Ufumbuzi mpya wa kukabiliana na upara unamaanisha nini kwa wanawake?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Bado nakumbuka vizuri wakati nywele zangu zilipoanza kunyonyoka.

Nilikuwa nimeinama juu ya beseni nikiosha nywele zangu katika chumba cha hoteli Jumamosi moja jioni, nikiwa tayari kusherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwa rafiki yangu. Siku 17 kabla ya hapo, nilikuwa nimefanyiwa matibabu ya kwanza kati ya sita ya tiba ya saratani ya matiti, lakini siku zilikuwa zimepita bila dalili yoyote ya kupoteza nywele.

Nilijiaminisha kuwa naweza kuwa mmoja wa waliobahatika.

Lakini nilipokuwa nikipitisha maji juu ya kichwa changu ghafla niliona nyele zangu ndefu za kahawia zinapukutika. Si kuwa na la kufanya ili kuizuia hilo.

Nilijiambia, "Ee Mungu wangu," kwa sababu ya uaminifu wangu kwako sikutarajia itokee hivi.

Wakati wa matibabu yangu ya saratani, nilivalia kofia ili kusaidia kuhifadhi nywele zangu japo nilifahamishwa hatua haimsaidii kila mtu.

Mtu anaweza kushisi pengine naltilia chumvi, lakini kwangu, kupoteza nywele ilikuwa ngumu zaidi kuliko kupoteza titi kupitia upasuaji wa mastectomy. Kwa nini? Kwa sababu bila nywele zangu, nilihisi kutojitambua tena. Kabla zianze kupukutika, sikuwa nimegundua ni kwa kiasi gani nywele zangu zilikuwa sehemu ya utambulisho wangu.

Wanasayansi nchini Japan wanaamini kuwa wanakaribia kubadilisha hali ya upotezaji wa nywele kwa mamilioni ya watu.

Katika kile ambacho watafiti wanakiita "mafanikio makubwa ya kisayansi," timu inayoongozwa na Profesa Takashi Tsuji inasema imefanikiwa kuunda mzunguko kamili wa ukuaji wa nywele kwenye panya, kumaanisha kuwa nywele zinaweza kukua, kupukutika na kukua tena kama kawaida. Ingawa nywele zilizopandikizwa tayari zina uwezo wa kukua, kutengeneza upya vinyweleo ambavyo vinafanya kazi sawa na vinyweleo vya asili ndani ya mwili—kukua, kuanguka, na kumea tena na tena baada ya muda—imekuwa changamoto kubwa zaidi.

Kwa wanawake wanaokabiliwa na hali ya kupoteza nywele, iwe kwa sababu ya matibabu ya saratani, alopecia areata, au kuzeeka, mafanikio kama haya hufungua mlango kwa uwezekano ambao hapo awali ulionekana hauwezekani: uwezekano wa kudhibiti upotezaji wa nywele na kurejesha ukuaji wake.

Uctafiti unaonyesha kwamba tatizo hili huathiri mamilioni ya watu kote duniani , na kwamba takriban theluthi moja ya wanawake wanaweza kupoteza nywele wakati fulani katika maisha yao. Lakini kwa nini athari ya kisaikolojia ya kupoteza nywele mara nyingi haipewi umuhimu mkubwa? Jinsi tunavyopokea hali hii inamaanisha nini kuhusu utambulisho wetu, hisia za kudhibiti maisha yetu, na jinsi tunavyojiona?

Hali ilivyokua zamani

Katika Misri ya kale, mafarao na wanawake wakuu walivaa wigi zilizosokotwa na kupambwa ili kuonyesha uwezo na hadhi. Katika Zama za Kati, nywele ndefu kwa wanawake zilihusishwa na hulka na wema. Wanaume wa karne ya kumi na saba walivaa wigi—nywele ndefu, nene, zilizopinda—ili kuashiria utajiri na hadhi ya juu katika jamii. Kufikia miaka ya 1920, nywele fupi, za mtindo wa bob zilikuwa ishara ya uhuru wa wanawake na uasi.

Mwanasaikolojia Silvia Carasso anasema, "Nywele huchangia kuimarisha utambulisho wetu. Ni alama ya kibayolojia, kisaikolojia na kijamii ambayo inahusishwa na hatua tofauti za maisha yetu."

Bila shaka, nywele ni kitu cha kwanza tunachoona wakati tunapotangamana na wenzetu. Carasso anaongeza: "Kupitia hilo, jinsia, rangi, au uhusiano wa kidini mara nyingi unaweza kukadiriwa kikamilifu. Inahusishwa kwa karibu sana na utambulisho kiasi kwamba ni jambo muhimu katika jinsi tunavyowapanga watu katika kategoria."

Niliwahoji wanawake kadhaa kuhusu uhusiano wao na hisia zao kwa podcast ninayowasilisha kwa ushirikiano na shirika la usaidizi la Future Dreams liitwalo "Kisha Ikaja Saratani ya Matiti." Wazo moja ambalo linijia mara kwa mara na kuhusu wanawake niliozungumza nao lilikuwa: sio juu ya ubatili hata kidogo.

Nikki Elkington, mfanyakazi wa saluni, anasema alikuwa amedhamiria kutopoteza nywele zake wakati akifanyiwa matibabu yasaratani.

Changamoto kubwa inayowakabili wanawake wanaougua saratani ni hali ya kupoteza udhibiti wa karibu kila kitu, iwe ni utambuzi, matibabu, au madhara. Kwa hiyo, kwa baadhi ya wanawake, uamuzi wa kunyoa nywele zao kabla hazijaanguka huwa njia ya kurejesha udhibiti wa maisha yao kwa kiwango fulani.

Kilichonishangaza wakati wa matibabu yangu ya saratani ni jinsi hofu yangu ya kupotezaji wa nywele ilivyopuuzwa.

Baadhi yao wangesema, "Kwa nini unahangaikia nywele zako? Shukuru Mungu uko hai." Na ni swali halali. Ndio, nilikuwa na bahati ya kuokoka. Lakini kunusurika ugonjwa na kuhuzunika kwa kupoteza sehemu fulani ya utambulisho wako si mambo ya pekee.

Kama Silvia Carasso aliniambia, kwa wengi wetu, kupoteza nywele "kunaashiria kwamba sisi ni wagonjwa."

Wanasayansi hawajapata ufumbuzi

Wanasayansi bado wako mbioni kutafuta majibu ya biolojia inayozunguka hali ya kupoteza nywele.

Kulingana na Claire Higgins, profesa wa uhandisi wa tishu katika Chuo cha Imperial London, tafiti kuhusu upotezaji wa nywele zimeteseka kwa miaka mingi kutokana na ukosefu wa ufadhili, haswa linapokuja suala la wanawake.

Anasema: "Kipengele kinachohusiana na wanawake bado hakijazingatiwa kikamilifu."

Anaeleza kuwa sehemu kubwa ya utafiti huo imezingatia upotezaji wa nywele kwa wanaume, kwa sababu wanaume wana uwezekano mkubwa wa kupandikizwa nywele, jambo ambalo limefanya sampuli za kichwa kuwa rahisi kupatikana kwa wanasayansi.

Anaongeza: "Wanaume na wanawake mara nyingi huhudumiwa kwa njia sawa kwa sababu watu wanadhani tatizo ni sawa, lakini sidhani kama inapaswa kuwa hivyo."

Hii inazingatia uchunguzi wa kina wa vinasaba juu ya upara wa muundo wa kiume, ambao kwa kawaida una sifa ya kupungua kwa nywele kunyokwa kwenye utosi wa kichwa. Tafiti hizi, zinazojulikana kama tafiti za muungano wa jenomu kote, zimebainisha idadi ya jeni zinazohusiana na hali hii. Walakini, zote zimefanywa kwa wanaume.

Hivi majuzi, watafiti nchini Ujerumani walifanya tafiti kuhusu jeni zinazohusiana na upara kwa wanawake, ambao kwa kawaida huonekana kama nywele kuwa hafifu au kupoteza nywele katika sehemu ya juu ya kichwa. Wanasayansi walitarajia kupata jeni zinazohusiana na upara kwa wanaume na wanawake.

Lakini, kama Claire Higgins anasema, "hilo halikufanyika."

Matokeo yalionyesha kuwa upara kwa wanaume na wanawake unaweza kutokana na sababu tofauti, ingawa wanasayansi bado hawajang'amuakabisa sababu hizi ni nini.

Higgins anaongeza: "Tunajua kwamba baadhi ya seli hupotea kutoka kwenye folikali ya nywele, lakini hatujui kama zinakufa au kuhamia mahali pengine. Bado hatujajiridhisha kikamilifu kuhusu kile kinachosababisha nywele kunyonyoka."

Matumaini mapya ya kutibu upara

Hii ndiyo sababu utafiti wa Profesa Tsuji huko Japan ni muhimu sana. Yeye na timu yake wanaamini wamepata kipande kilichokosekana cha fumbo.

Kwa muda mrefu, wanasayansi waliamini kuwa kuna aina mbili kuu za seli zinazohusika na ukuaji wa nywele: seli za shina za epithelial, ambazo huunda folikali ya nywele mahali pa kwanza, na seli za papilla za ngozi, ambazo hutuma ishara kwa nywele kukua.

Seli hizi haziwezi kukuza nywele kwenye maabara; hufanya hivyo tu wakati wa kuingizwa kwenye ngozi na kuunganishwa na tishu zilizo chini.

Lakini Tsuji anasema utafiti wake ulibainisha "aina mpya ya seli ya tatu," iitwayo seli ya kukuza upya folikali ya nywele.

Kiini hiki kipya kinaweza kuwasogeza wanasayansi hatua moja karibu na uwezekano wa kukuza nywele katika maabara.

Tsuji anasema, "Utafiti wetu ulibainisha seli ambayo inasaidia muendelezo, ukuaji na kuzaliwa upya kwa follikali ya nywele."

Tsuji anaelezea matokeo haya kama "mafanikio makubwa ya kisayansi" ambayo yanaweza kuimarisha pakubwa matibabu ya alopecia areata.