Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump: Vita vya Iran vinaweza kumalizika baada ya uchaguzi wa Marekani

Kauli hiyo aliitoa akiwa njiani kuelekea Texas kuhudhuria mkutano wa kwanza wa chama chake wa kuelekea uchaguzi huo wa katikati ya muhula, ambao unaweza kubadilisha nguvu ndani ya serikali ya Marekani.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Arsenal haikamatiki, Liverpool yang'ara Madrid katika Ligi ya Mabingwa

    Arsenal imeanza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Napoli, huku nahodha Martin Odegaard akiendelea kuonyesha kiwango bora baada ya kufunga bao pekee la mchezo. Liverpool nayo imeanza vyema kwa kuichapa Atletico Madrid 2-1, huku Barcelona ikiifunga Feyenoord 5-1.

    Paris Saint-Germain imepata ushindi mkubwa zaidi wa usiku huo baada ya kuifunga Slovan Bratislava 6-1. Sporting CP pia imeanza kampeni kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Galatasaray, wakati Stuttgart imeifunga Viking 3-1.

    Ushindi wa Arsenal dhidi ya Napoli ulitokana na bao la Odegaard dakika ya 75, akipiga shuti kali kwa mguu wa kushoto lililomshinda kipa Jan Oblak. Arsenal ilitawala mchezo huo kwa sehemu kubwa na kuondoka na alama zote tatu.

    Kwa upande wa Liverpool, Alexis Mac Allister alifunga bao la ushindi dhidi ya Atletico Madrid, siku moja baada ya kuzungumza kwa hisia kuhusu kutopatiwa mkataba mpya na klabu hiyo. Mchezaji huyo wa Argentina alionyesha thamani yake uwanjani kwa kuisaidia Liverpool kupata ushindi huo wa 2-1.

    Matokeo hayo yanaifanya Arsenal, Liverpool, Barcelona na PSG kuanza hatua ya ligi kwa ushindi, huku Arsenal ikitoa ishara nyingine ya uwezo wake wa kushindania tena mataji makubwa msimu huu.

  2. Iran yashambulia kituo cha Marekani Jordan na kuharibu ndege za kijeshi

    CBS News imeripoti, ikinukuu vyanzo vyenye ufahamu wa moja kwa moja kuhusu tukio hilo, kwamba ndege kadhaa za kijeshi za Marekani ziliharibiwa katika shambulio la makombora ya Iran dhidi ya kituo cha anga cha Mowaffaq Salti nchini Jordan mapema Jumatano asubuhi, kwa saa za huko.

    Vyanzo hivyo, vilivyozungumza bila kutajwa majina kutokana na unyeti wa suala hilo, vilisema takriban ndege nane za kivita aina ya F-15 zilipata uharibifu mdogo, lakini zilirudi katika operesheni baada ya kutengenezwa.

    Vyanzo hivyo pia vilisema ndege ya mashambulizi aina ya A-10 Thunderbolt, inayojulikana kama “Warthog”, ilipoteza moja ya mabawa yake baada ya kugongwa na kombora.

    Kwa mujibu wa CBS, chanzo cha ujasusi kinachofahamu suala hilo kiliwaambia kwamba hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyeuawa katika mashambulizi hayo.

    Mashambulizi hayo yalitokea saa kadhaa baada ya Marekani kusema imezishambulia meli tano za mafuta za Iran, ikisema hatua hiyo ilikuwa ya kujibu shambulio la Iran dhidi ya meli ya kivita ya Jeshi la Wanamaji la Marekani.

    Walinzi wa Mapinduzi ya Iran pia walisema walilenga meli nane za mafuta na meli mbili za kivita za Marekani, pamoja na kituo cha anga cha Mowaffaq Salti nchini Jordan.

    CBS pia iliripoti kwamba majeshi ya Marekani nchini Jordan yalifyatua makombora zaidi ya 30 ya Patriot kuzuia mashambulizi hayo.

