China: Jinsi Mbappé alivyozua hasira ambayo wengi hawakujua chanzo chake

Wapita-njia wanapita karibu na tangazo la kinywaji chenye elektroliti linalomwonyesha mchezaji wa soka wa Ufaransa, Kylian Mbappé, katika njia ya chini ya ardhi jijini Shanghai, Uchina, mnamo Juni 30, 2026.
    • Author, Fan Wang
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kylian Mbappé ni mmoja wa wanasoka maarufu zaidi duniani. Lakini mzaha alioufanya kuhusu picha yake iliyochanganywa na sura ya kiongozi wa zamani wa China, Mao Zedong, ulimweka katikati ya utata mkubwa nchini humo.

Kampuni zilivunja ushirikiano wa kibiashara naye, matangazo ya mechi za ligi ya Uhispania (La Liga) yakasitishwa na hatimaye mchezaji huyo akaomba radhi.

Hata hivyo, kulikuwa na jambo lisilo la kawaida katika mjadala huo: wakati hasira dhidi yake zikiongezeka kwenye mitandao ya kijamii nchini China, watumiaji wengi hawakujua hasa alikuwa amesema nini.

Utata huo ulianza Jumatatu usiku, wakati Mbappé akihudhuria hafla ya tuzo za Ballon d'Or jijini London. Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonyesha akitania kuhusu picha ya mtandaoni (meme) aliyosema humfanya acheke zaidi. Katika picha hiyo, uso wake ulikuwa umewekwa juu ya sura ya Mao Zedong.

Mjadala ulienea haraka nchini China, huku baadhi ya kampuni zikisitisha ushirikiano wao na nyota huyo. Wakati huohuo, China Media Group, shirika mama la televisheni ya taifa ya CCTV, lilisitisha matangazo ya mechi za La Liga.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema kuwa kauli au vitendo vinavyodaiwa kuumiza hisia za Wachina hukumbana na upinzani kutoka kwa jamii.

Lakini licha ya hasira hizo, wengi wa watumiaji wa mitandao hawakueleza wazi kilichokuwa chanzo cha malalamiko hayo, wala kutaja moja kwa moja jina la Mao Zedong.

Mfumo wa udhibiti wa habari nchini China, ambao unazuia upatikanaji wa baadhi ya maudhui kutoka kwenye intaneti ya kimataifa kwa watu wake wapatao bilioni 1.4, ulifanya iwe vigumu kwa wengi kufahamu kilichotokea.

Mpappe
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tuhuma kwamba Mbappé alikuwa ameumiza hisia za Wachina zilitosha kuchochea hasira, huku mifumo ya algoriti kwenye mitandao ya kijamii ikiendeleza mjadala huo katika mazingira ambamo watu wanaweza kuogopa kutoa maoni yanayopingana na mtazamo wa wengi.

Haikuchukua muda mrefu kabla ya Mbappé kutoa tamko la kuomba radhi "kwa dhati" kutokana na kauli yake ambayo alisema "haikufikiriwa vyema".

Klabu yake, Real Madrid, pamoja na La Liga, nazo ziliomba radhi. China ni soko kubwa kwa soka, jambo linalofanya utata wa aina hii kuwa na athari za kibiashara.

Baadaye, Beijing ilithibitisha kuwa inachukulia ombi la radhi la mchezaji huyo "kwa uzito". Hata hivyo, China Media Group bado haijatoa tamko kuhusu iwapo matangazo ya La Liga yatarejea.

Wakati huohuo, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii waliendelea kudai hatua kali zaidi dhidi ya Mbappé.

"Kuomba radhi ni jambo la msingi alilopaswa kufanya, lakini hiyo haitoshi kunifanya nimsamehe. Naunga mkono apigwe marufuku," lilisema moja ya maoni yaliyopata uungwaji mkono mkubwa kwenye Weibo.

Kwa nini jina la Mao halikutajwa wazi?

Nchini China, ni kosa kisheria ''kuwadhalilisha'' au ''kuwachafua'' sifa za wale wanaotambuliwa kuwa mashujaa wa vita na vielelezo vya kihistoria vya Chama cha Kikomunisti.
Maelezo ya picha, Nchini China, ni kosa kisheria ''kuwadhalilisha'' au ''kuwachafua'' sifa za wale wanaotambuliwa kuwa mashujaa wa vita na vielelezo vya kihistoria vya Chama cha Kikomunisti.

Katika mahojiano hayo, Mbappé hakumtaja Mao Zedong kwa jina. Hata hivyo, kwa baadhi ya Wachina, mzaha wowote unaomhusisha mwanzilishi wa China ya Kikomunisti ulionekana kuvuka mipaka.

"Je, unajua umemdhalilisha nani? Yeye ni nguzo ya kiroho ya watu wa China," ilisema moja ya maoni maarufu kwenye Weibo.

Mtumiaji mwingine aliandika kuwa Mao ni mmoja wa watu muhimu zaidi katika historia ya taifa hilo na kwamba kuomba radhi pekee hakutoshi kurekebisha kilichotokea.

Cha kushangaza ni kwamba, wakati hasira hizo zikiendelea kuongezeka, baadhi ya Wachina waliendelea kutafuta kujua Mbappé alisema nini hasa.

Baadhi yao walielekea kwenye majukwaa ya mazungumzo yanayotumia akili mnemba (AI), lakini mifumo hiyo, ambayo nayo inafanya kazi chini ya masharti ya udhibiti wa taarifa nchini China, haikutoa majibu ya moja kwa moja.

Wengine walijaribu kueleza kilichotokea, lakini waliepuka kulitaja jina la Mao. Badala yake, walitumia mafumbo kama vile "mtu aliye kwenye noti ya yuan 100" au "Mwalimu", mojawapo ya majina ambayo Mao aliwahi kutumia kujitambulisha.

Picha za skrini za meme hiyo na mahojiano ya Mbappé zilisambazwa mtandaoni, lakini baadhi zilikuwa zimehaririwa, huku neno "dikteta" na sura ya mchezaji huyo zikififishwa au kufichwa.

Hata taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China pamoja na maombi ya radhi yaliyotolewa na Mbappé, Real Madrid na La Liga hayakumtaja Mao kwa jina.

Mao, aliyeongoza Chama cha Kikomunisti cha China kushinda vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuanzisha Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949, alifariki mwaka 1976.

Licha ya urithi wake wenye sura mbili, bado ni mmoja wa viongozi wanaoheshimiwa zaidi nchini China. Sera zake, zikiwemo Great Leap Forward na Mapinduzi ya Utamaduni, zinahusishwa na vifo vya mamilioni ya watu na machafuko makubwa ya kijamii.

Hata hivyo, nafasi yake katika kuasisi China ya kisasa imemfanya aendelee kuwa mtu muhimu katika simulizi rasmi la historia ya taifa hilo.

Nchini China, ni kosa kisheria kuwadhalilisha au kuchafua sifa za watu wanaotambuliwa kuwa mashujaa wa vita na vielelezo vya kihistoria vya Chama cha Kikomunisti.

Picha ya Mao bado inaonekana katika sehemu mbalimbali nchini humo, ikiwemo eneo la Uwanja wa Tiananmen jijini Beijing, ambako inaashiria nafasi yake ya kipekee katika historia ya China.

Tofauti na viongozi wengine wa zamani wa China, mwili wake uliohifadhiwa unaonyeshwa hadharani katika eneo hilo na kuvutia maelfu ya wageni kila siku.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa pia na mwamko mpya wa kumvutia miongoni mwa vijana, ambao husoma maandiko yake na kutazama maudhui yanayomhusu kwenye mitandao ya kijamii.

Vitabu vya historia nchini China kwa kiasi kikubwa hupunguza uzito wa maafa yaliyotokea wakati wa utawala wake. Mtazamo rasmi wa Chama cha Kikomunisti ni kwamba mafanikio ya Mao yalizidi makosa yake.

Kwa chama hicho, Mao anasalia kuwa "mwanamapinduzi mkuu na M-Marxist mkuu", sifa zinazoonyesha nafasi yake katika historia rasmi ya taifa hilo.

Screengrab from Weibo
Maelezo ya picha, Watumiaji wa Weibo walieneza video hiyo kwa kuficha picha iliyozua mjadala na kuondoa marejeleo ya Mao.

Mitazamo tofauti ndani na nje ya China

Mchoro huu unaoonyesha picha unaonyesha akaunti ya Weibo—mtandao wa kijamii wa China—ya nyota wa soka wa Ufaransa, Kylian Mbappe, ikiwa na ujumbe unaosomeka: "Mtumiaji huyu amezuiwa kufuatilia wengine kutokana na kukiuka sheria za Kanuni za Jumuiya ya Weibo."
Maelezo ya picha, Akaunti ya Mbappé kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo ilizuiwa kupokea wafuasi wapya siku ya Jumanne.

Wakati baadhi ya Wachina walipokuwa wakimtaka Mbappé achukuliwe hatua kali, maoni kutoka kwa Wachina wanaoishi nje ya nchi yalikuwa tofauti kwa kiasi kikubwa.

Kwa baadhi ya wanaharakati na familia zilizokimbia China wakati wa utawala wa Mao, kiongozi huyo anakumbukwa zaidi kwa ukandamizaji na mateso yaliyotokea chini ya uongozi wake.

Chini ya taarifa ya Mbappé kwenye mtandao wa X, ambao haupatikani ndani ya China, baadhi ya watumiaji walimuunga mkono mchezaji huyo.

"Huna haja ya kuomba radhi; hukufanya kosa lolote," liliandika moja ya maoni yaliyopata uungwaji mkono mkubwa.

Mtumiaji mwingine aliandika kuwa ni Chama cha Kikomunisti cha China kinachopaswa kuomba radhi kwa kile alichokitaja kuwa udhibiti na propaganda vilivyowekwa kwa wananchi kwa miongo mingi.

Kwenye X na Threads, majukwaa ambayo hayapatikani ndani ya China, utata huo uliibua wimbi jipya la meme. Baadhi zilionyesha uso wa Mbappé ukiwekwa kwenye picha mbalimbali za Mao, huku nyingine zikimwonyesha akiwa na mwili wa rais wa sasa wa China, Xi Jinping.

Picha hii inaonyesha kampeni ya matangazo ya chapa ya bidhaa za maziwa ya China, 'Mengniu', inayowashirikisha nyota wa soka Kylian Mbappe wa Ufaransa (katikati), Lionel Messi wa Argentina (kushoto), na Lamine Yamal wa Uhispania, katika duka kubwa jijini Beijing mnamo tarehe 28 Oktoba 2026.
Maelezo ya picha, Mengniu, kampuni kubwa ya bidhaa za maziwa nchini China ilisitisha ushirikiano wake na Mbappé baada ya kuzuka kwa malalamiko makali.

Wakati huo huo, kampuni kubwa ya bidhaa za maziwa nchini China, Mengniu, ilisimamisha ushirikiano wake na Mbappé baada ya malalamiko makali.

Nje ya China, sehemu kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walionekana kushangazwa na ukubwa wa hasira na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mchezaji huyo.

"Ni vigumu kuelewa hasira hizi. Inaonekana watu hawaruhusiwi kuwakosoa viongozi wao, lakini bado wanatarajia wengine wafikiri kama wao," liliandika moja ya maoni yaliyoungwa mkono zaidi chini ya chapisho la Real Madrid la kuomba radhi kwenye Instagram.

"Kumuita dikteta kuwa dikteta sasa ni kosa?" alihoji mtumiaji mwingine kwenye X.

Wakati huo huo, akaunti ya Mbappé kwenye mtandao wa Weibo ilizuiwa kupokea wafuasi wapya siku ya Jumanne.

Hata hivyo, nje ya China, sehemu kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walionekana kushangazwa na ukubwa wa mjadala huo na hatua zilizochukuliwa dhidi ya Mbappé.

"Ni vigumu kuelewa hasira hizi. Inaonekana watu hawaruhusiwi kuwakosoa viongozi wao, lakini bado wanatarajia wengine wafikiri kama wao," liliandika moja ya maoni yaliyoungwa mkono zaidi chini ya chapisho la Real Madrid la kuomba radhi kwenye Instagram.

"Kumuita dikteta kuwa dikteta sasa ni kosa?" alihoji mtumiaji mwingine kwenye mtandao wa X.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi