Safari ya Katiba mpya Tanzania inavyopitia misukosuko na matumaini

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa zaidi ya miongo mitatu, Tanzania imekuwa katika safari ya kutafuta Katiba mpya, mchakato ambao umeibua matarajio makubwa ya mabadiliko ya mfumo wa utawala, demokrasia na uwajibikaji, lakini pia umekumbwa na misuguano ya kisiasa na kutokubaliana kuhusu aina ya Katiba inayohitajika. Katika kipindi hicho, suala la Katiba limekuwa likijitokeza katika awamu tofauti za uongozi, huku kila hatua ikionekana kufungua ukurasa mpya wa matumaini.
Mjadala wa kuwa na Katiba mpya ulipata nguvu zaidi baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Wito huo ulihusishwa na hoja kwamba Katiba iliyokuwepo, iliyotungwa mwaka 1977 wakati Tanzania ikiwa chini ya mfumo wa chama kimoja, ilihitaji kufanyiwa mabadiliko ili kuendana na mazingira mapya ya kisiasa na kuongeza uwajibikaji katika uendeshaji wa serikali.
Mwaka 2011, chini ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, serikali ilianzisha mchakato rasmi wa kupitia upya Katiba, uliosababisha kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu iliyofikishwa katika Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014. Hata hivyo, tofauti kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu hiyo, hasa muundo wa Muungano, ziliibua mvutano na hatimaye mchakato haukukamilika.
Katika awamu zilizofuata za uongozi, suala hilo liliendelea kuwa ajenda ya vyama vya upinzani na makundi ya kiraia, huku juhudi za kulifufua zikichukuliwa katika utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan. Hata hivyo, tofauti kuhusu namna ya kuendesha mchakato na ushiriki wa wadau zimeendelea kujitokeza, zikiwemo hoja kuhusu kama kuanzia upya au kutumia nyaraka zilizotokana na mchakato wa awali.
Sasa, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na matukio yaliyofuata, matumaini mapya yameibuka baada ya Rais Samia kutangaza kuwa Tanzania inatarajiwa kuwa na Katiba mpya au iliyorekebishwa ifikapo mwaka 2028 au 2029. Lakini, wakati serikali ikijiandaa kuanzisha Tume ya Maridhiano, baadhi ya wadau wanahoji kama hatua hizo zitashughulikia sababu zilizofanya mchakato uliopita kukwama, au kama taifa linaweza kuingia tena katika mzunguko mwingine wa matumaini na misuguano misukosuko.
Nia na mchakato ulivyoanza

Chanzo cha picha, Mpekuzi
Mizizi ya safari ya Katiba mpya Tanzania inarejea katika kipindi cha mabadiliko ya mfumo wa kisiasa mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakati nchi ilipokuwa ikijiandaa kuachana na mfumo wa chama kimoja na kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Mwaka 1991, Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, aliteua Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa iliyoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali, kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa kisiasa walioutaka.
Tume hiyo ilipendekeza kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini pia ilitoa mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba, yakiwemo kuhusu muundo wa Muungano na mgawanyo wa madaraka. Mwaka 1992, Tanzania ilirejesha rasmi mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini mjadala kuhusu mabadiliko mapana ya Katiba uliendelea.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka 1998, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alianzisha hatua nyingine kupitia Kamati ya Jaji Robert Kisanga, iliyokusanya na kuchambua maoni kuhusu masuala ya Katiba. Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa mapendekezo yaliyotangulia, suala la kupata Katiba mpya halikufikia hatua ya kukamilika.
Hatua kubwa zaidi ilifikiwa mwaka 2011, wakati serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilipopitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoweka utaratibu wa kuanzisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa rasimu na hatimaye kuifikisha kwa wananchi kupitia kura ya maoni.
Aprili 2012, Rais Kikwete alimteua Jaji Joseph Warioba kuongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo ilifanya mikutano katika maeneo mbalimbali nchini, ikikusanya maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa utawala, Muungano, madaraka ya Rais, haki za binadamu, uwajibikaji na masuala mengine ya msingi.
Desemba 2013, Tume iliwasilisha Rasimu ya Katiba iliyokuwa na mapendekezo kadhaa ya mabadiliko. Miongoni mwa mapendekezo yaliyozua mjadala mkubwa ni kuanzishwa kwa muundo wa serikali tatu, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar, badala ya mfumo wa serikali mbili uliokuwepo.
Rasimu hiyo iliwasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba lililoanza Februari 2014, likiwa na jukumu la kujadili na kupitisha Katiba inayopendekezwa. Bunge hilo liliongozwa na Samuel Sitta akisaidiwa na Samia Suluhu Hassa (sasa Rais) kama makamu mwenyekiti na lilikuwa na wajumbe kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo wabunge na wawakilishi wengine walioteuliwa kwa mujibu wa sheria.
