizochangia kushindwa kwa chama cha Republican katika uchaguzi huo.

    Kauli hiyo imeonekana kuwafanya wawekezaji kutathmini upya hofu ya kuongezeka zaidi kwa mvutano katika Mashariki ya Kati.

    Wawekezaji pia wamezingatia wito wa Vance wa kusitishwa kwa vita, kuchukuliwa kwa hatua za kupunguza makali ya mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha, pamoja na kupitia upya uhusiano wa Marekani na Israel.

    Hali hiyo imeimarisha matumaini katika masoko ya fedha, huku baadhi ya wawekezaji wakiamini kuwa mwelekeo mpya wa kisiasa baada ya uchaguzi unaweza kupunguza uwezekano wa kuzuka kwa mzozo mkubwa wa kijeshi kati ya Marekani na Iran.

    Wakati huohuo, soko la hisa nchini Marekani lilishuhudia ongezeko kubwa la thamani ya hisa.

    Fahirisi ya Dow Jones Industrial Average ilifunga biashara ikiwa imepanda kwa asilimia tatu, huku S&P 500 ikiongezeka kwa asilimia 1.6 na Nasdaq, inayojumuisha kwa wingi hisa za kampuni za teknolojia, ikipanda kwa asilimia 1.4.

    Soma Pia:

  11. Wabunge Marekani wakosoa kuondolewa kwa Afrika Kusini AGOA

    .

    Wabunge waandamizi wa Marekani, Gregory Meeks na Jeanne Shaheen, wamekosoa uamuzi wa utawala wa Rais Donald Trump wa kuiondoa Afrika Kusini kwenye mpango wa biashara wa African Growth and Opportunity Act (AGOA).

    Katika taarifa ya pamoja, walisema hatua hiyo inaweza kudhoofisha maslahi ya kiuchumi ya Marekani na kuipa China nafasi kubwa zaidi ya ushawishi wa kiuchumi barani Afrika.

    Walieleza kuwa AGOA imekuwa chombo muhimu cha kuimarisha biashara kati ya Marekani na mataifa ya Afrika, ikichangia ukuaji wa uchumi wa Afrika na kutoa fursa kwa kampuni za Marekani.

    Meeks na Shaheen walionya kuwa kuondoa Afrika Kusini kwenye mpango huo kunaweza kuvuruga minyororo ya usambazaji, kupunguza fursa za biashara kwa wazalishaji wa Marekani na kudhoofisha uhusiano wa kiuchumi uliodumu kwa muda mrefu.

    Pia wameitaka Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani (USTR) na Ikulu ya White House kutumia kipindi cha siku 60 cha taarifa rasmi kufanya mazungumzo na Afrika Kusini ili kutafuta suluhu kwa masuala yanayohusu ustahiki wa nchi hiyo katika AGOA.

  12. Marekani yaonya 'wanaoendelea kuiunga mkono Iran'

    g

    Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, ametoa onyo kwa wale wanaoendelea kuiunga mkono serikali ya Iran, kufuatia tangazo la vikwazo vipya dhidi ya mtandao mkubwa wa uhalifu.

    Marekani imesema mtandao huo unahusika na kusaidia shughuli za meli za mafuta za Iran zinazofanya biashara kwa siri, zinazojulikana kama shadow fleet.

    Bessent amesema vikwazo hivyo vipya ni sehemu ya operesheni ya kiuchumi inayolenga kuitenga Iran na kuzuia shughuli zake za kifedha.

    Vikwazo hivyo, ambavyo vimekuwa vikiongezwa katika miezi ya hivi karibuni, ni sehemu ya mkakati wa Marekani wa kuongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran kwa kulenga maslahi yake ya kifedha katika mataifa mbalimbali duniani.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 05/11/2026.