Picha zafichua uharibifu mkubwa katika kambi za Marekani uliosababishwa na Iran

.

Chanzo cha picha, CBS News

Maelezo ya picha, Picha isiyo na tarehe inaonyesha gari ambalo liliripotiwa kuharibiwa katika shambulio la Iran dhidi ya Kambi ya Buehring nchini Kuwait.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Picha zilizotolewa na CBS, ambayo ni mshirika wa BBC nchini Marekani, zinaonyesha uharibifu mkubwa katika vituo mbalimbali vya Marekani Mashariki ya Kati kutokana na mashambulizi ya Iran.

Picha hizo, zilizotolewa na wanajeshi waliopo kazini, zinaonyesha mfumo wa rada uliokatika, trela zilizopondwa, na majengo yaliyoharibiwa vibaya.

Picha hizo, ambazo hazina tarehe, zilipigwa katika kambi na vituo vya Marekani nchini Saudi Arabia na Kuwait.

Mwanajeshi mmoja, ambaye utambulisho wake haukufichuliwa na CBS, alisema: "Huu ni uharibifu mkubwa kwa kambi zetu ambao haujafahamishwa kwa umma wa Marekani."

"Tumesimama, huku macho yetu yakiwa yamefumbwa, tukipokea ngumi usoni," alilalamika.

Ikulu ya White House iliishauri BBC kuwasiliana na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom), ambayo haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.

Uharibifu huo, kwa picha

Picha hizo, ambazo hazijathibitishwa na chombo huru kama vile BBC, zilichapishwa siku moja baada ya ripoti ya chombo cha uangalizi cha Pentagon kuthibitisha kuwa mamia ya majengo na miundombinu katika kambi za Marekani Mashariki ya Kati vilikuwa vimeharibiwa au kusambaratishwa na Iran.

Mojawapo ya picha hizo inaonyesha ndege aina ya Boeing E-3 Sentry iliyoharibiwa katika Kambi ya Jeshi la Anga ya Prince Sultan nchini Saudia.

.

Chanzo cha picha, CBS News

Maelezo ya picha, Picha isiyo na tarehe ya ndege aina ya Boeing E-3 Sentry iliyoharibiwa katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Prince Sultan nchini Saudi Arabia, takriban kilomita 100 kusini-mashariki mwa mji mkuu, Riyadh.

Ingawa picha hiyo haina tarehe, BBC Verify ilikuwa tayari imethibitisha mnamo mwezi Machi kuwepo kwa picha inayofanana na hiyo, ambayo inaonekana kutoka kwenye ndege hiyo hiyo ya rada.

Ndege za Boeing E-3 AWACS hutumiwa kutambua na kufuatilia shabaha zinazoweza kulengwa kutoka umbali mrefu, na kutoa tahadhari ya mapema kuhusu vitisho vinavyoweza kutokea.

Wakati huo, afisa mmoja wa Marekani aliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanajeshi 12 wa Marekani walijeruhiwa wawili kati yao vibaya katika shambulio la Iran dhidi ya kambi hiyo ya jeshi la anga.

Picha mbili zisizo na tarehe, zinazodaiwa kupigwa katika Kambi ya Buehring nchini Kuwait, zinaonyesha trela zilizopondwa na muundo mkubwa unaofanana na hema ambao umeharibiwa vibaya na kubaki vipande vipande, huku moshi ukifuka kutoka eneo hilo.

.

Chanzo cha picha, CBS News

.

Chanzo cha picha, CBS News

Maelezo ya picha, Picha isiyo na tarehe inaonyesha moshi ukifuka kutoka kwenye jengo lililoharibiwa katika shambulio la Iran kwenye Kambi ya Buehring, Kuwait.

Picha nyingine inaonyesha jengo la ghorofa nne lililoharibiwa na shambulio la Iran katika Kambi ya Arifjan, pia nchini Kuwait.

Uharibifu wa miundombinu hiyo, ikiwa ni pamoja na vifaa vya mawasiliano ya satelaiti, uliripotiwa mwezi Machi, ingawa haijulikani wazi ikiwa picha hii inahusiana na shambulio hilo hilo.

Brian Katulis, afisa wa zamani wa usalama wa taifa aliyewahi kuhudumu katika serikali za vyama vya Democrats na Republicans, alisema uharibifu unaoonekana kwenye picha hizo unaonyesha kuwa "Marekani haikuandaa vyema mifumo yake ya ulinzi."

"Na kuna ushahidi thabiti kwamba maadui wa Marekani, kama vile China na Urusi, huenda walisaidia Iran kuchagua maeneo yaliyolengwa," aliongeza Katulis, ambaye kwa sasa ni mtafiti mkuu katika Taasisi ya Mashariki ya Kati (Middle East Institute).

"Serikali ya Trump haijachukua hatua yoyote kushughulikia udhaifu huo."

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hasara ya mamilioni ya dola

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Picha hizo zilitolewa muda mfupi baada ya ripoti ya chombo cha uangalizi cha Pentagon kufichua kuwa mashambulizi ya Iran "yaliharibu na kubomoa mamia ya majengo na miundombinu katika kambi za Marekani nchini Kuwait, Bahrain, Qatar, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Iraq, Oman na Jordan wakati wa mzozo huo."

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa hasara ya vifaa ilifikia dola bilioni 3.7 za Marekani.

Kwa ujumla, Marekani ilikuwa imetumia dola bilioni 33.4 za Marekani katika vita hivyo kufikia tarehe 29 Juni, kulingana na ripoti hiyo.

Katika miezi iliyofuata kuanza kwa vita hivyo, "ndege nyingi za Marekani ziliharibiwa ," ripoti hiyo inaendelea kusema.

Hati hiyo inaorodhesha baadhi ya ndege zilizoathirika, ikiwa ni pamoja na ndege tano za kuongeza mafuta angani ambazo ziliharibiwa zikiwa ardhini nchini Saudi Arabia kutokana na silaha za Iran.

Ripoti huru kutoka Ofisi ya Bajeti ya Bunge la Marekani (CBO) inaonyesha kuwa ndege aina ya E-3 haitengenezwi tena na ingehitaji kubadilishwa na ndege nyingine ya kisasa zaidi yenye uwezo sawa: E-7.

CBO ilionyesha kuwa gharama ya ndege moja ya E-3 ni dola milioni 500 za Marekani na kwamba jumla ya makadirio ya gharama ya vifaa vilivyopotea vitani, ikiwa ni pamoja na, ndege zisizo na rubani (drones) na mfumo wa ulinzi wa eneo la juu (THAAD), inafikia dola bilioni 1.9 za Marekani.

Shirika hilo lilionyesha kuwa uchambuzi wake unaweza kuwa na "kutokuwa na uhakika," kwani Idara ya Ulinzi haikujibu maombi yake ya kupata taarifa, jambo lililolilazimisha kutegemea hifadhidata za serikali na ripoti za umma.

Aidha, kulingana na ripoti hiyo, ukubwa wa kazi za ukarabati na ujenzi ambazo jeshi la Marekani linapanga kufanya hauko wazi.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Brian Katulis wa Taasisi ya Mashariki ya Kati (Middle East Institute) alibainisha kuwa, ingawa "gharama hizi zinaonyesha jinsi utawala wa Trump ulivyopoteza rasilimali muhimu za kijeshi bila kupata matokeo ya maana," madhara makubwa zaidi yalikuwa kwa utayari wa jumla wa kijeshi wa Marekani.

"Marekani ililazimika kuhamisha rasilimali za kijeshi kutoka Asia hadi Mashariki ya Kati, jambo lililoiacha nchi hiyo na washirika wake wa Asia katika hali ya hatari zaidi na urahisi wa kushambuliwa na China," alidai.

Aliongeza kuwa "zaidi ya hayo, kupungua kwa akiba ya zana za kivita za Marekani kunaiweka Urusi katika hali ya kutaka zaidi kujaribu udhaifu wa washirika wa NATO na kuendeleza vita vyake vya uchokozi dhidi ya Ukraine."

Ingawa Marekani ina uwezo wa kifedha wa kukabiliana na upungufu wa vifaa, tayari inakabiliwa na matatizo ya bajeti na huenda isiweze kuchukua hatua za haraka za kuvibadilisha vifaa vilivyopotea ili kujiandaa kwa uwezekano wa kuzuka kwa migogoro Mashariki ya Kati au kwingineko duniani, aliongeza.

Shinikizo la kumaliza vita

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kadiri miezi ilivyopita, shinikizo la umma na la kisiasa limeongezeka dhidi ya Ikulu ya Marekani (White House) kuhitimisha mgogoro na Iran, ambao ulianza tarehe 28 Februari wakati Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya nchi hiyo.

Tangu kuanza kwa vita hivyo, Iran imeshambulia mara kwa mara kambi za Marekani na nchi washirika katika eneo la Ghuba, pamoja na Israel.

Usiku wa Jumanne, Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipiga kura kwa mara ya tatu kuhitimisha vita dhidi ya Iran, likipitisha azimio litakalolazimisha Rais Donald Trump kusitisha hatua za kijeshi za Marekani iwapo hatakuwa na idhini ya Bunge.

Azimio hilo lilipitishwa kwa uungwaji mkono wa baadhi ya wabunge wa chama cha Republican, katika hatua ambayo inaweza kuwa kura ya mwisho ya Baraza hilo kuhusu suala hilo kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba.

Kupitishwa kwake kunakabiliwa na hali ya kutokuwa na uhakika, kwani Seneti ya Marekani haijaonyesha kama italishughulikia suala hilo.

Siku hiyo hiyo, mbunge wa Republican Thomas Massie alitangaza mpango wa kuanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth, huku taarifa mpya zikijitokeza kuhusu gharama ambazo Marekani imeingia kutokana na vita dhidi ya Iran.

Utawala wa Trump ulimuunga mkono Hegseth, na Mwanasheria Mkuu wa Marekani Todd Blanche aliwaambia waandishi wa habari kuwa anafanya "kazi ya kipekee."