Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi ya kuimarisha vifundo vya miguu na kuepuka majeraha
Kifundo cha mguu ni mojawapo ya sehemu muhimu zaidi za mwili zinazosaidia kufyonza mshtuko na kudumisha usawaziko wakati wa kusimama, kutembea na kukimbia. Vifundo vya miguu pia vina jukumu muhimu katika kubeba uzito wa mwili na kusaidia harakati mbalimbali za kila siku.
Hata hivyo, watu wengi hawatambui umuhimu wake hadi wanapopata jeraha.
Kwa mujibu wa Dk. Genevieve Tavaia, mkufunzi wa mazoezi na mtaalamu wa utendaji wa mwili, majeraha ya vifundo vya miguu ni ya kawaida sana. Taasisi ya Kitaifa ya Afya na Utunzaji wa Afya ya Uingereza (NICE) inakadiria kuwa yanachangia asilimia tano ya wagonjwa wote wanaofika katika idara za dharura.
Majeraha haya yanaweza kutokea kwa wanariadha na watu wa kawaida. Sababu zake ni pamoja na kujikanyaga vibaya, kuanguka, kukimbia kwenye eneo lisilo sawa, kuvaa viatu visivyofaa au kuwa na misuli dhaifu inayozunguka kifundo cha mguu.
Tavaia anasema kuwa watu wengi huzingatia kuimarisha misuli ya mapaja, mikono au tumbo lakini husahau kwamba vifundo vya miguu ndiyo msingi wa harakati nyingi za mwili.
Anasema majeraha mengi yanaweza kuzuilika kwa kuimarisha vifundo vya miguu na kuongeza ufahamu wa jinsi miguu inavyofanya kazi.
1. Boresha mawasiliano kati ya ubongo na mwili
Hatua ya kwanza ni kuboresha uwezo wa mwili kutambua na kudhibiti harakati za miguu na vifundo vya miguu.
Wataalamu wa mazoezi wanaita uwezo huu proprioception, yaani uwezo wa mwili kutambua nafasi na mwendo wa viungo vyake bila kuangalia.
"Kwa kutuma taarifa kutoka ubongoni hadi kwenye mguu na kifundo cha mguu, tunaweza kuimarisha uthabiti wa mwili na kujenga msingi mzuri wa mazoezi mengine," anasema Tavaia.
Ili kuboresha ufahamu huo, anashauri mazoezi yanayohusisha vidole vya miguu.
Kubonyeza kidole kikubwa cha mguu chini
Bonyeza kidole kikubwa cha mguu ardhini kwa sekunde chache, kisha zingatia jinsi upinde wa mguu unavyoitikia. Zoezi hili husaidia kuamsha misuli midogo inayosaidia uthabiti wa mguu.
Kusogeza kidole kikubwa pembeni
Weka kalamu sakafuni karibu na kidole kikubwa cha mguu, kisha jaribu kukisogeza kuelekea kwenye kalamu.
Ingawa linaonekana rahisi, zoezi hili husaidia kuboresha udhibiti wa misuli ya mguu na kuongeza uwezo wa mwili kujirekebisha unapopoteza usawaziko.
2. Imarisha misuli, usawaziko na udhibiti wa harakati
Kazi kuu za vifundo vya miguu ni kubeba uzito wa mwili, kudumisha usawaziko na kusambaza nguvu wakati wa harakati.
Kadiri misuli inayozunguka kifundo inavyokuwa imara, ndivyo hatari ya majeraha inavyopungua.
Kuinua visigino
Simama karibu na kitu imara, kisha inua visigino kutoka sakafuni ukiwa umeegemea sehemu ya mbele ya nyayo.
Hakiksha vifundo vya miguu haviegemei pembeni wakati wa zoezi.
Mazoezi haya huimarisha misuli ya ndama na tendon ya Achilles, ambayo yote yana mchango mkubwa katika uthabiti wa kifundo.
Mazoezi ya usawaziko
Jaribu kusimama kwa mguu mmoja kwa sekunde 20 hadi 30. Kadiri uwezo wako unavyoongezeka, unaweza kufanya zoezi hilo huku umefumba macho au juu ya sakafu isiyo tambarare kidogo.
