Maghala ya biashara ya mtandaoni Urusi yalengwa katika mashambulizi ya Ukraine
Watu saba wameuawa na wengine 49 kujeruhiwa baada ya ndege zisizo na rubani za Ukraine kushambulia maghala mawili ya kuhifadhi bidhaa yanayomilikiwa na kampuni kubwa zaidi ya Urusi ya biashara ya mtandaoni, Wildberries, kulingana na maafisa wa Urusi.
Vifo vyote na majeruhi 25 kati ya hao yalitokea katika ghala moja jijini Tambov, takriban maili 295 (kilomita 475) kusini-mashariki mwa Moscow. Majeraha mengine 24 yalitokea katika ghala jingine la Wildberries huko Elektrostal, katika eneo la Moscow.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema mashambulizi hayo yalilenga "vituo muhimu vya usafirishaji na ugavi" ambavyo vilikuwa vikitumika "kusambaza vipengele vilivyowekewa vikwazo kwa ajili ya utengenezaji wa ndege zisizo na rubani na vifaa vya urambazaji".
Aliongeza kuwa Ukraine pia ilishambulia maeneo lengwa katika Bahari ya Azov, Bahari Nyeusi, na Crimea, eneo lililochukuliwa na Urusi.
Zelensky alisema operesheni za Ukraine zilikuwa majibu dhidi ya "mashambulizi ya Urusi kwenye miundombinu yetu ya kiraia na kwenye miji na jamii zetu". Katika usiku wa kuamkia Jumatano, watu 14 waliuawa katika mashambulizi ya Urusi kote Ukraine.
Wildberries mara nyingi huchukuliwa kama kampuni ya Urusi inayolingana na Amazon. Kundi la RWB lililoundwa kwa kuunganisha Wildberries na kampuni ya matangazo ya Russ, lilikadiriwa kuwa na thamani ya takriban dola bilioni 12.6 (pauni bilioni 9.3) na jarida la Forbes Russia.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wildberries, Tatyana Kim, alisema ulikuwa "usiku wa kutisha" kwa Urusi na kwa kampuni hiyo.
"Watu saba waliokuwa wakifanya kazi zamu ya usiku walifariki papo hapo," gavana wa eneo la Tambov, Evgeniy Pervyshov, aliandika kwenye Telegram, akiongeza kuwa ndege zisizo na rubani 28 pia zilidunguliwa wakati zikikaribia eneo hilo.
Wakati huo huo, gavana wa eneo la Moscow, Andrei Vorobyov, alisema baadhi ya watu waliojeruhiwa katika mashambulizi kwenye ghala la Wildberries huko Elektrostal walikuwa katika "hali mbaya".
Aliongeza kuwa jumla ya ndege zisizo na rubani 48 zilidunguliwa katika eneo la Moscow usiku huo, na kwamba ghala la mafuta la Urusi pia lilishambuliwa na ndege isiyo na rubani iliyoanguka, tukio ambalo alilielezea kuwa lenye "madhara makubwa zaidi".
"Wazima-moto, huduma za dharura, na Wizara inayosimamia shughuli za udhibiti wa hali za dharura wanaendelea kufanya kazi katika eneo la tukio," aliandika kwenye Telegram.
Hakuelezea kwa kina kiwango cha uharibifu. Zelensky alithibitisha kivyake kuwa Ukraine ilishambulia "kituo cha mafuta".
Soma Zaidi: