Video mpya zafichua siri kuhusu Msaudi anayehusishwa na shambulio la 9/11

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 14

Mtu anayekabiliwa na kesi ya kisheria ya dola trilioni iliyofunguliwa na familia za waathirika wa mashambulizi ya 9/11 alikuwa na uhusiano mkubwa na maafisa wa serikali ya Saudi Arabia.

Zaidi ya hayo, alishiriki katika michezo ya paintball pamoja na mmoja wa viongozi wa al-Qaeda, kulingana na video zilizopatikana na BBC.

Picha hizo, ambazo ziliifikia FBI siku chache baada ya mashambulizi ya mwaka 2001, zinapingana na kauli ambazo Omar al-Bayoumi amekuwa akitoa kwa miaka 25, akikanusha madai kwamba alikuwa mfuasi wa itikadi kali na jasusi wa Saudi Arabia.

Katika mojawapo ya video hizo, Bayoumi, ambaye alidai kuwa alikuwa mwanafunzi wakati akiiishi Marekani, anaonekana akimkumbatia Anwar al-Awlaki, ambaye baadaye angekuwa kiongozi wa al-Qaeda katika Rasi ya Arabia.

Katika video nyingine, Bayoumi na Awlaki wanaonekana wakicheza paintball karibu na San Diego, pamoja na afisa kutoka Wizara ya Masuala ya Kiislamu ya Saudi Arabia.

Picha hizi ni sehemu ya kesi ya kisheria iliyofunguliwa na familia za waathirika wa mashambulizi ya 9/11 dhidi ya Saudi Arabia, na hazijawahi kuwekwa hadharani hapo awali.

Kesi hiyo inadai kwamba Saudi Arabia ilihusika katika mashambulizi hayo, na kwamba Bayoumi alitoa msaada kwa watu 2 kati ya watekaji nyara 19 waliotekeleza mashambulizi hayo kwa kuangusha ndege kwenye World Trade Center huko New York na Pentagon huko Virginia.

Bayoumi alikamatwa nchini Uingereza na Polisi wa Metropolitan siku chache baada ya mashambulizi ya 9/11.

Video hizo zilipatikana miongoni mwa vitu vyake binafsi, pamoja na ushahidi mwingine muhimu.

Miongoni mwa ushahidi huo kulikuwa na mchoro wa ndege ulioambatana na kanuni ya kushuka kwa ndege wakati wa safari.

Mawakala kadhaa wa FBI walipokea nakala za mchoro huo, lakini haukuwahi kuoneshwa wachunguzi wa Uingereza, licha ya kwamba ulitumwa kwa njia ya mjumbe hadi kituo cha polisi ambako Bayoumi alikuwa anashikiliwa.

Mpango huo pia ulifichwa kutoka kwa baadhi ya mawakala wa FBI waliokuwa wakimchunguza Bayoumi, pamoja na Tume ya 9/11, chombo huru kilichopewa jukumu la kuchunguza shambulio baya zaidi la kigaidi katika historia ya Marekani, ambapo karibu watu 3,000 walipoteza maisha. Bayoumi hakuwahi kufunguliwa mashtaka.

Yeye wala serikali ya Saudi Arabia hawakujibu maombi ya BBC ya kutoa maoni, ingawa wote wamekuwa wakikanusha mara kwa mara kuhusika katika mashambulizi hayo au kuwa na taarifa zake kabla hazijatokea. FBI ilikataa kutoa maoni.

Baada ya uamuzi wa mahakama wa mwaka 2018 ulioruhusu kesi hiyo kuendelea, maelfu ya nyaraka, pamoja na video na picha, ziliwasilishwa mahakamani na baadaye zikaondolewa kwenye usiri kwa amri ya rais Joe Biden.

BBC Panorama na Radio 4 wamechunguza nyaraka hizo na kuzungumza na mawakala maalumu na wachunguzi kadhaa ili kufuatilia ushahidi ambao FBI ilikusanya kuhusu Bayoumi na madai ya kuhusika kwa Saudi Arabia katika mashambulizi ya Septemba 11, na pia kuelewa kwa nini suala hilo halikuchunguzwa kwa kina kwa kipindi cha miaka 25.

Kile ambacho uchunguzi wa BBC umebaini

  • Mchoro wa ndege ulitumwa katika ofisi ya FBI huko New York na ukachambuliwa, kulingana na chanzo kutoka ndani ya shirika hilo.
  • Hata hivyo, afisa wa Wizara ya Sheria ya Marekani aliiambia BBC kwamba hakuwahi kuwasilishwa pendekezo lolote la kumfungulia Bayoumi mashtaka kwa kutegemea ushahidi huo, ingawa alisema: "Tumewahi kuwahukumu watu kwa ushahidi mdogo kuliko huo."
  • Mawakala wa FBI huko San Diego, jiji ambalo Bayoumi aliishi wakati alipokuwa Marekani, waliomba mara kwa mara nakala za ushahidi huo, lakini hawakuwahi kupokea sehemu kubwa ya ushahidi huo.
  • Ofisi za FBI huko San Diego na Los Angeles zilizuiwa kuwahoji watu waliokuwa na uhusiano na Bayoumi ndani ya serikali ya Saudi Arabia.
  • Wafanyakazi wa Tume ya 9/11 hawakukubaliana na hitimisho kwamba ilikuwa "haiwezekani" kwamba Bayoumi alikuwa na uhusiano na watu wenye msimamo mkali.
  • Hilo lilifanya ripoti hiyo ihusishe dai hilo na "watafiti wetu ambao walishughulika naye moja kwa moja."

Michezo ya kulenga shabaha iliyodaiwa kutumika kama mafunzo ya jihadi

Omar al-Bayoumi aliwasili San Diego kutoka Saudi Arabia mwaka 1994.

Alidai kwamba alikuwa akisoma Kiingereza, lakini kumbukumbu za mahakama zinaonesha kwamba baada ya miaka michache aliacha masomo yake.

Mara nyingi alionekana akiandaa matukio ya kidini, na mara nyingi alikuwa na kamera ya video mkononi au karibu na jicho lake.

Katika video iliyorekodiwa na Bayoumi kati ya mwaka 1997 na mwanzoni mwa 1998, wanaume kadhaa, akiwemo Anwar al-Awlaki, wanaonekana wakishiriki katika mchezo wa paintball.

Video hiyo, iliyorekodiwa karibu na San Diego, inaonesha kundi hilo likiiga mapigano ya mijini na kufanya mazoezi ya kulenga shabaha; wengi wa washiriki walikuwa wamevaa sare za kijeshi.

Wakati fulani, baadhi ya wanaume hao wanaanza kushambulia huku wakipiga kelele "Allahu Akbar" (Mungu ni Mkuu).

Sheikh mmoja wa Saudi Arabia aliyekuwa mgeni anaandamana na kundi hilo, na Bayoumi pia anaweza kusikika akimuita Anwar al-Awlaki kwa cheo cha heshima "Sheikh Anwar."

Paintball ikawa moja ya mada zilizovutia katika uchunguzi wa kukabiliana na ugaidi uliofanywa na FBI baada ya mashambulizi ya Septemba 11, na Wizara ya Sheria ilitumia ushahidi unaohusiana na shughuli hiyo katika kesi kadhaa za ugaidi.

Omar al-Bayoumi na Anwar al-Awlaki walishiriki katika michezo ya paintball huko San Diego kwa takribani miaka mitatu, kati ya mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.

FBI ilipoanza uchunguzi wake baada ya 9/11, mawakala walipokea taarifa kwamba baadhi ya washiriki walikuwa wakishiriki katika michezo hiyo kwa ajili ya kufanya mafunzo ya jihadi.

Ingawa kauli za Awlaki zenye misimamo mikali zilipata umaarufu zaidi baada ya 9/11, wakati video ya mchezo wa paintball iliporekodiwa, tayari alikuwa na uhusiano na wafuasi wa al-Qaeda, na alikuwa karibu kuanza kuchunguzwa na FBI.

