Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Faida sita za swala kwa afya ya binadamu
Swala ni nguzo ya pili ya Uislamu na ni wajibu kwa kila Muislamu mwenye akili timamu kutekeleza swala tano za kila siku. Lengo kuu la swala ni kumuabudu Mwenyezi Mungu, kutafuta radhi zake, na kudumisha uhusiano wa karibu kati ya mja na muumba wake.
Mbali na kuwa ibada ya msingi, swala ina hekima na manufaa mengi kwa maisha ya mwanadamu. Huimarisha imani, huleta utulivu wa moyo, na humkumbusha Muislamu kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila hali. Pia huwafundisha Waislamu nidhamu, usafi, uvumilivu, na heshima.
Umuhimu wa swala katika Uislamu
Sheikh Imran Garba Bukar, mhubiri katika Msikiti wa Sultan Bello uliopo Kaduna nchini Nigeria, anasema kuwa baada ya tamko la Shahada, jambo muhimu zaidi katika Uislamu ni swala. Aliongeza kuwa Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake) alieleza kwamba swala ndiyo jambo la kwanza ambalo Mwenyezi Mungu atawahoji watu siku ya kiyama.
Anasema,
"Imepokewa katika kitabu cha Al-Muwatta cha Imam Malik kutoka kwa Umar ibn Al-Khattab kwamba aliwaandikia magavana wake akisema, 'Jambo muhimu zaidi katika mambo yenu mbele yangu ni swala. Mwenye kuhifadhi swala yake ameihifadhi dini yake, na mwenye kuipuuza swala yake atakuwa rahisi zaidi kupuuza mambo mengine ya dini."
Sheikh huyo aliongeza kuwa kadri maisha yanavyoendelea, wataalamu wa afya na wa masuala ya kijamii wanaendelea kugundua mbinu mbalimbali za kumsaidia mwanadamu kudumisha afya yake ya mwili na akili.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa Muislamu, swala tano za faradhi za kila siku tayari zinajumuisha mambo yote hayo. Swala huleta afya, usafi, utulivu wa nafsi, na humsaidia mtu kudumisha ustawi wa mwili, akili na roho kwa wakati mmoja.
Faida za swala kwa mwili, akili na roho
Sheikh Imran Garba Bukar alisema kuwa uchunguzi wa aya za Qurani Tukufu na hadithi za Mtume Muhammad zinaonyesha kwamba swala si ibada ya kutekeleza sheria ya Kiislamu pekee, bali pia ina mchango wa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya binadamu kwa njia nyingi.
Alitaja baadhi ya faida kuu za swala kwa afya ya mwili, utulivu wa nafsi, usafi binafsi na ustawi wa maisha kwa ujumla.
Kinga dhidi ya magonjwa
Sheikh Imran alisema kuwa kabla ya kila swala, Muislamu hutakasa mwili wake kwa kutawadha. Alielezea kuwa kuosha sehemu za mwili ambazo hukumbana mara kwa mara na vumbi na vijidudu kutoka mazingira ya nje, kama vile mikono, mdomo, pua, uso na miguu, angalau mara tano kwa siku, ni njia muhimu ya kudumisha afya na kujikinga dhidi ya magonjwa.
Alinukuu hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim, ambamo Mtume Muhammad alisema,
"Je, mnaonaje kama mmoja wenu angekuwa na mto mbele ya mlango wake na akaoga humo mara tano kila siku, je, ungeacha uchafu wowote mwilini mwake?" Wakasema, "Hapana, usingebaki uchafu wowote." Mtume akasema, "Huo ndio mfano wa swala tano za kila siku, kwa kupitia swala hizo, Mwenyezi Mungu hufuta dhambi."
Kupunguza msongo wa mawazo
Katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na ongezeko la matatizo ya afya ya akili na hofu, Sheikh Imran alisema kuwa swala ni daraja maalumu linalomtenganisha mtu na kelele za dunia ili aweze kusimama mbele ya mungu wake.
Anasema kuwa muda wa swala huipa akili utulivu wa kipekee na huleta amani ya moyo. Qurani Tukufu inaelekeza mahali pa kupata msaada kwa kusema,
"Enyi mlioamini! Tafuteni msaada kwa subira na kwa swala. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri." (Surat Al-Baqarah: 153).
Sheikh Imran aliongeza kuwa utamu na faraja ya swala ndivyo vilivyomfanya Mtume Muhammad kumwambia muadhini wake, Bilal,
"Tupumzishe kwa swala, ewe Bilal."
Mazoezi ya mwili
Mikao inayofanywa wakati wa swala kuanzia kusimama, kurukuu, kusujudu hadi kukaa ni aina ya mazoezi ya mwili.
Sheikh Imran anasema kuwa tafiti za kisayansi zimeonyesha kuwa harakati hizi husaidia kunyoosha misuli ya mwili, kuimarisha magoti, na kulinda uti wa mgongo dhidi ya majeraha.
Aliongeza kuwa katika Surat Al-Fath, aya ya 29, Mwenyezi Mungu anawaelezea waumini kwa kusema:
"Utawaona wakirukuu na wakisujudu, wakitafuta fadhila kutoka kwa Mola wao na radhi Zake." (Surat Al-Fath: 29).
Kulingana na Sheikh Imran, afya njema ya mwili na nguvu za kuendesha maisha ni miongoni mwa neema ambazo Mwenyezi Mungu huwajaalia waumini wake.
Kuboresha mzunguko wa damu
Jambo jingine alilolitaja ni kuwa kusujudu husaidia kuboresha mzunguko wa damu kuelekea kwenye ubongo.
Alisema kuwa kwa upande wa afya ya mwili, wakati wa kusujudu ni muhimu sana. Mtu anapoweka kichwa chake chini, huwa kiko chini kuliko kiwango cha moyo. Hali hii huruhusu damu kutiririka kwa urahisi zaidi kuelekea kwenye ubongo, macho na uso, jambo ambalo linaweza kusaidia kuongeza umakini, kupunguza msongo wa mawazo na kusaidia utendaji mzuri wa mishipa ya damu katika eneo la kichwa.
Sheikh Imran alinukuu hadithi ya Mtume Muhammad iliyopokelewa na Muslim,
"Mja huwa karibu zaidi na Mola wake akiwa katika hali ya kusujudu."
Kuweka mpangilio wa maisha
Sheikh Imran pia alisema kuwa swala husaidia kupanga ratiba ya maisha kwa kuoanisha shughuli za kila siku na nyakati maalumu za ibada. Alieleza kuwa kuswali kwa nyakati zilizowekwa husaidia mwili kufuata mpangilio wa asili wa usingizi na shughuli za kila siku, unaojulikana kisayansi kama mdundo wa saa ya mwili au Circadian Rhythm.
Kulingana naye, kuamka alfajiri na kugawanya shughuli za siku kwa kufuata nyakati za swala hufundisha mtu matumizi mazuri ya muda, husaidia kupunguza uchovu uliopitiliza, na huufanya mwili kubaki wenye nguvu na uchangamfu siku nzima.
Qurani Tukufu inasema,
"Hakika swala imefaradhishwa kwa Waumini kwa nyakati maalumu." (Surat An-Nisa: 103).
Kwa ujumla, Sheikh Imran alisisitiza kuwa swala si njia ya kupata malipo ya Akhera pekee, bali pia ni mfumo wa maisha unaochangia kuboresha afya ya mwili, kuleta utulivu wa akili, kuimarisha nidhamu, na kudumisha usafi wa binafsi hapa duniani.
Jinsi swala inavyoboresha afya
Ili kupata mtazamo wa kitabibu kuhusu suala hili, BBC ilizungumza na Dkt. Umar Sani Ibrahim, daktari katika Hospitali ya Kufundishia ya Barau Dikko, Kaduna. Daktari huyo alisema kuwa swala inaweza kuwa na mchango katika kuboresha afya ya mwili na akili.
Alieleza kuwa kwa kawaida mtu hutumia kati ya dakika 10 hadi 20 kuswali, na kwamba katika sayansi ya mazoezi ya viungo kuna mazoezi ya kiwango cha wastani na yale ya nguvu zaidi.
"Wataalamu wa afya wameeleza kuwa mwili unahitaji mazoezi ya kiwango cha wastani kila siku. Ikiwa mtu ataswali kwa utaratibu na kwa kufanya harakati zote ipasavyo, anaweza kupata kiwango fulani cha mazoezi kinachofanana na kutembea kwa ajili ya mazoezi," alisema.
Dkt. Umar alisema kuwa utafiti uliofanywa katika Chuo Kikuu cha King Saud nchini Saudi Arabia uliwahusisha watu 60. Kati yao, watu 30 walikuwa wakitekeleza swala tano za kila siku kwa kipindi cha miaka mitano, huku watu wengine 30 wakiwa hawakuwa wakitekeleza swala hizo.
Kwa mujibu wake, matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa wale waliokuwa wakiswali walikuwa na nguvu bora za mwili, afya nzuri zaidi ya mfumo wa neva, na walikumbwa na matatizo machache ya mifupa, misuli na viungo ikilinganishwa na wale ambao hawakuswali.
Daktari huyo aliongeza kuwa tafiti nyingine zimeonyesha kuwa swala inaweza kuwa kama tiba kwa nafsi.
"Swala husaidia kuboresha afya ya akili na inaweza kupunguza baadhi ya matatizo ya kiafya bila kutumia dawa. Kwa mfano, inaweza kusaidia kupunguza maumivu ya mgongo na viungo," alisema.
Aidha, alisema kuwa utafiti uliochapishwa katika International Journal of Sport and Science ulionyesha kuwa swala ina manufaa makubwa kwa afya ya binadamu.
Kwa mujibu wake, harakati za kusimama, kurukuu, kusujudu na kukaa wakati wa swala huchangia kuboresha afya ya moyo na mishipa ya damu kwa kuchochea mzunguko mzuri wa damu mwilini.
Dkt. Umar pia alieleza kuwa mtu anapokuwa amesimama au amekaa kwa muda mrefu, mara nyingi huhisi nafuu anaporukuu na kusujudu, kwani harakati hizo husaidia kulegeza mgongo na kupunguza mkazo kwenye viungo vya mwili.
Aliongeza kuwa swala huongeza utulivu wa nafsi, hupunguza msongo wa mawazo, na husaidia kudhibiti upumuaji wakati wa ibada. Pia alisema kuwa swala inaweza kuchangia kupunguza mafuta mwilini na uzito wa mwili, ingawa alisisitiza kuwa ni vyema kuunganisha swala na mazoezi mengine ya mwili ili kupata manufaa makubwa zaidi ya kiafya.