Mwili wa mwanamke wa tisa wapatikana huku polisi Afrika Kusini wakichunguza mfululizo wa vifo

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Polisi nchini Afrika Kusini wamethibitisha kupatikana kwa mwili wa tisa wa mwanamke ndani ya kipindi cha miezi miwili, huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu mfululizo wa vifo visivyoeleweka mashariki mwa Johannesburg.
Mwathiriwa wa hivi karibuni alipatikana akiwa amevua sehemu ya nguo na amefunikwa kwa shuka kando ya barabara katika eneo la Dawn Park, Alhamisi asubuhi, polisi wamesema. Utambulisho wake bado haujatangazwa.
Ugunduzi huo unafuatia vifo vya wanawake wengine wanane ambao miili yao imepatikana tangu mwezi Julai katika maeneo mbalimbali ya Ekurhuleni, eneo kubwa la mijini mashariki mwa Johannesburg.
Baadhi ya wanawake hao walipatikana wakiwa wamevuliwa sehemu ya nguo na wakiwa na majeraha, lakini polisi wamesisitiza kuwa bado hawajabaini ikiwa vifo vyote vina uhusiano au ikiwa muuaji wa watu mfululizo ndiye anayehusika.
Rais Cyril Ramaphosa ameahidi kwamba "hakuna jiwe litakaloachwa bila kugeuzwa" katika kuwatafuta waliohusika na mauaji hayo, ambayo alisema "yanasababisha hofu na sintofahamu katika jamii zetu".
Miongoni mwa waathiriwa alikuwa Elizabeth "Tsontso" Moselakgomo mwenye umri wa miaka 38, ambaye alipotea wiki iliyopita baada ya kuondoka nyumbani kwake kwa ajili ya kukimbia mchana. Mwili wake ulipatikana siku tatu baadaye nyuma ya hoteli huko Kempton Park.
Waathiriwa wengine wawili wametambuliwa kuwa Itumeleng Kekana, ambaye alikuwa ameripotiwa kutoweka tangu mwezi Julai, na Dineo Evelyn Motapane mwenye umri wa miaka 38, ambaye mwili wake ulipatikana kando ya barabara huko KwaThema siku ya Jumanne.
Mwili wa kwanza kati ya miili hiyo tisa uligunduliwa Kempton Park tarehe 15 Julai. Mtuhumiwa alikamatwa siku mbili baadaye kuhusiana na kisa hicho na bado yuko kizuizini, lakini polisi hawajamhusisha mtuhumiwa huyo na vifo vingine.


