Alifariki mwaka 2011 kutokana na shambulio la ndege isiyo na rubani la CIA.

Saudi Arabia imesema kwamba video ya paintball haioneshi ni nani aliyeitengeneza au aliyeirekodi.

Alipoulizwa maswali kwa njia ya mtandao mwaka 2021 kama sehemu ya kesi iliyofunguliwa na familia za waathirika wa 9/11, Bayoumi alisisitiza kwamba hakumjua Awlaki.

Ushahidi wa video uliopingana na madai yake haukukabidhiwa mahakamani kwa siri hadi mwaka mmoja baadaye, na haukuongezwa kwenye kumbukumbu za umma hadi Septemba 4 mwaka huu.

Video nyingine ambayo haikuwa imetolewa hadharani hapo awali inaonesha Bayoumi akimkumbatia Awlaki mwezi Januari 1998.

Picha nyingine zinaonesha mikutano mingi ya Bayoumi na maafisa pamoja na wahubiri kutoka Wizara ya Masuala ya Kiislamu huko Riyadh.

Katika video moja, anaonekana SeaWorld akiwa pamoja na maafisa wawili wa wizara, mmoja wao akiwa amebeba jalada la nyaraka; Bayoumi anamkabidhi mwanawe kamera, kisha anaingia haraka kwenye picha ili kurekodi uwepo wake akiwa pamoja na maafisa hao.

Wizara ya Masuala ya Kiislamu, iliyoanzishwa mwaka 1993, ilionekana kutawaliwa na viongozi wa dini waliounga mkono mtazamo mkali wa Uislamu wa Sunni na kuusambaza duniani kote.

Taasisi hiyo iliwekeza mamia ya mamilioni ya dola duniani kote katika ujenzi wa misikiti na ilituma maafisa kadhaa kwenda Marekani.

Baadhi yao walisimamia mtandao wa wahubiri waliokuwa na misimamo mikali.

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, Omar al-Bayoumi aliorodheshwa kuwa mmoja wa washukiwa wa kwanza katika uchunguzi wa FBI.

Jina lake lilionekana kwenye mkataba wa kukodisha nyumba uliotiwa saini na watekaji nyara wawili wa kwanza kuwasili Marekani, Nawaf al-Hazmi na Khalid al-Mihdhar, ambao walikuwa wafuasi wa kundi la watu watano lililoangusha ndege kwenye Pentagon.

FBI ilimpata Bayoumi huko Birmingham, Uingereza, jiji ambalo alikuwa amehamia pamoja na familia yake kabla ya Septemba 11.

Mnamo Septemba 21, 2001, mawakala kutoka kitengo maalumu cha operesheni cha idara ya kukabiliana na ugaidi ya Polisi wa Metropolitan (Met Police) walimkamata Bayoumi katika moja ya nyumba zake.

Aliwekwa chini ya ulinzi mkali wa polisi katika kituo cha polisi cha Paddington Green huko London, ambako wapelelezi walianza kumhoji.

Kwa mujibu wa sheria ya Uingereza wakati huo, maafisa waliweza kumshikilia kwa siku saba tu bila kumfungulia mashtaka rasmi.

Mchoro wa ndege uliopatikana Birmingham

Asubuhi iliyofuata huko Birmingham, mawakala walianza mchakato wa uchunguzi wa kina na ufungaji wa ushahidi uliopatikana katika nyumba/mali zake: kiasi kikubwa cha nyaraka zenye jumla ya maelfu ya kurasa, mamia ya picha, vipande vya tiketi za ndege na kadi za simu, pamoja na mifuko na masanduku yaliyokuwa na takribani kanda 80 za video.

Saa chache baada ya utafutaji kuanza, baadhi ya ushahidi, uliowekwa katika kundi la kipaumbele cha juu sana kwa maelekezo ya FBI, ulichukuliwa na polisi moja kwa moja hadi Paddington Green, ambako FBI ilikuwa imemweka wakala wake.

