Rais Faye wa Senegal azindua chama kipya cha kisiasa

Chanzo cha picha, Bassirou Diomaye Faye/ X
Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, amezindua chama kipya cha kisiasa, hatua inayozidisha mgawanyiko unaoonekana wazi kati yake na mshirika wake wa zamani na aliyekuwa Waziri Mkuu, Ousmane Sonko.
Chama hicho kipya, Kiiray (Chama cha Wazalendo wa Jamhuri), kilizinduliwa katika mji mkuu, Dakar, siku ya Jumamosi na muungano unaomuunga mkono Bw. Faye.
Mamia ya wafuasi walihudhuria hafla hiyo ya uzinduzi.
Wakati huo huo, Bw. Sonko alikuwa akihutubia wafuasi wake umbali wa kilomita 100 (maili 62) katika mji wa Bambey, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kitaifa inayolenga kutafuta uungwaji mkono kwa chama chake cha Pastef.
Mapema mwezi huu, Bw. Faye alimteua mshauri mkuu Aminata Touré kuongoza kikosi kazi cha kuanzisha vuguvugu hilo jipya la kisiasa.
Hapo awali, Bw. Faye alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha Pastef cha Bw. Sonko, chama kilichoingia madarakani mwaka 2024 baada ya miaka mingi ya kuwa upinzani.
Hata hivyo, uhusiano kati ya wawili hao umezorota katika miezi ya hivi karibuni, hali iliyofikia kilele wakati Bw. Faye alipomwondoa Bw. Sonko katika wadhifa wa Waziri Mkuu mwezi Mei.
Uzinduzi wa chama hicho kipya unafanyika huku kukiwa na wimbi la wanachama kuhama chama cha Pastef na kujiunga na kambi ya rais, wakiwemo viongozi kadhaa wa ngazi ya juu wa chama hicho.
Pastef imejitahidi kudhibiti hali ya wanachama kuhama.
Bw. Sonko, ambaye kwa sasa ni Spika wa Bunge la Kitaifa, amekuwa mstari wa mbele kutetea marekebisho ya katiba yatakayozuia rais aliyeko madarakani kuongoza chama cha kisiasa.
Bunge liliidhinisha mabadiliko hayo yaliyopendekezwa, lakini Bw. Faye ameamua kuyafikisha kwa wananchi kupitia kura ya maoni ya kitaifa.
Tarehe ya kupiga kura hiyo bado haijatangazwa.
Mgogoro huo wa kisiasa unaendelea huku Senegal ikikabiliwa na changamoto za kiuchumi kufuatia kufichuliwa kuwa deni la serikali chini ya utawala uliopita lilikuwa limeripotiwa kwa kiwango cha chini kuliko uhalisia.
Faye na Bw. Sonko, pia wanatazamia uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika mwaka 2027, ambao unatarajiwa kuwa kipimo kikubwa cha kwanza cha uungwaji mkono wao kisiasa tangu ushirikiano wao ulipovunjika.
Mgawanyiko kati ya wawili hao ni hatua muhimu ya mabadiliko katika siasa za Senegal.
Wakiwa washirika wa karibu hapo awali waliofanya kampeni pamoja kwa ahadi ya kufanya marekebisho makubwa, sasa wanaongoza kambi pinzani za kisiasa zinazoshindania mustakabali wa nchi hiyo.





















