Baba aliyegundua mauaji ya binti yake kupitia Facebook

Okuhle is pictured smiling outdoors, standing in front of a tree. She has short hair and is wearing a white, short-sleeved top with yellow flowers on it
Maelezo ya picha, Okuhle alipatikana ametupwa karibu na mto mwezi Agosti. Alikuwa na watoto wawili wa umri wa miaka mitatu na tisa, na alikuwa mwanafunzi wa uhandisi wa kiraia.
    • Author, Nomsa Maseko, Eleanor Smallwood and Thuthuka Zondi
    • Nafasi, BBC World Service
    • Akiripoti kutoka, Ekurhuleni
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Tuku Nkosiyaphantsi aligundua kuwa binti yake alikuwa ameuawa kupitia chapisho la Facebook.

Ilikuwa mwezi Agosti na alikuwa hajafanikiwa kuwasiliana na Okuhle mwenye umri wa miaka 27 kwa siku kadhaa, ingawa haikuwa jambo la kushangaza kwake kupoteza mawasiliano mara kwa mara.

Kisha siku moja ya Jumamosi, majirani wawili wa Tuku walimpigia simu kumwambia kuwa walikuwa wameona kwenye Facebook kwamba Okuhle ameripotiwa kupotea na polisi. Pia walikuwa wameona picha ya mtu aliyeonekana kuwa ni Okuhle akiwa amejeruhiwa.

"Nilipotazama picha hiyo, niliona kwamba mtu aliyekuwa ndani yake alikuwa amekufa, na nilipoitazama kwa makini zaidi nikagundua kwamba alikuwa ni Okuhle," anasema Tuku, 50.

Baada ya kuona picha hiyo, Tuku alipiga simu kwa afisa wa polisi aliyemfahamu. Polisi huyo alithibitisha kuwa mwanamke aliyekuwa kwenye picha alikuwa ameuawa na mwili wake kutupwa karibu na mto huko Kokstad, kitovu cha kilimo katika jimbo la KwaZulu-Natal mashariki mwa Afrika Kusini.

Lakini kutokana na kuwa chumba cha kuhifadhia maiti kilikuwa kimefungwa mwishoni mwa wiki, Tuku aliweza kuutambua mwili wa Okuhle Jumatatu asubuhi pekee.

Alipofanya hivyo, Tuku aliona kwamba Okuhle alikuwa ameharibiwa mwili na uso wake ulikuwa umepondwa vibaya.

"Ilikuwa uchungu sana, kiasi kwamba siwezi kukubali."

Tuku Nkosiyaphantsi looks at the camera. He's wearing a dark blue polo shirt and is standing in front of a bush or trees
Maelezo ya picha, Baba wa Okuhle, Tuku, anasema anahisi "kupuuzwa" na serikali baada ya kifo cha binti yake
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Okuhle alikuwa na watoto wawili wa umri wa miaka tisa na mitatu, na alikuwa mwanafunzi wa uhandisi wa kiraia.

Yeye ni mmoja wa wanawake 581 waliouawa nchini humo kati ya Julai na Septemba, kwa mujibu wa Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini.

Kwa ujumla, kulikuwa na mauaji 5,590, idadi ambayo ni chini kwa 204 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Haijulikani wazi kama idadi ya wanawake waliouawa imeongezeka au imepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita kwa kuwa polisi walikuwa wameacha kutoa takwimu hizi kwa mujibu wa jinsia hadi sasa.

Mwaka huu kumekuwa na kilio kipya cha kitaifa kuhusu ukubwa wa ukatili dhidi ya wanawake baada ya miili ya wanawake 12, iliyokuwa imejeruhiwa na baadhi yao wakiwa nusu uchi, kupatikana imetupwa katika maeneo ya umma huko Ekurhuleni, wilaya iliyoko mashariki mwa Johannesburg, kipindi hiki cha kiangazi.

Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu zaidi duniani vya ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake, yaani mauaji ya makusudi ya mwanamke au msichana.

Kujibu mauaji hayo ya kiangazi, Rais Cyril Ramaphosa aliahidi kufanya ukaguzi wa usalama katika kila manispaa ili kubaini na kushughulikia maeneo hatari kwa wanawake, pamoja na kuongeza uwepo wa polisi katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Lakini katika maeneo kama Kokstad na Kempton Park, yote yakiwa ndani ya Ekurhuleni, BBC World Service ilishuhudia wananchi wakichukua jukumu la kulinda wanawake wao wenyewe.

Kwa Tuku, hilo linamaanisha kuchunguza mauaji ya binti yake mwenyewe.

Miezi kadhaa baada ya kuuawa kwake, anasema hakuna mtu aliyekamatwa.

"Ilikuwa kimya tu baada ya kumzika Okuhle. Hakukuwa na chochote kabisa. Natamani sana polisi wangesimama na kufanya uchunguzi."

Anaamini polisi walishindwa kukagua picha za CCTV kutoka jengo la serikali ya eneo hilo ambazo huenda zingeonyesha alikuwa na nani siku aliyopotea. Anasema picha hizo hufutwa kila baada ya siku saba.

BBC iliwasiliana na Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini kuomba maoni yao lakini hadi wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, hakuna jibu lililokuwa limepokelewa.

Huduma hiyo ya polisi hapo awali imekiri mapungufu katika mwitikio wake dhidi ya ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake, ikiongeza kuwa inaendelea kuwekeza katika kushughulikia changamoto hizi. Waziri wa Polisi kaimu, Firoz Cachalia, amesema kunahitajika "juhudi kubwa zaidi" za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Crowds, dressed in black, can be seen protesting and holding placards. One says "A woman is somebody not some body" while another says "Respect female existence or expect our resistance"
Maelezo ya picha, Mauaji ya wanawake kipindi hiki cha kiangazi yalizua maandamano makubwa kote Afrika Kusini

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2024 ya Baraza la Utafiti wa Tiba la Afrika Kusini, idadi ya kesi za mauaji ya wanawake ambazo hazijatatuliwa ilikuwa inaongezeka.

Mwaka huu, Amnesty International ilisema huduma ya polisi ya Afrika Kusini "ina uhaba wa rasilimali, vifaa duni na mafunzo yasiyotosha ili kujibu kwa ufanisi na kwa hisia zinazostahili visa vya ukatili wa kijinsia".

Tuku anasema sasa anatafuta picha za CCTV na kuwasaka watu waliomfahamu binti yake kwa matumaini ya kupata vidokezo.

Licha ya ahadi za Ramaphosa, hana imani kubwa kwamba mambo yatabadilika.

"Nimsikilize Ramaphosa? Serikali huchukua hatua tu baada ya jambo kutokea. Sisi huku Kokstad tunahisi tumepuuzwa na hatuonekani. Serikali haitujali."

Alipoulizwa mapema mwezi huu na BBC kuhusu maendeleo ya Afrika Kusini katika kulinda usalama wa wanawake, Ramaphosa alisema serikali itatenga fedha za ziada katika Bajeti ya Februari kushughulikia ukatili wa kijinsia.

Akizungumza alipokuwa akipiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, Ramaphosa aliongeza kuwa serikali imeongeza idadi ya polisi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita "na tutaendelea kufanya hivyo ili kuwe na polisi wengi zaidi wanaoonekana mitaani."

A dozen men who comprise the patrol group are picture standing together at night. Some are holding whips and sticks. Most are wearing coats and hats.
Maelezo ya picha, Kundi la wanaume hufanya doria za usiku huko Kokstad na kutekeleza muda wa kutotoka nje unaowashauri watoto kuwa ndani kabla ya machweo

Okuhle si mwanamke pekee aliyeuawa kikatili mwaka huu huko Kokstad.

Kati ya Januari na Oktoba mwaka huu, miili ya wanawake watano na watoto wadogo watatu ilipatikana mjini humo, huku kukiwa na kukamatwa kwa watuhumiwa katika kesi mbili pekee.

Kutokana na hali hiyo, jamii iliunda doria za mitaani na kuweka muda wa kutotoka nje kwa wanawake na watoto kipindi hiki cha kiangazi.

Tangu Juni, watoto wanaelekezwa kuwa majumbani kabla ya machweo huku wanawake wakitakiwa kuwa ndani kabla ya saa 3:00 usiku.

Kamvalethu Cetywayo, 34, kutoka kundi la ulinzi wa jamii, anaongoza kundi la takriban wanaume 15 wanaofanya doria katika maeneo yenye viwango vya juu vya uhalifu usiku, ikiwemo maeneo ambayo miili imewahi kupatikana au ambako matukio ya uhalifu yameripotiwa.

Doria hizo kwa kawaida hufanyika kati ya Alhamisi na Jumapili kwa sababu huo ndio wakati watu hutumia pombe nyingi zaidi, anasema Kamvalethu.

Wengi wa wanaofanya doria hubeba fimbo, viboko na tochi, lakini Kamvalethu ana bunduki halali. Anasema kundi hilo huwaita polisi wanapohitaji msaada.

Alipoulizwa jinsi anavyohisi kuhusu kuweka vikwazo kwa uhuru wa wanawake na watoto, Kamvalethu alisema muda huo wa kutotoka nje husaidia kuwaweka salama, ni wa hiari, na ni hatua ya muda hadi polisi watakapowakamata wauaji.

"Kwa maazimio tuliyofikia na jamii, tunaweza kuwasaidia kwa hili, lakini kama watu wanakataa hakuna tunachoweza kufanya."

Hata hivyo, si wahanga wote hushambuliwa usiku au mitaani.

Kgothatso is sitting in a living room. She has auburn hair and is wearing a black, sleeveless top and has a headband.
Maelezo ya picha, Kgothatso anasema alikuwa akielekea kazini kwa teksi wakati dereva alipojaribu kumteka nyara

Kgothatso Mojela alitekwa nyara akiwa njiani kwenda kazini mwaka 2018 huko Kempton Park, ndani ya manispaa ya Ekurhuleni.

