Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nani mkali kati ya Messi na Maradona?
Alipoingia uwanjani siku ya Jumatano tarehe 15 mwezi Julai, kucheza dhidi ya England, Lionel Messi hakufunga bao, lakini alikuwa kiungo muhimu katika ushindi wa Argentina wa 2-1 dhidi ya England.
Nyota huyo wa Argentina alitoa pasi mbili za mabao zilizoiwezesha timu yake kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia la 2026.
Katika fainali yake ya tatu, Messi alikuwa anashindania zaidi nafasi ya kushinda taji lake la pili la Kombe la dunia.
Akiwa na umri wa miaka 39, mshambuliaji huyo mwenye jezi namba 10 bado ndiye jina kubwa katika timu ya taifa ya Argentina.
Kwa mara nyingine tena anawania tuzo ya mfungaji bora wa mashindano hayo, huku akiendelea kuongeza rekodi nyingi alizojikusanyia katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili ya maisha yake ya soka.
Kwa wachambuzi wengi, Kombe la Dunia linalofanyika nchini Marekani, Mexico na Canada linawakilisha sura nyingine katika safari ya mchezaji ambaye tayari amejiweka katikati ya mjadala mkubwa zaidi katika soka, Je, Messi ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea?
Swali hilo limemuandama Messi kabla hata ya kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022. Hata hivyo, nchini Argentina mjadala huo umechukua sura ya kipekee. Kwa miaka mingi, ulinganisho umekuwa kati yake na Diego Maradona, nahodha aliyeiongoza Argentina kushinda Kombe la Dunia mwaka 1986 na mtu ambaye ushawishi wake unapita mipaka ya mchezo wa soka.
"Maradona alikuwa mfalme wa Argentina. Na mfalme hachaguliwi, bali anaiwakilisha nchi yake," anasema mwandishi wa habari wa Hispania Guillem Balagué, mmoja wa waandishi wakuu wa wasifu wa Messi, katika mahojiano na BBC Brazil.
Mitazamo kuhusu Messi ilianza kubadilika baada ya ushindi wa Copa América mwaka wa 2021 na Kombe la Dunia la Qatar, wakati Messi alipoiongoza Argentina kushinda taji lao la tatu la dunia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Balagué, ushindi huo haukumaliza kabisa mjadala huo.
"Leo Messi tayari amempita Maradona kama mchezaji wa soka. Lakini bado kutakuwa na Waargentina ambao wataendelea kusema kuwa Maradona ndiye aliyewakilisha taifa hilo vizuri zaidi."
Ni zaidi ya soka
Kama takwimu zingekuwa ndizo pekee za kuamua nani ni mchezaji bora zaidi katika historia ya soka, huenda mjadala huo ungekuwa tayari umekwisha.
Messi ndiye mchezaji mwenye tuzo nyingi zaidi za Ballon d'Or katika historia.
Ameshinda karibu kila taji linalowezekana akiwa na Barcelona, Paris Saint-Germain, Inter Miami na timu ya taifa ya Argentina. Amenyakua mataji ya Copa América na Kombe la Dunia, na anashikilia rekodi nyingi za mabao na pasi za mabao au assist akichezea klabu na timu ya taifa ya Argentina.
Hata hivyo, kwa miaka mingi, Waargentina wameendelea kumweka Maradona juu yake.
Kwa mujibu wa Guillem Balagué, mwandishi wa habari wa Hispania ambaye amefuatilia maisha ya Messi kwa zaidi ya miongo miwili na kuandika wasifu kuhusu mchezaji huyo mwenye jezi namba 10, anasema ni kwasababu Maradona alikuwa ishara ya utambulisho wa Argentina.
Maradona aliiwakilisha Argentina kando na kuwa mchezaji nyota.
"Alitoka katika familia ya hali ya chini, alipinga mamlaka yoyote, angeweza kumwambia Papa au rais kile alichofikiria. Alikuwa mtu asiyeogopa kusema, alikuwa na kipaji kikubwa, na alikuwa na mchanganyiko wa ujasiri na mvuto ambao Waargentina wengi wanaona kama sehemu ya utambulisho wao wenyewe."
Messi alifuata njia tofauti.
Ni mtu wa kimya nje ya uwanja, asiye na tabia ya kutoa kauli za kisiasa na asiye na hamu kubwa ya kujijengea taswira ya umma, alitumia sehemu kubwa ya maisha yake ya soka akisema kwamba alitaka tu kucheza mpira.
Tofauti hii pia inaonekana katika mtazamo wa mchezaji wa zamani wa Australia Craig Foster.
Katika mahojiano na gazeti la Uingereza The Guardian, Foster alisema kwamba alimpenda Maradona zaidi kwa sababu Muargentina huyo "alisema mawazo yake"
"Simpendi Messi kama nilivyompenda Maradona kwa sababu yeye hafungui kinywa chake kamwe. Ni kama David Beckham au Cristiano Ronaldo, wanamichezo wa kisasa ambao hawasemi chochote kuhusu mambo mengine. Ni kana kwamba dunia nje ya soka haipo," Foster aliambia The Guardian.
Baada ya ushindi wa Copa América mwaka 2021, na hasa baada ya kutwaa Kombe la Dunia nchini Qatar, Waargentina wengi walianza kuona sifa mpya ndani ya nahodha wao.
Wakati wa Kombe hilo la Dunia, Messi alionyesha matukio ambayo haikuwa kawaida kwa mtu aliyejenga taswira ya kuwa kiongozi wa kimya alibishana na wapinzani, aliwachokoza wapinzani, na akaonyesha hisia nyingi ambazo watu wengi walizihusisha zaidi na Maradona.
"Alionyesha sura mpya za utu wake. Alianza kuonekana kama jenerali wa timu, jambo ambalo pia lilitokea kwa Maradona," anasema Balagué.
Mchezo tofauti
Mchezo wa soka umebadilika sana katika kipindi cha miongo mitano iliyopita.
Wakati Pelé aliposhinda Kombe lake la kwanza la Dunia mwaka 1958, wachezaji bado walikuwa wakisafiri kwa ndege za kawaida za kibiashara, walicheza kwenye viwanja ambavyo mara nyingi havikuwa na ubora sawa, hawakuwa na msaada wa teknolojia ya video, na maandalizi ya kimwili yalikuwa katika kiwango ambacho leo kinaonekana kuwa cha msingi sana.
Katika enzi ya Maradona, miaka ya 1980, soka tayari ilikuwa mchezo maarufu duniani, lakini bado ilikuwa mbali na kuwa sekta yenye thamani ya mabilioni ya dola ambayo ilikuja kuimarika katika miongo iliyofuata.
Messi, kwa upande mwingine, amejenga maisha yake yote ya soka katika mazingira tofauti kabisa.
Vilabu vimebadilika na kuwa kama mashirika makubwa ya kimataifa, mapato kutokana na matangazo ya televisheni na udhamini yameongezeka kwa kiwango kikubwa, huku idara za afya na uchambuzi wa utendaji zikianza kufuatilia kila kipengele cha maandalizi ya wanamichezo.
Wataalamu wa lishe, wanasaikolojia, wataalamu wa fiziolojia, na wataalamu wa kurekebisha majeraha ya mwili wameongeza muda wa kazi wa wachezaji, ambao zamani mara nyingi zilikuwa zikimalizika mapema zaidi.
Teknolojia pia imebadilisha namna mchezo unavyochezwa na kuchambuliwa.
Leo karibu kila mechi hurekodiwa kwa kutumia kamera nyingi, jambo linalowezesha uwepo wa uchambuzi wa kina wa uwezo wa mchezaji na kupunguza nafasi ya matukio ambayo zamani yangepita bila kuonekana.
Mfumo wa VAR umebadilisha maamuzi ya refa, huku takwimu za kisasa zikianza kupima kila kitu kuanzia shinikizo analoweka mchezaji bila mpira hadi uwezekano wa kufunga bao.
Je kuhusu Pele?
Pelé na Maradona walicheza katika enzi ambayo mechi zao nyingi hata hazikuwa zikionyeshwa kimataifa kwenye televisheni. Messi, kwa upande mwingine, karibu maisha yake yote ya soka yamerekodiwa kwa ubora wa juu, yakichambuliwa moja kwa moja na wataalamu, mitandao ya kijamii, na mamilioni ya mashabiki.
Mshambuliaji wa zamani Ronaldo pia hivi karibuni alisema kuwa jaribio la kubaini nani alikuwa mchezaji bora zaidi linategemea kwanza kabisa vigezo vinavyotumika.
Katika mahojiano na Romário TV, mshambuliaji huyo wa zamani wa Brazil alisema kuwa Messi ni "mwenye kipaji kikubwa sana" na yuko miongoni mwa wachezaji watano bora zaidi katika historia kwake, lakini alisema hajui kama Muargentina huyo amempita Maradona.
"Tunapaswa kupata kigezo cha kujadili jambo hili. Tunawezaje kuchagua bila kuwa na kigezo?" alisema.
Je, inawezekana kuwalinganisha wachezaji waliotengana kwa zaidi ya nusu karne, waliocheza chini ya sheria tofauti, ratiba tofauti, mifumo tofauti ya mazoezi, na hata matarajio tofauti kabisa kutoka kwa jamii?
Ni nini kinachomfanya Messi kuwa bora?
Ingawa hakuna makubaliano kuhusu nani alikuwa mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea, kuna hoja kadhaa zinazojitokeza mara kwa mara miongoni mwa wale wanaomweka Messi kileleni.
Hoja ya kwanza ni muda aliodumu akiwa kileleni.
Muda wa Pelé na Maradona kama wachezaji haukudumu kwa muda mrefu sana.
Messi ameendelea kuwa miongoni mwa wachezaji bora duniani kwa takriban miongo miwili, akishinda mataji ya kitaifa, ya bara na kimataifa katika hatua mbalimbali za maisha yake ya soka.
Kudumu huko mara nyingi hutajwa kuwa moja ya nguvu zake kubwa. Lakini pia unaonyesha jinsi soka lilivyobadilika.
Kulingana na Thierry Henry, ushindani wa hali ya juu ulimsaidia Messi kudumisha kiwango chake
Katika mahojiano yaliyochapishwa na gazeti la Hispania Marca, Henry alikumbuka mazoezi yao katika klabu ya Barcelona na kusema kwamba kilichohitajika tu ni Messi kuhisi ametendewa vibaya ndipo angebadilika kabisa na kuonyesha upande wake wa ushindani.
Katika mahojiano na Radio Villa Trinidad ya Argentina mwaka 2021, mchezaji wa zamani wa Brazil Tostão alisema kuwa Messi tayari amempita Maradona, lakini bado yuko nyuma ya Pelé.
"Nimekuwa na mtazamo huu kwa miaka mingi. Messi, baada ya Pelé, ndiye mchezaji bora zaidi katika historia. Yuko juu ya Maradona kwa sababu amekuwa na maisha marefu zaidi ya soka," alisema.
Kwa Tostão, tofauti kubwa kati ya Pelé na Messi iko katika uwezo wao wa kimwili.
"Tofauti pekee kati ya Pelé na Messi ni kwamba Pelé alikuwa na nguvu zaidi kimwili na alikuwa mkali zaidi. Messi yuko sawa na Pelé katika kipaji," alisema.
Pelé, Maradona na Messi walicheza katika nyakati tofauti, chini ya sheria tofauti, kwenye ratiba tofauti, na katika mchezo ambao umefanyiwa mabadiliko makubwa katika miongo michache iliyopita.
Pelé alisaidia kueneza mtindo wa soka duniani wakati mchezo huo ulikuwa bado unaanza kujijenga kama burudani ya kimataifa.
Maradona aligeuka kuwa alama ya michezo, siasa na utamaduni katika Argentina iliyokuwa ikipitia migogoro na mabadiliko makubwa.
Messi amejenga mafanikio yake katika enzi ya utandawazi, sayansi ya michezo, na uwepo mkubwa wa mitandao ya kijamii.
Ni mchanganyiko huu wa mazingira tofauti ndio unaofanya jibu la nani ndiye mchezaji bora zaidi kuwa gumu kupatikana.