Mazoezi haya huufundisha mwili kuitikia haraka unapokaribia kupoteza usawaziko, jambo linalosaidia kuzuia majeraha.
Mazoezi ya udhibiti wa harakati
Mazoezi kama kusimama kutoka kwenye kiti, kupanda na kushuka ngazi, au kusimama kwa mguu mmoja yanaweza kusaidia kuimarisha vifundo vya miguu.
"Ikiwa umezoea kutumia mguu mmoja kila mara unapopanda ngazi, anza kufanya mazoezi ya kutumia mguu mwingine pia," anashauri Tavaia.
Kwa watu wanaopata nafuu baada ya kuteguka kifundo cha mguu, mazoezi ya kurusha na kudaka mpira wakiwa wamesimama kwa mguu mmoja yanaweza kusaidia kurejesha udhibiti wa mwili.
Kwa wanaokabiliwa na maumivu ya muda mrefu kutokana na matatizo ya kano (tendinopathy), mazoezi yenye mzigo mdogo lakini yanayoimarisha misuli yanaweza kusaidia, kama vile mazoezi ya kunyanyua miguu kwa kutumia uzani.
3. Chagua viatu sahihi
Viatu vina nafasi kubwa katika kulinda afya ya vifundo vya miguu.
Tavaia anasema watu wengi huvaa viatu vya kupendeza machoni lakini visivyotoa msaada unaohitajika kwa miguu.
"Watu wengi hufanya kosa la kuvaa viatu vya mbele nyembamba au viatu visivyotoa msaada wa kutosha kwa miguu."
Anashauri kuchagua viatu vinavyotoa nafasi ya kutosha kwa vidole na msaada kwa upinde wa mguu ili kusaidia usambazaji sahihi wa uzito wa mwili.
Viatu vinavyoiga kutembea miguu peku vinaweza kuwa na manufaa kwa baadhi ya watu kwa sababu huruhusu miguu kufanya kazi kwa asili zaidi. Hata hivyo, matumizi yake yanapaswa kuanza taratibu ili miguu ipate muda wa kuzoea.
Pia ni muhimu kuchagua viatu kulingana na shughuli unayofanya:
Mazoezi ya kuchuchumaa: viatu vyenye soli tambarare vinafaa zaidi.
Kukimbia: viatu vyenye uwezo mzuri wa kufyonza mshtuko vinapendekezwa.
Kutembea kwenye maeneo yenye miinuko au ardhi isiyo tambarare: buti za matembezi zinaweza kusaidia kupunguza hatari ya kuteguka.
Hata hivyo, kuvaa buti hizo kila siku kwa muda mrefu kunaweza kupunguza unyumbufu wa kifundo cha mguu na kufanya harakati kuwa ngumu zaidi.
Kwa nini ni muhimu kuimarisha vifundo vya miguu?
Wataalamu wanasema kifundo dhaifu cha mguu kinaweza kuongeza hatari ya kuanguka, kuteguka mara kwa mara na hata maumivu ya magoti au nyonga kutokana na namna mwili unavyolazimika kufidia udhaifu huo.
Kuimarisha vifundo vya miguu si muhimu kwa wanariadha pekee. Ni hatua inayoweza kuwafaidi watu wa rika zote, hasa wazee ambao wako kwenye hatari kubwa ya kuanguka.
Kwa ufupi
Ili kuimarisha vifundo vya miguu na kupunguza hatari ya majeraha:
Boresha mawasiliano kati ya ubongo na mwili kupitia mazoezi ya kuongeza ufahamu wa harakati za miguu.
Imarisha misuli na usawaziko kwa kufanya mazoezi ya nguvu na udhibiti wa harakati.
Vaa viatu vinavyofaa kulingana na aina ya shughuli unayofanya.
Kwa kufanya mazoezi haya mara kwa mara na kuchagua viatu sahihi, unaweza kupunguza hatari ya majeraha na kuboresha afya ya miguu yako kwa muda mrefu.