Alikuwa ndani ya teksi wakati dereva alifunga milango na kuanza kuendesha kuelekea upande usio sahihi.

Kgothatso alipomwambia dereva kwamba alikuwa amekosa mgeuko, anasema alianza kumpiga ngumi na makofi.

"Mara moja nilijua maisha yangu yalikuwa hatarini," anasema Kgothatso, ambaye sasa ana umri wa miaka 35.

Kgothatso anasema alifungua mlango wa upande wa abiria kwa nguvu na kujirusha nje ya teksi iliyokuwa ikienda, jambo lililosababisha jeraha kubwa kwenye goti lake na uharibifu wa mishipa ya macho. Walinzi wawili waliokuwa karibu walimsaidia.

Anasema mshambuliaji wake baadaye alifungwa kwa makosa kadhaa ya jinai, yakiwemo aliyomtendea yeye, lakini aliachiwa huru mwaka jana. Kgothatso anasema sasa ana hofu kwa maisha yake.

Hata hivyo, wakati Kgothatso alishambuliwa na mgeni, kwa mujibu wa Baraza la Utafiti wa Tiba la Afrika Kusini, asilimia 60 ya wanawake waliouawa nchini kati ya 2020 na 2021 waliuawa na wapenzi wao au wenza wao wa karibu.

Baada ya kushambuliwa, Kgothatso amefanya mabadiliko katika maisha yake, ikiwa ni pamoja na kununua bunduki ya kuigiza ili kuwatisha washambuliaji wanaoweza kumvamia.

Pia aliacha kukimbia peke yake na anahakikisha anaongozana na mtu mwingine anapokutana na mteja ambaye hajawahi kukutana naye hapo awali kazini.

Tahadhari kama hizo zimekuwa jambo la kawaida kwa wanawake wengi nchini Afrika Kusini.

Zama is sitting indoors on a chair in front of a window. She's wearing a black sports vest.
Maelezo ya picha, Zama anasema kikundi chao cha wakimbiaji sasa huchukua tahadhari za ziada wakati wa kukimbia, ikiwemo kubeba dawa ya pilipili na filimbi

Mwezi Septemba polisi waliwashauri wanawake katika eneo la Kempton Park kuepuka kutembea au kukimbia peke yao, "hasa katika maeneo yaliyotengwa", baada ya kuuawa kwa mama wa watoto mwenye umri wa miaka 38, Elizabeth Moselakgomo.

Alipotea tarehe 9 Septemba alipokuwa amekwenda kukimbia. Mwili wake uliokuwa na majeraha makubwa na sehemu ya mavazi yake kuondolewa ulipatikana karibu na barabara kuu yenye shughuli nyingi huko Kempton Park siku tatu baadaye.

Mauaji hayo yaligusa kwa kina jamii ya wakimbiaji nchini Afrika Kusini, wakiwemo dada Zonke na Zama Mthethwa. Miaka tisa iliyopita walianzisha The Pack, kikundi cha wanawake wakimbiaji mjini Johannesburg. Elizabeth alikuwa akihudhuria baadhi ya matukio ya The Pack.

Wakimbiaji kutoka kote jijini walijiunga katika juhudi za kumtafuta baada ya kutoweka kwake, na walishiriki katika maandamano ya kutaka ukatili dhidi ya wanawake ukomeshwe.

Kikundi cha Zonke na Zama sasa huchukua tahadhari za ziada wakati wa kukimbia, ikiwa ni pamoja na kubeba dawa ya pilipili na filimbi. Pia hupata magari ya kuwafuata na wameanza kutoa mafunzo ya kujilinda kwa wanawake katika kikundi chao.

"Tunahitaji kujaribu kuhamasisha na kuunda maeneo salama ambapo wanawake wanaweza kujitokeza kwa uhalisia wao na kufanya kile wanachopenda kufanya," anasema Zama, 37.

Kgothatso is seen speaking outdoors into a microphone to a small audience who are covered by a marquee. She's wearing a red cap and shawl - others in the crowd are also dressed in red
Maelezo ya picha, Kgothatso alisimulia hadithi yake kwa jamii yake kwa mara ya kwanza katika matembezi ya maombi ya kuwakumbuka wanawake waliouawa

Baada ya tukio hilo, Kgothatso alihama Kempton Park na sasa anaishi karibu na wazazi wake katika sehemu nyingine ya nchi.

Mama yake, ambaye ni mwanaharakati wa jamii, hivi karibuni aliandaa matembezi ya maombi ya kuwakumbuka wanawake waliouawa.

Kgothatso alisimulia hadithi yake kwa jamii yake kwa mara ya kwanza katika matembezi hayo.

Akiwa anafuta machozi, alisema:

"Kwa manusura yeyote anayenisikiliza sasa, nataka kusema kwamba wewe si mchafu, hujavunjika kiasi cha kutoweza kurekebishwa. Huna lawama na hauko peke yako."