Jenerali mstaafu wa Uganda akamatwa kwa madai ya uasi

Chanzo cha picha, Chris Magezi/X
Aliyekuwa Naibu Mkuu wa Majeshi nchini Uganda, Luteni Jenerali mstaafu Peter Elwelu, amekamatwa na vyombo vya usalama kwa madai ya kuhusika katika shughuli za uasi na mipango ya kuvuruga usalama katika ukanda wa Teso mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa ya kukamatwa kwake ilitangazwa Jumatatu jioni na kaimu msemaji wa Jeshi la Uganda (UPDF), Kanali Chris Magezi, kupitia mtandao wa X.
"Afisa wa zamani wa Jeshi la Uganda (UPDF), Peter Elwelu, amekamatwa jioni ya leo na vyombo vya usalama katika Jiji la Soroti," aliandika Magezi.
Kwa mujibu wa jeshi, Elwelu alikuwa amejificha huku akitafutwa na vyombo vya usalama kufuatia tuhuma za kujihusisha na shughuli zinazodaiwa kuhatarisha utulivu wa eneo la Teso.
Hata hivyo, Elwelu mwenyewe bado hajatoa tamko lolote kuhusu madai hayo. Jeshi limesema atafunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi.
Madai ya kukusanya silaha
Kukamatwa kwa Elwelu kunafuatia kauli kadhaa zilizotolewa katika siku za hivi karibuni na Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Katika chapisho lake la tarehe 27 Oktoba kupitia mtandao wa X, Muhoozi alidai kuwa Elwelu alikuwa akikusanya silaha kwa wingi katika mojawapo ya makazi yake yaliyoko ukanda wa Teso.
"Tumepata silaha nyingi na risasi kutoka nyumbani kwake. Ana saa chache za kujisalimisha kabla hatujamtangaza kuwa muasi na kuchukua hatua stahiki dhidi yake," aliandika Muhoozi.
Mkuu huyo wa majeshi pia alidai kuwa wanajeshi wapatao 20 walikamatwa katika operesheni zilizofanywa katika makazi ya Elwelu.
Kwa upande wake, Kanali Magezi amesema vikosi vya usalama vilivyofanya upekuzi katika makazi ya mwanajeshi huyo wa zamani vilikamata bunduki 15, sare za kijeshi pamoja na magari mawili aina ya pick-up.
Nani ni Peter Elwelu?
Peter Elwelu ni mmoja wa maafisa wa juu wa jeshi ambao wamewahi kushikilia nyadhifa muhimu katika UPDF.
Alijulikana zaidi mwaka 2016 alipokuwa akisimamia operesheni ya kijeshi dhidi ya Kasri la Mfalme wa Rwenzururu katika magharibi mwa Uganda. Operesheni hiyo ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 100 na ilivuta ukosoaji kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu.
Mfalme wa Rwenzururu alikuwa akituhumiwa kuongoza vuguvugu la kutaka kujitenga na Uganda, madai ambayo yamekuwa yakikanushwa na wafuasi wake.
Mwaka 2021, Rais Yoweri Museveni alimteua Elwelu kuwa Naibu Mkuu wa Majeshi kabla ya baadaye kupewa nafasi ya mshauri mwandamizi wa rais.
Mwaka 2024, Marekani iliweka vikwazo dhidi yake kutokana na madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, yakiwemo mauaji yaliyodaiwa kufanywa nje ya mfumo wa sheria na vikosi vya usalama. Elwelu alistaafu rasmi kutoka jeshi mwezi Agosti mwaka huo.
Kuna nini nyuma ya kukamatwa kwake?
Kukamatwa kwa Elwelu kumezua mjadala mkubwa nchini Uganda, huku baadhi ya wachambuzi wakiamini kuwa huenda suala hilo lina mizizi ya kisiasa zaidi ya madai yanayotolewa rasmi.
Wengine wanaamini kuwa vyombo vya upelelezi vya jeshi huenda vilikusanya ushahidi wa kutosha unaodaiwa kuonesha ukiukwaji wa kanuni za UPDF na hivyo kusababisha hatua dhidi yake.
Pia kumekuwa na maswali kuhusu uhusiano wake na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na dalili za kuwepo kwa mvutano kati ya wawili hao. Muhoozi aliwahi kumkosoa hadharani Elwelu katika baadhi ya machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii, hatua iliyoibua maswali kuhusu hali ya uhusiano wao.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya Uganda, Elwelu amekuwa akitajwa mara kwa mara kwa mtindo wake wa uongozi unaodaiwa kuwa mkali, hali ambayo imewahi kumuingiza kwenye migogoro mbalimbali ikiwemo na viongozi wa kijadi katika eneo la Teso.
Athari kwa wanajeshi wastaafu
Kesi ya Elwelu pia imezua mjadala kuhusu nafasi na majukumu ya maafisa wa jeshi waliostaafu nchini Uganda.
Sio mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi ya juu aliyestaafu kukabiliwa na hatua za kisheria. Wengine, akiwemo Luteni Jenerali Henry Tumukunde, waliwahi kukamatwa baada ya kuondoka jeshini.
Baadhi ya wachambuzi wanaona tukio hilo kama ujumbe kwamba maafisa waliostaafu bado wanatarajiwa kuzingatia maadili, desturi na kanuni za jeshi hata baada ya kuondoka katika utumishi.
Hata hivyo, wengine wanaonya kuwa hatua dhidi ya maafisa wa zamani zinaweza pia kuzua hofu miongoni mwa wanajeshi wastaafu, hasa ikiwa zitatazamwa kama zinazohusishwa na tofauti za kisiasa au migongano ya madaraka.
Kwa sasa, macho mengi yanaelekezwa kwenye mahakama ya kijeshi, ambako Elwelu anatarajiwa kufikishwa ili kujibu tuhuma zinazomkabili. Hatua hiyo huenda ikatoa picha kamili zaidi kuhusu sababu za kukamatwa kwake na ushahidi unaomkabili.



