Baada ya mijadala na mabadiliko yaliyofanyika huku wapinzani wakisusia na kutoka, Bunge Maalumu lilipitisha Katiba Inayopendekezwa Oktoba 2014. Hatua iliyofuata ilikuwa ni kuifikisha kwa wananchi kupitia kura ya maoni ili waamue kama wanaikubali au la.
Misukosuko ya kukumbukwa

Chanzo cha picha, Mwananchi
Licha ya hatua kubwa zilizokuwa zimefikiwa, mchakato huo ulikumbwa na misuguano mikubwa ya kisiasa, hasa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, ambako kulikuwa na tofauti kuhusu mapendekezo ya Tume ya Warioba.
Moja ya hoja zilizogawa wajumbe ilikuwa pendekezo la serikali tatu. Baadhi ya wajumbe walitaka mfumo huo upitishwe kama ulivyopendekezwa na Tume, huku wengine wakipendelea kuendelea na mfumo wa serikali mbili. Tofauti hizo zilijitokeza pia katika mjadala kuhusu mamlaka ya Rais na mgawanyo wa madaraka.
Mvutano uliongezeka Aprili 2014 baada ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliokuwa wakijumuisha wawakilishi wa vyama vya upinzani, kujiondoa katika vikao vya Bunge Maalumu. Walipinga mwenendo wa majadiliano na mabadiliko yaliyokuwa yakifanywa kwenye rasimu ya Tume ya Warioba.
Hata hivyo, Bunge Maalumu liliendelea na shughuli zake na kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Lakini kura ya maoni iliyopangwa kufanyika mwaka 2015 iliahirishwa. Jaji Warioba anasema wakati huo Tume ya Taifa ya Uchaguzi, iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Damian Lubuva, ilieleza kuwa ilikuwa na jukumu la kuandaa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na isingeweza kusimamia shughuli zote mbili kwa wakati mmoja.
"Tume ya Uchaguzi ya Jaji Lubuva ilisema sasa hivi tunaandaa uchaguzi mkuu, hatuna uwezo wa kufanya yote mawili. Kwa hiyo tunaomba hii ya kura ya maoni (referendum) ihairishwe, na ndivyo ilivyofanya," anasema Warioba.
Anasema ilitarajiwa kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, utaratibu wa kura ya maoni ungeendelea, lakini hilo halikufanyika.
"Ilitegemewa kwamba baada ya uchaguzi wa mwaka 2015, utaratibu ungefanywa wa kupata kura ya maoni, haukufanyika, lakini bado maoni yote yako pale, ni kwenda kwenye kura ya maoni," anasema alipozungumza na Mwanana=chi.

Chanzo cha picha, Pingo
Baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani mwaka 2015, mchakato huo haukuendelezwa hadi kufikia kura ya maoni. Suala la Katiba mpya liliendelea kujadiliwa na vyama vya upinzani na asasi za kiraia, lakini halikuwa miongoni mwa vipaumbele vya serikali yake.
Kwa mtazamo wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, Tanzania imekwama mara mbili katika safari ya kutafuta Katiba mpya, akitaja hatua iliyofuatia Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 na mchakato wa Tume ya Jaji Warioba mwaka 2014.
Akizungumza na ITV, Mnyika anasema katika mchakato wa kwanza CCM ilikataa mapendekezo yaliyotolewa kupitia vikao vyake, huku katika mchakato wa pili chama hicho kikikataa baadhi ya maoni yaliyokuwa kwenye rasimu ya Tume ya Warioba, yakiwemo kuhusu muundo wa serikali tatu.
Anasema kwa sasa Tanzania ina nyaraka mbili muhimu zinazoweza kutumika katika mchakato unaofuata, ambazo ni Rasimu ya Katiba ya Tume ya Warioba na Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba.
"Sasa tuna nyaraka mbili, rasimu ya Warioba na Katiba Inayopendekezwa. Tunapoanza mchakato upya lazima tuanzie hapo kuondoa mkwamo au mgogoro uliotokea wakati ule," anasema Mnyika.
Mwaka 2021, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, mjadala wa mageuzi ya kisiasa ulianza kurejea katika mazungumzo ya serikali na wadau. Desemba mwaka huo, serikali iliunda kikosi kazi kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala, kilichopewa jukumu la kutathmini hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini na kutoa mapendekezo ya maboresho.
Ripoti ya kikosi kazi hicho iliyowasilishwa mwaka 2022 ilipendekeza hatua mbalimbali za mageuzi, zikiwemo kuhusu sheria za uchaguzi, mfumo wa vyama vingi na kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba mpya. Hata hivyo, tofauti ziliendelea kuhusu namna ya kuanza mchakato huo, huku baadhi ya wadau wakitaka Rasimu ya Warioba itumike kama msingi na wengine wakisisitiza kwanza kujenga mwafaka wa kitaifa.
Matumaini yasiyokwisha
Licha ya misukosuko hiyo, matumaini ya kupata Katiba mpya hayajafifia. Katika vipindi tofauti, vyama vya siasa na makundi ya kiraia vimeendelea kudai mabadiliko ya kikatiba, vikieleza umuhimu wa kuimarisha taasisi za umma, uwajibikaji, mgawanyo wa madaraka na mfumo wa uchaguzi.
Chini ya Rais Samia, suala hilo lilirejea katika ajenda ya serikali kupitia mazungumzo ya mageuzi ya kisiasa na mapendekezo ya kikosi kazi cha Mukandala. Hata hivyo, matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 yaliongeza uzito wa mjadala kuhusu maridhiano, haki, uwajibikaji na namna ya kuimarisha misingi ya utawala nchini.
Jaji Warioba anasema kuundwa kwa tume nyingine hakuwezi peke yake kufuta kumbukumbu za yaliyotokea mwaka 2025, akionya kuwa suala la Katiba linahitaji kushughulikiwa kwa kuzingatia changamoto zilizojitokeza.
"Mimi naona hizi tume ni kama utaratibu wa kwenda mpaka tusahau, lakini yaliyotokea mwaka jana huwezi kusahau," anasema.
Anasema bila Katiba mpya inayoweza kushughulikia changamoto zilizojitokeza, kuna hatari ya hali kama hiyo kujirudia au kuwa mbaya zaidi.
"Kwa yaliyotokea mwaka jana, kama hatutakuwa na Katiba mpya ambayo inaweza kutumika, yaliyotokea mwaka jana yanaweza kuwa mabaya zaidi," anaongeza.
Novemba 16, 2026, Rais Samia alitangaza mpango wa kuunda Tume ya Maridhiano na Usuluhishi, ambayo alisema itasaidia kuimarisha umoja wa kitaifa na kuweka msingi wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Novemba 20, akizungumza mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, Rais Samia alisema serikali inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na Katiba mpya au iliyorekebishwa ifikapo mwaka 2028 au 2029.
"Kama tulivyoahidi kwenye ilani, ikifika 2028/2029, tayari tutakuwa na Katiba iliyorekebishwa au jina lolote linalopendwa kuitwa Katiba mpya. Katiba iliyorekebishwa tutakuwa tayari tuko nayo mkononi," alisema Rais Samia.
Alisema serikali ilikuwa katika hatua za kuandaa tume hiyo kwa kuwasiliana na taasisi za dini, vyama vya siasa na asasi za kiraia ili kupata wawakilishi watakaoshiriki katika mchakato wa maridhiano.
Hata hivyo, bado kuna maswali kuhusu namna tume hiyo itakavyoundwa, wadau watakaoshirikishwa na kama itatumia nyaraka zilizopo au kuanza mchakato mpya wa kukusanya maoni ya wananchi.
Kwa upande wa CHADEMA, Mnyika anasisitiza kuwa mchakato mpya unapaswa kuanzia kwenye nyaraka zilizotokana na Tume ya Warioba na Bunge Maalumu la Katiba, huku akitaka tofauti zilizokwamisha mchakato wa awali zishughulikiwe.
Kwa mtu kama Warioba anaona, jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa hatua zinazochukuliwa haziwi njia ya kuahirisha tena mjadala wa Katiba, bali zitoe nafasi ya kushughulikia matatizo ambayo yamekuwa yakijadiliwa kwa miaka mingi.
Kwa hiyo, ahadi ya Rais Samia ya kuwa na Katiba mpya au iliyorekebishwa ifikapo mwaka 2028 au 2029 imefungua ukurasa mwingine katika safari hiyo. Lakini kufikia lengo hilo kutategemea namna serikali na wadau wengine watakavyokubaliana kuhusu msingi wa mchakato, maudhui ya Katiba na nafasi ya wananchi katika kutoa maamuzi.
Baada ya zaidi ya miaka 30 ya mijadala na miaka 15 tangu kuanzishwa kwa mchakato rasmi wa mwaka 2011, je safari hii Tanzania itafanikiwa kupata Katiba mpya au iliyorekebishwa ifikapo mwaka 2028/2029, au matumaini hayo yataendelea kusubiri safari nyingine?



































