Ushindi wa Democrats waibua maswali kuhusu hatma ya Trump

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Wanachama wa Democratic katika Bunge la Congress nchini Marekani tayari wanapanga namna watakavyotumia mamlaka yao ya wingi wa viti katika Bunge la Wawakilishi na Seneti .

Ushindi wao wa bunge la wawakilishi kunawapa mamlaka ya kutoa wito rasmi wa kuwataka watu au taasisi kutoa ushahidi na kupata ufadhili zaidi wa kuanzisha uchunguzi kuhusu utawala wa Rais Donald Trump.

Kulingana na wa watu wanaofahamu majadiliano hayo, tayari kazi imeanza ya kuandaa orodha ya masuala yanayoweza kuchunguzwa pamoja na watu ambao wanaweza kuitwa kutoa ushahidi.

Haya ni baadhi ya masuala yanayopewa kipaumbele na viongozi wa Democratic baada ya kushinda wingi wa viti katika bunge la Congress.

Familia ya Trump na shughuli zake za kifedha

Viongozi wa Democratic wameweka wazi kuwa mikataba yenye faida kubwa inayohusishwa na biashara ya familia ya Trump itakuwa miongoni mwa masuala ya kwanza kulengwa katika uchunguzi wowote unaoweza kufanyika.

"Mambo tunayotaka kuhakikisha ni kwamba fedha za walipa kodi wa Marekani zinatumika ipasavyo na haziibiwi au kuelekezwa katika mifuko ya watu fulani kupitia vitendo vya ufisadi," alisema Suhas Subramaniam, mbunge wa Democratic kutoka Virginia na mwanachama wa Kamati ya Uangalizi ya Bunge la Wawakilishi, alipozungumza na BBC.

Miongoni mwa masuala yanayozingatiwa kuchunguzwa ni uhusiano kati ya serikali na kampuni za kibiashara, hususan zile zinazojihusisha na biashara ya sarafu za kidijitali.

Pia, shughuli za kibiashara za kimataifa za Jared Kushner, mkwe wa Rais Trump, zinaweza kuchunguzwa.

Masuala mengine yanayoweza kuangaziwa ni pamoja na ndege yenye thamani ya dola milioni 400 iliyotolewa na Qatar kwa ajili ya kutumiwa kama ndege rasmi ya Rais wa Marekani, pamoja na mikataba ya ulinzi yenye thamani ya mamilioni ya dola iliyotolewa kwa kampuni zinazohusishwa na familia ya Trump.

"Kinachonishangaza si tu kwamba serikali hii, mawaziri wake na hata Rais mwenyewe pamoja na familia yake wamejihusisha na vitendo vya ufisadi na kujinufaisha binafsi, bali pia ni namna walivyofanya hivyo waziwazi bila hata kujaribu kuficha," alisema Subramaniam.

Ikulu ya Marekani imekuwa ikikanusha mara kwa mara madai yoyote ya ukiukaji wa sheria.

Afisa mmoja wa Ikulu ya White House, alisema kuwa utawala wa Trump "uko tayari wakati wote" kujibu maombi ya uchunguzi na uangalizi kutoka kwa Bunge la Congress, bila kujali ni chama gani kitakachokuwa na udhibiti wake.

Hegseth na Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon)

Picha ya Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi
Maelezo ya picha, Picha ya Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wabunge wa Democratic wameahidi kufanya uchunguzi kuhusu namna Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth alivyoshughulikia vita dhidi ya Iran, vilivyoanza mwezi Februari.

Uchunguzi huo utajumuisha idadi ya raia waliouawa, upungufu wa silaha na risasi, gharama za vita pamoja na madai kwamba wanajeshi na vituo vya kijeshi havikuwa vimejiandaa vya kutosha.

Kwa mujibu wa chanzo kinachofahamu majadiliano hayo, masuala mengine yanayoweza kuchunguzwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya boti katika eneo la Carribean, ambayo serikali inasema inalenga kuzuia dawa za kulevya kuingizwa nchini Marekani.

