Maeneo 5 ya siri ambayo serikali na wanasayansi wanayalinda na watu hawaruhusiwi kufika

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kutoka maeneo yanayohifadhi vifaa hatari hadi maeneo yenye vitu vya thamani vya kihistoria, kuna sayansi inayosimamia baadhi ya maeneo yaliyozuiliwa na kulindwa zaidi duniani.

Kwa kawaida binadamu huwa na hamu ya kutaka kujua kuhusu maeneo ambayo wamezuiwa kuingia.

"Mguu wa tembo"

Inajulikana kama moja ya vitu vyenye mionzi mikali zaidi katika historia, "Mguu wa Tembo" ni kipande cha takriban tani mbili cha lava chenye nyenzo zilizoyeyuka na kinapatikana katika kiwanda cha nyuklia cha Chernobyl nchini Ukraine.

Imeundwa na nyenzo adimu inayoitwa "corium" mchanganyiko wa nishati ya nyuklia.

Eneo hilo liligunduliwa mwaka wa 1986, miezi minane baada ya ajali ya nyuklia ya Chernobyl, na ilikuwa na kiwango cha mionzi kilichokuwa kikubwa hadi ungesimama karibu nacho ungeweza kufariki ndani ya dakika tatu.

Miundombinu ya chuma ilijengwa kuzunguka kiwanda hicho kilichotelekezwa ili kudhibiti mionzi, kwa sasa eneo hilo liko chini ya ulinzi mkali.

Hifadhi ya mbegu ya Svalbard Global Seed Vault

Hii ni hifadhi ilioko chini ya ardhi inayohifadhi baadhi ya sampuli muhimu zaidi za kibaolojia duniani.

Imejengwa kwa barafu katika kisiwa cha Spitsbergen, Svalbard.

Hifadhi hiyo ya dunia ya mbegu inahifadhi zaidi ya mbegu milioni moja, ambazo ziko chini ya uangalizi mkali.

Lengo lake ni kulinda nyenzo za kijenetiki na kuweka akiba ya mbegu iwapo maghala mengine ya mbegu duniani yataharibiwa kutokana na hitilafu za vifaa, vita, magonjwa au majanga asili.

Mapango ya Lascaux

Ni tovuti ya kiakiolojia yenye thamani kubwa kiasi kwamba ni watu wachache tu walioidhinishwa ndiyo wanaoruhusiwa kuitembelea.

Ndani ya Mapango ya Lascaux kuna zaidi ya michoro 600 ya miamba inayohusishwa na kipindi cha 'Upper Palaeolithic,' takriban miaka 17,000 iliyopita.

Awali mapango hayo yalikuwa wazi kwa umma, lakini maelfu ya wageni waliokuwa wakitembelea eneo hilo kila siku, walileta uharibifu kwa sanaa hiyo ya kale.

Mwaka wa 1963, mapango hayo yalifungwa, na wahifadhi wakaweka mifumo ya viyoyozi ili kulinda michoro ya miambani.

Zone Rouge

Eneo la "Zone Rouge" limekuwa limefungwa tangu Vita vya Kwanza vya Dunia.

Eneo hili la zamani la vita limejaa mabomu na risasi ambazo hazikulipuka, na udongo wake umechafuliwa na zebaki na kemikali zinazotiririka kutoka kwenye silaha zilizotelekezwa

Katika maeneo yaliyoathirika zaidi, eneo moja lina hadi mabaki 300 ya makombora kwa kila ekari moja ya ardhi.

Timu maalum inayosafisha eneo hilo inakadiria kuwa itachukua angalau miaka 300 kulisafisha kabisa.

Kisiwa cha Surtsey

Hiki ni kisiwa kisicho na wakazi, kilichoko katika Bahari ya Atlantiki, ambapo ni wanasayansi wachache tu walioidhinishwa ndio wanaoruhusiwa kufika eneo hilo.

Kisiwa hiki kimehifadhiwa kwa uangalifu mkubwa ili kuruhusu utafiti wa kipekee kuhusu jinsi maisha yanavyoanza katika mazingira mapya ya kijiolojia bila kuingiliwa na binadamu.

Kisiwa hicho kipo kusini mwa Iceland, na kiligunduliwa mwaka wa 1963 wakati volkano ya chini ya bahari ilipotokea, na tangu wakati huo kimekuwa kikifuatiliwa kwa karibu sana.

Hii ni kwa sababu kinatoa "majaribio ya asili" ya kipekee kuhusu jinsi maisha huanza kutokea katika eneo jipya.

Wanasayansi wameandika kuhusu kuwasili kwa mamia ya spishi za mimea na wanyama, na utafiti huu bado unaendelea hadi leo.