Mwanasayansi huyu anataka uache kumwaga maji chooni baada ya kujisaidia

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kila unapokwenda chooni, huenda unatupa rasilimali yenye thamani kubwa bila kujua - mkojo wako.

Leo, mkojo huchukuliwa zaidi kama taka ya mwili inayopaswa kutupwa haraka. Hata hivyo, kihistoria, ulikuwa na matumizi mbalimbali, yakiwemo kusindika ngozi za wanyama, kutia rangi vitambaa na kutengeneza baruti. Mwandishi wa Kirumi Pliny Mzee hata aliwahi kupendekeza utumike kusafisha meno, ingawa hilo si jambo la kujaribu nyumbani.

Hata hivyo, siku hizi, tunaona mkojo kama majimaji ya mwili yasiyopendeza ambayo yanapaswa kutupwa haraka iwezekanavyo. Mkojo hufichwa kwenye mfumo wa maji taka hadi unapofika kwenye kituo cha kutibu maji taka, ambako huondolewa.

Matibabu hayo hutumia nishati nyingi. Hata hivyo, kadiri tunavyozidi kutambua athari za taka zetu kwa mazingira, watafiti wanatafuta njia za kubadilisha mkojo wetu kuwa kitu chenye manufaa zaidi.

Miongoni mwa wanaotafiti matumizi mapya ya mkojo ni Profesa Kai Udert kutoka Taasisi ya Shirikisho ya Uswisi ya Sayansi na Teknolojia ya Maji. Kwa sehemu kubwa ya taaluma yake, amekuwa akichunguza namna ya kuboresha mifumo ya usafi wa mazingira na kurejesha virutubisho vilivyomo kwenye mkojo kwa matumizi mengine.

Tulizungumza naye kuhusu sababu zinazomfanya aamini kuwa mkojo unaweza kuwa na manufaa makubwa zaidi kuliko tunavyofikiri.

BBC Science Focus: Unawezaje kutumia mkojo upya?

Profesa Kai Udert: Mkojo una virutubisho muhimu kwa kilimo, vikiwemo nitrojeni, potasiamu na fosforasi. Tunavipata kupitia chakula tunachokula, lakini sehemu ya virutubisho hivyo hutolewa nje ya mwili kupitia mkojo. Badala ya kuviruhusu vipotee kwenye mfumo wa maji taka, tunaweza kuvikusanya na kuvitumia kutengeneza mbolea.

Zamani, mkojo na kinyesi cha binadamu vilitumika kama mbolea katika maeneo mbalimbali duniani. Wakulima walitambua kuwa taka hizo zingeweza kusaidia mimea kukua.

Hata hivyo, kuenea kwa mifumo ya kisasa ya maji taka kulifanya tuanze kuzingatia zaidi kuondoa taka hizo kwenye makazi ya watu kuliko kurejesha virutubisho vilivyomo. Leo, watafiti wanachunguza namna ya kubadilisha mtazamo huo.

Mkojo pia umefanyiwa utafiti kwa matumizi mengine, yakiwemo uzalishaji wa umeme, utengenezaji wa matofali na urejeshaji wa baadhi ya kemikali zenye manufaa.

Takribani miaka 170 iliyopita, tulianza kujenga mifumo mikubwa ya maji taka. Mwanzoni, lengo lilikuwa kuboresha mwonekano wa mazingira na usafi. Tulitaka tu kuondoa kinyesi na mkojo kwa kuviosha na maji bila kufikiria zaidi kuhusu matumizi yake. Tulisahau kwamba taka hizo zingeweza kutumika kama mbolea.

Pia, kumekuwa na tafiti kuhusu kutengeneza matofali au kuzalisha umeme kwa kutumia mkojo. Hapo awali, tulikuwa pia tukitoa homoni na kutengeneza dawa kwa kutumia mkojo wa binadamu, kabla ya maendeleo makubwa ya teknolojia ya kisasa ya kibayoteknolojia. Kwa hiyo, mkojo una matumizi mengi yanayowezekana.

SF: Je, watu wanaunga mkono wazo la kutumia mkojo wao upya?

KU:

Kwa kweli, watu wengi wanaunga mkono wazo la kurejesha mkojo katika matumizi, lakini wanataka kuhakikisha kuwa mbolea inayozalishwa ni salama. Wasiwasi wao ni pamoja na vimelea vya magonjwa, mabaki ya dawa na harufu.

Mkojo unaweza kuwa na vijidudu, hivyo unahitaji kutibiwa kabla ya kutumiwa. Baadhi ya mbinu za uchakataji huhusisha joto ili kupunguza au kuua vimelea vya magonjwa. Hata hivyo, usalama hutegemea mchakato mzima wa uchakataji, si joto pekee.

SF: Je, mbolea inayotokana na mkojo inaweza kuboresha mazingira?

KU: Tuna tatizo kubwa la virutubisho kupita kiasi duniani. Sote tunazungumzia hewa ya ukaa na mabadiliko ya tabianchi, lakini tunapaswa pia kuzungumzia jinsi tunavyozidisha kiasi cha nitrojeni na fosforasi katika bahari.

Wakati mifumo yetu ya sasa ya maji taka ilipoanzishwa, mwanzoni haikutibu taka hizo. Ilizipeleka tu sehemu nyingine na kuzimwaga kwenye mazingira ya asili. Watu walidhani kwamba mazingira yanayopokea taka hizo, kama vile mito, maziwa na bahari, yalikuwa na uwezo wa kutosha wa kuhimili uchafuzi huo.

Hilo halikuwa kweli. Kwa muda mfupi, mito na maziwa hayo yakaanza kuchafuliwa.

Kwa muda mrefu, tumekuwa tukijitahidi kupunguza uchafuzi huu kwa kujenga vituo vya kutibu maji taka na kuondoa mabaki ya viumbe hai, pamoja na nitrojeni na fosforasi.

Tatizo ni kwamba virutubisho hivyo hufanya kazi kama mbolea kwa mwani katika bahari, mito na maziwa. Mwani huo haupaswi kukua kwa wingi katika mazingira hayo. Hili ni tatizo kubwa kwa sababu mwani unapokufa na kutua chini ya maji, viumbe vinavyouoza hutumia oksijeni, na hivyo kupunguza oksijeni inayopatikana kwa samaki na wanyama wengine wa majini.

Kwa hiyo, kwa kurejesha nitrojeni na fosforasi kutoka kwenye maji taka, tayari tunasaidia kulinda mazingira.

Pia kuna suala la mabaki ya dawa. Takribani theluthi mbili ya viambato hai vilivyomo katika dawa hutolewa nje ya mwili kupitia mkojo. Hivi ni kemikali zenye nguvu. Kwa mfano, tunajua kwamba homoni za kutengenezwa zinaweza kuathiri samaki. Baadhi ya nchi, kama Uswisi, tayari zimeanza kuondoa mabaki ya dawa kwenye maji taka.

Kwa kutenganisha mkojo na maji taka, tunaweza kuzuia mabaki hayo ya dawa yasiingie kabisa katika mazingira ya majini.

SF: Je, hii ni njia bora kuliko mbinu zinazotumika sasa kutengeneza mbolea?

KU: Kwa sasa, tunapata nitrojeni kutoka kwenye hewa ya angahewa kupitia mchakato unaotumia nishati nyingi. Fosforasi huchimbwa ardhini. Kuna makadirio kuhusu muda ambao rasilimali hizi zitaendelea kupatikana, lakini tatizo si wingi wake pekee. Pia, tunapaswa kuzingatia vitu vingine vinavyopatikana katika madini hayo, kama vile metali ya kadimiamu, ambayo hatutaki isambazwe kwenye mashamba yetu.

Pia, tunategemea nchi za nje. Kwa mfano, Ulaya haizalishi fosforasi yake yenyewe.

Minyororo ya uzalishaji na usambazaji wa mbolea za kisasa tayari imeimarika, hivyo kwa sasa mbolea hizo ni nafuu zaidi kuliko ile inayotokana na mkojo uliorejeshwa katika matumizi.

Lakini fikiria teknolojia ya nishati ya jua. Miaka 10, 20 au 30 iliyopita, ilikuwa ghali sana. Sasa imekuwa nafuu zaidi. Nadhani hali hiyo hiyo itatokea pia katika teknolojia ya kutibu mkojo.

SF: Ni changamoto zipi kubwa zinazokabili matumizi ya mkojo katika kutengeneza mbolea?

KU: Maji taka ni mchanganyiko wa aina nyingi za taka. Virutubisho vyenye thamani tunavyovitoa kupitia mkojo na, kwa kiasi fulani, kinyesi, huchanganyika na uchafu mwingi. Hali hii hufanya iwe vigumu kutenganisha na kupata virutubisho hivyo.

Hii ndiyo hasa hatua ya mwanzo ya mjadala mzima. Badala ya kuchanganya mkojo na maji taka mengine, tunapaswa kuutenganisha mapema iwezekanavyo, karibu na mahali unapotoka, ili tuweze kupata virutubisho na kutengeneza mbolea.

Tulianza kuangalia mifumo ya matumizi ya choo, yaani teknolojia ambazo watu hutumia moja kwa moja katika shughuli zao za usafi.

Kimsingi, tunahitaji vyoo maalumu vinavyotenganisha mkojo na kinyesi au maji mengine ya chooni tangu mwanzo. Kuna vyoo vinavyotenganisha mkojo bila kutumia maji ya kuvuta, pamoja na vingine vinavyotumia maji na kutoa kiwango kilekile cha faraja ambacho tumezoea.

Nadhani mojawapo ya changamoto kubwa ni kwamba usimamizi wa maji taka huanzia nyumbani. Hii itakuwa njia mpya kabisa ya kusimamia usafi wa mazingira. Ghafla, wasanifu wa majengo watalazimika kuanza kufikiria: "Tutaweka wapi mfumo wa kurejesha virutubisho kutoka kwenye mkojo au matanki ya kuuhifadhi?"

Katika majengo mapya, tunaweza kufunga mabomba ya ziada ya kutoa na kukusanya mkojo.

Hata hivyo, tunapokumbuka wakati mifumo ya sasa ya usafi ilipoanzishwa, miji kama London tayari ilikuwa mikubwa na yenye majengo mengi. Hali hiyo pia ilikuwa hivyo kwa Paris. Lakini bado iliwezekana kuanzisha mifumo ya vyoo vinavyotumia maji kuvuta taka.

Kwa hiyo, nadhani mabadiliko hayo yalikuwa makubwa zaidi kuliko yale tunayohitaji kufanya leo.