Makumi ya meli zimepita Mlango Bahari wa Hormuz baada ya Marekani na Iran kusaini makubaliano

Hata hivyo, idadi hiyo bado iko chini ya wastani wa kabla ya mzozo huo, ambapo takriban meli 138 zilikuwa zikivuka kila siku.

Muhtasari

Skip Video and continue reading
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisa matangazo yetu ya moja kwa moja

  2. Makumi ya meli zimepita katika Mlango Bahari wa Hormuz baada ya Marekani na Iran kusaini makubaliano

    .

    Kwa mujibu wa data mpya kutoka kampuni ya ujasusi wa masuala ya baharini Kpler, takriban meli 172 zimevuka kupitia njia hiyo tangu tarehe 18 Juni, siku iliyofuata kusainiwa kwa makubaliano hayo. Kati ya hizo, meli 42 zilivuka siku ya Jumamosi pekee.

    Hata hivyo, idadi hiyo bado iko chini ya wastani wa kabla ya mzozo huo, ambapo takriban meli 138 zilikuwa zikivuka kila siku.

    Takwimu za ufuatiliaji wa meli zilizochambuliwa na BBC Verify zinaonyesha kuwa zaidi ya meli 200 za kusafirisha mafuta zinaonekana kusubiri ndani ya mlango wa bahari huo kufikia Jumanne, huku takriban meli 10 zikiwa zimeanza kuelekea magharibi kuingia katika Ghuba ya Uajemi.

    Wakati huo huo, bei ya mafuta ghafi duniani imeshuka hadi kiwango chake cha chini zaidi tangu vita hivyo vilipoanza.

    Soma Zaidi:

  3. Israel inafanya mauaji ya kimbari Gaza kwa kulenga watoto kwa makusudi - UN

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa Israel imelenga kwa makusudi watoto wa Kipalestina, jambo ambalo limechangia kutokea kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita katika Ukanda wa Gaza, pamoja na uhalifu wa kivita katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Ripoti mpya ya tume hiyo inadai kuwa mamlaka na vikosi vya usalama vya Israel "vimefanya kwa makusudi vitendo vilivyosababisha vifo na madhara makubwa ya kimwili na kisaikolojia kwa mamia ya maelfu ya watoto wa Kipalestina".

    Ripoti hiyo inaongeza kuwa mauaji hayo yaliendelea hata baada ya kusitishwa kwa mapigano huko Gaza mnamo mwezi Oktoba mwaka jana.

    Tume hiyo imesema ina misingi ya kuridhisha kuhitimisha kwamba vitendo hivyo "ni sehemu ya mkakati wa makusudi wa kuharibu mustakabali wa Wapalestina wa Gaza kwa kuwalenga watoto wao".

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imekataa vikali ripoti hiyo, ikiitaja kuwa "ya uongo na ya kashfa", na kuiita "kipande cha propaganda kisicho na msingi kama ripoti zake zilizopita".

    Jeshi la Israel lilianzisha operesheni ya kijeshi huko Gaza kufuatia shambulio lisilo la kawaida lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na 251 kutekwa nyara.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, watu wasiopungua 73,035 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu wakati huo, wakiwemo zaidi ya watoto 21,280. Takwimu hizo zinachukuliwa kuwa za kuaminika na Umoja wa Mataifa.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Kupunguzwa kwa ufadhili wa HIV Afrika Kusini kunaweza kupoteza maisha - UN

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mpango wa Marekani wa kusitisha ufadhili wa miradi ya kukabiliana na Virusi vya Ukimwi (HIV) na Ukimwi nchini Afrika Kusini utadhuru watu wengi.

    Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la UNAIDS, Winnie Bya-nyima, amesema amesikitishwa na uamuzi huo na kuitaka Marekani kuufikiria upya.

    Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kupunguzwa kwa ufadhili huo kunahusishwa na kile ilichokiita kushindwa kwa Afrika Kusini kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya sera yaliyotolewa na utawala wa Rais Donald Trump.

    Mpango wa Marekani umekuwa ukiipatia Afrika Kusini zaidi ya dola milioni 400 za Marekani kwa mwaka, fedha ambazo zimekuwa zikigharamia maelfu ya wahudumu wa afya.

    Afrika Kusini ina takriban watu milioni nane wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.

    Soma Zaidi:

  5. Hatua zilizochukuliwa kukabiliana na Ebola DRC zaonyesha ufanisi - WHO

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema visa vya Ebola vilivyothibitishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo vimezidi vile vilivyoripotiwa katika mwezi wa kwanza wa mlipuko mwingine wowote wa ugonjwa huo.

    Zaidi ya visa 1,000 vimethibitishwa, huku watu 267 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

    Wagonjwa 100 wamepona hadi kufikia sasa.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema hali hiyo inaonyesha ufanisi wa hatua za dharura zilizochukuliwa kukabiliana na mlipuko huo.

    Amesema juhudi sasa zinaelekezwa katika kupanua vituo vya matibabu, kuimarisha uwezo wa maabara na mifumo ya ufuatiliaji wa maambukizi, pamoja na kutoa mafunzo kwa wahudumu zaidi wa afya.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Familia ya rais wa zamani wa Zambia yashinda vita vya kisheria juu ya atakapozikwa Lungu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mahakama ya Rufaa ya Afrika Kusini imeamua kwamba rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, anaweza kuzikwa nchini Afrika Kusini kulingana na matakwa ya familia yake.

    Hata hivyo, bado haijulikani iwapo uamuzi huo uliotolewa Jumanne na Mahakama Kuu ya Rufaa mjini Bloom-fon-tein utakuwa mwisho wa mzozo wa kisheria kuhusu hatima ya mwili wake, kufuatia uhasama wa muda mrefu kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema.

    Macho yote sasa yanaelekezwa kwenye hatua itakayochukuliwa na serikali ya Zambia, huku mawakili wake wakisubiri maelekezo kuhusu hatua zinazofuata.

    Kwa muda mrefu, serikali ya Zambia imekuwa ikisisitiza kwamba, kwa kuwa alikuwa mkuu wa zamani wa nchi, Lungu anapaswa kupewa heshima za kitaifa na kuzikwa nchini Zambia.

    Serikali ilitaka azikwe pamoja na marais wengine waliotangulia katika eneo maalumu la mazishi ya marais lililopo katika mji mkuu, Lusaka.

    Hata hivyo, familia ya Lungu ilitaka mazishi yawe ya faragha baada ya mazungumzo na serikali kuhusu maandalizi ya mazishi kuvunjika bila makubaliano.

    Agosti mwaka uliopita, Mahakama Kuu ya Afrika Kusini mjini Pretoria iliamua kwamba serikali ya Zambia inaweza kurejesha mwili wake na kumpa mazishi ya kitaifa, uamuzi ambao uliwaacha jamaa wa Lungu wakiwa wamefadhaika.

    Familia hiyo ilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, lakini katika tangazo la kushtukiza mwezi wa Aprili, serikali ya Zambia ilisema kwamba mwili wa Lungu ulikuwa ume “hamishwa rasmi” na kukabidhiwa serikali na mahakama ya Afrika Kusini.

    Hata hivyo, saa chache baadaye, mahakama hiyo hiyo ya Afrika Kusini iliagiza serikali ya Zambia kurudisha mwili huo hadi suala hilo lisikilizwe tena mahakamani.

    Rais huyo wa zamani alifariki kutokana na ugonjwa ambao haukufahamika akiwa na umri wa miaka 68 katika kliniki ya Pretoria. Machafuko yalitokea kufuatia kifo chake, huku waombolezaji wakipokea taarifa zinazokinzana kutoka kwa serikali na chama chake cha kisiasa, Patriotic Front (PF).

    Lungu aliongoza Zambia kuanzia mwaka wa 2015 hadi 2021, na katika kipindi hicho alikuwa na migogoro ya mara kwa mara na Hichilema, ambaye kwa miaka mingi alikuwa kiongozi wa upinzani kabla ya kumshinda mpinzani wake huyo katika uchaguzi.

    Baada ya kifo cha Lungu, familia yake ilisema kwamba rais huyo wa zamani hakutaka Hichilema kuhudhuria mazishi yake wala “kuwa karibu kwa namna yoyote” na mwili wake.

  7. Wachezaji 3 wa Ghana ambao England wanapaswa kuwa makini nao

    Ghana ilikuwa na maandalizi yenye changamoto kuelekea Kombe la Dunia baada ya kocha Otto Addo kufutwa kazi kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya, siku 72 tu kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

    Kocha mwenye uzoefu mkubwa Carlos Queiroz aliteuliwa kuchukua nafasi hiyo, akiongoza timu yake ya tano mfululizo katika Kombe la Dunia baada ya michuano na timu za taifa za Ureno na Iran.

    Bila shaka atafurahishwa na mwanzo mzuri wa timu yake, ambapo ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Panama uliibua matumaini ya Ghana kufuzu kwa hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza tangu safari yao ya kihistoria hadi robo fainali mwaka 2010.

    BBC Sport inaangazia wachezaji watano muhimu ambao England wanapaswa kuwa waangalifu nao.

    Antoine Semenyo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Klabu: Manchester City

    Umri: Miaka 26Nafasi: WingaMechi za Kimataifa: 35Mabao: 3

    Unapozungumzia kikosi hiki cha Ghana, ni vigumu kutomuanza na nyota wao mkubwa, winga wa Manchester City, Antoine Semenyo.

    Aliwasili kwenye Kombe la Dunia akiwa katika kiwango bora baada ya kumaliza wa tatu katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya England msimu wa 2025–26, akiwa amefunga mabao 17 kupitia vipindi vyake vya kuchezea Bournemouth na Manchester City.

    Alizoea haraka maisha katika Uwanja wa Etihad baada ya kuhamia Manchester City baada ya kuhamia huko kwa ada ya pauni milioni 65 mnamo mwezi Januari, na akasaidia klabu hiyo kutwaa mataji mawili.

    Pia alifunga bao la ushindi katika fainali ya Kombe la FA, jambo lililoimarisha hadhi yake kama mmoja wa wachezaji hatari zaidi wa Ghana.

    Caleb Yirenkyi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Klabu: NordsjaellandUmri: Miaka 20Nafasi: Kiungo wa Kati (Midfielder)Mechi za Kimataifa: 12Mabao: 2

    Mmoja wa viungo vijana wanaotafutwa sana barani Ulaya, Yirenkyi aliongeza thamani yake baada ya kufunga bao la ushindi katika dakika ya 94 kwenye mechi ya ufunguzi ya Ghana dhidi ya Panama.

    Kocha wa zamani wa Black Stars, Otto Addo, alikuwa akimtumia kiungo huyu mwenye uwezo wa kucheza sehemu nyingi kama beki wa kulia, nafasi ambayo si yake ya asili.

    Hata hivyo, kocha mpya Carlos Queiroz amemrudisha katika nafasi ya kiungo wa kati, ambako ameonyesha ubora mkubwa zaidi akiwa klabuni kwake.

    Jordan Ayew

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Klabu: Hana klabu (Unattached)Umri: Miaka 34Nafasi: Mshambuliaji / Kiungo mshambuliajiMechi za Kimataifa: 121Magoli: 34

    Jordan Ayew alikua mchezaji mwenye rekodi ya juu zaidi ya mechi za kimataifa katika mechi ya ufunguzi ya Ghana dhidi ya Panama, akimpita ndugu yake Andre Ayew aliyekuwa na rekodi ya mechi 120.

    Alipoteuliwa kuwa nahodha wa Ghana mwaka 2025,

    Alijiunga na historia ya familia yao maarufu ya soka ya ‘Nyota’ akiwa pamoja na baba yake mashuhuri Abedi Pelé na ndugu yake Andre—wote wakipata nafasi ya kuongoza Black Stars kama manahodha.

  8. Idadi ya waliokufa kwa wimbi la joto kali yaongezeka Ufaransa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watu 40 wamekufa kutokana na wimbi la joto kali nchini Ufaransa tangu Alhamisi iliyopita, Waziri Mkuu Sébastien Lecornu amesema, huku halijoto ikifikia viwango vya rekodi ya juu katika miji kadhaa mikubwa na joto hilo kufikia kilele katika nchi kadhaa za Ulaya.

    "Sio jambo la kuchukuliwa kirahisi, kuogelea katika maeneo yasiyodhibitiwa wakati wa wimbi la joto," Waziri wa Michezo na Vijana Marina Ferrari aliambia redio ya Ufaransa.

    Ufaransa, pamoja na Uhispania na Italia, zimeathiriwa zaidi na wimbi la joto hadi kufikia sasa.

    Usiku wa kuamkia leo ulikuwa usiku wenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Ufaransa tangu vipimo vya hali ya hewa vianze mwaka 1947, kwa mujibu wa Météo-France.

    Shirika hilo lilirekodi kiwango cha wastani wa joto la usiku cha nyuzi joto 21.6 katika vituo 30 vya vipimo kati ya Jumatatu na Jumanne.

    Nchini Ufaransa, shule 845 za msingi wa juu na sekondari za chini zimefungwa kutokana na joto kali, huku shule nyingine 1,800 zikibadilisha ratiba za masomo. Hiyo ni takribani asilimia tano ya shule zote nchini humo.

    Tahadhari za juu zaidi pia zimetolewa nchini Ujerumani, Italia, Switzerland na Luxembourg.

    Nchini Ujerumani, wananchi wanajiandaa kwa viwango vya joto vya juu zaidi kuwahi kurekodiwa mwezi Juni siku ya Ijumaa, ambapo joto linaweza kufikia nyuzi 40 katika maeneo ya magharibi na kusini-magharibi mwa nchi.

    Kuongezeka kwa joto kunasababishwa na hewa moto inayosogea kaskazini kutoka jangwa la Sahara, ambayo kwa upande wake inazuia hewa ya moto kubaki juu ya maeneo yaliyoathirika.

    Watabiri wa hali ya hewa wanasema hali hiyo inaweza kusababisha moja ya mawimbi marefu zaidi ya joto katika miaka ya karibuni.

    Wanasayansi wamesema kuwa mawimbi ya joto yanayojirudia ni moja ya dalili za ongezeko la joto duniani.

  9. Waziri wa afya Kenya aomba msamaha juu ya Kituo cha Ebola cha Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Citizen TV

    Wizara afya nchini Kenya imesema kuwa imeagiza usitishwaji wa ujenzi wa kituo cha kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kinachofadhiliwa na serikali ya Marekani, katika kambi ya jeshi mjini Nanyuki.

    Akiongea mahakamani, waziri wa afya adan duale, alisema kuwa serikali tayari imesitisha ujenzi huo baada ya agizo la mahakama kuu.

    Duale ambaye alipatikana na hatia ya kupuuza maagizo ya mahakama alifika mahakamani huku akiwa ameambatana na maafisa kadhaa wakuu wa wizara ya afya na pia mawakili wa serikali.

    Waziri huyo aliomba msamaha mahakama akisema kuwa hakuna na dhamira yoyote ya kudharau au kupuuza maagizo ya mahakama.

    Mpango wa serikali ya Kenya wa kujenja kituo hicho, kulizua hasira miongoni mwa wakenya ambao waliandamana kuupinga, hatua ambayo ilisababisha vifo vya watu kadhaa.

    Kituo hicho kilidhamiria kuwahudumia raia wa Marekani wanaofanya kazi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambao wameambukizwa virusi vya Ebola.

    Hadi sasa taifa la DRC limethibitisha zaidi ya maambukizi elfu moja ya virusi hivyo.

    Soma Zaidi:

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Kwa mujibu wa picha za satelite, vyumba kadhaa vya hema, barabara mpya na majumba kadhaa yamejengwa katika kambi hiyo ya jeshi.

    Akitoa hukumu dhidi ya Waziri huyo jaji Patricia Nyaundi Mande alimuonya Waziri Duale dhidi ya kupuuza maagizo ya mahakama na kumuachilia huru bila adhabu yoyote.

    Kwa mujibu wa kifaa cha kuchunguza safari za ndege na vyanzo vya Kibalozi vya Marekani, ndege kadhaa zilizosheheni vifaa vya matibabu na madaktari zimeendelea kuwasili katika uwanja wa ndege katika kambi hiyo mjini Nanyuki.

    Afisa mmoja wa serikali ya Marekani, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters, akisema kuwa ndege zimeendelea kusafirisha vifaa vya matibabu hadi kambi hiyo na pia wafanyakazi wanaendelea kupewa mafunzo.

  10. Upinzani Sudan Kusini waonya kuwa nchi haiko tayari kwa Uchaguzi Mkuu

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Chama kikuu cha upinzani nchini Sudan Kusini, SPLM-IO, kimeonya kuwa nchi haiko tayari kwa uchaguzi, kikisema kwamba masuala ya kisiasa na kiusalama ambayo bado hayajatatuliwa yanaweza kufanya mchakato huo kuwa hatari.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye Facebook siku ya Jumatatu, kaimu mwenyekiti wa chama hicho, Nathaniel Pierino, aliishutumu serikali kwa kusongeza mbele uchaguzi huku vipengele muhimu vya makubaliano ya amani vikiwa bado havijatekelezwa.

    Onyo hilo linakuja wakati nchi ikiendelea na maandalizi ya uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 22 Desemba.

    Pierino alionya kwamba mtu yeyote atakayeingia katika maeneo yanayodhibitiwa na SPLM-IO kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura au kufanya kampeni atachukuliwa kama mfungwa wa vita.

    Uchaguzi huo umeahirishwa mara kadhaa kutokana na migogoro, ukosefu wa usalama, na kuchelewa kwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya nchi hiyo.

    Mvutano wa kisiasa pia unaendelea kuwa mkubwa kati ya Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani Riek Machar. Machar, ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, alisimamishwa kazi mwaka jana baada ya kushtakiwa kwa uhaini. Bado haijulikani ikiwa ataruhusiwa kugombea urais.

    Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Sudan Kusini ikisema maandalizi yanaendelea, bado kuna wasiwasi kuhusu ufadhili na utayari wa uchaguzi huo.

    Mnamo mwezi Machi, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Abednego Akok Kacuol, alifichua kuwa tume hiyo ilikuwa imepokea asilimia 4 pekee ya bajeti inayohitajika kuandaa uchaguzi.

    Makundi ya kiraia pia yameeleza wasiwasi kuhusu uaminifu wa uchaguzi huo. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Sudan Kusini limesema kuwa kuendesha uchaguzi kwa kutumia mipaka ya uchaguzi iliyochorwa mwaka 2010, bila sensa mpya ya watu, kunaweza kusababisha wananchi wengi kutowakilishwa ipasavyo.

    Sudan Kusini ilipata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011, lakini miaka ya kuyumba kwa kisiasa na migogoro imezuia nchi hiyo kufanya uchaguzi wa kitaifa hadi sasa.

    Soma zaidi:

  11. Dettol yaomba radhi baada ya tangazo lake jipya China kwenda mrama

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kampuni ya Dettol imeomba radhi baada ya tangazo lake huko nchini China, iliyodai kuwa lililenga kupinga ubaguzi wa kijinsia, kupokelewa vibaya na kuzua ukosoaji mkubwa mtandaoni.

    Tangazo hilo la dakika tano la dawa ya usafi wa matumizi mbalimbali lilionyesha mwanaume anayesema anatafuta mwenza “msafi” na ambaye “hajaguswa na wanaume wengine”.

    Mwishoni mwa simulizi, mpenzi wake anamkosoa kwa mtazamo wake wa kudhalilisha wanawake na kuamua kuachana naye.

    Katika sehemu ya mwisho ya tangazo hilo, Dettol iliwasilishwa kama suluhisho dhidi ya “wanaume wanaoumiza wanawake kihisia”, ikiwafananisha na bakteria.

    Tangazo hilo lilizua hasira kwenye mitandao ya kijamii nchini China. Baadhi ya watumiaji walidai kuwa linawadhalilisha wanawake, huku wengine wakitaka bidhaa za kampuni hiyo zisusiwe.

    Katika taarifa yake, Dettol ilisema lengo la tangazo hilo lilikuwa kuonyesha na kukosoa mitazamo potofu ya kijinsia, lakini vipande vya video vilivyosambazwa mtandaoni vilipotosha ujumbe uliolengwa.

    “Tunatambua kuwa tangazo hili limewaudhi watu wengi, hasa wanawake. Tunawajibika kwa mapungufu yoyote katika utengenezaji na ukaguzi wa maudhui ya tangazo hili,” ilisema kampuni hiyo.

    Kufuatia malalamiko hayo, tangazo hilo limeondolewa na kampuni imeahidi kupitia upya taratibu zake za ukaguzi wa maudhui kabla ya kuchapishwa.

    Dettol ilisisitiza kuwa dhamira yake tangu kuanzishwa kwake imekuwa kulinda afya ya familia, lakini ikaongeza kuwa ulinzi wa kweli unajumuisha heshima, usawa na utu wa kila mtu.

  12. Kombe la Dunia 2026: Algeria yaiondoa Jordan hatua ya makundi, Ufaransa yaichapa Iraq 3-0

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Algeria imejikakamua na kutoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jordan katika mchezo wa Kundi la 10 wa Kombe la Dunia 2026 uliochezwa Jumatatu mjini Santa Clara.

    Jordan walikuwa wa kwanza kutikisa nyavu kupitia Nizar Al-Rashdan dakika ya 36, lakini Algeria walirejea kwa nguvu kipindi cha pili. Mchezaji wa akiba Nadhir Bouali alisawazisha dakika ya 69 kabla ya Amin Gouiri kufunga bao la ushindi dakika ya 82.

    Ushindi huo umeiweka Algeria kwenye nafasi nzuri ya kuwania kufuzu, ikiwa na pointi tatu sawa na Austria, huku mabingwa watetezi Argentina wakiongoza kundi baada ya ushindi wao dhidi ya Austria uliopatikana kupitia mabao mawili ya Lionel Messi.

    Sasa macho yote yataelekezwa kwenye pambano la mwisho kati ya Algeria na Austria tarehe 27 mwezi huu, ambapo mshindi atanyakua nafasi ya pili ya kundi. Sare itainufaisha Austria.

    Wakati huohuo, France ilionyesha ubora wake kwa kuichapa Iraq mabao 3-0 na kuimarisha nafasi yake katika mashindano hayo.

    Soma zaidi:

  13. Mauzo ya makaa ya mawe na gesi ya Australia yanakiuka haki za binadamu UN yaelezwa

    Prof Anne Poelina, ni mmoja wa wanaharakati kutoka jamii ya wachache

    Chanzo cha picha, Rebecca Parker

    Maelezo ya picha, Prof Anne Poelina, ni mmoja wa wanaharakati kutoka jamii ya wachache

    Kundi la raia wa Australia limeishutumu serikali yao kwa kukiuka haki za binadamu kwa kuendelea kuruhusu usafirishaji wa makaa ya mawe na gesi, na sasa wanataka ichukuliwe hatua hatua.

    Walalamikaji hao wanasema maisha yao yameathiriwa na matukio makali ya hali ya hewa yanayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi, yakiwemo moto mkubwa wa misitu, mafuriko, mawimbi ya joto kali, kupanda kwa kina cha bahari na kuongezeka kwa mwani wenye sumu. Wanaamini kuwa msaada wa serikali kwa kampuni za nishati ya mafuta ya kisukuku umechangia hali hiyo.

    Hii ndiyo kesi ya kwanza kupelekwa katika chombo au mahakama ya kimataifa tangu uamuzi wa mwaka 2025 wa International Court of Justice uliobainisha kwamba nchi zinaweza kushtakiwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

    Ingawa uamuzi wowote wa Umoja wa Mataifa hautakuwa wa lazima kisheria, Australia,moja ya wauzaji wakubwa duniani wa makaa ya mawe na gesi, inatarajiwa kutoa majibu rasmi.

    Miongoni mwa walalamikaji hao ni Barry Traill, mtaalamu wa ikolojia ya wanyamapori na mzima moto wa kujitolea.

    Traill alisema kwamba mwaka 2009 baadhi ya marafiki zake walifariki katika moto mkubwa wa misitu wa Black Saturday bushfires katika jimbo la Victoria, licha ya kuwa walikuwa na uzoefu na maandalizi ya kukabiliana na majanga hayo.

    “Tukio hilo lilibadilisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa,” alisema Traill, akiongeza kwamba ilidhihirika kuwa kanuni za zamani za kukabiliana na moto na kuishi hazikuwa tena zinafanya kazi.

    Mwaka 2019, akiwa mstari wa mbele katika kupambana na moto mkubwa wa misitu huko Queensland wakati wa msimu uliojulikana kama Black Summer bushfires, Traill alisema alishuhudia moja kwa moja kwamba mabadiliko ya tabianchi si tatizo la baadaye.

    “Tayari yanaua watu na kuharibu maisha, mazingira na jamii kote Australia,” alisema.

    Kesi hiyo inaongeza shinikizo kwa serikali ya Australia kuhusu sera zake za nishati na wajibu wake katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

  14. Mwanamke afariki baada ya gari la Tesla kutoka barabarani na kugonga nyumba

    Gari ya Tesla

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa usalama wa usafiri nchini Marekani wanafanya uchunguzi kuhusu ajali mbaya iliyohusisha gari la Tesla lililotoka barabarani na kugonga nyumba.

    National Highway Traffic Safety Administration ilitangaza Jumatatu kuwa imefungua uchunguzi rasmi kuhusu ajali hiyo iliyotokea tarehe 19 Juni katika jimbo la Texas, ambapo gari la Tesla lilitoka nje ya barabara na kugonga nyumba ya makazi.

    Kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo, mwanamke aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo alipata majeraha mabaya na baadaye alifariki kutokana na ajali hiyo.

    Polisi walisema kuwa dereva hakuwa chini ya ushawishi wa pombe au dawa za kulevya. Dereva huyo aliwaambia wachunguzi kwamba gari lilikuwa likitumia mfumo wa usaidizi wa uendeshaji wa kiotomatiki wakati ajali ilipotokea.

    Msemaji wa NHTSA alisema:

    “Wakala umeanzisha uchunguzi maalumu kuhusu ajali hii.”

    Kwa upande mwingine, mwakilishi wa Tesla, kampuni inayomilikiwa na bilionea wa Marekani Elon Musk, hakujibu maombi ya kutoa maoni kuhusu tukio hilo au uchunguzi unaoendelea.

    Ajali hiyo ilitokea takribani saa 2:00 usiku kwa saa za eneo hilo siku ya Ijumaa.

    Ripoti ya polisi inaeleza kuwa dereva wa gari aina ya Tesla Model 3 “alishindwa kudhibiti gari akiwa katika njia ya kupita magari mengine, akatoka nje ya barabara na kugonga nyumba ya makazi.”

    Uchunguzi huo unalenga kubaini sababu halisi ya ajali hiyo na iwapo mfumo wa usaidizi wa uendeshaji wa gari ulikuwa na mchango wowote katika tukio hilo.

    Unaweza kusoma;

  15. Pesa za kikombozi zasababisha kifo cha Nancy Guthrie

    Noti liyotumwa kama kikombozi siku chache baada ya mama yake mtangazaji wa Marekani Savannah Guthrie kutekwa nyara kutoka nyumbani kwake kudai kuwa amefariki, kulingana na wachunguzi.

    Ujumbe huo ulikuwa kati ya mbili zilizoelekezwa kwa familia ya Nancy Guthrie na kutumwa kwa vyombo vya habari siku chache baada ya kutekwa nyara kwake Januari.

    Wa kwanza alidai mamilioni ya bitcoin ili aachiliwe, lakini wa pili alisema kuwa alikuwa amekufa, kulingana na vyanzo vilivyotajwa na vyombo vya habari vya Marekani.

    Barua kutoka kwa watekaji nyara inasemekana ilisema hawakuwa na nia ya kumuua na ilijumuisha kuomba msamaha kwa familia.

    Idara ya Polisi Kaunti ya Pima ilikataa kutoa maoni yake kuhusu yaliyomo kwenye maelezo hayo, lakini ilisema uchunguzi "unaendelea".

  16. Iran yakanusha madai ya Vance kuhusu wakaguzi wa nyuklia

    m.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Iran imekanusha madai ya Makamu wa Rais JD Vance kwamba itawaruhusu wakaguzi wa nyuklia kurejea nchini, baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Washington na Tehran kufikia makubaliano ya mwisho ya kumaliza vita.

    Kufuatia mazungumzo nchini Uswizi, Vance alisema majadiliano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) yanaweza kuzuru nchi hiyo "hata leo".

    Lakini wizara ya mambo ya nje ya Iran iliambia vyombo vya habari vya serikali kwamba Tehran haikutoa "ahadi mpya" kuhusu ukaguzi wa nyuklia.

    Hayo yamejiri baada ya Marekani kutangaza kuwa imeiondolea Iran vikwazo kwa muda ili kuiwezesha kuuza mafuta kwa dola za Marekani kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa.

    Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatatu, wapatanishi wa Qatar na Pakistan walisema kwamba baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo katika mjini Bürgenstock Uswizi, Marekani na Iran zilikubaliana "njia ya kuelekea kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60".

    Vance alielezea mazungumzo hayo kuwa "na tija".

    Makamu wa rais wa Marekani alisema timu hizo zilijadili kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na "kumaliza mzozo kwa usitishaji mapigano wa kikanda".

    Soma pia:

  17. Lionel Messi mfungaji bora wa muda wote kwenye Kombe la Dunia

    Messi

    Chanzo cha picha, Robbie Jay Barratt - AMA/Getty Images

    Nahodha wa Argentina, Lionel Messi, alifunga mabao mawili katika mechi ya pili ya Kundi J ya Kombe la Dunia dhidi ya Austria, na kuiongoza Argentina katika ushindi wa mabao 2-0.

    Messi, ambaye pia alikosa penalti mapema katika mchezo huo, alifunga mabao yake katika dakika ya 38 na dakika ya 90+5, na kuhakikisha timu yake inapata ushindi muhimu.

    Nyota huyo wa Argentina, ambaye atatimiza miaka 39 tarehe 24 Juni, anaendelea kuweka historia kama mfungaji bora wa muda wote katika fainali za Kombe la Dunia, akiwa amefunga mabao 18 katika mechi 28 alizocheza.

    Baada ya Messi katika orodha hiyo ni Miroslav Klose wa Ujerumani na Kylian Mbappe wa Ufaransa, ambao kila mmoja ana mabao 16. Nafasi inayofuata inashikiliwa na Ronaldo wa Brazil mwenye mabao 15.

    Ushindi huo umeimarisha nafasi ya Argentina katika Kundi J huku Messi akiendelea kuonesha ubora wake licha ya umri wake mkubwa katika soka la kimataifa.

    Lionel Messi, ambaye amefunga mabao yote matano ya Argentina katika Kombe la Dunia 2026 hadi sasa, pia amesawazisha rekodi ya kufunga mabao katika mechi sita mfululizo za mashindano hayo.

    Messi sasa anajiunga na nyota wengine wawili wa soka waliofanikiwa kuweka rekodi hiyo: Just Fontaine wa Ufaransa na Jairzinho wa Brazil, ambao walifanya hivyo katika Kombe la Dunia la mwaka 1958.

    Unaweza kusoma;

  18. Pacha waoa pacha katika harusi ya pamoja Nigeria

    Harusi ya pacha

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Wakati wageni walipokusanyika katika kanisa jijini Ibadan kusini-magharibi mwa Nigeria mwishoni mwa wiki, walijua walikuwa wakishuhudia tukio la kipekee.

    Ndugu mapacha wawili wa kiume, Taiwo na Kehinde Oguntoye, walifunga ndoa na dada mapacha wawili wa kike, Taiwo na Kehinde Adediran, katika sherehe ya pamoja iliyojaa furaha.

    Jamii ya Wayoruba, ambao ni wengi eneo la kusini-magharibi mwa Nigeria, inajulikana kwa kuwa na kiwango cha juu cha kuzaliwa kwa mapacha. Hata hivyo, si jambo la kawaida kuona jozi mbili za mapacha wakifunga ndoa kwa wakati mmoja.

    Akizungumza siku ya harusi yake, Taiwo Oguntoye alisema:

    "Tunawafahamu mapacha wengi, lakini ndoa hii inaonekana kama ilipangwa na Mungu. Siku zote tumekuwa na ndoto ya kuoa mapacha."

    Aliongeza kuwa yeye na mke wake wanaomba wapate watoto mapacha katika watoto wao wa kwanza na wa pili, kwani hilo ndilo tamanio lao kubwa.

    Katika utamaduni wa Wayoruba, mapacha huchukuliwa kuwa baraka maalumu. Majina yao pia hupewa kwa kufuata mila za kitamaduni. Mtoto anayezaliwa kwanza huitwa Taiwo, ambalo maana yake ni "yule anayekwenda kuujaribu ulimwengu", huku anayezaliwa baadaye akiitwa Kehinde, likimaanisha "yule aliyekuja baada yake".

    Tukio hilo limevutia watu wengi kutokana na nadra yake na umuhimu wake wa kitamaduni katika jamii ya Wayoruba.

  19. Trump: Sehemu ya fedha za Iran zimeachiwa na zitatumika kununua chakula

    Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuachiliwa kwa sehemu ya kwanza ya mali za Iran zilizokuwa zimezuiwa, akisema kuwa Iran itatumia fedha hizo kununua chakula kutoka kwa wakulima wa Marekani.

    Abdolnaser Hemmati, mkuu wa Benki Kuu ya Iran, pia amethibitisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja taarifa hizo. Amesema kuwa dola bilioni 6 za kwanza zilizofunguliwa zitatumika kununua chakula na dawa kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na Washington mwaka 1402 kwa kalenda ya Iran.

    Hemmati aliongeza kuwa dola bilioni 6 za pili, baada ya kuachiliwa, zitatumika kununua bidhaa ambazo hazijafungwa na vikwazo vya kimataifa.

    Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, aliondoka kuelekea Muscat saa moja baada ya kurejea kutoka Uswisi.

    Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni kwa ajili ya “maandalizi ya Iran ya usimamizi wa Mlango-Bahari wa Hormuz” pamoja na kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.

    Aidha, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, anatarajiwa kufanya ziara nchini Pakistan katika siku zijazo kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia na kuimarisha mahusiano ya kikanda.

    Kwa ujumla, hatua hizi zinaashiria kuendelea kwa mazungumzo na ushirikiano kati ya Iran, Marekani na nchi washirika wa eneo hilo, huku masuala ya uchumi, biashara na usalama wa njia ya bahari ya mlango bahari wa Hornuz yakipewa kipaumbele.

    Unaweza kusoma;

  20. Marekani yapunguza vikwazo vya mafuta huku Iran Ikikanusha madai ya Vance kuhusu wakaguzi wa nyuklia

    Vance

    Chanzo cha picha, Reuters

    Iran imekanusha madai ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, kwamba itaruhusu wakaguzi wa nyuklia kurejea nchini humo, baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Washington na Tehran yenye lengo la kufikia makubaliano ya mwisho ya kumaliza vita.

    Baada ya mazungumzo yaliyofanyika nchini Uswisi, Vance alisema kuwa majadiliano na Shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki (IAEA) kuhusu ukaguzi wa nyuklia yanaweza kuanza “hata leo”.

    Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iliambia vyombo vya habari vya serikali kwamba Tehran haijatoa “ahadi mpya yoyote” kuhusu kuruhusu ukaguzi wa nyuklia.

    Wakati huo huo, Marekani imepunguza kwa muda baadhi ya vikwazo vyake dhidi ya Iran, na kuiruhusu kuuza mafuta kwa kutumia dola za Marekani kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa.

    Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatatu, wapatanishi Qatar na Pakistan walisema kuwa baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo katika mji wa mapumziko wa Bürgenstock nchini Uswisi, Marekani na Iran zilikubaliana kuhusu mwelekeo wa kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60.

    Vance alieleza kuwa mazungumzo hayo yameweka “msingi mzuri sana” wa maendeleo ya baadaye.

    Makamu huyo wa Rais pia alisema kuwa pande hizo zilijadili kufunguliwa tena kwa mlango bahari wa Hormuz pamoja na hatua za kuzuia migongano katika utekelezaji wa usitishaji mapigano wa kikanda.

    Msamaha wa vikwazo wa siku 60 uliotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani Jumatatu umeondoa kwa muda baadhi ya vipengele muhimu vya vikwazo vya muda mrefu vya Washington dhidi ya Iran, ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikidhoofisha uchumi wa Tehran.

    Unaweza kusoma;