Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Marekani yasubiri jibu la Iran kuhusu mapendekezo ya kusitisha mapigano - Rubio

Kauli hiyo imejiri baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, kusema kila jitihada za kutafuta suluhisho la kidiplomasia zinapofanywa, Marekani huchagua njia ya operesheni za kijeshi zinazoleta hatari kubwa zaidi.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Usiku mwema.

  2. Mapigano mapya yazuka kati ya Iran na Jeshi la Wanamaji la Marekani katika Mlango wa Hormuz

    Shirika la habari la Fars, linalohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran IRGC, limesema kuwa “kwa saa moja iliyopita, kumekuwa na mapigano ya hapa na pale kati ya vikosi vya Iran na meli za Marekani katika Mlango wa Hormuz.”

    Iran haijatoa maelezo zaidi kuhusu mapigano hayo,.

    Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), meli mbili tupu za mafuta zilizokuwa zikipeperusha bendera ya Iran na kujaribu kuingia katika bandari ya Iran kwenye Ghuba ya Oman zilishambuliwa na kuzimwa uwezo wake wa kufanya kazi.

    Iran na Marekani zilirushiana makombora katika Ghuba ya Uajemi usiku wa kuamkia leo, huku kila upande ukiilaumu mwingine kwa kuanzisha mapigano hayo.

    Marekani imesema kuwa licha ya mvutano huo, makubaliano ya kusitisha mapigano bado hayajavunjwa na yanaendelea kutekelezwa.

  3. EU: Zaidi ya wakaazi milioni tatu wa Lebanon wanahitaji misaada ya kibinadamu

    Umoja wa Ulaya umesema kuwa zaidi ya nusu ya wananchi wa Lebanon kwa sasa wanategemea misaada ya kibinadamu ili kuendelea kuishi, huku mashambulizi ya Israel yakiendelea kuathiri maisha ya maelfu ya watu nchini humo.

    Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya usimamizi wa majanga, Hadja Lahbib, amesema hali ya kibinadamu nchini Lebanon inaendelea kuwa mbaya kutokana na mzozo huo.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini Beirut baada ya kukutana na Rais wa Lebanon Joseph Aoun, Lahbib alisema zaidi ya watu milioni tatu nchini humo wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

    Ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya umetenga euro milioni 100 kusaidia Lebanon tangu kuanza kwa vita Machi 2 mwaka huu.

    Kwa mujibu wake, hadi sasa ndege sita zilizobeba misaada ya kibinadamu zimewasili Lebanon, huku ndege ya saba ikitarajiwa kuwasili hivi karibuni.

    Maafisa wa Lebanon wanasema zaidi ya watu 2,700 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel tangu mwanzoni mwa Machi.

    Tangu wakati huo, zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na kuongezeka kwa mapigano na mashambulizi nchini humo.

  4. Rais wa Afrika Kusini akabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kufuatia uamuzi wa mahakama

    Kiongozi wa upinzani nchini Afrika Kusini, Julius Malema, amemtaka Rais Cyril Ramaphosa ajiuzulu kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba uliobaini kuwa Bunge lilikiuka Katiba kwa kuzuia mchakato wa kumwondoa madarakani mwaka 2022.

    Uamuzi huo umetokana na kesi iliyofunguliwa na chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Malema pamoja na washirika wake, na unaweza kufungua njia ya kuanzishwa upya kwa mchakato wa kumvua madaraka dhidi ya rais huyo.

    Ofisi ya Ramaphosa imesema inaheshimu uamuzi wa mahakama.

    Mwaka 2022, jopo huru la uchunguzi lilibaini kuwa rais huenda akawa na maswali ya kujibu baada ya dola 580,000 taslimu kuibiwa nyumbani kwake kijijini, fedha zilizokuwa zimefichwa kwenye sofa. Tukio hilo lilizua maswali kuhusu chanzo cha fedha hizo, madai ambayo Ramaphosa ameyapinga.

    Hata hivyo, Bunge lilizuia mchakato wa kumwondoa madarakani kupitia kura miaka minne iliyopita, wakati chama chake cha African National Congress (ANC) kikiwa na wingi wa wabunge. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2024, ANC sasa inaongoza serikali ya mseto.

    Kufuatia uamuzi wa mahakama, ofisi ya rais imesema Ramaphosa “anaimarisha dhamira yake kwa Katiba, uhuru wa mahakama na utawala wa sheria,” akisisitiza kuwa amekuwa akishirikiana kikamilifu na uchunguzi wote unaohusiana na suala hilo.

    “Rais Ramaphosa anaamini kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba tuhuma zozote lazima zichunguzwe kwa haki na kwa kuzingatia taratibu za kisheria,” imesema taarifa hiyo.

    Akizungumza nje ya mahakama mjini Johannesburg, Malema amesema rais anapaswa kujiuzulu ili ajikite katika mchakato wa kuondolewa madarakani, akionya kuwa mchakato huo una athari kubwa binafsi na kisiasa.

    EFF ilifungua kesi hiyo katika Mahakama ya Juu zaidi mwaka 2024, kwa kushirikiana na vuguvugu la African Transformation Movement.

    Malema, ambaye pia anakabiliwa na rufaa katika kesi tofauti inayohusu kumiliki bunduki kinyume cha sheria na kuifyatua hadharani, amesema wabunge wa ANC huenda wakaiunga mkono hatua ya kumwondoa madarakani Ramaphosa iwapo ushahidi utawekwa wazi.

    Chama chake pia kimeiandikia Spika wa Bunge la Taifa, Thoko Didiza, kikitaka maelezo ndani ya saa 48 kuhusu hatua zitakazochukuliwa kufuatia uamuzi huo, kwa mujibu wa taarifa ya News24.

    Soma zaidi:

  5. Jibu la Iran kuhusu mapendekezo ya Marekani ya kusitisha mapigano lasubiriwa - Marcos Rubio

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Marekani inatarajia kupokea jibu kutoka Iran Ijumaa (leo) kuhusu mapendekezo ya kumaliza vita.

    Akizungumza na waandishi wa habari nchini Italia, Rubio amesema: “Tutaona jibu litakuwa na nini (baada ya kupokea majibu kutoka Iran). Tunatarajia litakuwa jambo linaloweza kutupeleka katika mchakato wa mazungumzo ya kina.”

    Soma zaidi:

  6. Iran yaanzisha mamlaka ya baharini kudhibiti usafiri katika Mlango wa Hormuz

    Iran imeanzisha mamlaka ya usimamizi wa baharini katika Mlango wa Hormuz itakayotoa vibali kwa meli za kibiashara kupita katika njia hiyo muhimu ya kimataifa, huku ikitoza ada ya usafiri kama sharti la kupita.

    Hatua hiyo inajiri wakati Marekani na Iran zikiendelea na mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya kumaliza mzozo wa vita.

    Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la sekta ya meli na biashara ya baharini, Lloyd’s List, mamlaka hiyo mpya ya Ghuba ya Uajemi imeanza utaratibu unaowataka wamiliki wa meli kupata kibali cha kupita na kulipa ada kabla ya safari.

    Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamlaka hiyo imeanza kusambaza fomu kwa kampuni za meli, zikitakiwa kutoa taarifa za umiliki, bima, wafanyakazi na njia ya safari kabla ya kuruhusiwa kupita.

    Shirika la utangazaji la serikali ya Iran, Press TV, limesema Tehran imeanzisha mfumo wa kusimamia mamlaka yake katika Mlango wa Hormuz na imeanza kutuma kanuni na taratibu kwa meli kupitia barua pepe.

    Iran imekuwa ikisisitiza kuimarisha udhibiti wake katika Mlango wa Hormuz tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel mwezi Februari, hali iliyosababisha misukosuko katika masoko ya nishati duniani.

    Baada ya tangazo la kusitisha mapigano mwezi Aprili, Marekani iliongeza ulinzi wa kijeshi karibu na bandari za Iran, hatua inayohusishwa na kuendelea kwa mashinikizo katika njia hiyo muhimu ya baharini.

    Maafisa wa Iran wamekuwa wakisisitiza kuwa wanakusudia kurekebisha kanuni za usafiri katika mlango huo, ambapo Tehran ingekuwa na udhibiti mkubwa zaidi na kutoza ada za usafiri, huku mapato yakipangwa kugawanywa pia na Oman, iliyoko upande wa pili wa mlango huo.

    Mwezi Aprili, Naibu Spika wa Bunge la Iran, Hamid Reza Haji Babaei, alitangaza kuwa nchi hiyo imepokea mapato ya kwanza kutokana na ada hizo, ingawa hakutoa maelezo ya kina.

    Kabla ya hatua hiyo, Bunge la Iran lilikuwa likijadili uwezekano wa kutoza ada kwa meli zinazopita Mlango wa Hormuz, huku maafisa wakionya kuwa hali ya usafiri katika eneo hilo “haitarejea kama ilivyokuwa kabla ya vita.”

    Soma zaidi:

  7. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran asema hawatakubali shinikizo

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema Iran haitasalimu amri kwa shinikizo lolote, akisisitiza kuwa kila jitihada za kutafuta suluhisho la kidiplomasia zinapofanywa, Marekani huchagua njia ya operesheni za kijeshi zinazoleta hatari kubwa zaidi.

    Akizungumza kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Araghchi amehoji iwapo hatua hizo ni mbinu ya shinikizo la kisiasa au ni njama ya makusudi inayomsukuma Rais wa Marekani kuingia katika mgogoro mpya usio na kikomo.

    Amesema, bila kujali sababu, matokeo yake hubaki yale yale, kwamba “Wairani hawababaishwi na shinikizo.”

    Waziri huyo pia amepinga takwimu zilizotolewa na Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, kuhusu akiba ya makombora ya Iran, akizitaja kuwa si sahihi.

    Amedai kuwa uwezo wa akiba ya makombora na mifumo ya kurushia nchini Iran hauko katika kiwango cha asilimia 75 kama ilivyodaiwa kufikia Februari 28, bali ni asilimia 120.

    Kauli hiyo imekuja kufuatia mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran katika eneo la Mlango wa Hormuz usiku uliopita.

    Marekani ilisema ilifanya mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi ndani ya Iran, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi baada ya mashambulizi dhidi ya meli za Marekani katika Mlango huo muhimu wa bahari.

    Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump baadaye alidai kuwa, licha ya mapigano hayo ya kubadilishana mashambulizi, makubaliano ya kusitisha mapigano bado yalikuwa yanaendelea.

    Soma zaidi:

  8. Shirika la Kimataifa la Nishati latangaza utayari wa kuachilia akiba kubwa ya mafuta

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati, Fatih Birol, amesema shirika hilo liko tayari kuachilia sehemu zaidi ya akiba yake ya mafuta iwapo hali ya soko la dunia itaendelea kuzorota kutokana na vita vya Iran na mvutano unaoendelea katika Mlango wa Hormuz.

    Birol amesema hadi sasa shirika hilo limetumia asilimia 20 pekee ya akiba yake ya dharura ya mafuta, akisisitiza kuwa hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa ikiwa kutahitajika kudhibiti msukosuko wa bei za nishati duniani.

    Kauli hiyo inatolewa wakati bei ya mafuta ghafi aina ya Brent ikipanda hadi zaidi ya dola 101 kwa pipa, kufuatia kuzorota kwa usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya nishati duniani.

    Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati, vita kati ya Marekani, Israel na Iran tayari vimeathiri usambazaji wa gesi kimiminika duniani, huku takriban mita za ujazo bilioni 120 zikitarajiwa kupotea kati ya mwaka 2026 na 2030.

    Akizungumza katika mkutano wa Budapest LNG Summit, mchambuzi wa shirika hilo Gergely Molnar amesema mzozo huo umebadili matarajio ya soko la gesi kwa kipindi cha kati, na kwamba hali ya uhaba inaweza kuendelea kwa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa awali.

    Molnar amesema usambazaji wa gesi duniani umeshuka kwa karibu asilimia 15 kutokana na mgogoro huo, ingawa ongezeko la uwezo mpya wa uchakataji wa gesi linatarajiwa kusaidia kufidia upungufu uliotokea Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Mashambulizi ya Iran pia yameathiri asilimia 17 ya uwezo wa Qatar wa kusafirisha gesi, hali inayotishia usambazaji wa nishati kwa Ulaya na Asia kuelekea msimu wa kujaza akiba kabla ya majira ya baridi.

    Molnar ameongeza kuwa kiwango cha akiba ya gesi katika Umoja wa Ulaya kwa sasa kiko chini kwa asilimia 30 ikilinganishwa na wastani wa miaka mitano iliyopita, jambo linalomaanisha kuwa Ulaya itahitaji ziada ya mita za ujazo bilioni 10 za gesi ili kufikia kiwango chake cha uhifadhi kinacholengwa.

  9. Wizara ya Mafuta ya Iraq yakataa tuhuma za Marekani dhidi ya naibu waziri wake kuhusu kusaidia Iran kukwepa vikwazo

    Wizara ya Mafuta ya Iraq imekanusha tuhuma za Marekani dhidi ya Naibu Waziri wa Mafuta wa nchi hiyo, ambaye amewekewa vikwazo na Washington kwa madai ya kusaidia Iran.

    Marekani imekuwa ikiongeza shinikizo kwa Iraq ili ijitenge na makundi yanayoonekana kuwa karibu na Iran.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza jana kuwa imemwekea vikwazo Ali Ma'arij Bahadli, Naibu Waziri wa Mafuta wa Iraq, ikidai kuwa “alitumia vibaya nafasi yake serikalini kuelekeza mafuta ya Iraq kwa njia isiyo halali kwa manufaa ya Iran na washirika wake.”

    Marekani pia imemtuhumu kwa “kuchanganya mafuta ya Iran na ya Iraq kinyume cha sheria ili yauzwe kwa manufaa ya Iran,” kama sehemu ya mpango wa kusaidia Tehran kukwepa vikwazo vya kimataifa.

    Hata hivyo, Wizara ya Mafuta ya Iraq imekanusha madai hayo kupitia taarifa rasmi, ikisisitiza kuwa inatoa umuhimu mkubwa kwa uwazi katika kushughulikia tuhuma zozote kwa kuzingatia ushahidi na ukweli.

    Wizara hiyo imeeleza kuwa iko tayari kuchunguza suala hilo, lakini ikabainisha kuwa shughuli za usafirishaji wa mafuta ghafi, masoko, upakiaji wa meli na taratibu zinazohusiana hazikuwa chini ya mamlaka ya afisa huyo.

    Awali, Kampuni ya Masoko ya Mafuta ya Iraq ilikuwa imekanusha kuwepo kwa operesheni yoyote ya kuchanganya mafuta katika bandari au maji ya Iraq kwa lengo la kusaidia Iran.

    Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imeweka vikwazo dhidi ya biashara ya mafuta ya Iran na imekuwa ikitishia kuchukua hatua dhidi ya nchi au taasisi yoyote inayosaidia ununuzi au uuzaji wa mafuta ya Iran.

    Soma zaidi:

  10. Jeshi la majini la Iran laripoti kukamata meli ya mafuta iliyokiuka sheria

    Idara ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Iran imetangaza kupitia taarifa kuwa jeshi la majini limeikamata meli ya mafuta iliyodaiwa “kukiuka sheria” katika Bahari ya Oman.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli iliyokamatwa inajulikana kama Ocean Quay na ilikuwa “imebeba shehena ya mafuta kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

    Jeshi la Iran limesema meli hiyo “ilikuwa ikitumia mazingira ya sasa ya eneo hilo kuhujumu na kuvuruga mauzo ya mafuta pamoja na maslahi ya taifa la Iran.”

    Sambamba na taarifa hiyo, Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia limetoa video inayodaiwa kuonyesha operesheni ya kukamatwa kwa meli hiyo usiku wa manane.

  11. FAO: Bei za chakula duniani zapanda kwa mwezi wa tatu mfululizo

    Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, limetangaza kuwa bei za vyakula duniani zimeongezeka kwa mwezi wa tatu mfululizo mwezi Aprili.

    Ongezeko hilo limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei ya mafuta ya mimea kufuatia usumbufu uliosababishwa na vita vya Iran.

    Kielezo cha Bei za Chakula cha FAO, ambacho hupima mabadiliko ya bei za bidhaa mbalimbali za chakula katika masoko ya kimataifa, kiliongezeka kwa asilimia 1.6 mwezi Aprili.

    Baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28 na kuzuka kwa vita, shughuli za meli katika Mlango wa Hormuz zilianza kudhibitiwa, na licha ya kusitishwa kwa mapigano, vizuizi hivyo bado havijaondolewa.

    Mlango wa Hormuz ni njia muhimu inayopitisha asilimia 20 ya mafuta na gesi kimiminika duniani.

    Wakati huo huo, karibu theluthi moja ya biashara ya kimataifa ya mbolea za kemikali na malighafi zake hupitia katika Mlango wa Hormuz. Kufungwa kwa njia hiyo ya majini kumeongeza shinikizo katika sekta ya kilimo na uzalishaji wa chakula duniani.

    Bei ya mbolea za kemikali imeongezeka kwa asilimia 80 tangu kuanza kwa vita hivyo.

  12. Iran yaionya UAE na kuitaja kama 'kambi ya adui' na sio jirani tena

    Ali Khazrian, mwanachama wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Bunge la Iran, amesema kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, umetoa ushirikiano muhimu wa kijeshi na kiintelijensia wakati wa vita dhidi ya Iran, na kwamba kuna “tuhuma nzito kuwa ndege za UAE, baada ya kuondoa bendera zao, zilishambulia moja kwa moja ardhi ya Iran.”

    Mbunge huyo amesema kuwa “mlinganyo wa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu eneo la Kurdistan sasa pia umeihusisha UAE, na wanapaswa kutarajia wakati wowote kwamba kama ilivyo kwa kambi za adui mjini Erbil zinazolengwa, vivyo hivyo kambi za 'adui' ndani ya UAE zinaweza kulengwa.”

    Kwa mujibu wake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiitazami tena UAE kama jirani, bali kama “kambi ya adui.”

    Iran imekuwa ikilenga maeneo ya UAE pamoja na sehemu nyingine kwa mashambulizi ya droni na makombora tangu kuanza kwa vita vilivyoendelea kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita.

  13. China yazungumzia kushambuliwa kwa meli yake Hormuz

    Wizara ya Mambo ya Nje ya China imethibitisha Ijumaa kuwa meli ya mafuta iliyokuwa imewabeba raia wa China ilishambuliwa katika Mlango wa Hormuz, huku Beijing ikieleza wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa meli zilizoathiriwa na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, ameiambia mkutano na waandishi wa habari kwamba kulikuwa na raia wa China ndani ya meli hiyo, akibainisha kuwa hadi sasa hakuna taarifa za majeruhi miongoni mwa wafanyakazi wa meli hiyo.

    Shirika la habari la Xiamen la China liliripoti Alhamisi kuwa meli ya mafuta ya China ilishambuliwa karibu na Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu.

  14. Vilabu vya England vyatinga fainali zote tatu za Ulaya kwa mara ya kwanza

    Vilabu vya England vimeandika historia baada ya kufanikiwa kutinga fainali zote tatu za mashindano ya Ulaya katika msimu mmoja kwa mara ya kwanza kabisa.

    Hii imejiri baada ya Arsenal kufuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid siku ya Jumanne.

    Baadaye katika wiki hiyo hiyo, Aston Villa na Crystal Palace nazo zilifuata nyayo kwa kufuzu katika mashindano yao husika ya Ulaya, na kukamilisha historia hiyo ya kipekee kwa England.

    Aston Villa chini ya kocha Unai Emery walifuta pengo la kufungwa 1-0 katika mechi ya kwanza na kuibuka na ushindi wa jumla wa 4-1 dhidi ya Nottingham Forest, na hivyo kufuzu fainali ya Europa League watakayocheza dhidi ya Freiburg ya Ujerumani mjini Istanbul Mei 20.

    Wakati huo huo, Crystal Palace waliendeleza ubora wao baada ya ushindi wa awali wa 3-1 dhidi ya Shakhtar Donetsk, kisha wakamaliza kazi kwa ushindi wa 2-1 katika mechi ya pili iliyochezwa Selhurst Park. Sasa watakutana na Rayo Vallecano katika fainali ya Conference League Mei 27.

    Mashindano ya Conference League yalianzishwa miaka mitano iliyopita kama mashindano ya tatu kwa ukubwa barani Ulaya, baada ya Kombe la Washindi wa Mataifa kuondolewa mwaka 1999.

    Katika historia ya hivi karibuni, England ilikuwa karibu kufanikisha jambo hili msimu uliopita, lakini haikukamilika baada ya Chelsea kushinda Conference League na Tottenham kushinda Europa League, huku Arsenal ikishindwa katika nusu fainali ya ligi ya Mabingwa

    Tayari England imewahi kuwa na mafanikio makubwa Ulaya, ikiwa ni pamoja na mwaka 2019 na 2021 ambapo vilabu vyake vilicheza fainali mbalimbali, lakini msimu huu unakuwa wa kipekee zaidi kwa kufika fainali zote tatu kwa mara ya kwanza.

    Katika historia ya soka Ulaya, mataifa kama Italia na Hispania pia yamewahi kufanikiwa kuwa na timu katika fainali nyingi kwa msimu mmoja, Hispania ikifanya hivyo katika msimu wa 1985-86.

  15. Ajifungua mapacha watano baada ya miaka 12 ya kusubiri mtoto

    Mwanamke mmoja nchini Ethiopia amejifungua watoto watano mapacha katika tukio la nadra baada ya kusubiri kupata mtoto kwa miaka 12, katika Jimbo la Harari.

    Taarifa za hospitali ya Hiwot Fana, imesema Bedriya Adem, mwenye umri wa miaka 35, alijifungua watoto wa kiume wanne na wa kike mmoja, wote wakiwa wako katika hali nzuri ya afya.

    Akizungumza na BBC, Bedriya alisema yeye na mumewe wamefurahia sana “kubarikiwa watoto watano kwa pamoja” baada ya miaka mingi ya maumivu ya kihisia na kuzongwa na jamii kutokana na kuchelewa kupata mtoto.

    “Siwezi kueleza furaha yangu kwa maneno. Nilikuwa nikisubiri (mtoto) kwa maumivu makubwa hadi ndoto yangu ilipotimia,” alisema.

    Daktari mkuu wa hospitali hiyo, Dkt Mohammed Nur Abdulahi, alisema mama na watoto wanaendelea vizuri chini ya uangalizi wa madaktari. Watoto hao walizaliwa kwa njia ya upasuaji na walikuwa na uzito wa kati ya kilo 1.3 na 1.4.

    Hospitali hiyo ilisema ujauzito huo ulitungwa kawaida bila kutumia teknolojia ya upandikizaji ya IVF, jambo linalofanya tukio hilo kuwa la nadra zaidi, kwani uwezekano wa kupata mapacha (idadi hiyo) kwa njia ya asili ni mmoja kati ya milioni 55.

    Bedriya alisema awali alielezwa kuwa alikuwa na watoto wanne tumboni, lakini alishangaa kujifungua mtoto wa tano.

    “Nilikuwa nikiomba mtoto mmoja tu, lakini Mwenyezi Mungu amenipa watano,” alisema.

    Watoto hao wamepewa majina ya Naif, Ammar, Munzir, Nazira na Ansar.

  16. Watu watatu wafariki kwenye mlipuko wa volkano Indonesia, 20 hawajapatikana

    Watu watatu wamefariki dunia baada ya volkano ya Mlima Mount Dukono kulipuka katika jimbo la North Maluku nchini Indonesia, polisi wa eneo hilo wamesema leo Ijumaa. Wakati huohuo, watu wengine takribani 20 bado hawajapatikana huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

    Mamlaka za uokoaji zimesema mapema kwamba timu za uokoaji zilikuwa zikijaribu kuwahamisha wapanda milima waliokuwa wamekwama kutokana na mlipuko huo. Watu hao walinaswa baada ya mlima huo kulipuka asubuhi ya Ijumaa majira ya saa 7:40 kwa saa za eneo hilo.

    Mlima Dukono ulilipuka na kutoa wingu kubwa lililopanda hadi kilomita 10 angani, kwa mujibu wa shirika la ufuatiliaji wa volkano nchini Indonesia. Tukio hilo lilisababisha hali ya tahadhari kubwa katika maeneo ya karibu.

    Polisi wamethibitisha kuwa waliokufa ni watu watatu wakiwemo raia wawili wa kigeni na mmoja mkazi wa eneo hilo kutoka Ternate. Aidha, shirika la taifa la usimamizi wa majanga limesema watu wasiopungua watano wamejeruhiwa.

    Mamlaka za uokoaji zimeonya wananchi kuepuka shughuli ndani ya umbali wa kilomita nne kutoka kwenye eneo la mlima huo, huku zikisema kuna uwezekano wa mtiririko wa tope la volkano kutokea endapo mvua itanyesha.

    Juhudi za uokoaji bado zinaendelea katika mazingira magumu huku mamlaka zikijaribu kuwafikia watu waliokwama, wakati hofu ya ongezeko la madhara zaidi ikisalia katika eneo hilo la volkano hai.

  17. UAE yazima mashambulizi ya makombora na droni za Iran

    Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imesema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa ikikabiliana na mashambulizi ya makombora na droni kutoka Iran mapema leo Ijumaa, katika mzozo unaoendelea mashambulizi yanayotikisa usitishaji wa vita uliotangazwa kati ya Marekani na Iran.

    Tukio hilo limekuja wakati mvutano katika eneo la Mlango wa Hormuz ukiendelea kuongezeka, kufuatia mapigano ya mara kwa mara kati ya pande hizo mbili na washirika wao katika Ghuba ya Uajemi.

    Marekani imesema hakuna uharibifu uliotokea kwa meli zake za kijeshi baada ya mashambulizi ya hivi karibuni, huku Rais Donald Trump akisisitiza kuwa sitisho la vita bado linaendelea licha ya mivutano hiyo.

    Iran kwa upande wake imeilaumu Marekani kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano na kusema ilijibu mashambulizi dhidi ya maeneo yake na meli zake katika eneo la Hormuz.

    Baada ya saa kadhaa za mapigano, ripoti kutoka UAE na Iran zilisema hali katika maeneo yaliyoathirika imerejea kuwa ya kawaida, huku pande zote zikiendelea kuilaumiana kuhusu nani alikiuka makubaliano ya kusitisha vita.

  18. Meli 1,500 na mabaharia 20,000 wakwama Hormuz kutokana na vita vya Iran

    Shirika la kimataifa la masuala ya bahari la Umoja wa Mataifa (IMO) limesema takribani meli 1,500 pamoja na mabaharia zaidi ya 20,000 wamekwama katika eneo la Ghuba ya Uajemi kutokana na vikwazo vya Iran kwenye njia ya Mlango wa Hormuz.

    Katibu Mkuu wa IMO, Arsenio Dominguez, alitangaza taarifa hiyo Alhamisi akiwa nchini Panama wakati wa Mkutano wa Bahari wa Inter-American Maritime Summit.

    Mvutano huo ulianza Februari 28 baada ya mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, huku Tehran ikijibu kwa mashambulizi katika maeneo mbalimbali na kuzuia usafiri wa meli kupitia Mlango wa Hormuz, njia muhimu kwa biashara ya dunia.

    Dominguez amesema mabaharia hao ni watu wasio na hatia waliokwama kutokana na mivutano ya kisiasa isiyowahusu moja kwa moja. Marekani ilitangaza operesheni ya kusindikiza meli katika eneo hilo Jumatatu, lakini ikaifuta siku moja baadaye.

    Ripoti zinaeleza kuwa Iran kwa sasa inatafakari mapendekezo ya Marekani kuhusu namna ya kumaliza mgogoro huo na kufungua tena njia ya Hormuz kwa usafiri wa kimataifa.

  19. Tshisekedi adokeza kuongeza muhula wa tatu wa urais DRC

    Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, amesema anaweza kuwania muhula wa tatu wa urais baada ya muda wake wa sasa kumalizika mwaka 2028 ikiwa wananchi wataridhia kupitia kura ya maoni. Katiba ya nchi hiyo kwa sasa inaruhusu mihula miwili pekee ya urais.

    Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Tshisekedi alisema hajataka muhula wa tatu moja kwa moja, lakini yuko tayari kuendelea kuongoza ikiwa wananchi watamhitaji. Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa nchini humo huku upinzani ukihofia jaribio la kubadili katiba ili kuongeza muda wa utawala wake.

    Rais huyo pia amesema uchaguzi mkuu wa mwaka 2028 unaweza usifanyike kwa wakati kutokana na hali mbaya ya usalama mashariki mwa nchi. Waasi wa M23 wameendelea kudhibiti maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, yakiwemo miji muhimu ya Goma na Bukavu.

    Tshisekedi ameilaumu Rwanda kwa kuchelewesha juhudi za amani na kunufaika na rasilimali za madini kutoka DR Congo. Rwanda imeendelea kukanusha kuunga mkono waasi wa M23 licha ya madai na ushahidi kutoka mataifa mbalimbali.

    Kauli za Tshisekedi zimekuja wakati muswada wa kuruhusu kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba ukiendelea kujadiliwa bungeni. Upinzani umeonya kuwa jaribio lolote la kubadili ukomo wa mihula ya urais litakuwa “mapinduzi ya kikatiba” yenye lengo la kumweka madarakani Tshisekedi kwa muda mrefu zaidi.

  20. China yawahukumu vifo Mawaziri wake wawili wa zamani wa Ulinzi kwa rushwa

    Mahakama ya kijeshi nchini China imewahukumu kifo mawaziri wawili wa zamani wa ulinzi baada ya kupatikana na hatia ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Hukumu hiyo ilitangazwa Alhamisi kupitia vyombo vya habari vya serikali ya China.

    Mawaziri hao ni Wei Fenghe na Li Shangfu, ambao walifikishwa katika mahakama ya kijeshi na kuhukumiwa kifo huku adhabu hiyo ikisitishwa kwa miaka miwili. Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, baada ya kipindi hicho hukumu zao zitabadilishwa kuwa kifungo cha maisha bila nafasi ya msamaha au kupunguziwa adhabu.

    Mahakama ilisema viongozi hao walipokea kiasi kikubwa cha rushwa na kutumia nyadhifa zao kujinufaisha binafsi pamoja na kuwapa wengine upendeleo usio halali. Mali zote binafsi za wawili hao pia zimechukuliwa na serikali.

    Li Shangfu alikuwa Waziri wa Ulinzi kuanzia Machi 2023 kabla ya kuondolewa madarakani Oktoba mwaka huo baada ya kutoweka hadharani kwa muda mfupi. Naye Wei Fenghe alihudumu katika nafasi hiyo kuanzia 2018 hadi 2023 kabla ya kurithiwa na Li.

    Hukumu hizo zinatajwa kuwa sehemu ya kampeni kubwa ya kupambana na rushwa inayoendeshwa na Rais Xi Jinping ndani ya jeshi na serikali ya China. Hata hivyo, wakosoaji wa serikali wanasema kampeni hiyo pia hutumika kuwaondoa wapinzani wa kisiasa wa rais huyo.