Magonjwa 7 hatari zaidi kuwahi kutokea duniani

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Zaidi ya visa elfu moja vya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola vimeripotiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku watu 246 wakiripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo.
Mwezi uliopita, shirika la Afya Duniani (WHO) ilitangaza mlipuko wa Ebola unaosababishwa na aina ya virusi vya Ebola vya Bundibugyo, kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa nchini DRC na Uganda, ila bado haijafikia kiwango cha kuwa janga la kimataifa.
Huu ukiwa ni mlipuko wa 17 kutokea nchini DRC, ni mlipuko wa pili mkubwa kushuhudiwa kulingana na shirika la kudhibiti kuenea kwa magonjwa Africa CDC.
Leo hii mlipuko wa ugonjwa huo unaendelea kuhatarisha maisha ya watu, huku msaada zaidi ukihitajika kuimarisha huduma ya afya inayotolewa na kuzuia maambukizi zaidi.
Ebola ni mojawapo ya magonjwa ambayo husababisha viwango vya juu ya vifo kwa wale wanaopatikana na ugonjwa huo. 50% ya wale ambao huungua ugonjwa huu hufariki.
Lakini yapo magonjwa mengi yaliyowahi na yanayoendelea kutikisa dunia kwa hatari, ukiwemo wa kipundupindu. Magonjwa haya 7 yanachukuliwa hatari zaidi kutokana na kusababisha vifo vya watu wengi zaidi katika historia ya magonjwa duniani, ingawa mengine yameanza kudhibitiwa.
COVID-19

Chanzo cha picha, Getty Images
COVID-19 na SARS ni magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na virusi vya familia moja ya coronaviruses, lakini tofauti yao kubwa ipo kwenye uwezo wa kuenea na ukubwa wa madhara yao duniani.
COVID-19 (inayosababishwa na SARS-CoV-2) inachukuliwa kuwa moja ya magonjwa hatari zaidi katika historia ya dunia kwa sababu ya kasi yake ya kuenea na kuathiri kila kona ya dunia. Ugonjwa huu ulisababisha janga kubwa la kimataifa na unakadiriwa kuua zaidi ya watu milioni 7.1 waliothibitishwa rasmi, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likikadiria kuwa vifo halisi vinaweza kufikia karibu milioni 15 ikijumuisha vifo vya moja kwa moja na visivyo vya moja kwa moja.
Kwa upande mwingine, SARS (inayosababishwa na SARS-CoV-1) ilikuwa na kiwango cha juu zaidi cha vifo kwa wagonjwa walioambukizwa, lakini iliambukiza watu wachache zaidi na ilidhibitiwa haraka. Ilianza mwaka 2003 na kuenea katika zaidi ya nchi 20, lakini kufikia 2004 ilifanikiwa kudhibitiwa kabisa, ikiwa imeambukiza watu 8,098 na kusababisha vifo 774 pekee.
Kwa ujumla, COVID-19 inaonekana kuwa hatari zaidi kwa kiwango cha kimataifa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuenea na kusababisha vifo vingi, wakati SARS ilikuwa kali zaidi kwa mtu binafsi lakini haikuenea sana na ilizimwa mapema kabla ya kuwa janga kubwa la dunia.
HIV/UKIMWI

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
HIV/UKIMWI ni mojawapo ya magonjwa hatari zaidi duniani, unaosababishwa na virusi vya HIV vinavyoshambulia kinga ya mwili na kuufanya mwili kushindwa kupambana na magonjwa mengine. Tangu kuanza kwa janga hili, mamilioni ya watu wameathirika duniani kote.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 44.1 wamefariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI tangu kuanza kwa mlipuko huo. Pia, kwa baadhi ya makadirio ya kesi zilizorekodiwa, takribani asilimia 51 ya watu wazima na asilimia 59 ya watoto waliopata UKIMWI wamefariki dunia.
Hadi mwaka 2024, watu takribani milioni 40.8 walikuwa wanaishi na HIV duniani, huku zaidi ya watu milioni 1.3 wakipata maambukizi mapya katika mwaka huo huo. Takwimu zinaonyesha pia kwamba wanawake na wasichana wanabeba mzigo mkubwa wa maambukizi mapya, hasa katika maeneo ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako asilimia 63 ya maambukizi mapya hutokea kwa kundi hilo.
Kwa ujumla, HIV/UKIMWI ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa njia ya majimaji ya mwili kama damu, manii na maziwa ya mama, na bado unaendelea kuwa changamoto kubwa ya kiafya duniani licha ya maendeleo ya dawa za kudhibiti ugonjwa huo.
Homa ya Mafua/Influenza

Chanzo cha picha, Getty Images
Ugonjwa wa homa ya mafua, hasa ya 1918 (Influenza ya 1918), unaojulikana pia kama H1N1, unakadiriwa kusababisha vifo vya watu kati ya milioni 50 hadi 100 duniani kote. Hii ilikuwa moja ya milipuko mibaya zaidi katika historia ya binadamu, ikienea haraka katika mabara mengi na kuathiri jamii kwa kiwango kikubwa.
Maambukizi ya homa ya mapafu huathiri takriban 10% ya watoto na 30% ya watu wazima kila mwaka. Homa hii huathiri zaidi ya watu million tano kila mwaka na kusababisha takriban vifo laki tano.
Janga hili lilikuwa na athari kubwa zaidi kuliko hata Vita kuu ya kwanza ya Dunia, kwani liliua watu wengi zaidi ndani ya kipindi kifupi cha miezi michache tu. Kasi ya maambukizi na ukosefu wa tiba wakati huo vilifanya ugonjwa huu kuwa hatari sana, na kuacha kumbukumbu ya maafa makubwa ya kiafya duniani.
Tauni

Chanzo cha picha, Getty Images
Tauni hasa ya karne ya 14 (Black Death) ilikuwa mojawapo ya magonjwa mabaya zaidi katika historia ya dunia. Ilitokea kati ya mwaka 1347 hadi 1351 na kuua takribani watu milioni 75, ingawa baadhi ya makadirio yanafikia hadi milioni 200. Inaelezwa na vyanzo mbalimbali wakati huo, dunia ilikuwa na idadi ya watu takribani milioni 450, na karibu nusu ya watu wa Ulaya waliweza kupoteza maisha.
Ugonjwa huu ulisambaa kwa haraka kupitia wafanyabiashara na wasafiri waliopita Ulaya kupitia bandari za Sicilia. Unasababishwa na bakteria unaojulikana kama bubonic plague, na ulipewa jina "Black Death" kutokana na alama nyeusi zilizokuwa zikionekana kwenye miili ya waathirika.
Maambukizi yanhusishwa kutoka kwa panya na viroboto na yametajwa kuwa hatari kwa binadamu.
Ndui

Chanzo cha picha, Getty Images
Ugonjwa wa ndui (smallpox) unakadiriwa kusababisha vifo vya takribani watu milioni 300 katika karne ya 20 pekee, na mamia ya mamilioni zaidi katika milenia zilizotangulia. Ugonjwa huu husababishwa na virusi vinavyojulikana kama variola virus, ambao huambukiza kwa kasi kubwa na unaweza kusababisha vifo kwa hadi asilimia 30 ya walioambukizwa.
Ndui ilikuwa miongoni mwa magonjwa hatari zaidi katika historia ya binadamu, lakini habari njema ni kwamba ilifanikiwa kutokomezwa kabisa duniani kufikia mwaka 1980.
Mlipuko wa mwisho wa ugonjwa huu ulishuhudiwa nchini Somalia mwaka wa 1977.
Hili liliwezekana kupitia kampeni kubwa ya chanjo ya kimataifa iliyoongozwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), ambayo ilisaidia kuzuia maambukizi na hatimaye kuufuta ugonjwa huu duniani kote. Chanjo ya Ndui hupewa watoto ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo hatari.
Kabla ya ugonjwa huu kuangamizwa karne ya ishirini, ilikuwa mojawapo ya magonjwa hatari sana katika historia ya binadamu.
Kifua Kikuu (TB)

Chanzo cha picha, Getty Images
Ugonjwa wa kifua kikuu (TB) unakadiriwa kuwa umesababisha vifo vya zaidi ya watu bilioni 1 katika historia ya binadamu kwa karne kwa karne. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayejulikana kama Mycobacterium tuberculosis, ambaye hushambulia hasa mapafu na huenea kwa njia ya hewa mtu anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza.
Kifua kikuu ni ugonjwa wa zamani, ulikuwepo miongo na miongo na ndiyo maana iadai ya vifo ni kubwa hasa vilivyotokea kale, na ushahidi wake umepatikana hata katika maiti za watu huko Misri, zilizohifadhiwa tangu takribani mwaka 2400. Hii inaonyesha kwamba ugonjwa huu umekuwepo kwa maelfu ya miaka na umeendelea kuathiri jamii mbalimbali duniani licha ya maendeleo ya tiba za kisasa.
Ingawa leo TB inaweza kutibiwa kwa dawa maalum za antibiotiki, bado ni miongoni mwa magonjwa hatari ya kuambukiza zaidi duniani. Kugundua mapema, kupata matibabu kwa wakati, na kuepuka msongamano wa watu katika maeneo yasiyo na hewa safi ni muhimu katika kupunguza kuenea kwake.
Malaria

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Malaria ni ugonjwa ambao umekuwa tishio la muda mrefu kwa binadamu tangu karne na karne. Ingawa mara nyingine hudaiwa kuwa uliua nusu ya watu wote waliowahi kuishi duniani, taarifa hii inaonekana kuwa ya kuzidisha, kwani ukweli ni kwamba watu wengi zaidi walikuwa "hatarini" kuliko kuwa wamekufa kutokana na ugonjwa huo.
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya Plasmodium vinavyosambazwa na mbu aina ya Anopheles, na haukueleweka vizuri hadi mwaka 1897 ambapo kisababishi chake kiligunduliwa. Kabla ya hapo, malaria ilikuwa ikisababisha vifo vingi bila kueleweka chanzo chake halisi.
Hadi leo, malaria bado ni tatizo kubwa la kiafya duniani, hasa barani Afrika, ambapo watoto ndio huathirika zaidi. Inakadiriwa kusababisha zaidi ya vifo 600,000 kila mwaka.
Kwa ujumla, magonjwa yanayosambazwa na mbu kwa pamoja (ikiwemo malaria na mengine) husababisha zaidi ya vifo 700,000 kila mwaka duniani, na kuifanya mbu kuwa miongoni mwa wanyama hatari zaidi kwa binadamu katika historia.
Ila ugonjwa huu unaweza kuzuiwa na kutibiwa, huku chanjo ya Malaria ambayo imeidhinishwa na WHO ikiendelea kutumika.














