Israel: Kwa nini Netanyahu anadai vyama vya Waarabu viliiba uchaguzi?

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Tom Bennett
- Akiripoti kutoka, Jerusalem
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Israel, Gadi Eisenkot, pamoja na viongozi wa vyama vinavyoongozwa na Waarabu, wamemshutumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa kujaribu kudhoofisha uhalali wa matokeo ya uchaguzi, baada ya muungano wake kushindwa kupata wingi wa viti bungeni.
Chama cha Likud cha Netanyahu kimevituhumu vyama vya Waarabu kwa "kuiba" uchaguzi, kikidai kuwa wapiga kura walihongwa ili kuvipigia kura. Shirika la usalama wa ndani la Israel, Shin Bet, linafanya uchunguzi kubaini iwapo kulikuwa na ufadhili haramu kutoka mataifa ya kigeni, yakiwemo Qatar na Uturuki.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imekanusha madai hayo iliyoyaita "ya kipuuzi na hatari", huku ikiishutumu Israel kwa kuendesha kampeni ya kusambaza taarifa za upotoshaji dhidi ya Doha.
Mzozo huo umeibuka wakati matokeo ya uchaguzi yakionyesha kuwa hakuna upande uliopata viti 61 vinavyohitajika kuunda serikali ya wengi katika bunge la Israel, Knesset.
Muungano wa Netanyahu umepata viti 53 kati ya 120, huku kambi ya upinzani inayoongozwa na Eisenkot ikipata viti 48. Vyama viwili vya Waarabu, The Joint List na Ra'am, vimepata viti 19, matokeo yanayovipa nafasi muhimu katika mazungumzo ya kuunda serikali ijayo.
Hali hiyo imezua mvutano mpya kuhusu nafasi ya vyama vya Waarabu katika siasa za Israel, huku kukiwa na maswali kuhusu iwapo kambi ya upinzani itakuwa tayari kushirikiana navyo ili kumaliza utawala wa Netanyahu.
Madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi

Chanzo cha picha, EPA
Mzozo ulizidi siku ya Alhamisi baada ya chama cha Likud kudai kuwa baadhi ya wapiga kura "walihongwa" ili kuvipigia kura vyama vya Waarabu.
Hatua hiyo ilifuatia ombi la mkuu wa Kamati Kuu ya Uchaguzi (CEC) kwa shirika la usalama wa ndani, Shin Bet, kuchunguza kile kilichoelezwa kuwa "tuhuma nzito" za kuingiliwa kwa uchaguzi na mataifa ya kigeni.
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa kamati hiyo iliwasilishwa madai kwamba Qatar ilitoa fedha kwa lengo la kuongeza idadi ya wapiga kura katika maeneo yenye jamii nyingi za Waarabu.
Hata hivyo, Qatar imekanusha madai hayo kwa nguvu. Wizara yake ya Mambo ya Nje ilisema madai hayo ni ya kipuuzi na hatari, na kuishutumu Israel kwa kutumia taarifa zisizo sahihi kuichafua nchi hiyo.
Vyama vya Waarabu pia vimekataa tuhuma hizo. Muungano wa The Joint List umesema madai hayo hayana msingi, huku viongozi wake wakisema yanatumiwa kupunguza umuhimu wa ushindi wao wa kisiasa.
Netanyahu na chama chake cha Likud wameelezea madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi kama "tetemeko la kisiasa" na "shambulizi dhidi ya demokrasia", wakidai kuwa hatua hizo zinalenga kuiondoa serikali yao ya mrengo wa kulia madarakani.
Hata hivyo, Shin Bet baadaye ilifafanua kuwa uchunguzi wake hauwahusishi wanajamii wote wa Kiarabu waliopiga kura kihalali. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kamati Kuu ya Uchaguzi, Dean Livne, pia alisema hakuna msingi wa madai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa kimfumo wa uadilifu wa uchaguzi.
Maelezo hayo yanaweka tofauti kati ya uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuingiliwa kwa uchaguzi na madai kwamba matokeo yote ya uchaguzi yalikiukwa. Hadi sasa, hakuna uthibitisho uliotolewa hadharani kwamba kura zilizopigwa na jamii za Waarabu zilipatikana kwa njia isiyo halali.
Kwa nini upinzani unasema Netanyahu anadhoofisha matokeo?
Wakosoaji wa Netanyahu wanaona kuwa madai dhidi ya vyama vya Waarabu yanaweza kuwa na athari zaidi ya uchunguzi wenyewe. Wanadai kuwa yanaweza kuifanya iwe vigumu kisiasa kwa Eisenkot kushirikiana na vyama hivyo, licha ya kuwa msaada wao ndio unaoweza kumpa kambi yake idadi ya kutosha kuunda serikali.
Eisenkot, ambaye alipewa taarifa kuhusu uchunguzi huo, alisema bado ni mapema kufikia hitimisho kuhusu madai hayo.
"Ni mapema mno kuamua kilichotokea, au iwapo kuna chochote kilichotokea," alisema.
Hata hivyo, alimtuhumu Netanyahu kwa kuendesha "kampeni iliyoratibiwa na kupangwa ya kudhoofisha uhalali wa matokeo ya uchaguzi".
Mwenyekiti wa chama cha Balad, Sami Abu Shehadeh, ambaye ni sehemu ya muungano wa The Joint List, pia alikataa madai ya Likud.
"Upande ulioshindwa unajenga tuhuma za chuki za kibaguzi na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kutumia nguvu ili kubatilisha matokeo ya uchaguzi," alisema.
Kwa upande wa wakosoaji wa Netanyahu, suala kubwa si tu iwapo kulikuwa na jaribio la kuingilia uchaguzi, bali pia namna madai hayo yanavyoweza kutumiwa katika mvutano wa kuunda serikali.
Kwa nini kura za Waarabu zimekuwa muhimu?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Waarabu wa Israel, ambao wengi wao hujitambulisha kama Wapalestina wenye uraia wa Israel, wanaunda takriban asilimia 20 ya wakazi wa nchi hiyo.
Kwa miaka mingi, ushiriki wao katika uchaguzi wa Israel umekuwa ukikabiliwa na changamoto, huku baadhi yao wakiamua kususia uchaguzi wakisema kushiriki katika upigaji kura kungehalalisha mfumo ambao, kwa mujibu wao, unawachukulia kama raia wa daraja la pili.
Malalamiko kuhusu ubaguzi na kutoshughulikiwa kwa mahitaji ya jamii za Waarabu yamekuwa miongoni mwa masuala yanayoathiri uhusiano wao na serikali za Israel.
Hata hivyo, katika uchaguzi huu, idadi ya wapiga kura kutoka jamii hizo iliongezeka kwa kiwango kikubwa, na kuchangia The Joint List na Ra'am kupata jumla ya viti 19 katika Knesset.
Ongezeko hilo limeelezwa kuwa lilichochewa kwa sehemu na hamu ya kuiondoa madarakani serikali ya Netanyahu, inayoongozwa na muungano wa mrengo wa kulia zaidi katika historia ya Israel.
Katika siku ya uchaguzi, Netanyahu alitumia muda mwingi kuchapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akielezea ongezeko la wapiga kura Waarabu kama "hali ya dharura" na "suala la uhai au kifo" kwa mrengo wa kulia nchini humo.
Pia alisambaza picha zilizotengenezwa kwa akili bandia (AI) zikionyesha wapiga kura Waarabu katika vituo vya kupigia kura, katika jaribio la kuwahamasisha wafuasi wa mrengo wa kulia kujitokeza kupiga kura.
Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha umuhimu wa kura hizo katika siasa za Israel. Ingawa vyama vya Waarabu havikupata viti vya kutosha kuunda serikali peke yao, idadi ya viti walivyoshinda inaweza kuamua ni upande gani utakaoweza kupata uungwaji mkono wa kutosha kuongoza nchi.
Je, Israel inaweza kupata serikali ya aina gani?
Matokeo ya uchaguzi yanaacha uwezekano wa aina tatu kuu za serikali kuundwa.
Uwezekano wa kwanza ni serikali ya umoja wa kitaifa itakayowajumuisha Netanyahu na Eisenkot. Serikali ya aina hiyo ingeweza kuunganisha baadhi ya vyama vya mrengo wa kulia na vya upinzani ili kupata wingi wa viti bungeni.
Uwezekano wa pili ni Netanyahu kuunda serikali mpya ya mrengo wa kulia kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge watakaohama kutoka kambi ya Eisenkot.
Hata hivyo, uwezekano wa tatu, ambao umeibua mjadala mkubwa zaidi, ni Eisenkot kuunda serikali itakayoungwa mkono na vyama vya Waarabu.
Kwa muda mrefu, viongozi wengi wa upinzani nchini Israel wamekuwa wakisita kushirikiana na vyama vya Waarabu katika kuunda serikali. Eisenkot na karibu kila mwanachama wa kambi yake, isipokuwa mmoja, wamewahi kukataa kuingia katika serikali pamoja na vyama hivyo.
Hata hivyo, hali ya sasa imeibua mijadala kuhusu uwezekano wa kubadilika kwa msimamo huo, kutokana na hesabu za viti bungeni.
Moja ya mapendekezo yanayojadiliwa ni Eisenkot kuunda serikali ya wachache kwa kushirikiana na chama cha Ra'am, huku The Joint List ikiunga mkono serikali hiyo kutoka nje bila kujiunga rasmi nayo.
Utafiti wa maoni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Hebrew ulionyesha kuwa hilo ndilo chaguo lililopata uungwaji mkono mkubwa zaidi miongoni mwa wapiga kura wa vyama mbalimbali katika kambi ya upinzani.
Serikali ya wachache ni ile inayoundwa bila kuwa na wabunge wengi wanaoiunga mkono moja kwa moja ndani ya bunge, lakini inaweza kuendelea kutawala ikiwa itapata uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa wabunge wengine katika kura muhimu.
Hivyo, hata kama The Joint List haitajiunga rasmi na serikali ya Eisenkot, uamuzi wake wa kuiunga mkono katika masuala muhimu unaweza kuwa na athari kubwa katika uimara wa serikali hiyo.
Kwa sasa, changamoto kubwa kwa Eisenkot ni kufikia makubaliano na vyama vya Waarabu bila kupoteza uungwaji mkono wa vyama vingine katika kambi yake.
Kwa upande wa Netanyahu, matokeo hayo yana maana kuwa licha ya chama chake kupata viti vingi zaidi kuliko chama chochote katika kambi pinzani, hakina uhakika wa kuendelea kuongoza serikali.
Hali hiyo imeifanya nafasi ya vyama vya Waarabu kuwa kiini cha mvutano wa kisiasa nchini Israel, huku mazungumzo ya kuunda serikali yakitarajiwa kuamua iwapo Netanyahu ataendelea kubaki madarakani au nchi hiyo itaongozwa na muungano mpya wa kisiasa.



























