Mahakama Kenya yaitaka polisi kueleza alipo Twaha Mwaipaya
Twaha Mwaipaya aliripotiwa kuchukuliwa Nairobi tarehe 25 Oktoba na tangu wakati huo hajulikani alipo.
Muhtasari
- Mahakama Kenya yaitaka polisi kueleza alipo Twaha Mwaipaya
- Iran na Marekani bado mbali na makubaliano ya kumaliza vita
- Wadukuzi wa mitandao washambulia majokofu ya maduka makubwa Ulaya
- Tishio la Trump dhidi ya Iran lafufua hofu ya vita Ghuba ya Uajemi
- Mkulima wa Afrika Kusini apigwa risasi na kukatwa masikio, watu watano wakamatwa
- Urusi na Ukraine zajibu tahadhari za uongo zilizosambazwa
- Televisheni ya taifa China yasitisha matangazo ya mechi za La Liga kufuatia utani wa Mbappé
- Uganda yaanza kuwaondoa wanajeshi wake Somalia baada ya miaka 20
- Waislamu watatu wahukumiwa kifungo cha maisha nchini India kwa kuchinja ng'ombe
- Urusi yaanza majadiliano ya kujenga mitambo ya nyuklia katika nchi nne za Afrika
- Watu tisa wafariki dunia baada ya ndege kuanguka Florida
- Tetesi za soka Jumatatu: Man Utd yammezea mate Balde wa Barcelona
- Kaka wa Tundu Lissu kuzikwa baada ya hukumu ya kesi ya uhaini
- Iran: Hormuz kufunguliwa ndani ya siku mbili iwapo Marekani itatimiza masharti yake
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid
Mahakama Kenya yaitaka polisi kueleza alipo Twaha Mwaipaya

Chanzo cha picha, MITANDAONI
Mahakama Kuu ya Milimani nchini Kenya leo imeendelea kusikiliza kesi inayohusu kupotea kwa mwanaharakati wa upinzani kutoka Tanzania, Twaha Mwaipaya, huku polisi wakisema hawajui alipo na kwamba hayuko mikononi mwao.
Mwaipaya, ambaye ni mkosoaji wa serikali ya Tanzania, anaripotiwa kuchukuliwa na watu wanaodhaniwa kuwa maafisa wa usalama katika eneo la Kamulu, Nairobi, tarehe 25 Oktoba. Tangu wakati huo, mahali alipo bado hapajulikani.
Siku ya Ijumaa, Oktoba 30, Mahakama Kuu iliamuru polisi wamfikishe Mwaipaya mahakamani leo akiwa hai au amefariki dunia, pamoja na hati yoyote ya kuzuiliwa kwake na maelezo ya kwa nini hapaswi kuachiliwa huru mara moja.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkuu Mtendaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa, Hussein Khalid, ambaye amezungumza na BBC, polisi walipofika mahakamani walieleza kuwa hawajamshikilia Mwaipaya na hawakuhusika na kukamatwa kwake, hivyo wakasema hawawezi kutekeleza agizo la mahakama.
Polisi pia waliiambia mahakama kuwa uchunguzi bado unaendelea. Wamesema wamewahoji mashahidi waliokuwepo wakati wa tukio hilo na kuchukua taarifa zao. Kwa mujibu wa mashahidi hao, watu waliomchukua Mwaipaya walikuwa wamevalia barakoa, jambo ambalo limefanya iwe vigumu kutambua utambulisho wao.
Aidha, polisi wanasema wanaendelea kupitia kamera za CCTV na vielelezo vingine katika juhudi za kubaini waliohusika, lakini hadi sasa hakuna aliyefahamika.
Kesi hiyo ilifunguliwa na shirika la Vocal Africa kupitia ombi la habeas corpus, likiitaka mahakama kuamuru mamlaka kubaini alipo Mwaipaya na kuhakikisha anapatikana.
Katika hoja zao mahakamani, Vocal Africa ilirejelea tukio la mwanasiasa wa Uganda Kizza Besigye, ambaye walidai aliwahi kuchukuliwa kwa mazingira yanayofanana na baadaye kupatikana nchini Uganda. Shirika hilo limesema lina wasiwasi kuwa huenda Mwaipaya alichukuliwa kinyume cha sheria na kuhamishwa nje ya Kenya.
Pia lilieleza kuwa mashahidi walioshuhudia tukio hilo walidai utekaji ulifanyika hadharani mchana kweupe, hali ambayo, kwa mujibu wa shirika hilo, imeibua maswali kuhusu nani waliokuwa wakitekeleza operesheni hiyo.
Kuhusu juhudi za serikali za Kenya na Tanzania kutafuta mwanaharakati huyo, Vocal Africa imesema hadi sasa haijaona hatua zozote za wazi isipokuwa taarifa ya polisi kwamba uchunguzi unaendelea.
Shirika hilo pia limesema Mkuu wa Polisi wa Kenya, ambaye alitakiwa kufika mahakamani kutoa maelezo kuhusu suala hilo, bado hajafika, na mahakama imeagiza afike haraka iwezekanavyo.
Vocal Africa imeonya kuwa ikiwa mamlaka hazitaweza kueleza alipo Mwaipaya, itaendelea kutumia njia nyingine za kisheria, ikiwemo kupeleka suala hilo katika taasisi za kikanda na kimataifa za haki za binadamu pamoja na mahakama nyingine zinazohusika na ukiukaji wa haki za binadamu.
Mamlaka za Tanzania hazijatoa tamko lolote hadi sasa kuhusu madai ya kutekwa kwa Mwaipaya.
Soma Zaidi Pia:
Iran na Marekani bado mbali na makubaliano ya kumaliza vita

Chanzo cha picha, Reuters
Iran imesema mawasiliano kati yake na Marekani kuhusu kumaliza vita vilivyodumu kwa miezi minane yanaendelea, licha ya mazungumzo ya siku kadhaa yaliyofanyika kupitia wapatanishi wa Qatar kumalizika bila mafanikio makubwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema pande hizo mbili zinaendelea kubadilishana ujumbe kupitia wapatanishi, ingawa alikiri kuwa suala hilo ni tata na linahitaji muda zaidi.
Kauli hiyo inakuja wakati kukiwa na hofu kwamba mapigano yanaweza kurejea baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani utakaofanyika Jumanne. China na Urusi pia zimeonya dhidi ya uwezekano wa kurejea kwa hatua za kijeshi katika mzozo huo ambao umeathiri uchumi wa dunia.
Ingawa bei za mafuta zilishuka kwa karibu asilimia nne kutokana na matumaini ya suluhisho la kidiplomasia, vyanzo vya Iran vimesema vinaamini uwezekano wa mashambulizi mapya ya Marekani bado ni mkubwa kuliko wa kufikiwa kwa makubaliano.
Baghaei amesema mpango wa Iran wa hatua saba uliowasilishwa mwezi Septemba bado ndio msingi wa mazungumzo. Hata hivyo, amethibitisha kuwa mpango huo umefupishwa ili uweze kutekelezwa ndani ya siku mbili.
Rais wa Marekani Donald Trump aliukataa mpango huo mwezi Septemba.
Mpango huo ulipendekeza Marekani iondoe vizuizi katika bandari za Iran, Iran ifungue tena njia ya maji ya Hormuz, Marekani iruhusu mauzo ya mafuta ya Iran, pamoja na kufuta baadhi ya vikwazo vipya dhidi ya Tehran kabla ya mazungumzo kuhusu masuala mengine kuanza.
Iran imesisitiza kuwa kufupisha mpango huo hakubadilishi msimamo wake kwamba mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia hayawezi kurejelewa hadi ihakikishe masharti yake yote yametimizwa.
Aidha, Baghaei amekanusha kuwa suala la kuhamisha akiba ya Iran ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu kwenda nchi nyingine lilijadiliwa katika mazungumzo hayo, akisema Tehran haijatoa ishara yoyote ya kukubali hatua hiyo.
Soma Zaidi:
Wadukuzi wa mitandao washambulia majokofu ya maduka makubwa Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images
Bidhaa katika majokofu ya maduka kadhaa ya ICA nchini Sweden zimemwagwa baada ya shambulio kubwa kupitia njia ya mtandao.
Makumi ya maduka makubwa nchini Ubelgiji na Sweden yamekumbwa na shambulio hilo la kimtandao, lililoathiri mifumo yake yote ya majokofu na friza.
Takribani maduka 40 ya Delhaize nchini Ubelgiji na Luxembourg yaliathirika pia, huku maduka kadhaa ya ICA na Coop nchini Sweden yakikumbwa na tatizo hilo. Maduka 13 ya SuperValu nchini Ireland pia yameathirika.
Chakula chenye thamani ya mamilioni ya euro kimelazimika kutupwa, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya ndani. Duka moja la ICA nchini Sweden lilisema kuwa halijoto ya friza zake ilikuwa imewekwa kwenye nyuzi 50°C (122 Fahrenheit).
Haijafahamika ni nani aliyehusika na shambulio hilo, ambalo limekuja baada ya tukio kama hilo mwezi uliopita lililoathiri mamia ya maduka makubwa nchini Ufaransa.
Mashirika ya kitaifa ya usalama wa mtandao nchini Ubelgiji na Sweden yamesema yanafuatilia tukio hilo.
Delhaize, mojawapo ya misururu ya maduka makubwa nchini Ubelgiji, iliambia vyombo vya habari vya Ubelgiji kuwa tukio la "hitilafu ya mfumo wa kompyuta" lilitokea usiku katika maduka 40.
Tawi la Delhaize lililopo Hoeilaart, katika jimbo la Flemish Brabant, eneo la Flanders, liliiambia Het Laatste Nieuws kuwa limepoteza bidhaa zenye thamani ya euro 100,000.
Carrefour, kampuni ya maduka makubwa inayomilikiwa na Ufaransa, ilisema tukio hilo limeathiri maduka yake 15 pekee nchini Ubelgiji. Iliongeza kuwa hatua zilichukuliwa mara moja kuhakikisha maduka yote yanaendelea kufunguliwa.
Maduka saba kati ya 800 ya Coop nchini Sweden pia yameathirika, lakini kampuni hiyo iliiambia BBC kuwa "hali kwa sasa inadhibitiwa na iko chini ya udhibiti".
Pia unaweza kusoma:
Tishio la Trump dhidi ya Iran lafufua hofu ya vita Ghuba ya Uajemi

Chanzo cha picha, Reuters
Tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kuishambulia tena Iran limeziweka nchi washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi katika hali ngumu, zikihofia kujikuta tena katikati ya vita vilivyoamuliwa Washington huku kambi za kijeshi za Marekani zilizojengwa kwa ajili ya kuwalinda zikigeuka kuwa malengo ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran.
Makombora ya Iran yaliyolenga vituo vya kijeshi vya Marekani na miundombinu ya nishati katika eneo hilo wakati wa mapigano ya awali yalionyesha udhaifu uliopo katika mfumo wa usalama ambao Marekani imeujenga kwa miongo kadhaa katika Ghuba ya Uajemi. Badala ya kuizuia Tehran, uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani uliipa Iran malengo ya moja kwa moja ya kushambulia na njia za kuishinikiza nchi zinazoikaribisha.
Hofu hiyo ilitawala majadiliano kati ya mawaziri, watunga sera na maafisa wa usalama katika Mkutano wa Usalama wa Manama uliofanyika Bahrain mwishoni mwa wiki, huku serikali zikitathmini athari ambazo duru nyingine ya vita inaweza kuwa nazo kwa vikosi vya Marekani na nchi zinazovihifadhi.
Wasiwasi umeongezeka baada ya Trump kutishia tena kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran. Alisema anaweza kuzindua "Operesheni Epic Fury nyingine ndogo" baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula uliopangwa kufanyika Jumanne, akirejelea operesheni ya pamoja ya Marekani na Israel iliyoanza Februari 28.
Kwa mujibu wa maafisa wanne wa Ulaya, Marekani imekusanya wanajeshi na rasilimali za kutosha katika eneo hilo kiasi cha kuweza kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa muda mfupi, huenda hata ndani ya wiki hii.
Soma Pia:
Mkulima wa Afrika Kusini apigwa risasi na kukatwa masikio, watu watano wakamatwa

Chanzo cha picha, South African police
Onyo: Makala hii ina maelezo yanayoweza kuwasumbua baadhi ya wasomaji.
Polisi wa Afrika Kusini wamewakamata watu watano kwa tuhuma za kuhusika na shambulio la kikatili dhidi ya mfugaji wa ng'ombe, Donovan Marx, ambaye alipigwa na kuteswa katika tukio lililoelezwa kuwa la "ukatili usio na maana".
Marx, mwenye umri wa miaka 50, alishambuliwa wakati wa uvamizi wa nyumba yake katika shamba lililoko Ventersdorp, mji mdogo katika mkoa wa Northwest, Jumatano iliyopita.
Kwa mujibu wa polisi, Marx alivamiwa alipokuwa akirejea nyumbani, akapigwa risasi, kuchomwa kisu na kukatwa masikio katika tukio hilo la kutisha.
Washukiwa wote watano walikamatwa mwishoni mwa wiki, hatua iliyopokelewa kwa furaha na mke pamoja na familia ya Marx, ambao walisema sasa wanaamini mchakato wa sheria utachukua mkondo wake.
Tukio hilo limezua hasira kubwa nchini Afrika Kusini, taifa ambalo tayari linakabiliwa na viwango vya juu vya uhalifu wa kutumia nguvu.
Shambulio lilivyotokea
Polisi walisema kundi la watu waliovaa barakoa na wenye silaha lilimvamia mfanyakazi wa shambani alipokuwa akikata nyasi katika eneo la nyumba ya Marx.
Washambuliaji hao walitaka kujua alipo Marx kabla ya kumfunga mfanyakazi huyo mikono na miguu kwa kamba za plastiki.
Marx aliporejea nyumbani, washukiwa wawili walimkaribia na kumpiga risasi sehemu ya juu ya mwili.
Baadaye walimvuta hadi ndani ya nyumba, wakamfunga mikono na miguu na kudaiwa kumchoma kwa kisu mara kadhaa.
Washambuliaji hao walivuruga nyumba wakitafuta mali na kuondoka na bunduki tatu kutoka kwenye sanduku la kuhifadhia silaha, pamoja na gari la Marx.
Tukio hilo lilimalizika baada ya mfanyakazi aliyefungwa kufanikiwa kujinasua na kuomba msaada.
Marx alikimbizwa hospitalini ambako bado anaendelea kupatiwa matibabu. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, huenda akahitaji masikio ya bandia baada ya madaktari kushindwa kuyaokoa masikio yake ya asili.
Viongozi walivyolaani tukio hilo
Waziri wa Kilimo wa Afrika Kusini, Willie Aucamp, alilaani shambulio hilo akisema hakuna nafasi nchini humo kwa vitendo vya kikatili na visivyo na sababu kama hivyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Polisi, Ian Cameron, aliwapongeza polisi kwa kufanya ukamataji wa haraka na kusisitiza umuhimu wa uchunguzi wa kina ili kuhakikisha haki inatendeka.
Washukiwa hao watano, wenye umri wa kati ya miaka 26 na 56, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne wakikabiliwa na mashtaka ya uvamizi wa nyumba kwa kutumia silaha, jaribio la mauaji na kumiliki silaha pamoja na risasi kinyume cha sheria.
Mjadala kuhusu mashambulizi ya wakulima
Baadhi ya makundi ya mrengo wa kulia yamekuwa yakitumia mashambulizi dhidi ya wakulima weupe, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Waafrikaans, kudai kuwa kuna mauaji ya halaiki dhidi ya wazungu nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, madai hayo yamekataliwa na vyama vyote vya siasa nchini humo, ikiwemo vile vinavyowakilisha jamii ya Waafrikaans.
Takwimu za hivi karibuni za uhalifu nchini Afrika Kusini zinaonyesha kuwa wahanga wengi wa uhalifu, ikiwemo kwenye mashamba, ni watu weusi. Aidha, takwimu hizo hazionyeshi ongezeko maalum la mashambulizi dhidi ya wakulima weupe.
Urusi na Ukraine zajibu tahadhari za uongo zilizosambazwa

Chanzo cha picha, Reuters
Urusi
Wizara ya Dharura ya Urusi ilitangaza kuwa programu yake ya simu ililengwa na shambulio kubwa la mtandao saa chache baada ya mfumo wa tahadhari wa Ukraine pia kuathiriwa. Haijulikani kama matukio hayo mawili yanahusiana.
Katika ujumbe kwenye Telegram, wizara hiyo ilisema washambuliaji walipata uwezo wa kusambaza taarifa za uongo kwa umma kupitia programu hiyo. Iliongeza kuwa hatua zilikuwa zinaendelea kurekebisha dosari hiyo na kurejesha huduma katika hali ya kawaida.
Takriban dakika 90 baadaye, ilisema udukuzi huo haukuathiri na hauwezi kuathiri mfumo rasmi wa tahadhari kwa umma. Wizara hiyo ilieleza kuwa njia kuu za kutoa tahadhari ni ving'ora, vipaza sauti, ujumbe mfupi wa simu (SMS), pamoja na matangazo ya redio na televisheni, huku programu hiyo ikiwa ni huduma ya ziada ya taarifa.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ukraine
Huduma ya Dharura ya Ukraine baadaye ilichapisha ujumbe kwenye Telegram, ikiwataka wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa kupitia vipaza sauti na kuepuka kubofya viunganishi ambavyo chanzo chake hakijulikani.
“Mfumo wa kitaifa wa kutoa tahadhari unaendelea kufanya kazi kama kawaida,” ilisema huduma hiyo.
Waukraine wapokea mfululizo wa tahadhari za dharura za uongo
Tahadhari hizo za uongo zilianza kusambazwa majira ya saa 22:47 (20:47 GMT) Jumapili, huku tahadhari za mashambulizi ya anga za kiwango cha juu zikionekana kutumwa kote nchini Ukraine kwa lugha ya Kiukraine.
Tahadhari nyingine zilitumwa kwa wakazi wa Kyiv, ya kwanza ikisema:
"Tishio la mionzi. Tishio la mionzi limetangazwa mjini Kyiv."
Dakika moja baadaye, saa 22:48, ujumbe mwingine uliandikwa kwa Kirusi ukisema:
"Habari! Kutakuwa na tahadhari ya nyuklia kote Ukraine. Msijali, ni Oreshnik tu inapaa."
Oreshnik ni jina la kombora la masafa ya kati la Urusi linaloweza kubeba vichwa vya nyuklia au vya kawaida vya vilipuzi.
Tahadhari ya tatu, iliyotumwa saa 22:49 kwa lugha ya Kiukraine, ilisema:
"Tishio la kemikali. Kuna hatari ya shambulizi la kemikali mjini Kyiv. Msitoke nje."
Pia saa 22:49, tahadhari ya nne ilidai kuwa:
"Kuna tishio la mapigano mitaani. Mapigano yanaendelea mjini Kyiv. Msitoke nje."
Baadaye, saa 23:53, watumiaji walipokea mfululizo wa ujumbe wa kuondoa tahadhari hizo, kila mmoja ukieleza kuwa tishio husika lilikuwa limekwisha.
Kwa upande wa Urusi, taarifa kuhusu ujumbe uliosambazwa ni chache. Hata hivyo, kama ilivyoripotiwa awali, kundi la ujasusi la Ukraine lilidai kuwa tahadhari za uongo kuhusu mashambulizi ya nyuklia ndani ya Urusi pia zilitumwa kwa watumiaji wa baadhi ya mifumo ya tahadhari.
Soma Zaidi:
Iraola: Nitaanza kuwaambia wachezaji wangu wajiangushe tupate penati

Chanzo cha picha, Getty Images
Kocha wa Liverpool, Andoni Iraola, amesema atawaambia wachezaji wake kujiangusha wanapochezewa rafu ndani ya eneo la hatari baada ya timu hiyo kunyimwa mkwaju wa penati katika mchezo dhidi ya Arsenal uliomalizika kwa ushindi wa Arsenal wa bao 1-0 Jumapili.
Liverpool ikiwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa na Kai Havertz, Jurrien Timber alimvuta jezi mshambuliaji wa Liverpool, Alexander Isak alipokuwa akienda kuwania mpira wa kichwa uliopigwa na Bradley Barcola katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, mshambuliaji huyo hakuanguka, aliendelea kusimama na mwamuzi Andy Madley hakutoa penati.
Mwamuzi wa VAR, Stuart Attwell, aliamua kuwa tukio hilo halikuwa na uzito wa kutosha kubadilisha uamuzi wa mwamuzi wa uwanjani. Lakini Iraola hakukubaliana na uamuzi huo, akisema kulikuwa na kitendo cha wazi cha kuvutwa jezi ya Isak kilichomzuia kuucheza mpira ama kufunga. Alisema kama mshambuliaji huyo angeanguka chini, Liverpool ingepewa penati kwa asilimia 100.
Akizungumza na BBC Sport, Iraola alisema ni jambo la kusikitisha kulazimika kuwaambia wachezaji kuanguka ili waamuzi watoe penati, huku akisisitiza kuwa Isak alikuwa mwaminifu na alijaribu kuucheza mpira badala ya kuanguka. Aliongeza kuwa makocha wanapaswa kuwaambia wachezaji wao waanguke kwa sababu wasipofanya hivyo, waamuzi hawatoi penati.
Aliyekuwa mwamuzi msaidizi wa Ligi Kuu England, Darren Cann, alisema Timber alijiweka katika hatari kubwa kwa kuivuta jezi ya Isak na kwamba tukio hilo lingeweza kuwa penati.
Televisheni ya taifa China yasitisha matangazo ya mechi za La Liga kufuatia utani wa Mbappé

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la utangazaji la televisheni la China, CCTV, halikuonyesha mechi ya Real Madrid iliyochezwa Jumapili, licha ya mshambuliaji nyota wa klabu hiyo, Kylian Mbappé, kuomba radhi kuhusu matamshi yake aliyokiri kuwa hayakuwa ya busara kuhusu aliyekuwa kiongozi wa China, Mao Zedong.
Mbappé alikosolewa vikali baada ya kusema kuwa picha ya kuchekesha zaidi kwake ni ile inayoweka uso wake kwenye mwili wa dikteta wa China anayefanana na Mao.
China Media Group, ambayo ni mmiliki wa CCTV, ilitangaza Jumanne iliyopita kuwa itasitisha matangazo ya mechi za Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, kufuatia malalamiko yaliyoibuliwa na kauli hiyo. Tukio hilo pia limesababisha baadhi ya kampuni za China kusitisha ushirikiano wao na Mbappé.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema imepokea kwa uzito ombi la radhi la Mbappé. Real Madrid na La Liga pia zimeomba radhi.
Awali, China Media Group ilikuwa imetaka pande zote tatu ziombe radhi, ikisema hilo lilikuwa sharti la msingi ili kuhitimisha suala hilo.
Shirika hilo limepokea maombi hayo ya radhi, lakini halijatoa maelezo kuhusu muda ambao kusitishwa kwa matangazo hayo kutaendelea.
Mbappé, ambaye anaripotiwa kutoa kauli hiyo alipokuwa akishiriki katika kipindi cha mazungumzo cha televisheni cha Ufaransa, The Bridge, aliomba radhi baadaye siku hiyo ya Jumanne.
“Kauli yangu haikuwa ya busara, na sasa ninaelewa kuwa iliwaumiza watu wengi nchini China na katika jamii za Wachina duniani kote,” alisema.
Utani huo haukupokelewa vizuri nchini China, ambako Mao anaheshimiwa na Chama cha Kikomunisti, licha ya kuhusishwa na moja ya vipindi vilivyogharimu maisha ya watu wengi zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Katika mechi ya Jumapili, Real Madrid iliifunga Racing Santander mabao 3 kwa 0. Mbappé, Jude Bellingham na Yan Diomande walifunga mabao hayo.
Soma Pia:
Uganda yaanza kuwaondoa wanajeshi wake Somalia baada ya miaka 20

Chanzo cha picha, AFP
Uganda imeanza rasmi kuwaondoa wanajeshi wake nchini Somalia kwa awamu na kwa sehemu, baada ya takribani miongo miwili ya kushiriki katika operesheni za kijeshi za kuimarisha usalama katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Kikosi cha kwanza chenye wanajeshi 109 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) kinaripotiwa kuondoka mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, siku ya Ijumaa. Kuondoka kwao kumekuja baada ya mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kutangaza kuwa nchi hiyo imeanza kuondoa vikosi vyake Somalia.
“Kama tulivyoahidi, tumeanza kuwaondoa wanajeshi wa UPDF kutoka Somalia. Baada ya miaka 20 ya umwagaji mkubwa wa damu na kujitolea, tunakabidhi jukumu la usalama kwa ndugu zetu Wasomali,” Jenerali Muhoozi aliandika kwenye mtandao wa X.
Msemaji kaimu wa jeshi la Uganda, Chris Magezi, hakujibu ombi la BBC la kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Uganda ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kupeleka wanajeshi Somalia chini ya operesheni ya awali ya Umoja wa Afrika nchini humo, iliyojulikana kama AMISOM.
Wanajeshi wake walipigana pamoja na Jeshi la Taifa la Somalia dhidi ya kundi la wanamgambo wa Al Shabaab, wakisaidia kurejesha maeneo muhimu yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi hilo na kulinda miundombinu muhimu ya serikali.
Mwaka 2024, operesheni ya AMISOM ilibadilishwa na kuwa Misheni ya Umoja wa Afrika ya Kusaidia na Kuleta Utulivu Somalia (AUSSOM). Misheni hiyo mpya inalenga kuimarisha taasisi za usalama za Somalia na kuandaa vikosi vya ndani ili hatimaye viweze kuwajibika kikamilifu kwa usalama wa nchi hiyo.
Hata hivyo, Uganda haijamaliza kabisa ushiriki wake wa kijeshi nchini Somalia. Uondoaji unaoendelea ni sehemu ya kupunguza idadi ya wanajeshi wake walioko nchini humo chini ya makubaliano tofauti ya kijeshi kati ya Kampala na Mogadishu.
Uganda itaendelea kuchangia wanajeshi katika misheni ya usalama nchini Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Afrika.
Waislamu watatu wahukumiwa kifungo cha maisha nchini India kwa kuchinja ng'ombe

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama moja katika mji wa Gandhinagar, jimbo la Gujarat nchini India, imewahukumu Waislamu watatu kifungo cha maisha jela kwa kosa la kuchinja ng'ombe.
Katika hukumu yake, mahakama ilirejelea maandiko matakatifu ya dini ya Kihindu, yakiwemo Manu Smriti na Vedas, kueleza umuhimu wa ng'ombe katika imani hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Press Trust of India, Naibu Waziri Mkuu wa jimbo la Gujarat, Harish Singhvi, amepongeza uamuzi huo akisema unatuma ujumbe ulio wazi kuwa sheria za jimbo hilo hazitawasamehe wanaochinja ng'ombe.
Katika hukumu iliyotolewa Jumatatu, Jaji B.R. Rajput aliwaamuru washtakiwa hao kulipa faini ya rupia 300,000 za India, pamoja na adhabu ya kifungo cha maisha.
Mahakama ilisema katika uamuzi wake kuwa iwapo watu wanaotuhumiwa kwa makosa hayo hawataadhibiwa kwa mujibu wa sheria, ng'ombe anayeheshimiwa kama mtakatifu katika imani ya Kihindu, anayejulikana kama “Gau Mata”, huenda akatoweka duniani kadiri muda unavyopita.
Katika uamuzi mwingine, mahakama hiyo pia iliwaadhibu washtakiwa kwa kifungo cha miaka 10 jela na faini ya rupia 100,000 kila mmoja, chini ya Sheria ya Ulinzi wa Wanyama ya Gujarat ya mwaka 1954.
Hata hivyo, adhabu hizo zitatekelezwa kwa wakati mmoja.
Uamuzi huo wa mahakama pia umeibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku watumiaji mbalimbali wakitoa maoni yao.
Mtumiaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Satya aliutetea uamuzi huo, akisema washtakiwa wana haki ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Mtumiaji mwingine, J. Mehta, pia aliunga mkono uamuzi huo, akisema hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya wachinjaji na wafanyabiashara wanaouza nyama kando ya barabara.
Urusi na Ukraine zakumbwa na mashambulizi ya kimtandao

Chanzo cha picha, Getty Images
Programu za tahadhari za dharura nchini Ukraine na Urusi zimedukuliwa katika mashambulizi ya kimtandao, kwa mujibu wa taarifa kutoka pande zote mbili.
Ujumbe wa kupotosha uliotumwa kupitia programu ya tahadhari ya dharura ya Urusi uliwaonya watumiaji kuwa vichwa vya silaha za nyuklia vilivyofungwa kwenye ndege zisizo na rubani aina ya P1-Sun za Ukraine vilikuwa vimerushwa kuelekea maeneo yote ya Urusi.
Ujumbe huo ulianza kwa kuwaambia wakazi kuwa kulikuwa na hatari ya kushambuliwa, kabla ya kuwataka kujipatia chakula cha kutosha kwa wiki tatu na kujificha.
Wakati huo huo, Kituo cha Mawasiliano ya Kimkakati cha Ukraine kimeilaumu Urusi kwa kudukua programu ya tahadhari ya mashambulizi ya anga nchini humo.
Katika ujumbe kiliochapisha kwenye mtandao wa X, kituo hicho kilichapisha picha za baadhi ya jumbe zisizo za kawaida zilizoonekana kwenye programu hiyo na kuwaonya wakazi wazipuuze.
Kituo hicho pia kilisema mojawapo ya jumbe hizo ilikuwa imeandikwa kwa lugha ya Kirusi na ilihusu silaha aina ya Oreshnik.
Saa chache baadaye, Moscow nayo ilitangaza kuwa programu yake ya tahadhari za dharura ilikuwa imeshambuliwa katika tukio ililolitaja kuwa shambulizi kubwa la kimtandao. Hata hivyo, haikubainisha mara moja ni nani aliyekuwa nyuma ya shambulizi hilo.
Jumbe hizo za uongo zilitumwa dakika chache kabla ya kumalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika mji wa Oleshky, ulio mstari wa mbele nchini Ukraine na ambao umekuwa chini ya udhibiti wa Urusi tangu mwaka 2022.
Makubaliano hayo ya nadra ya kusitisha mapigano kwa siku sita yaliwezesha mamia ya watu kuondoka katika mji huo. Makubaliano hayo yalifikiwa kwa usaidizi wa Mke wa Rais wa Marekani, Melania Trump, na Papa Leo wa 14.
Huo ulikuwa muda mrefu zaidi ambao usitishaji mapigano ulikuwa umedumu tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili nchini Ukraine.
Urusi yaanza majadiliano ya kujenga mitambo ya nyuklia katika nchi nne za Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi inafanya mazungumzo na Uganda, Ghana, Ethiopia na Misri kuhusu uwezekano wa kujenga mitambo mikubwa ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia, kwa mujibu wa mkuu wa shirika la serikali la nishati ya nyuklia la nchi hiyo, Rosatom.
Mkurugenzi Mkuu wa Rosatom, Alexei Likhachev, amesema Urusi iko tayari kushirikiana na nchi za Afrika kuanzisha mitambo ya nyuklia yenye ukubwa na mifumo mbalimbali, kulingana na mahitaji ya kila nchi.
Akizungumza Ijumaa, Likhachev alisema ushirikiano huo haujafungamanishwa na mradi mmoja wa aina moja, bali unazingatia mazingira na mahitaji mahususi ya kila nchi.
“Ushirikiano wetu umejengwa katika msingi kwamba Afrika ina nchi zenye mahitaji na mazingira tofauti. Kwa hiyo, tunafuata mkakati maalumu kwa kila nchi, ambao hauishii katika mradi mmoja pekee,” alisema.
Ushirikiano katika sekta ya nishati ya nyuklia ulikuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika Mkutano wa Urusi na Afrika uliofanyika mjini Moscow wiki jana.
Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi kutoka takribani nchi 50 za Afrika, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali.
Jukwaa hilo, lililoanzishwa mwaka 2019, ni sehemu ya juhudi za Urusi za kuimarisha uhusiano wake wa kisiasa na kiuchumi na nchi za Afrika.
Baada ya mkutano huo, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema nchi za Afrika zimeonyesha nia kubwa ya kushirikiana na Urusi katika ujenzi wa mitambo ya kuzalisha nishati ya nyuklia, teknolojia ndogo za nyuklia na matumizi ya teknolojia hiyo katika sekta za tiba na kilimo.
Soma Pia:
Watu tisa wafariki dunia baada ya ndege kuanguka Florida

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege ya kibinafsi iliyokuwa imewabeba watu tisa imeanguka katika eneo la Palm Beach, jimbo la Florida nchini Marekani, na kusababisha vifo vya wote waliokuwamo ndani yake.
Ajali hiyo ilitokea Jumapili jioni, Novemba Mosi, umbali wa takribani kilomita 12 kutoka katika makazi ya mapumziko ya Mar-a-Lago yanayomilikiwa na Rais Donald Trump. Mamlaka zimeitaja ajali hiyo kuwa ya kutisha.
Utambulisho wa abiria waliokuwa ndani ya ndege hiyo bado haujatangazwa rasmi. Ndege hiyo, inayoripotiwa kuwa aina ya Learjet 60, ilikuwa ikisafiri kutoka jimbo la Texas kuelekea Bahamas.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) imesema imetuma timu ya wataalamu katika eneo la ajali kuchunguza chanzo chake.
Picha zilizochukuliwa katika eneo la tukio zinaonyesha mabaki ya ndege yaliyoteketea kwa moto pamoja na shimo lililotokana na athari za kugonga ardhi.
Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani pamoja na uchambuzi wa takwimu za safari ya ndege zinaashiria kuwa ndege hiyo ilikuwa ikipoteza mwinuko kwa kasi ya mamia ya futi kwa sekunde kabla ya kuanguka.
Video ambayo haijathibitishwa, iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na inayoonekana kurekodiwa na kamera ya gari, inaonyesha wakati ndege hiyo ilipoanguka. Katika video hiyo, magari yanaonekana yakipita kwenye barabara ya makazi katika viunga vya mji, kabla ndege hiyo haijaanguka kwa ghafla ikiwa imeelekeza pua yake chini. Mlipuko mkubwa unafuata, huku moto na vipande vya mabaki vikirushwa hewani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano ulioitishwa baada ya ajali hiyo, Gavana wa Florida, Ron DeSantis, amesema video hiyo inashtua.
“Unapoitazama video hii, kwa kweli inashtua sana. Ni kana kwamba kombora linashuka kutoka angani, kisha kunatokea mlipuko mkubwa na vipande vya mabaki kurushwa kila upande,” alisema DeSantis.
Soma Pia:
Tetesi za soka Jumatatu: Man Utd yammezea mate Balde wa Barcelona

Chanzo cha picha, Getty Images
Beki wa kushoto wa Barcelona, Alejandro Balde, huenda akaondoka klabuni hapo katika dirisha la usajili la Januari, hatua inayoweza kuipa Manchester United nafasi ya kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania. (Record, via Marca - in Portuguese)
Manchester United imeonyesha kuvutiwa naye. Iwapo Balde ataondoka Barcelona, huenda klabu hiyo ya La Liga ikapata nafasi ya kumsajili beki wa Argentina, Lisandro Martinez, mwenye umri wa miaka 28, kutoka Manchester United. (Mirror)
Liverpool imewaorodhesha beki wa kati wa Nottingham Forest, Murillo, mwenye umri wa miaka 24, kutoka Brazil, na Nico Schlotterbeck wa Borussia Dortmund, mwenye umri wa miaka 26, kutoka Ujerumani, kama wachezaji wanaoweza kuchukua nafasi ya nahodha wake Virgil van Dijk, mwenye umri wa miaka 35, kutoka Uholanzi. (Caught Offside)
Manchester United huenda ikamuuza kiungo wa kati Bruno Fernandes, mwenye umri wa miaka 32, kutoka Ureno, badala ya kumruhusu kuondoka bure mkataba wake utakapomalizika majira ya kiangazi mwakani.(Mail - subscription required)
Real Madrid inamfuatilia kipa wa Brighton, Bart Verbruggen, mwenye umri wa miaka 24, kutoka Uholanzi, kama mrithi wa baadaye wa Thibaut Courtois, mwenye umri wa miaka 34, kutoka Ubelgiji. (Fichajes - in Spanish)
Mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, mwenye umri wa miaka 29, huenda akatafuta kuondoka klabuni hapo iwapo hatapewa nafasi ya kucheza mara kwa mara baada ya kurejea kutoka kwenye jeraha. (Football Insider)
Tottenham bado inavutiwa na kiungo wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs-White, mwenye umri wa miaka 26, kutoka England, na huenda ikawasilisha ofa ya kumsajili katika dirisha la Januari.(Football Insider)
Barcelona na Real Madrid zinaendelea kumuwania beki wa kulia wa Tottenham na timu ya taifa ya Hispania, Pedro Porro, mwenye umri wa miaka 27.Bei ya pauni milioni 62 inayotajwa na Tottenham haijaonekana kuzizuia klabu hizo. (Sport - in Spanish)
Mshambuliaji wa Monaco, Folarin Balogun, mwenye umri wa miaka 25, kutoka Marekani, huenda akaondoka klabuni hapo Januari. Manchester United ni miongoni mwa klabu zinazotajwa kuwa zinaweza kumsajili. (Teamtalk)
Arsenal inakabiliwa na ushindani kutoka AC Milan, Aston Villa na Roma katika jitihada za kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Endrick, mwenye umri wa miaka 20, kutoka Brazil. (Calcio Mercato - in Italian)
Tottenham, Manchester City na Manchester United ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia beki wa Villarreal, Alex Freeman, mwenye umri wa miaka 22, kutoka Marekani.(Football Insider)
Soma pia:
Kaka wa Tundu Lissu kuzikwa baada ya hukumu ya kesi ya uhaini

Chanzo cha picha, Mitandaoni
Mazishi ya Alute Mughwai Lissu, kaka yake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, yameahirishwa hadi baada ya Novemba 6, 2026, siku ambayo ndugu yao anatarajiwa kusomewa hukumu katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Familia imeamua kusogeza mbele mazishi hayo ili wanafamilia wapate fursa ya kufika Dar es Salaam kuhudhuria usomaji wa hukumu hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Dk. Vincent, ambaye ni mmoja wa ndugu wa familia hiyo, amesema wamekubaliana kufanya mazishi baada ya tukio hilo muhimu, akieleza kuwa wanataka kwanza kuwa pamoja wakati wa kusikiliza hukumu ya ndugu yao.
“Tumepanga mazishi ya kaka Alute yatafanyika Singida. Tunatarajia tutasukuma mbele mazishi ili Ijumaa (Novemba 6, 2026), wanafamilia tuweze kuwepo Dar es Salaam kuhudhuria hukumu ya kesi ya ndugu yetu Tundu,” amesema.
Alute alikuwa akiugua kwa muda mrefu. Katika siku zake za mwisho, alilazwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha, hali yake ilizidi kuwa mbaya kuanzia juzi kabla ya kufariki dunia Jumamosi usiku.
Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika katika kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, baada ya familia kushiriki katika usomaji wa hukumu ya kesi ya Tundu Lissu.
Lissu amekuwa mahabusu tangu Aprili mwaka 2025, akikabiliwa na shtaka la uhaini. Hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kutolewa Novemba 6, 2026.
Unaweza kusoma;
Iran: Hormuz kufunguliwa ndani ya siku mbili iwapo Marekani itatimiza masharti yake

Chanzo cha picha, Reuters
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa mpango wa siku saba uliopendekezwa na Iran umepunguzwa hadi siku mbili.
Amesema iwapo Marekani itatimiza masharti ya Iran siku ya kwanza, basi Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa siku inayofuata.
Kauli za Araqchi zinakuja wakati meli kadhaa za mafuta na gesi zikishambuliwa katika Ghuba ya Uajemi. Miongoni mwa meli zilizolengwa ni moja iliyokuwa imebeba gesi ya Qatar, tukio lililolaaniwa vikali na wadau mbalimbali.
Akizungumza Jumapili, Araqchi alisema kuwa hakukuwa na mpango wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani wakati wa ziara yake.
Alisema mashauriano kuhusu mpango huo wa siku mbili yanaendelea kati ya Iran na wapatanishi, huku pande hizo zikielekea kuutekeleza. Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado hakuna makubaliano ya mwisho yaliyofikiwa.
Aliongeza kuwa kufikiwa kwa maridhiano kutategemea majibu yatakayotolewa na upande wa pili kuhusu maswali yaliyowasilishwa na Iran.
Araqchi alisisitiza tena kuwa Iran iko tayari kujilinda pamoja na kushiriki katika diplomasia.
Alisema njia ambayo Marekani itaamua kufuata itategemea busara na uamuzi wake.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 02/11/2026.



















