Maamuzi manne ya kisheria yaliyotikisa soka duniani

.
Maelezo ya picha, Jean-Marc Bosman kushoto akiwa na Markus Merk
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Uamuzi wa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) wa kuirejeshea Senegal ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 ni mojawapo ya maamuzi makubwa ya kisheria katika historia ya soka la Afrika. Uamuzi huo wa Novemba 24, 2026, ulihitimisha kwa upande wa Senegal mzozo ulioanza baada ya fainali ya Januari dhidi ya Morocco, lakini pia umeibua mjadala kuhusu mamlaka ya vyombo vya soka katika kusimamia mashindano.

Senegal ilikuwa imeshinda fainali hiyo kwa bao 1-0 baada ya muda wa ziada, lakini Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kupitia kamati yake ya rufaa, lilibatilisha matokeo hayo na kuipa Morocco ushindi wa mezani wa mabao 3-0 mwezi Machi 2026.

Senegal ilikata rufaa CAS, ambayo ilibatilisha uamuzi wa kamati ya rufaa ya CAF na kuthibitisha uamuzi wa awali wa kamati ya nidhamu, hivyo kuirejeshea Senegal ubingwa. CAS ilizingatia kuwa mwamuzi alikuwa na mamlaka ya kuendelea na mchezo baada ya wachezaji wa Senegal kurejea uwanjani, na kwamba mchezo haukuwa umetangazwa kuwa umevunjika rasmi.

Morocco imesema itafuata njia nyingine za kisheria kupinga uamuzi huo, huku CAF ikisema itaheshimu na kutekeleza hukumu ya CAS. Tukio hilo linaongeza kwenye orodha ya kesi za kisheria zilizowahi kubadilisha mwelekeo wa soka duniani, kuanzia haki za wachezaji hadi mamlaka ya waandaaji wa mashindano.

Kesi ya Jean-Marc Bosman - 1995

s

Kwa miaka mingi, wachezaji wa soka barani Ulaya hawakuwa na uhuru kamili wa kujiunga na klabu nyingine hata baada ya mikataba yao kumalizika. Klabu iliyokuwa inamiliki mikataba yao ingeweza kudai ada ya uhamisho kabla ya mchezaji kuruhusiwa kujiunga na timu nyingine. Mfumo huo ulibadilika kufuatia kesi ya mchezaji wa Ubelgiji, Jean-Marc Bosman.

Mwaka 1990, Bosman alikuwa akiichezea RFC Liège ya Ubelgiji na alitaka kujiunga na Dunkerque ya Ufaransa baada ya mkataba wake kumalizika. Hata hivyo, uhamisho huo haukukamilika baada ya klabu ya Ubelgiji kudai ada ambayo Dunkerque haikutaka kulipa. Bosman alijikuta katika hali ngumu ya kikazi na akaamua kufungua kesi dhidi ya klabu yake, Shirikisho la Soka Ubelgiji na UEFA.

Desemba 15, 1995, Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya ilitoa uamuzi uliomuunga mkono Bosman. Mahakama ilisema mfumo wa kudai ada ya uhamisho kwa mchezaji ambaye mkataba wake umemalizika unakiuka kanuni za uhuru wa raia wa Umoja wa Ulaya kufanya kazi katika nchi nyingine wanachama. Pia ilipinga vizuizi vilivyowekwa kwa idadi ya wachezaji raia wa Umoja wa Ulaya ambao klabu ingeweza kuwatumia katika mechi.

Uamuzi huo ulipokelewa kama ushindi mkubwa kwa haki za wachezaji na vyama vyao, lakini pia ukabadilisha kwa kiasi kikubwa soko la usajili barani Ulaya mpaka leo mkataba ukimaliza mchezaji anakuwa huru kwenda anakotaka. Wachezaji wengi waliweza kuhamia klabu nyingine bila ada ya uhamisho baada ya mikataba yao kuisha.

Bosman mwenyewe, hata hivyo, hakupata mafanikio makubwa ya kifedha aliyotarajia kutokana na kesi hiyo, na baadaye alieleza gharama binafsi alizolipa katika mapambano hayo.

Kesi dhidi ya European Super League - 2023

.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka 2021, baadhi ya klabu kubwa barani Ulaya zilitangaza mpango wa kuanzisha mashindano mapya yaliyoitwa European Super League, ambayo yangekuwa na klabu zenye hadhi kubwa na mapato makubwa ya kibiashara. Mpango huo ulihusisha klabu 12 za awali, zikiwemo Real Madrid, Barcelona, Juventus, Manchester United, Liverpool na Manchester City.

Hata hivyo, UEFA na FIFA zilipinga mpango huo na kuonya kwamba klabu au wachezaji watakaoshiriki mashindano hayo wanaweza kukabiliwa na adhabu, ikiwemo kuzuiwa kushiriki mashindano mengine. Waandaaji wa Super League, kupitia kampuni ya European Superleague Company, walifungua kesi dhidi ya FIFA na UEFA wakipinga mamlaka yao ya kuzuia mashindano hayo.

