Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Marekani yatangaza ushuru mpya kwa washirika wake wa biashara ikiwemo China

Ushuru huo mpya unatarajiwa kuathiri washirika wakubwa wa kibiashara wa nchi hiyo, wakiwemo China, Umoja wa Ulaya na maeneo mengine 12.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Marekani yaipa SpaceX idhini ya kurusha satelaiti milioni moja angani

    Marekani imeipa kampuni ya SpaceX idhini ya kurusha satelaiti milioni moja katika angani ili kusaidia kujenga vituo vya kuhifadhi na kuchakata data angani.

    Hii ni idhini ya kwanza ya aina yake.

    Kampuni hiyo inayomilikiwa na Elon Musk inataka kutumia nishati ya mwanga wa jua kuendesha satelaiti hizo zitakazochakata data kwa ajili ya akili unde (AI) na kutuma matokeo yake kurejea duniani.

    Tume ya Mawasiliano ya Marekani (FCC) ilisema kuwa mradi huo unaojulikana kama Starmind utasaidia katika "ukuaji wa uchumi wa Marekani unaotokana na teknolojia ya akili unde."

    Idhini hiyo imetolewa wakati jamii mbalimbali nchini Marekani zimekuwa zikipinga upanuzi wa vituo vya kuhifadhi na kuchakata data vinavyojengwa ardhini.

    SpaceX inaamini kuwa "vituo vya kuchakata data vilivyo angani" ndiyo njia yenye gharama nafuu zaidi na inayotumia nishati kwa ufanisi kukidhi ongezeko la mahitaji ya uwezo wa kompyuta unaohitajika kuendesha teknolojia ya akili unde (AI), mahitaji ambayo kwa mujibu wa kampuni hiyo yanazidi uwezo wa miundombinu iliyopo duniani.

    Akijibu tangazo hilo, Musk aliandika kwenye mtandao wa X "Tunashukuru sana. Huu utakuwa mchango mkubwa kwa Marekani na dunia nzima."

    Soma pia:

  2. Tetesi za Soka: Liverpool yafikiria kumrejesha Quansah, PSG ikimuwinda nyota wa Chelsea

    Liverpoolhaijaondoa uwezekano wa kutumia kipengele cha mkataba kinachoiruhusu kumnunua tena beki wa Bayer Leverkusen, Jarell Quansah, mwenye umri wa miaka 23.

    Hatua hiyo itaiwezesha Liverpool kumsajili beki huyo wa timu ya taifa ya England mwaka 2027 kwa ada ya zaidi ya pauni milioni 50.

    Chelsea inakabiliwa na uwezekano wa kumpoteza mshambuliaji wake kutoka Brazil, Estevao Willian, mwenye umri wa miaka 19, ambaye analengwa na Paris Saint-Germain (PSG). Klabu hiyo ya Ufaransa inamtafuta mshambuliaji kutokana na baadhi ya wachezaji wake kuumia.

    Arsenal imemuongeza winga wa Club Brugge na timu ya taifa ya Ureno, Carlos Forbs, mwenye umri wa miaka 22, kwenye orodha ya wachezaji inayowalenga kuwasajili katika dirisha la usajili la Januari.

    Liverpool imekubali kumsajili winga wa Diambars FC, Sidy Barhama Ndiaye, Januari 2028. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 16 alivutia baada ya kufanya vizuri akiichezea Senegal katika Kombe la Dunia la vijana wasiozidi miaka 17.

    Beki wa kati wa England, Fikayo Tomori, mwenye umri wa miaka 28, huenda akaondoka AC Milan na kujiunga na Atletico Madrid huku mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kumalizika ndani ya miezi sita ijayo.

    Everton haitafanya jaribio la kumsajili mshambuliaji wa Senegal anayeichezea Cagliari, Paul Mendy, katika dirisha la Januari, lakini bado inaendelea kumfuatilia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 kwa ajili ya usajili wa baadaye.

    Kipa wa Arsenal, Kepa Arrizabalaga, hajapokea ofa yoyote kutoka Valencia licha ya taarifa zilizomuhusisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 na kurejea nchini kwao Hispania.

    Bayern Munich ina nafasi nzuri ya kumshawishi winga wa Ufaransa, Michael Olise, mwenye umri wa miaka 24, kuongeza muda wa mkataba wake ambao kwa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.

  3. Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi washambuliana, milipuko yasikika Riyadh

    Milipuko mikubwa ulisikika katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, jana jioni, baada ya kundi la Wahouthi kutangaza kuwa lilikuwa limelenga bandari za Jeddah na Jazan, kwa kile walichokiita, kujibu mashambulizi ya Saudi Arabia katika bandari ya Hodeidah, inayodhibitiwa na kundi hilo magharibi mwa Yemen.

    Saudi Arabia imesema kuwa imefanikiwa kuzuia shambulio la ndege isiyo na rubani la wahouthi lililolenga kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ras Tanura. Picha za satelaiti, hata hivyo, zilionyesha moshi mwingi ukitanda juu ya eneo hilo.

    Wakati huohuo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulitangaza kuwa umedungua ndege isiyo na rubani ya Wahouthi karibu na bandari ya Jeddah, katika pwani ya Bahari Nyekundu.

    Mapigano kati ya pande hizo mbili yameongezeka katika siku za hivi karibuni.

    Soma pia:

  4. Watu 31 wafariki baada ya lori ya mafuta kupata ajali mjini Cairo

    Watu 31 wamefariki na wengine 21 kujeruhiwa baada ya moto mkubwa kuzuka kwenye barabara moja kuu mjini Cairo, Misri.

    Ajali hiyo ilitokea baada ya lori ya mafuta kupenduka na kusababisha ajali, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

    Hospitali zilizo karibu zilipokea majeruhi waliokuwa na majeraha ya kuungua na matatizo ya kupumua kutokana na kuvuta moshi baada ya tukio hilo lililotokea jana jioni, katika barabara iliyoko eneo la Warraq.

    Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha miale mikubwa ya moto na moshi mweusi ukipaa juu angani, huku magari kadhaa yaliyokuwa karibu yakiteketea.

    Maafisa hawajatoa maelezo rasmi kuhusu chanzo cha moto huo. Hata hivyo, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali vimeripoti kuwa lori hilo la mafuta lilipinduka na kumwaga petroli kwenye magari yaliyokuwa karibu.

    Mwendesha mashtaka mkuu wa eneo hilo ameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na kuagiza sampuli za vinasaba (DNA) zichukuliwe kutoka kwa miili ya waliofariki.

    Gazeti la serikali la Al-Ahram limeripoti, likinukuu vyanzo vinavyofahamu uchunguzi huo, kuwa lori hilo lililokuwa likimilikiwa na kampuni binafsi lilikuwa likisafiri kwenye barabara hiyo, wakati nyaya za umeme zilianguka mbele yake na kumfanya dereva ashindwe kulidhibiti gari hilo.

  5. Trump atangaza ushuru mpya kwa bidhaa zinazoingia Marekani

    Marekani imetangaza ushuru mpya, dhidi ya bidhaa zinazoingia nchini humo.

    Ushuru huo mpya unatarajiwa kuathiri washirika wakubwa wa kibiashara wa nchi hiyo, wakiwemo China, Umoja wa Ulaya na maeneo mengine 12, yakiwemo Japan, Korea Kusini na Taiwan.

    China inakabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha ushuru, cha hadi asilimia 40, ikifuatiwa na Vietnam ambayo inaweza kutozwa hadi asilimia 35. Nchi nyingine zitatozwa ushuru wa asilimia 20 au 25.

    Mwakilishi wa Biashara wa Marekani alitangaza mapendekezo hayo ya ushuru pamoja na ripoti za kina zinazoeleza jinsi sera za biashara za kila eneo husika zinavyodaiwa kuathiri biashara ya Marekani.

    Ushuru huo mpya utaanza kutekelezwa mwaka ujao baada ya mashauriano.

    Mapendekezo hayo ya ushuru yataathiri bidhaa kutoka mataifa yafuatayo: China,Umoja wa Ulaya,Singapore,Uswisi,Indonesia,Malaysia,Cambodia,Thailand,Korea Kusini,Vietnam,Taiwan,Bangladesh,Japan, India

    Soma pia:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Alhamisi ya leo