Miongoni mwa ushahidi huo kulikuwa na kitabu cha anuani za simu kilichokuwa na majina zaidi ya 24 ya maafisa wa serikali ya Saudi Arabia waliokuwa Marekani na Saudi Arabia; programu ya kuiga uendeshaji wa ndege; tiketi na nyaraka za safari; pamoja na karatasi ya daftari yenye mistari ya njano iliyokuwa na mchoro wa ndege. Juu ya karatasi hiyo, wakala mmoja alikuwa ameandika: "Ina maelezo yaliyoandikwa kwa mkono na hesabu za hisabati zinazohusiana na urefu wa ndege angani."

Miaka kumi na minane baadaye, FBI iliikabidhi karatasi hiyo ya daftari mahakamani kama sehemu ya kesi iliyofunguliwa na familia za waathirika wa 9/11, kwa kufuata amri ya mahakama. Karatasi hiyo iliwekwa wazi kwa umma mwaka 2022.

"Hizi ni hesabu za hisabati za athari ya kugonga," Jodi Westbrook Flowers, ambaye alikuwa miongoni mwa timu ya wanasheria inayowawakilisha familia za waathirika wa 9/11, aliiambia BBC.

Na alisisitiza kwamba, "tulipogundua ilikuwa nini, tulijua kwamba ulikuwa ushahidi usioweza kukanushwa ambao tulikuwa tukitafuta."

Mlinganyo huo, ulioandikwa kwa mwandiko wa Omar al-Bayoumi mwenyewe, unaonesha urefu na umbali ambao rubani angehitaji ili kuelekeza ndege kuelekea shabaha maalumu iliyoko ardhini.

Chini yake kuna mchoro mdogo wa ndege pamoja na mfululizo wa namba.

Mwaka jana, jaji aliyekuwa akisimamia kesi ya familia hizo aliamua kwamba, kwa mtazamo wa kwanza, karatasi hiyo ya daftari "inamuhusisha Bayoumi na ujuzi kuhusu mashambulizi ya Septemba 11."

Mwaka 2021, alipoulizwa kuhusu karatasi hiyo mahakamani, Bayoumi alisema kwamba alikuwa na mchoro huo kwa sababu alipenda kutafuta na kusoma milinganyo, na kwamba hakukumbuka ni lini aliandika.

Kufikia alasiri ya Septemba 22, 2001, nakala za mchoro wa ndege zilikuwa tayari zimefika London, mikononi mwa FBI na polisi wa Uingereza wa kukabiliana na ugaidi, umbali wa mita chache tu kutoka kwenye chumba cha mahabusu ambako Omar al-Bayoumi alikuwa akihojiwa.

Kumbukumbu zinaonesha kwamba katika siku mbili zilizofuata, hati hiyo ilipita mikononi mwa takribani mawakala wengine watatu wa FBI.

Lakini hapa ndipo fumbo linapoanza.

FBI iliwaagiza maafisa wa Polisi wa Metropolitan wamuhoji Bayoumi kuhusu ushahidi mwingine uliowekwa kuwa wa kipaumbele cha juu, lakini wapelelezi waliokuwa wakisimamia mahojiano hayo hawakuwahi kupewa mchoro wa ndege wala kuambiwa kwamba mchoro huo ulikuwepo.

Mawakala wengi wa FBI wametuambia kwamba, baada ya mashambulizi ya 9/11, kulikuwa na msukosuko mkubwa wa shughuli za kila mara, mchana na usiku.

Hata hivyo, ni vigumu kuelewa jinsi ushahidi muhimu kiasi hicho, katika kesi iliyokuwa ikishughulikiwa kwa haraka sana, usingeweza kuwafikia wapelelezi waliokuwa wakifanya mahojiano.

FBI ilikataa kujibu maswali yetu. Na Idara ya Polisi wa Metropolitan ilituambia kwamba haiwezi kutoa maoni kwa sababu mchakato wa kisheria bado unaendelea.

Mifuko yenye kanda za video

Muda mfupi baada ya mchoro wa ndege kutumwa Paddington Green, video zote za Bayoumi pamoja na video ya mchezo wa paintball zilihamishwa kutoka Birmingham hadi New Scotland Yard ili zitengenezwe nakala.

Kufikia Septemba 24, kituo cha polisi cha Paddington Green, kilichokuwa umbali wa zaidi ya maili moja tu, kilikuwa tayari kimepokea kanda hizo za video.

Wapelelezi walichukua mifuko iliyokuwa na kanda hizo hadi kwenye chumba ambako Bayoumi alikuwa akihojiwa, na wakamuonesha baadhi ya video zilizorekodiwa.

Aliulizwa kuhusu kanda mbili zilizoonesha mkutano, lakini mawakala wa Uingereza hawakuwa wamepokea maagizo kutoka FBI ya kumuuliza kuhusu video ya mchezo wa paintball au kuhusu uhusiano wake na Anwar al-Awlaki.

Siku ambayo uamuzi ulipaswa kufanywa kuhusu kama afunguliwe mashtaka au aachiliwe, wapelelezi wa Scotland Yard walishiriki katika mazungumzo ya simu na maafisa kadhaa wa ngazi za juu kutoka Wizara ya Sheria ya Marekani na FBI.

Panorama na Radio 4 wamezungumza na wawili kati ya watu walioshiriki katika mkutano huo. Mmoja wao anakumbuka jinsi wapelelezi wa Uingereza walivyowasilisha ushahidi ambao, kwa maoni yao, ulikidhi masharti yaliyohitajika ili Marekani iombe Bayoumi arejeshwe Marekani na ashtakiwe huko.

Jibu kutoka kwa maafisa wa Wizara ya Sheria lilikuwa kwamba hawangeomba arejeshwe Marekani kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kutosha.

Mnamo Septemba 28, 2001, Bayoumi aliachiliwa.

Hata hivyo, wakati huo, FBI ilikuwa bado haijapeleka nchini Marekani ushahidi wote uliopatikana Birmingham, na zaidi ya hayo, ushahidi huo ulikuwa bado haujachambuliwa kwa kina.

Waraka kutoka kwa mwakilishi wa kisheria wa FBI huko London, uliotumwa wiki mbili baadaye, ulionesha kwamba "video kadhaa, diski za kompyuta na nyaraka" bado zilikuwa zikisubiri kuchunguzwa.

"Tumewahi kuwahukumu watu kwa ushahidi mdogo kuliko huu."

Baada ya Omar al-Bayoumi kuachiliwa, mawakala waliendelea kuchambua ushahidi dhidi yake.

BBC ina ushahidi kwamba mchoro wa ndege ulitumwa kutoka London kwenda katika ofisi ya FBI huko New York kwa ajili ya kuchambuliwa. Ofisi hiyo ndiyo iliyokuwa ikiongoza uchunguzi wa jumla kuhusu mashambulizi ya Septemba 11.

Hata hivyo, hatujaweza kupata kumbukumbu yoyote kuhusu uchambuzi huo au hitimisho lililofikiwa.

Amri ya rais ya mwaka 2021 iliitaka FBI kuondoa usiri kwenye makablasha yanayohusiana na uchunguzi wake kuhusu 9/11, ikiwa ni pamoja yanayohusiana na Bayoumi.

Hata hivyo, miongoni mwa makablasha yaliyotolewa hadharani, FBI imewasilisha hati moja tu inayorejelea mchoro huo, licha ya umuhimu wake kama ushahidi na hati hiyo iliandaliwa miaka 11 tu baada ya mchoro huo kugunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001.

Mchoro ulioandaliwa na Bayoumi unaonekana kana kwamba ulipotelea kwenye shimo jeusi.

Bayoumi hakurejeshwa San Diego, jiji ambalo alikuwa ameishi alipokuwa Marekani na ambako ofisi ya FBI ya eneo hilo pia ilikuwa ikimchunguza.

Kwa kweli, San Diego, ambako maafisa waliwahoji watu waliokuwa na uhusiano naye, walipekua msikiti wake na kuchambua rekodi zake za simu pamoja na taarifa zake za benki, ilipokea karibu hakuna sehemu yoyote ya kiasi kikubwa cha ushahidi kilichokamatwa na Polisi wa Metropolitan huko Birmingham.

Rick Lambert, ambaye alikuwa akiongoza uchunguzi wa FBI katika eneo hilo, aliiambia BBC kwamba ofisi yake iliomba mara kwa mara nakala za ushahidi wote kutoka New York.

Lambert alisisitiza kwamba New York haikujibu maombi ya ofisi yake: "Ninaamini kuna uwezekano kwamba, kama tungeupokea na kuuchambua ushahidi huo, tungeweza kuunganisha vipande vya fumbo hilo kwa haraka zaidi."

Nyaraka zinaonesha kwamba, katika majira ya kuchipua ya mwaka 2002, ofisi ya San Diego hatimaye iliweza kupata nakala za baadhi ya video, si kupitia New York, bali kupitia afisa wa FBI aliyekuwa kiungo huko London.

Kilichotokea kuhusu video hiyo ya mchezo wa paintball pia kinazua maswali.

Nakala ya video hiyo ilitumwa katika ofisi ya FBI mjini New York, ambako ilitazamwa, kama afisa mmoja alivyotuthibitishia.

Hata hivyo, video hiyo haikuingizwa katika muhtasari wa taarifa za ofisi hiyo zilizokuwa zikieleza kuhusu uhusiano wa Bayoumi na watu wenye misimamo mikali.

Nyaraka za FBI na Wizara ya Sheria za Marekani za mwaka 2002, ambazo BBC ilizipitia, zilirejelea baadhi ya vifaa vilivyokamatwa katika makazi ya Bayoumi huko Birmingham. Nyaraka hizo zilisema vifaa hivyo vinaweza "kuonesha hisia na misimamo yake dhidi ya Marekani," huku maandishi yake yakielezwa kuwa "yanaweza kutafsiriwa kuwa ya itikadi ya jihadi."

Hata hivyo, hakukuwa na kutajwa kwa video hiyo ya paintball wala uhusiano wa Bayoumi na Anwar al-Awlaki.

Chakula na Polisi wa Siri wa Saudi Arabia

Mnamo Oktoba 2003, Tume ya 9/11, iliyoanzishwa na Bunge la Marekani kwa lengo la kutoa maelezo "kamili na ya kina" kuhusu mashambulizi hayo ilifanya mahojiano na Omar al-Bayoumi huko Riyadh.

Alikuwa amerejea Saudi Arabia katika miezi iliyofuata baada ya kuachiliwa na polisi wa Uingereza.

Mahojiano hayo yalifanyika mbele ya maafisa wa polisi wa siri wa Saudi Arabia, yaani Mabahith, na yaliendeshwa na mkurugenzi mtendaji wa Tume hiyo, Philip Zelikow, aliyewahi kuwa mshauri wa Rais George W. Bush, akisaidiwa na afisa mwandamizi wa timu hiyo pamoja na afisa kutoka makao makuu ya FBI.

Kumbukumbu za Tume za wakati huo zinaonesha kwamba Bayoumi alipewa nafasi ya kujieleza akiwa katika mazingira yenye utulivu wa kushangaza.

Aliambiwa kwamba "hakuna anayeamini kwamba kwa makusudi aliwasaidia watekaji kutekeleza mpango wao wa kigaidi."

Bayoumi, kwa hasira, alijieleza kuwa yeye ni mtu anayependa amani ambaye alikuwa amegeuka kuwa "mwathirika wa wahanga."

Wakati wa mahojiano hayo, ujumbe wa Marekani ulisitisha shughuli zake kwa muda ili kuhudhuria chakula cha jioni cha kozi kadhaa kilichoandaliwa na Mabahith, ingawa Bayoumi mwenyewe hakuhudhuria.

Baada ya mahojiano kumalizika, Mabahith iliwaambia wajumbe wa Marekani kwamba "wangependa kumuona Bayoumi akiondolewa lawamani."

Wamarekani walijibu kwamba hawangeweza kufanya hivyo kabla ya ripoti yao kuchapishwa.

Ripoti ya Tume ya 9/11 ilipochapishwa mwezi Julai 2004, Bayoumi kwa hakika aliondolewa lawamani.

Waraka huo ulimweleza kama mtu "mwenye msaada na mchangamfu katika kushirikiana na watu," na kusema kwamba hakukuwa na ushahidi kwamba alikuwa na misimamo ya itikadi kali.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi wa Tume hawakuwa wameshawishika kwamba Bayoumi hakuwa na hatia. Waliona kuna uwezekano mkubwa kwamba alijua kuwa Hazmi na Mihdhar walikuwa mawakala wa al-Qaeda.

BBC inaweza kufichua kwamba baadhi ya wajumbe hao walipinga sentensi katika ripoti iliyohitimisha kwamba Bayoumi alikuwa "mtu ambaye si rahisi kuhusishwa na ushiriki wa siri katika shughuli za watu wenye misimamo mikali ya Kiislamu."

Hatimaye, walifikia suluhisho la maelewano: hitimisho hilo likaelezwa kuwa ni maoni ya "watafiti wetu ambao walizungumza naye moja kwa moja na kuchunguza historia yake."

Sentensi hiyo iliandikwa kutokana na saa nne na nusu ambazo ujumbe wa Tume ulitumia pamoja na Bayoumi, muda ambao ulihusisha pia mapumziko ya kwenda kula chakula cha jioni.

Tume hiyo haikuwahi kuona mchoro wa mpangilio wa ndege, video ya mchezo wa paintball, ushahidi wa maandishi kuhusu tuhuma za Bayoumi kuwa na misimamo ya itikadi kali, wala sehemu kubwa ya ushahidi mwingine uliokamatwa na Polisi wa Metropolitan.

Philip Zelikow hakujibu maswali mahususi tuliyomuuliza.

Aliiambia BBC kwamba matokeo ya Tume ya 9/11 yalikuwa yamefanyiwa mapitio na serikali mara mbili, mwaka 2015 na tena mwaka 2021,na kwamba Tume ilikuwa "wazi kuhusu tuhuma na mambo ambayo haikuwa na uhakika nayo."

"Tulikuwa waangalifu linapokuja suala la kumtuhumu mtu yeyote kwa kushiriki katika mauaji ya watu wengi," alisema.

Wizara ya Sheria ya Marekani ilitufahamisha kwamba haiwezi kutoa maoni kuhusu masuala na maamuzi yaliyofanywa miaka 25 iliyopita, yaliyohusisha wafanyakazi ambao kwa sasa hawafanyi kazi tena katika taasisi hiyo.

Mary Galligan, aliyeongoza uchunguzi wa FBI kuhusu mashambulizi ya 9/11, aliwahi kusema kwamba Tume ilikuwa na "ufikiaji wa kila kitu."

Tulijaribu kumtafuta Omar al-Bayoumi kupitia serikali ya Saudi Arabia, lakini hakujibu.

Katika matukio ya awali, amekanusha kwamba alijua Hazmi na Mihdhar walikuwa watekaji nyara, kwamba alikuwa jasusi wa Saudi Arabia, au kwamba alikuwa na uhusiano wowote na mashambulizi ya 9/11.

Ufalme wa Saudi Arabia haukujibu ombi letu la kutoa maoni.

Hapo awali, serikali hiyo ilisema kwamba madai yoyote kwamba Saudi Arabia au maafisa wake walihusika katika mashambulizi ya 9/11 hayana ukweli kabisa.