Malaria bila dalili, tishio kwa juhudi za kuuangamiza ugonjwa huu

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sarafina Robi
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Je, wajua kwamba unaweza kuwa na Malaria bila dalili kudhihirika?
Ndiyo hali ya watu wengi , huku ugonjwa huu ukiongezeka katika baadhi ya mataifa ya bara Afrika, haswa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchumi iliyotolewa na afisi ya kitaifa ya takwimu ya Kenya KBS ya mwaka wa 2026, visa vya malaria nchini Kenya vimeongezeka mara nne tangu mwaka jana, ikiwa ni visa million 3.8 katika mwaka wa 2024 hadi kufikia million 14.3 mwaka wa 2025.
Haya yanajiri huku shirika la Afya Duniani WHO lisema kwamba takriban nchi 37 zilirekodi idadi ya visa chini ya 1000 mwaka wa 2024 katika maadhimisho ya siku ya Malaria mwaka huu.
Profesa Sam Kinyanjui ni mkuu wa mafunzo ya utafiti katika kituo cha utafiti cha KEMRI-Wellcome nchini Kenya, ambapo utafiti wake unaelezea jinsi mwili unavyojikinga dhidi ya maambukizi ya Malaria katika juhudi za kutafuta chanjo ya malaria, kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Anaelezea kuwa unaweza kuwa na dalili za Malaria ila usiwe na Malaria, ila pia unaweza kuwa na viini vya Malaria ila usionyeshe dalili kwa sababu kadha wa kadha:

Chanzo cha picha, Getty Images
1.Muda wa maambukizi
Mojawapo ya sababu ya kuwa na viini vya Malaria na kutoonyesha dalili ni kuwa, mtu anapoambukizwa Malaria kupitia mbu, ni lazima viini hivyo vizaane na kuongezeka hadi kufikia kiwango cha kuonyesha dalili.
Hii ina maana kwamba mtu hatoweza kuwa na dalili katika kipindi hiki japo tayari ana viini vya Malaria.

Chanzo cha picha, Getty
2.Kinga ya Mwili
Kinga ya mwili ni muhimu sana katika kudhiiti magonjwa kama vile Malaria. Profesa Sam Kinyanjui anaelezea kwamba:
"Watu ambao wametokea au kuishi katika maeneo yaliyoathirika na Malaria, wanapoambukizwa mara ya kwanza, huwa ni kali sana, ndiyo maana unapata Watoto wachanga hawana kinga, na wengi hupata malaria na kusababisha kulazwa na wengine hata kufa. Ila mtu anapoendelea kupata Malaria mara kwa mara akitibiwa na kupona kinga inaimarika, hali inayomfanya kudhibiti viini hivyo anapoambukizwa "
Wakati huo mwathiriwa huwa na Malaria isio na dalili kutokana na kinga tosha ya kuvidhibiti.

Chanzo cha picha, Getty
3. Chanjo
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, chanjo za malaria za RTS,S na R21 hufanya kazi dhidi ya vimelea hatari zaidi vya malaria duniani vya P. falciparum,ambavyo vimeenea zaidi barani Afrika.
Chanjo zote mbili za malaria ni salama na zina ufanisi, na zote zimeidhinishwa awali na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Profesa Kinyanjui, anaelezea kwamba chanjo kwa mwanadamu huimarisha kinga ya mwili, na mtu anapoambukizwa inakabiliana na viini na kupunguza viwango vyake, ambapo mwathiriwa hukusa kuonesha dalili zozote, licha ya kuwa na viini hivyo.
Shirika la Afya Duniani linasema kuwa kufikia hivi sasa, nchi 25 barani Afrika zinatoa chanjo dhidi ya malaria kama sehemu ya programu za chanjo kwa watoto na kwa mujibu wa mipango ya kitaifa ya kudhibiti malaria.
Hii inajumuisha nchi 5 ambazo zimeanzisha utoaji wa chanjo hiyo kitaifa, na nchi 19 zinazotoa chanjo katika ngazi za chini ya taifa huku zikiwa na mipango ya kufikia maeneo zaidi kadiri muda unavyosonga.
Kwa ujumla, zaidi ya watoto milioni 10 kwa mwaka wanalengwa kupata chanjo ya malaria katika nchi hizi.
Nchi hizo ni pamoja na Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Central African Republic, Chad, Côte d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Ghana, Guinea, Guinea-Bissau, Kenya, Liberia, Malawi, Mali, Msumbiji, Niger, Nigeria, Sierra Leone, Sudan Kusini, Sudan, Togo, Uganda na Zambia

Chanzo cha picha, Getty Images
Athari ya kuwa na viini vya Malaria bila kuwa na dalili
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa hifadhi ya vimelea vya Malaria bila dalili ni mojawapo ya visababishi vikuu vya kuendelea kwa maambukizi ya malaria, jambo linalolemaza juhudi za kutokomeza ugonjwa huu duniani.
Baadhi ya Athari ni:
Kueneza Malaria
Kwa mujibu wa chupo cha London School of Hygiene & Tropical Medicine, Imperial College London, na West African Centre for Cell Biology of Infectious Pathogens (WACCBIP) pamoja na Chuo Kikuu cha Ghana, mtu kusalia kuwa na afya licha ya kuwa na viini vya Malaria, bila matibabu , vimelea vyake huweza kuishi na kuambukiza wengine.
Watu wenye kinga hafifu kama vile kina mama wajawazito na watoto wapo katika Athari ya kuathirika.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza mkakati wa vipengele vitatu ili kuzuia malaria kwa wanawake wajawazito wanaoishi katika maeneo yenye kiwango cha wastani hadi cha juu cha maambukizi:
- Vyandarua vilivyotibiwa na dawa ya kuua wadudu (ITNs)
-Matibabu ya kinga ya mara kwa mara wakati wa ujauzito (IPTp)
- Utambuzi na matibabu ya haraka.

Chanzo cha picha, Getty Images
Upungufu wa damu/ Anaemia
Kwa mujibu wa tovuti ya Malaria World, maambukizi ya malaria yasiyo na dalili, uhusishwa na upungufu wa damu na kupungua kwa viwango vya hemoglobini.
Hii inasisitiza umuhimu wa kutumia mbinu za uchunguzi za faragha kwa maambukizi hayo na kutambua athari zake kiafya.
Unapokuwa na viini vya Malaria mwilini, Uharibifu endelevu wa kiwango cha chini wa chembe za damu hupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya hemoglobini kadiri muda unavyopita.
Utafiti zaidi wa National Library of Medicine LIM, unasema kuwa:
"Katika maeneo ambapo malaria "isiyo na dalili" imeenea sana, upungufu wa damu unaosababishwa na malaria kunaweza kuwa changamoto.
Maambukizi ya helminth na hemoglobinopathy ni ya kawaida na yanaweza kuzidisha upungufu wa damu huku yakitoa kiwango cha ulinzi dhidi ya malaria yenye dalili .
Katika mazingira yenye rasilimali duni, watoto wachanga na watu wenye utapiamlo wanaweza kuambukizwa na helminth na upungufu wa madini ya iron; tatizo lolote la ziada la damu, ikiwa ni pamoja na hemolysis ya malaria, inaweza kumfanya mtu awe na upungufu mkubwa wa damu .
Kushuka kwa kasi ya mkusanyiko wa hemoglobin wakati unapoathirika na malaria yenye dalili kunaweza kusababisha kupungua kwa viwango vya damu .
Kadri viwango vya upungufu wa damu vinavyoongezeka, hatari ya kupungua kwa damu, vifo vinavyotokana na vimelea vya damu, magonjwa yanayoambatana na damu, na maambukizi ya bakteria huongezeka kwa kasi."
Afya kwa jumla huathirika
Maambukizi haya yanaweza kuendelea na kusababisha uvimbe unaogeuza virutubisho kutoka ukuaji hadi mwitikio wa kinga, na kuathiri vibaya lishe ya watoto na kuongeza hatari ya utapiamlo, upungufu wa damu, ukuaji wa kudumaa, na kushindwa kutambua vitu kwa haraka, kwa mujibu wa tovuti ya Science Report.
Katika maeneo ya vijijini Malawi, ambapo viwango vya malaria ni vya juu, na upatikanaji wa huduma za afya na usalama wa chakula ni mdogo, watoto wengi walio chini ya miaka mitano wanakabiliwa na udumavu, uzito mdogo na upotevu wa uzito.
Hii inasisitiza hitaji la haraka la hatua jumuishi zinazoshughulikia malaria na utapiamlo kwa watu hawa walio katika mazingira magumu.
Suluhisho

Chanzo cha picha, Prof. Sam Kinyanjui
Profesa Sam Kinyanjui ni mkuu wa mafunzo ya utafiti katika kituo cha utafiti cha KEMRI-Wellcome nchini Kenya, ambapo utafiti wake unaelezea jinsi mwili unavyojikinga dhidi ya maambukizi ya Malaria katika juhudi za kutafuta chanjo ya malaria, kwa zaidi ya miaka 20.
Anashauri umuhimu wa mataifa kuwekeza katika chanjo ya Malaria na utafiti, kusambaza vyandarua, na kuwashinikiza raia kuvitumia na vile vile kutoa tiba ya Pamoja katika jamii mara kwa mara.














