Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini aina hizi 11 za saratani zinaangamiza sana vijana?
Aina 11 za ugonjwa wa saratani zimeanza kuwa kuwaathiri vijana wengi nchini Uingereza.
Chanzo cha kuongezeka kwa ugonjwa wa saratani bado hakijulikani.
Ila kulingana na utafiti, watu wengi wanazidi kunenepa kupita kiasi, ila hili si hoja pekee.
Wanasayansi kutoka shirika la utafiti wa saratani kutoka taasisi ya Imperial College London, wanasema saratani bado ni adimu miongoni mwa vijana na watu wengi wanaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo iwapo wataishi maisha yenye afya.
Kwa nini saratani inaongezeka miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 20, 30 na 40? ni swali ambalo wanasayansi wamekuwa wakilifanyia utafiti kwa miaka mingi.
Bradley Coombs kutoka eneo la Portsmouth alikuwa na umri wa miaka 23 tu alipofariki kutokana na saratani ya utumbo.
Kulingana na mama yake, Caroline Mausdale, licha ya kuwa mwanawe alikuwa na dalili nyingi za saratani ya utumbo, madaktari walimwona kuwa bado mchanga sana kuweza kuwa na ugonjwa huo.
"Alikuwa kijana mwenye afya nzuri akiwa karibu kusaini mkataba wa soka wa kiwango cha chini kitaalamu,hakukuwa na hatari yoyote"
Hata hivyo, baada ya mwaka wake wa kwanza chuoni, alianza kupungua uzito bila sababu na kupata maumivu ya tumbo. Baadaye, alianza kuharisha na damu ilionekana akienda chooni.
Ilichukua miezi 18 kugundua ugonjwa huo. Alipofanyiwa uchunguzi wa 'colonoscopy', uchunguzi wa video wa utumbo, uvimbe ulikuwa tayari umekua mkubwa kiasi kwamba ulizuia kamera kuingia ndani ya utumbo.
Upasuaji na tiba ya kemotherapi hazikuweza kuzuia ukuaji wa uvimbe huo, na Bradley akafariki dunia.
Mara nyingi ni vigumu kuua kwanini baadhi ya watu hupata saratani.
Kundi la wanasayansi limechunguza mwenendo wa saratani na mtindo wa Maisha ya watu ili kupata uhusiano kati vitu hivyo na saratani.
Wanasayansi hao waligundua kwamba pamoja na saratani ya utumbo, saratani za tezi ya shingo , multiple myeloma, ini, figo, kibofu cha nyongo, kongosho, endometrium, kinywa, matiti na ovari zinaongezeka.
Saratani za utumbo na matiti ndizo zinazojitokeza zaidi kwa vijana, zikiwa na jumla ya kesi 11,500 kwa mwaka, wakati saratani za kongosho na kibofu cha nyongo ni chache zaidi.
Ni saratani ya utumbo na ovari pekee ambazo zimeonekana kuongezeka hasa kwa vijana, ilhali aina nyingine tisa za saratani pia zimeongezeka kwa watu wazee.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Saratani na Chuo Kikuu cha Imperial College London pia ulichambua tabia zinazochochea kuongezeka kwa hatari ya kupata saratani.
Utafiti huo ulionyesha kwamba viashiria kama uvutaji sigara, unywaji wa pombe, kutofanya mazoezi, ulaji wa nyama iliyosindikwa, pamoja na ulaji wa vyakula visivyo na nyuzinyuzi, matumizi yake yamepungua.
Ingawa tabia hizi zote zina mchango katika hatari ya kupata saratani, hazitoshi kueleza kikamilifu kwa nini ugonjwa huu unaendelea kuongezeka.
Kulingana na ripoti hiyo, takwimu pekee zinazoendana na ongezeko la saratani ni kiwango cha uzito kupita kiasi na unene uliopitiliza.
Tishu za mafuta zilizozidi mwilini hubadilisha homoni za mwili, kama vile insulini, na inaaminika kuwa zinaweza kuongeza hatari ya kupata saratani.
Hata hivyo, hili pia si jibu kamili.
Kwa mfano, kulingana na makadirio ya watafiti, kati ya visa 100 vipya vya saratani ya utumbo, 20 vinaweza kusababishwa na uzito kupita kiasi, lakini sababu za visa 80 zilizobaki bado hazijulikani.
Watafiti wanasema kuwa ni muhimu kuzuia aina zote za saratani, si tu visa vinavyosababisha ugonwa huo. Kulingana na makadirio, karibu asilimia 40 ya saratani zinaweza kuzuilika kwa kubadilisha mitindo ya maisha yenye madhara, kama vile kutovuta sigara.
Watafiti pia walisema ni muhimu kukumbuka kwamba ingawa saratani inaongezeka miongoni mwa vijana, bado idadi yake ni ndogo zaidi ikilinganishwa na wazee.
Vinywaji vyenye sukari, uvimbe wa mwili uchafuzi wa hewa, bakteria wa utumbo, na dawa za kuua magugu pia zimeelezwa kama sababu zinazowezekana kuchangia ongezeko la saratani.