  3. Tetesi za Soka Ulaya: Man Utd na Spurs zinamfuatilia Tresoldi

    Manchester United na Tottenham zote zilikuwa na wawakilishi nchini Ubelgiji Jumanne kumtazama mshambuliaji wa Ujerumani Nicolo Tresoldi, 22, wa Club Brugge. (Teamtalk, external)

    Newcastle bado inaweza kumuuza Lewis Hall majira ya joto yajayo licha ya beki huyo wa kushoto wa England mwenye umri wa miaka 22, ambaye hivi karibuni alihusishwa na uhamisho kwenda Manchester United, kuripotiwa kukubaliana mkataba mpya na Magpies hadi 2031. (Talksport, external)

    Lisandro Martinez, 28, atapewa mkataba mpya wa muda mrefu na Manchester United iwapo beki huyo wa kati wa Argentina ataendelea kuwa fiti bila majeraha na kufanya vizuri katika msimu wa 2026-27 huko Old Trafford. (Football Insider, external)

    Brighton wana imani kuwa mkataba mpya wa kiungo wa Sweden Yasin Ayari, 22, unaweza kukubaliwa hivi karibuni huku mazungumzo yakiendelea vizuri. (Teamtalk, external)

    Hata hivyo, mustakabali wa Kaoru Mitoma huko Brighton bado haujulikani, huku winga huyo wa Japan mwenye umri wa miaka 29 akitarajiwa kutoongeza mkataba wake unaomalizika majira ya joto yajayo na anaweza kuondoka mapema katika dirisha la Januari. (Teamtalk, external)

    Baada ya kushindwa kumsajili kiungo wa Ufaransa Manu Kone majira ya joto, Chelsea inaweza kurejea kumsajili mchezaji huyo wa AS Roma, mwenye umri wa miaka 25, mwezi Januari katika dili ambalo pia linaweza kumhusisha winga wa England Jamie Gittens, 22, kuelekea upande mwingine. (Simon Phillips, via CaughtOffside, external)

    Liverpool wana mipango ya kumsajili kiungo mwingine majira ya joto yajayo, jambo ambalo litamshusha zaidi Alexis Mac Allister, 27, kwenye kupata namba katika kikosi huko Anfield. (Talksport, external)

    Atletico Madrid hawana mpango wa kumuuza kiungo wa Hispania, Alex Baena, 25, hivi karibuni licha ya Manchester City kuvutiwa naye (Football Insider, external)

    Beki wa Austria David Alaba anaweza anaswaka na klabu ya Mexico Club Amerika baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 kuondoka Real Madrid majira ya joto. (Fichajes - in Spanish, external)

  4. Trump: Vita vya Iran vinaweza kumalizika baada ya uchaguzi wa Marekani

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema haamini kuwa vita vya Iran vitaisha kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani wa Novemba, akiongeza kuwa bei ya mafuta pia haitashuka hadi wakati huo.

    “Nadhani vita vitaisha mara tu baada ya uchaguzi kwa sababu hawawezi kuendelea tena,” Trump alisema Jumatano, akizungumzia Iran.

    Kauli hiyo aliitoa akiwa njiani kuelekea Texas kuhudhuria mkutano wa kwanza wa chama chake wa kuelekea uchaguzi huo wa katikati ya muhula, ambao unaweza kubadilisha nguvu ndani ya serikali ya Marekani.

    Trump anakabiliwa na kushuka kwa umaarufu katika kura za maoni, pamoja na shinikizo kutoka ndani ya chama chake cha Republican la kutaka amalize vita na Iran.

    Jumatano, bei ya mafuta ilipanda hadi dola 100 (£74) kwa pipa kwa mara ya kwanza tangu Julai, kutokana na kuongezeka kwa mapigano Mashariki ya Kati.

    “Mara tu baada ya uchaguzi, bei ya mafuta itaporomoka,” Trump aliwaambia waandishi wa habari. “Nadhani itachukua muda mrefu kidogo kuliko uchaguzi wa katikati ya muhula.”

    Aliongeza kuwa Iran ilikuwa “imekata tamaa kujaribu kuathiri uchaguzi, ili tupate kundi la watu dhaifu” akionekana kumaanisha chama cha Democrats “na kuwaacha peke yao na kuruhusu wapate silaha zao za nyuklia”.

    Tehran imekanusha mara kwa mara kuwa inatafuta kutengeneza silaha za nyuklia.

  5. Habari na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja leo