Desemba 21, 2023, Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya iliamua kuwa kanuni za FIFA na UEFA kuhusu kuidhinisha mashindano mapya hazikuwa na mfumo wa wazi na vigezo vya kutosha vya uwazi na usawa. Mahakama ilisema kanuni hizo zinaweza kukiuka sheria za ushindani za Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, haikuidhinisha moja kwa moja kuanzishwa kwa Super League wala kusema kuwa mashindano hayo lazima yaruhusiwe.

Uamuzi huo ulipokelewa kwa mitazamo tofauti. Real Madrid na Barcelona waliutaja kama ushindi kwa uhuru wa kuanzisha mashindano, huku UEFA ikisisitiza kuwa mahakama haikuidhinisha mradi wa Super League. Mashabiki wengi na klabu nyingine pia walikuwa wamepinga mpango huo tangu ulipotangazwa mwaka 2021, wakihofia athari zake kwa mfumo wa kawaida wa ligi na mashindano ya Ulaya

Kesi ya Lassana Diarra - 2024

.
Maelezo ya picha, Lassana Diarra

Mwaka 2014, kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Lassana Diarra, alihusika katika mgogoro wa kimkataba na klabu ya Lokomotiv Moscow ya Urusi. Klabu hiyo ilidai kuwa mchezaji huyo alivunja mkataba bila sababu za msingi na kuwasilisha malalamiko FIFA. Chombo cha utatuzi wa migogoro cha FIFA baadaye kilimwamuru Diarra kulipa fidia ya euro milioni 10.5 kwa klabu hiyo.

Diarra alitaka kujiunga na klabu ya Charleroi ya Ubelgiji mwaka 2015, lakini uhamisho huo ulikwama kutokana na kanuni za FIFA zilizohusisha utoaji wa hati ya kimataifa ya uhamisho na uwezekano wa klabu mpya kuwajibika kwa fidia iliyodaiwa na klabu ya zamani. Mchezaji huyo aliamua kupeleka suala hilo mahakamani akipinga kanuni hizo, akisema zilimzuia kupata ajira na kufanya kazi katika klabu nyingine.

Oktoba 4, 2024, Mahakama ya Haki ya Umoja wa Ulaya ilitoa uamuzi uliomuunga mkono Diarra, ikisema baadhi ya kanuni za FIFA kuhusu kuvunjwa kwa mikataba na uhamisho wa wachezaji zinakinzana na sheria za Umoja wa Ulaya kuhusu uhuru wa kufanya kazi na ushindani. Mahakama ilibaini kuwa kanuni hizo zinaweza kuzuia uhamaji wa wachezaji na kuathiri uwezo wa klabu kuwasajili.

Uamuzi huo ulipokelewa kwa furaha na chama cha kimataifa cha wachezaji wa kulipwa, FIFPRO, ambacho kilisema ulikuwa fursa ya kuboresha mfumo wa usajili na kulinda haki za wachezaji. Hata hivyo, uamuzi huo haukumaanisha kuwa kanuni zote za FIFA kuhusu uhamisho zimefutwa. Badala yake, uliweka shinikizo kwa FIFA kupitia upya baadhi ya taratibu zake ili ziendane na sheria.

Kesi ya Manchester City - (2020)

.

Mwaka 2020, Manchester City ilikabiliwa na moja ya kesi kubwa zilizohusisha kanuni za matumizi ya fedha katika soka la Ulaya. UEFA iliishutumu klabu hiyo kwa kuwasilisha taarifa zisizo sahihi kuhusu mapato yake ya udhamini na ukiukaji wa kanuni za Financial Fair Play (FFP), zilizowekwa kuhakikisha klabu hazitumii fedha kupita uwezo wao wa kifedha.

Februari 14, 2020, chombo cha UEFA kinachosimamia udhibiti wa fedha za klabu kiliamua kuipiga marufuku Manchester City kushiriki mashindano ya klabu za Ulaya kwa misimu miwili, pamoja na kuitoza faini ya euro milioni 30. Manchester City ilikataa uamuzi huo na kukata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), ikipinga madai ya UEFA.

Julai 13, 2020, CAS ilibatilisha adhabu ya kuifungia klabu hiyo kushiriki mashindano ya Ulaya, na kupunguza faini kutoka euro milioni 30 hadi milioni 10. CAS ilisema madai mengi ya ukiukaji hayakuthibitishwa kwa ushahidi wa kutosha au yalikuwa yamepitwa na muda wa kisheria. Hata hivyo, ilibaini kuwa Manchester City haikushirikiana ipasavyo na uchunguzi wa UEFA, jambo lililostahili adhabu ya kifedha.

Uamuzi huo uliibua mjadala mkubwa kuhusu namna UEFA inavyotekeleza kanuni za Financial Fair Play na uwezo wake wa kuiwajibisha klabu kubwa. Manchester City ilikaribisha uamuzi huo kama ushindi, wakati UEFA ilisema imeupokea na kusisitiza umuhimu wa kanuni za kifedha katika kuhakikisha klabu zinaendeshwa kwa uendelevu