Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Iran: Kwa nini Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran haonekani hadharani?
- Author, BBC Monitoring
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), hajawahi kuonekana kwenye vyombo vya habari tangu mwanzoni mwa mwezi Machi.
Mwezi huo huo wa Machi, kulitolewa taarifa kwamba aliteuliwa kushika wadhifa huo wa juu ndani ya IRGC.
Alionekana hadharani tangu mwezi Februari 11, alipotoa onyo kwa "adui" dhidi ya ya kuikadiria vibaya Iran katika mkutano uliofanyika mjini Shiraz, kusini mwa nchi, kuadhimisha miaka 47 ya mapinduzi ya 1979.
Tarehe 1 Machi, baadhi ya tovuti za habari ziliripoti kuwa Vahidi ameteuliwa kuwa kamanda mpya wa IRGC, ingawa taarifa hizo hazikutoka katika taasisi kubwa za serikali au vyombo vilivyo karibu na IRGC.
Taarifa hiyo ilitolewa siku moja baada ya kuuawa kwa Meja Jenerali Mohammad Pakpour pamoja na makamanda wengine wakuu katika mashambulizi ya Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kabla ya uteuzi huo, Vahidi alikuwa naibu kamanda mkuu wa IRGC.
End of unaweza pia kusoma:
Mchakato wa uteuzi na ukimya wa viongozi
Kwa mujibu wa katiba ya Iran, Kiongozi Mkuu wa nchi ana mamlaka ya kuteua viongozi wakuu wa kijeshi.
Tarehe 8 Machi, Mojtaba Khamenei alichaguliwa kuwa mrithi wa Ayatollah Ali Khamenei.
Iwapo taarifa hizo ni sahihi, inaashiria kuwa Vahidi aliteuliwa ama na baraza la muda la uongozi lililoundwa baada ya kifo cha Kiongozi Mkuu au kupitia mpango uliokuwa umepangwa awali.
Hata hivyo, Mojtaba Khamenei naye hajawahi kuonekana hadharani tangu kuteuliwa kwake.
Ingawa amekuwa akitoa taarifa kwa maandishi, bado haijathibitishwa kama ndiye aliyemteua Vahidi.
Ujumbe wa mwisho unaohusishwa na Vahidi ulitolewa Machi 19, akitoa rambirambi kufuatia kifo cha Brigedia Jenerali Gholamreza Soleimani, kamanda wa Basij, katika shambulio mjini Tehran.
Wakati huo, vyombo vya habari vya Iran vilikuwa vikiendelea kumtaja kama Kamanda Mkuu wa IRGC.
Tarehe 22 Aprili, shirika la habari la Fars linalohusishwa na IRGC liliripoti kuwa waziri wa ujasusi wa muda alimpongeza Vahidi kwa Siku ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, akimtaja kama kaimu kamanda mkuu, ingawa haikubainishwa ni nani aliyekuwa amechukua nafasi ya Waziri wa Ujasusi Ismail Khatib.
Kutokuwepo kwa Vahidi katika hadhira kuna utofauti mkubwa ukilinganishwa na maafisa wengine wakuu wa IRGC waliohudumu hapo awali.
Kinachomzuia kusafiri
Vahidi yuko chini ya hatua za vikwazo kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya.
Vikwazo hivyo vinazuia kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kusafiri, kuhamisha fedha, na kufanya shughuli za kibiashara kimataifa.
Marekani ilimwekea vikwazo kwa mara ya kwanza mwaka 2010 kutokana na uhusiano wake na programu za nyuklia na makombora za Iran.
Baadaye, mwaka 2022, aliongezwa tena kwenye orodha ya vikwazo kwa kutuhumiwa kuwa afisa wa serikali ya Iran aliyehusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya watu nchini Iran au raia na wakazi wa Iran, au familia zao, kuanzia tarehe 12 Juni 2009, bila kujali kama ukiukwaji huo ulitokea ndani au nje ya Iran.
Marekani pia ilimwekea vikwazo upya mwaka 2022 chini ya Amri ya Utendaji 13553 baada ya kifo cha Mahsa Amini, alipokuwa waziri wa mambo ya ndani na kusimamia majibu ya serikali katika kukabiliana na maandamano ya nchi nzima.
Kwa mujibu wa Wizara ya Hazina ya Marekani, Vahidi alihusishwa na kupanga kuzimwa kwa intaneti na kuongoza Jeshi la Utekelezaji wa Sheria la Iran linalojulikana kama NAJA wakati wa ukandamizaji wa maandamano.
Umoja wa Ulaya ulimwekea vikwazo kwa mara ya kwanza mwaka 2008, kisha ukaweka vikwazo vipya mwaka 2022 kutokana na matumizi ya risasi za moto, kukamata watu kiholela wakiwemo waandamanaji na waandishi wa habari, pamoja na ukandamizaji mkali wa maandamano.
Mvutano na tofauti za kisiasa kati yake na Ghalibaf
Kamanda wa Jeshi la Anga, Majid Mousavi, huonekana mara kwa mara kwenye mikutano ya hadhara na pia hutumia mitandao ya kijamii.
Katika video iliyotolewa Aprili 19, alionekana akitembelea kituo cha makombora kilichopo chini ya ardhi.
Tarehe 23 Aprili, wakati Rais wa Marekani Donald Trump aliposema kuwa kuna mgawanyiko ndani ya Iran, viongozi wa Iran walitoa ujumbe wa mshikamano, lakini Vahidi hakutoa tamko lolote.
Vahidi pia anatuhumiwa kuhusika katika shambulio la bomu la mwaka 1994 dhidi ya kituo cha jamii ya Wayahudi nchini Argentina lililosababisha vifo vya watu 85.
Vyombo vya upinzani vilivyo London vimeripoti madai ya tofauti zake za kisera na Rais Masoud Pezeshkian kuhusu maamuzi ya vita na usimamizi wa uchumi.
Pia inadaiwa kuwa alijaribu kupunguza ushawishi wa Spika wa Bunge Mohammad Bagher Ghalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi wakati wa mazungumzo na Marekani yaliyokuwa yakipatanishwa na Pakistan.
Tarehe 24 Aprili, CNN iliripoti kuwa mipango ya kijeshi ya Marekani inajumuisha uwezekano wa kushambulia viongozi wa kijeshi wa Iran, na jina la Vahidi pia lilitajwa katika ripoti hiyo.
Mustakabali wa uongozi Iran
Iran haijagawanyika katika mgawanyiko wa kiraia na kijeshi.
Kinachoshuhudiwa ni mchakato wa mpito baada ya Khamenei, ambapo mfumo wa zamani unapinga kuondolewa, mfumo mpya bado haujajikita kikamilifu, na Kiongozi Mkuu anaonekana kufanya kazi si kama msuluhishi wa mwisho asiyehojiwa, bali kama mshiriki katika makubaliano mapana yanayoongozwa na taasisi za usalama.
Hali hiyo inaweza kubadilika iwapo Mojtaba Khamenei atafanikiwa kuimarisha mamlaka yake.
Kwa sasa, mfumo unafanya kazi si kama uongozi wa msururu wa amri unaoongozwa na mtu mmoja mwenye nguvu kuu, bali kama muungano wa makundi ya misimamo mikali yanayojaribu kwa pamoja kusimamia vita, diplomasia na ushindani wa ndani kwa wakati mmoja.