Mwezi Aprili, kundi la wabunge wa Democratic katika Bunge la Wawakilishi lilichukua hatua isiyo ya kawaida kwa kuanzisha uchunguzi wa kumwondoa Hegseth madarakani, likimtuhumu kwa makosa makubwa ya ukiukaji wa sheria na ukiukaji wa wajibu wa wadhifa wake kuhusiana na vita vya Iran.

Mchakato wa kumwondoa Rais au afisa wa serikali madarakani unahitaji uungwaji mkono wa wingi wa kura katika Bunge la Wawakilishi.

Hata hivyo, ili afisa huyo apatikane na hatia na kuondolewa madarakani, kunahitajika uungwaji mkono wa theluthi mbili ya wajumbe wa Seneti.

Hakuna mwanachama wa Baraza la Mawaziri la Marekani ambaye amewahi kuondolewa madarakani kupitia utaratibu huo.

.

Uhamiaji na misako ya Shirika la Uhamiaji na Forodha la Marekani (ICE)

Viongozi waandamizi wa Democratic, akiwemo Robert Garcia kutoka California, ambaye atakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uangalizi ya Bunge la Wawakilishi, wametaja utekelezaji wa sheria za uhamiaji kuwa mojawapo ya vipaumbele vya juu katika uchunguzi unaoweza kufanywa na Congress.

Uchunguzi huo unaweza kuangazia madai ya ukiukaji wa sheria na utovu wa nidhamu unaofanywa na maafisa wa Shirika la Uhamiaji na Forodha la Marekani (ICE) wakati wa operesheni za kuwakamata na kuwazuilia wahamiaji katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Hata hivyo, uchunguzi wa aina hiyo unaweza kuwa mgumu na wenye kuibua mijadala mikali ya kisiasa.

Trump aliingia katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2024 akiahidi kuwafukuza nchini wahamiaji wasio na vibali halali vya kuishi Marekani. Ujumbe huo uliungwa mkono na wengi wa wafuasi wake.

Lakini tafiti za hivi karibuni za maoni ya wananchi zinaonyesha kuwa Wamarekani wengi, wakiwemo baadhi ya waliompigia kura Trump katika uchaguzi huo, hawaridhishwi na baadhi ya mbinu ambazo maafisa wa ICE wamekuwa wakitumia katika miji mbalimbali tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Jaribio la kumwondoa Trump madarakani

Wanademocratic wamegawanyika kuhusu uwezekano wa kuanzisha kwa mara ya tatu mchakato wa kumwondoa Trump madarakani.

Baadhi yao, akiwemo Alexandria Ocasio-Cortez, wameunga mkono hatua hiyo, wakitaja vita dhidi ya Iran ambavyo wanaamini havikuidhinishwa kisheria, pamoja na hatua nyingine wanazosema zinaweza kuchangia kumwondoa madarakani.

Trump amekuwa akikanusha mara kwa mara madai yote ya kufanya makosa.

Pia haijulikani iwapo Wanademocratic wataweza kukubaliana kuhusu sababu maalumu ya kuanzisha mchakato huo.

"Naweza kufanya chochote nikitaka," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ya Rais ndani ya Ikulu ya Marekani mwezi Oktoba.

Pia alielezea juhudi za kumwondoa madarakani wakati wa muhula wake wa kwanza pamoja na kesi za jinai zilizomkabili baadaye kuwa ni "vitendo vilivyokuwa kinyume kabisa cha sheria."

Hata hivyo, Suhas Subramaniam anaamini kuwa juhudi hizo zina ujumbe muhimu zaidi kwa mustakabali wa nchi.

"Ikiwa tutashindwa kuchukua hatua kwa sababu tuna wasiwasi kuhusu jinsi umma utakavyoitikia, au kwa sababu tunadhani hatutafanikiwa, au kwa sababu upande mwingine unazuia juhudi zetu, hilo litakuwa kosa," alisema.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi