Siri ya sayari isiyoonekana

    • Author, Fernando Duarte
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Tangu Pluto ipokonywe hadhi ya kuwa sayari mwaka 2006, tumekuwa tukiambiwa kuwa mfumo wa jua una sayari nane pekee.

Hata hivyo, baadhi ya wanasayansi wanaamini kuwa kuna sayari ya tisa isiyoonekana kwa urahisi, na huenda tuko karibu kuigundua kupitia darubini mpya zenye nguvu kubwa.

Vera C. Rubin Observatory iliyoko juu ya mlima kaskazini mwa Chile ilianza kazi yake rasmi Juni 2025, ikiwa na lengo la kuchunguza kwa kina mabadiliko ya uelewa wa binadamu kuhusu ulimwengu, ikiwemo hali ya mfumo wetu wa jua.

Uwepo wa Sayari ya Tisa umekuwa mada ya mjadala mkali na tofauti za kisayansi tangu mwaka 2016. Katika mwaka huo, wanaastronomia Konstantin Batygin na Michael Brown wa Taasisi ya teknolojia ya California walichapisha utafiti wakidai kuwa kuna sayari yenye uzito takribani mara kumi ya Dunia katika maeneo ya mbali ya mfumo wa jua.

Kwa mujibu wao, sayari hiyo inaweza kueleza mwenendo usio wa kawaida wa miili sita ya barafu inayopita Neptuni katika eneo linaloitwa Ukanda wa Kuiper. Mizunguko yake iliyoinama na kunyooka isivyo kawaida inaashiria uwepo wa nguvu ya uvutano ya kitu kikubwa kisichoonekana.

"Ikiwa Sayari ya Tisa haipo, hatutakuwa na maelezo ya matukio mengi ya kushangaza," Profesa Brown aiambia BBC.

Iwapo huvutiwi na undani na mafumbo ya unajimu, huenda usiligundue jambo la kushangaza lililomo. Profesa Brown, mmoja wa watetezi wakuu wa uwepo wa sayari mpya isiyoonekana, ndiye huyo huyo mwanasayansi ambaye juhudi zake za kuiondoa Pluto kwenye orodha ya sayari zilipata umuhimu mkubwa takribani miaka ishirini iliyopita.

Kumekuwa pia na muktadha wa kihistoria wa kushangaza. Mwanasayansi Michael Brown, mmoja wa watetezi wa uwepo wa Sayari ya Tisa, ndiye pia aliyeshiriki katika ugunduzi uliosababisha Pluto kupokonywa hadhi ya sayari.

Pluto iligunduliwa mwaka 1930 kama sayari ya mbali zaidi na ndogo zaidi katika mfumo wa jua. Hata hivyo, mwaka 2005 ugunduzi wa Eris ulilazimisha Jumuiya ya Kimataifa ya Unajimu kubadili ufafanuzi wa sayari, na Pluto ikashushwa hadhi kuwa sayari kibete.

Sayari isiyoonekana na iliyo mbali sana

Changamoto kubwa ni kuwa Sayari ya Tisa haijawahi kuonekana moja kwa moja.

Wanasayansi wanategemea mifano ya kompyuta na dalili za mizunguko ya miili ya angani.

Kama ipo, sayari hiyo iko mbali sana kiasi kwamba inachukua zaidi ya miaka 20,000 kuzunguka jua mara moja, na hivyo kuifanya iwe hafifu sana kuonekana kwa darubini za kawaida.

Ili kuongeza ugumu zaidi wa suala hilo, wanakadiria kuwa mzunguko wa Sayari ya Tisa utakuwa wa ajabu sana.

Wakati mizunguko ya sayari nane za mfumo wa jua karibu na Jua ikiwa ya duara kiasi na iliyonyooka, mwendo wa sayari hiyo ya tisa ya mfumo wa jua unatarajiwa kuwa wa umbo la duara lenye urefu (eliptikali), ukiwa na mkengeuko mkubwa na iko katika mpangilio mmoja

Uwezekano wa ugunduzi mpya

Kwa sasa, matarajio ya kuigundua yameongezeka kutokana na uwezo wa darubini mpya.

Tofauti na darubini za awali zinazolenga vitu maalum, Vera Rubin Observatory inachunguza anga nzima ya nusu ya kusini ya Dunia kila baada ya siku chache, kwa kutumia kamera kubwa zaidi ya kidijitali iliyowahi kutengenezwa.

Wanasayansi wanaamini kuwa kama Sayari ya Tisa ipo, huenda ikagundulika ndani ya miaka michache ijayo kupitia uchunguzi huu mpana.

Kituo hicho cha uchunguzi kimewekewa vifaa vya kisasa ikiwemo kamera kubwa zaidi ya kidijitali kuwahi kutengenezwa. Kamera hiyo imepangwa kupiga picha za mabilioni ya miili ya angani katika kipindi cha miaka kumi ya utafiti wake, ikiwa na lengo mojawapo la kukusanya zaidi ya picha 40,000 mpya za miili ya mbali iliyo nje ya obiti ya Neptune.

"Vera C. Rubin Observatory inaweza kuchunguza idadi kubwa ya miamba ya angani hafifu na ya mbali ambayo hatukuweza kuiona hapo awali," anasema Dkt. Sarah Greenstreet, mwanaastronomia katika kituo hicho.

"Ikipatikana katika ukubwa na eneo linalokadiriwa, Sayari ya Tisa inaweza kugunduliwa na kituo hicho cha Rubin," anasema.

Neptune tena?

Brown pia anaamini kuwa Vera C. Rubin Observatory "itaweza ama kuigundua Sayari ya Tisa moja kwa moja au kupata ushahidi wa kuaminika kuhusu uwepo au kutokuwepo kwake." Anaamini kwamba kama sayari hiyo ipo, itaweza kuonekana ndani ya mwaka mmoja au miwili ijayo, jambo ambalo lingekuwa tukio la kihistoria katika unajimu.

"Sayari ya Tisa ingekuwa sayari ya tano kwa ukubwa katika mfumo wa jua na ya kwanza kugunduliwa katika kipindi cha miaka 180," anasema.

Mwanasayansi huyo anarejelea ugunduzi rasmi wa Neptune mwaka 1846.

Uwepo wa Neptune ulitabiriwa baada ya kugunduliwa kwa mikengeuko isiyo ya kawaida na mifumo isiyoelezeka katika mzunguko wa jirani yake Uranus.

Mwanasayansi wa Ujerumani Johann Gottfried Galle aliweza kubaini mahali ilipo Neptune angani kwa kutumia hesabu za kikanuni za unajimu.

Baadaye ilibainika kuwa Galileo Galilei alikuwa ameiona Neptune mapema zaidi mwaka 1612, lakini hakuitambua kama sayari kwa sababu mwendo wake ulikuwa wa polepole sana na usioonekana kwa urahisi ukilinganisha na nyota na uwezo wa darubini za wakati huo.

Je, hali kama hiyo imewahi kutokea kwa Sayari ya Tisa?

Profesa Malena Rice wa Yale University katika taaluma ya unajimu na unajimu wa anga za mbali (astrophysics) anahisi kuwa huenda hali kama hiyo ipo kwa Sayari ya Tisa.

"Sikubali kuwa Sayari ya Tisa haipo kwenye data zetu," anasema. "Tunachohitaji ni kuichunguza kwa umakini zaidi."

Mwezi Aprili uliopita, kundi la wanasayansi kutoka Taiwan, Japan na Australia lilifanya hivyo hasa.

Walichambua uchunguzi wa anga kutoka kwa darubini mbili za infrared za angani, zilizozinduliwa mwaka 1983 na 2006 mtawalia, na kugundua nukta kadhaa hafifu ambazo zilidhaniwa huenda ni miili isiyojulikana ya angani inayosogea katika kipindi cha miaka 23 ya uchunguzi.

Baadhi ya wanaastronomia walipokea matokeo hayo kwa tahadhari, na hata timu ya utafiti yenyewe ilijizuia kutoa hitimisho la moja kwa moja.

"Bado ni mapema kusema kuwa utafiti wetu umegundua Sayari ya Tisa katika mfumo wa jua," anasema Terry Fan, mtafiti mkuu katika National Tsing Hua University. Badala yake, anaeleza ugunduzi huo kama "mgombea anayeweza kuwa Sayari ya Tisa."

Lakini kuna jambo la kueleweka: Kuwepo kwa Sayari ya Tisa hakutashangaza wanaastronomia kama akina Rice.

Sayari dhahania inatabiriwa kuwa kubwa kuliko Dunia na ndogo kuliko Neptune, na Rice anasema huo ndio saizi ya kawaida kwa sayari katika mifumo mingine ya jua.

"Tunaona aina hizi za sayari karibu nusu ya nyota zingine, na hatuna kama nazo katika mfumo wetu wa jua," anasema.

Ikiwa sio sayari, basi ni nini?

Hata hivyo, si wanasayansi wote wanaokubaliana na nadharia hii. Wengine wanasema huenda dalili hizo zinatokana na makosa ya uchunguzi au michakato mingine ya asili ya anga.

Utafiti uliofanywa na Batygin na Brown wakosolewa kwa historia ya awali ya sayari ya ajabu. Sayari X ya dhahania iliyofuata Uranus ilipendekezwa mwanzoni mwa karne ya 20 lakini ikakataliwa baadaye.

Timu nyingine za watafiti pia zimependekeza kuwa usumbufu wa mizunguko ya vitu vya mbali huenda ulisababishwa na kupita kwa nyota kubwa karibu na mfumo wa jua mabilioni ya miaka iliyopita.

Wakati huo huo, nadharia pinzani imewasilishwa na kundi la wanaastrofizikia kutoka Kituo cha Utafiti cha Jülich nchini Ujerumani.

Mwaka 2025, walifanya uigaji wa kompyuta unaoonyesha kuwa kupita kwa karibu kwa nyota kubwa mabilioni ya miaka iliyopita huenda kulisababisha mvurugiko mkubwa wa mvuto ambao hatimaye ulibadili mizunguko ya miili iliyo nje ya Neptune.

"Sisemi kuwa Sayari ya Tisa haiwezi kuwepo, lakini uwezekano wake ni mdogo sana," anasema Profesa Susanna Falzner, mkurugenzi wa utafiti huo.

Greenstreet anasema ushahidi wa uwepo wa sayari nyingine umepungua katika miaka ya hivi karibuni. Hata kama picha kutoka Vera C. Rubin Observatory zitashindwa kuionyesha Sayari ya Tisa, ana matumaini kuhusu kile ambacho huenda kitagunduliwa badala yake.

"Kuna eneo kubwa sana nje ya mfumo wa jua ambalo bado halijachunguzwa ipasavyo. Ni nani ajuaye tutakachokipata huko," anasema.

"Kwa kila swali tunalolijibu, maswali mapya hujitokeza daima."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid