“Msitumie muziki wangu,” Ariana Grande aiambia Ikulu ya Marekani

Chanzo cha picha, Noam Galai/Getty Images for MTV
Muimbaji maarufu wa muziki wa pop kutoka Marekani, Ariana Grande, ameomba Ikulu ya Marekani isitumie muziki wake baada ya kufanya hivyo katika video ya mitandao ya kijamii iliyokuwa ikitangaza sera za uhamiaji za serikali.
Video hiyo ya TikTok iliyochapishwa Jumatatu inaonesha maafisa wa ulinzi wa mipaka wakiwafunga pingu watu mbalimbali, huku wimbo wa Ariana Grande wa mwaka 2024, Bye, ukitumika kama muziki wa video hiyo.
Video hiyo ilikuwa na maelezo yaliyosema:
"Bye-bye... Rais Trump ametoa mpaka salama zaidi katika historia."
Grande alijibu kwenye chapisho hilo kwa kuandika:
"Tafadhali msitumie muziki wangu kuhusishwa na upuuzi huu wa kikatili, usio wa kibinadamu na wa kutisha."
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Abigail Jackson, alijibu kwa vyombo vya habari vya Marekani akisema:
"Kilicho cha kikatili, kisicho cha kibinadamu na cha kutisha ni wahamiaji haramu wahalifu ambao wamejeruhi na kuwaua raia wasio na hatia wa Marekani."
Video hiyo ilikuja baada ya Rais Donald Trump kutia saini sheria iliyotenga zaidi ya dola bilioni 70 kwa ajili ya mashirika ya uhamiaji katika kipindi kilichobaki cha muhula wake wa urais.
Video hiyo inaonesha maafisa wakiwafunga watu pingu, kuwaingiza kwenye magari na baadaye kuwapeleka katika vituo vya kuzuiliwa.
Baada ya Ariana Grande kutoa maoni yake, sauti ya wimbo huo iliondolewa kwenye video na maoni yake kufutwa. Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii walibaini kuwa maoni yake yalikuwa yameondolewa na kwamba video hiyo ilikuwa imezimwa sauti.
Muigizaji wa filamu ya Wicked amejiunga na orodha inayoongezeka ya wasanii ambao wameitaka timu ya Trump kutotumia muziki wao kutangaza sera au ajenda za kisiasa za rais huyo.
Mwaka jana, mwimbaji Sabrina Carpenter aliandika:
“Msinijumuishe mimi au muziki wangu kamwe ili kuunga mkono ajenda yenu isiyo ya kibinadamu”, baada ya video ya Ikulu ya Marekani kutumia sehemu ya wimbo wake wa 2024 Juno katika mkusanyiko wa video zilizoonesha operesheni za Idara ya uhamiaji ya Marekani.
Wanamuziki wa kundi ABBA, pamoja na Celine Dion na Beyoncé, pia walisisitiza kuwa timu ya kampeni ya Rais Donald Trump isitumie muziki wao wakati wa kampeni yake ya 2024 ya uchaguzi, ikiwemo katika mikutano ya kampeni.


















