Mohammad Bagher Ghalibaf: Mwanajeshi na mwanasiasa wa Iran atakayeongoza mazungumzo ya amani na Marekani

Mohammad Bagher Ghalibaf

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, anatarajiwa kuongoza mazungumzo na Marekani, yatakayoanza Jumamosi (11 Aprili).

Anasafiri kuelekea Islamabad, Pakistan kwa ajili ya mazungumzo hayo, huku Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance akitarajiwa kuongoza upande wa Marekani, kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Saeed Khatibzadeh aliyelikiambia kipindi cha Today cha BBC siku ya Alhamisi.

Mwishoni mwa Machi, shirika la Reuters liliripoti kwamba pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi, Ghalibaf aliondolewa kwenye orodha ya Israel ya watu waliolengwa kuuawa.

"Waisraeli walikuwa na taarifa za mahali walipo na walitaka kuwaondoa, tuliiambia Marekani kwamba kama nao wataondolewa basi hakutakuwa na mtu wa kuzungumza naye, hivyo Marekani iliwaomba Waisraeli waache," chanzo kimoja kutoka Pakistan kiliiambia Reuters.

Pakistan imeibuka kama mpatanishi mkuu kati ya Iran na Marekani.

Baada ya kushindwa mara kadhaa katika kugombea urais hapo awali, Ghalibaf sasa amepewa jukumu nyeti la kufanya mazungumzo na Marekani.

Kutokana na kuuawa kwa viongozi wengi waandamizi katika mashambulizi ya Marekani na Israel, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 64 anaweza kuwa na nafasi muhimu zaidi katika siku zijazo, hasa kutokana na uhusiano wake wa karibu na jeshi la Iran, uzoefu wake katika matawi mbalimbali ya serikali, na taswira yake kama msimamo mkali mwenye mtazamo wa kiutendaji.

m

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha,

"Ninajivunia kutumia fimbo"

Mohammad Bagher Ghalibaf alizaliwa katika familia ya kidini ya tabaka la wafanyakazi katika mji wa kaskazini-mashariki wa Torghabeh, kwa mujibu wa Al-Alam, kituo cha televisheni cha Kiarabu kinachomilikiwa na shirika la utangazaji la serikali ya Iran. Mji wake wa nyumbani uko karibu na Mashhad, ambako baadhi ya viongozi mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu waliwahi kuishi.

Akiwa na umri wa miaka 16, alianza kuhudhuria madarasa ya wanazuoni wa mapinduzi, wakiwemo Ali Khamenei, ambaye baadaye alikuja kuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, katika misikiti mikubwa ya Mashhad.

Muda mfupi baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, Ghalibaf alipigana katika vita dhidi ya Iraq na alijiunga na Islamic Revolutionary Guard Corps akiwa na umri wa miaka 20. Miaka miwili baadaye, aliteuliwa kuwa kamanda wa mojawapo ya vikosi vyake vya mapigano, nafasi aliyoshikilia hadi vita vilipomalizika mwaka 1988.

Mohammad Bagher Ghalibaf

Chanzo cha picha, Pacific Press/LightRocket via Getty Images

Maelezo ya picha,
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mohammad Bagher Ghalibaf alifunga ndoa mwaka huohuo aliokuwa kamanda katika Islamic Revolutionary Guard Corps, na sherehe hiyo ilisimamiwa na Kiongozi Mkuu wa wakati huo Ruhollah Khomeini, kwa mujibu wa Al-Alam. Wawili hao wana watoto watatu.

Ghalibaf aliendelea kupanda vyeo baada ya vita na mwaka 1997 akawa kamanda wa Kikosi cha Anga cha IRGC.

Mwezi Julai 1999, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitikiswa na maandamano ya wanafunzi, yaliyochochewa na kufungwa kwa gazeti la mageuzi. Harakati hiyo ilikandamizwa kwa nguvu, na kusababisha vifo kadhaa, na inaaminika kwamba yeye binafsi alihusika katika ukandamizaji huo.

"Sasa kuna picha yangu nikiwa juu ya pikipiki ya cc 1000 nikiwa nimeshika fimbo… Popote panapohitajika kwenda mitaani na kutumia fimbo, sisi ni miongoni mwa wanaofanya hivyo. Na tunajivunia hilo," anasikika akisema katika faili ya sauti iliyovuja.

Baada ya maandamano hayo, makamanda 24 wa IRGC waliandika barua kali kwa Mohammad Khatami, ambaye alikuwa rais wa Iran wakati huo, wakitishia kuingilia kati kwa jeshi hilo. Ghalibaf alisema alikuwa mmoja wa makamanda wawili walioandaa barua hiyo na kukusanya saini.

Watu wengi wanaona barua hiyo kama ishara wazi kwamba Islamic Revolutionary Guard Corps ina ushawishi mkubwa katika siasa, na ushawishi huo umeendelea kuongezeka.

Kutoka kuwa mkuu wa polisi hadi kuwa meya wa Tehran

Mwaka mmoja baada ya maandamano ya wanafunzi, Mohammad Bagher Ghalibaf aliteuliwa kuwa mkuu wa polisi akiwa na umri wa miaka 39.

Katika kipindi chake cha miaka mitano, alianzisha namba ya dharura ya kitaifa ya polisi na kurahisisha mchakato wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya maafisa wa polisi.

Pia aliona kuipatia polisi magari ya kigeni kama moja ya mafanikio yake makubwa, ingawa wakosoaji wanasema gharama yake ilikuwa kubwa sana.

Mwaka 2005, Ghalibaf alijiuzulu nafasi hiyo na kugombea urais. Baada ya kushindwa, alichaguliwa na baraza la jiji kuwa meya wa Tehran. Alikaa katika nafasi hiyo kwa miaka 12 na hadi sasa anashikilia rekodi ya kuwa meya aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika mji mkuu huo.

Anasifiwa kwa kupanua mfumo wa metro na kuboresha miundombinu ya usafiri kama vile Barabara ya Sadr katika mji huo wenye msongamano mkubwa wa magari.

Mohammad Bagher Ghalibaf and Mohammad Khatami

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Mohammad Bagher Ghalibaf and Mohammad Khatami

Hata hivyo, sifa ya Mohammad Bagher Ghalibaf ilipata pigo baada ya kashfa ya mwaka 2016 ya "mali za bei ya chini sana", ambapo baraza la jiji lilituhumiwa kuuza mamia ya mali kwa maafisa na vyombo vya usalama kwa punguzo kubwa, hadi asilimia 50 chini ya bei ya soko.

Miezi michache kabla ya kuondoka madarakani, jengo la ghorofa 17 la Plasco building, moja ya majengo ya mwanzo marefu nchini Iran, lilianguka baada ya moto, na kuua takribani maafisa zimamoto 20. Ajali hiyo ilionesha uzembe wa kimfumo ndani ya serikali ya jiji chini ya uongozi wake.

Hata hivyo, kashfa hizo hazikusababisha kuondolewa kwake madarakani wala kufunguliwa mashtaka ya kumng'oa, na aliweza kuvuka changamoto zote mbili.

Mwaka 2020, alishinda kiti katika uchaguzi wa bunge na kuwa spika.

Majaribio yaliyoshindikana ya kugombea urais na uspika

Mohammad Bagher Ghalibaf daima amekuwa na nia ya kuwa rais, lakini majaribio yake manne, mwaka 2005, 2013, 2017 na 2024 yote hayakufanikiwa.

Katika jaribio lake la kwanza, mwanajeshi huyo wa zamani wa Islamic Revolutionary Guard Corps alisisitiza historia yake ya kijeshi, lakini baadaye alibadilisha mkakati kwa kuangazia sifa zake kama mwenye shahada ya uzamivu (PhD) katika jiografia ya kisiasa na pia rubani aliyefunzwa. Amejijengea pia taswira ya kuwa "meneja wa jihadi", akijivunia ufanisi wa kijeshi na kujitolea.

Ingawa kwa muda mrefu amechukuliwa kuwa mpinzani wa wanamageuzi, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na dalili kwamba ameanza kuwa na tofauti na baadhi ya makundi ya kihafidhina.

Katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2024, kundi kubwa la wahafidhina wenye msimamo mkali lilipinga kugombea kwake na lilijaribu kumshawishi ajiondoe katika kinyang'anyiro hicho.

Mohammad Bagher Ghalibaf

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha,

Mohammad Bagher Ghalibaf alihusishwa tena na kashfa ya ufisadi mwaka 2022. Picha za familia yake zikibeba kiasi kikubwa cha bidhaa za watoto, ikiwemo toroli ya mtoto, katika uwanja wa ndege baada ya safari kwenda Uturuki zilisambaa, na kusababisha hasira kubwa miongoni mwa watu.

Wakosoaji wake walimshutumu kwa "unafiki, udanganyifu na kujifanya mcha Mungu", lakini yeye aliwaambia wafuasi wake kuwa suala hilo lilikuwa la kisiasa na jaribio la kumwondoa katika siasa za Iran.

Inaonekana Ghalibaf hakuathiriwa sana na kashfa hiyo na alichaguliwa tena kuwa spika mwaka 2024.

Huku Iran ikiwa katika kipindi muhimu, nafasi yake kisiasa inaweza kuongezeka zaidi kutokana na uwezo wake wa kusimamia mwendelezo wa vita na kuratibu kati ya makamanda wa juu wa kijeshi na viongozi wa mihimili mitatu ya dola.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi