Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Iran yasema haiwezi kuzuiwa kwa vikwazo vya ardhini huku Marekani ikiongeza vikwazo vya kiuchumi.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa, kuizuia Iran kupitia vikwazo vya ardhini ni jambo ambalo haliwezekani kutokana na ukubwa wa nchi hiyo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. NATO yaonya kuhusu mpango wa Urusi wa kutuma setilaiti ya nyuklia angani

    Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amesema muungano huo utajilinda dhidi ya vitisho vyovyote vinavyoweza kutokea angani, kufuatia taarifa kwamba Urusi ilikuwa ikijiandaa kurusha setilaiti yenye silaha za nyuklia.

    Kulingana na vyombo vya habari vya Ujerumani, taarifa za kijasusi kuhusu uwezekano wa Urusi kurusha setilaiti hiyo ndani ya siku 60 zijazo zilikuwa zimetumwa kwa nchi wanachama wa NATO mapema mwezi huu. Hata hivyo, haijabainika ni nchi gani iliyokuwa imetoa taarifa hizo.

    Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Rutte alisema: “Daima tutahakikisha tunalinda kila sehemu ya eneo la NATO, na hilo linajumuisha kuhakikisha usalama wetu katika masuala yanayohusu anga za juu.”

    Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alipoulizwa alijibu kwa kusema hakuwa ameskia taarifa hiyo,na kuongezea kuwa ripoti kutoka vyanzo visivyojulikana hazifai kupewa umakini wowote.

    Ubalozi wa Urusi mjini Berlin uliiambia vyombo vya habari vya Ujerumani kuwa unakataa kile ulichoita “madai yasiyo na msingi”,na kutaja madai hayo kuwa propaganda.

    Soma pia:

  2. Hakuna haja ya Israel kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran kwa sasa - Eisenkot

    Gadi Eisenkot, ambaye anashiriki mazungumzo ya kuunda serikali mpya nchini Israel, amesema haoni haja ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran kwa sasa.

    Gadi Eisenkot, ambaye aligombea nafasi ya Waziri Mkuu, amesema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika bunge la Israel, mjini Jerusalem, kwamba tishio kutoka Iran ndilo kubwa zaidi linaloikabili serikali ya Israel.

    Hata hivyo, amesema kwa sasa haoni tishio lolote la moja kwa moja na la dharura linalohitaji hatua za kijeshi kabla ya kuundwa kwa serikali mpya.

    Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa sasa wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na “vitisho vikubwa na vya hatari” ambavyo havipaswi kupuuzwa.

    “Wale wanaopuuza au kudharau vitisho hivi vya sasa na vilivyo vikubwa wanafanya hivyo kwa sababu za kisiasa,” Netanyahu alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari bungeni.

    Gadi Eisenkot ana hadi tarehe 6 mwezi Disemba kuunda serikali mpya, muda ambao unaweza kuongezwa kwa siku nyingine 14.

    Katika uchaguzi uliofanyika nchini Israel mwezi Oktoba, hakuna chama cha kisiasa kilichoweza kupata viti vya kutosha bungeni ili kuunda serikali.

    Soma pia:

  3. Kiongozi wa upinzani Zambia ashtakiwa rasmi kwa uhaini

    Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, pamoja na washirika wake zaidi ya 12, walifikishwa mahakamani hapo jana wakikabiliwa na mashtaka ya kupanga njama za kuipindua serikali, huku mahakama kuu ikitarajiwa kuanza kusikiliza kesi yao ya uhaini.

    Kulingana na hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamanihapo jana, Mundubile na wenzake wanatuhumiwa kupanga njama za kuipindua serikali kati ya mwezi Aprili na Agosti 2026.

    Mundubile na mgombea mwenza wake katika uchaguzi, Makebi Zulu, walikamatwa na kuhojiwa kuhusu tuhuma za uhaini muda mfupi baada ya uchaguzi wa urais kufanyika mwezi wa Agosti. Wawili hao walidai kuwa uchaguzi huo uliibwa.

    Rais Hakainde Hichilema alishinda uchaguzi huo na amekanusha madai ya kuwepo kwa udanganyifu wowote.

    Kulingana na hati ya mashataka, Mundubile na mfanyabiashara mmoja walitoa fedha kwa ajili ya kuwapeleka watu watano nchini Urusi kupata mafunzo ya kijeshi, kwa lengo la kutekeleza mpango wa kuipindua serikali.

    Wakili wa upande wa utetezi, Sakwiba Sikota, amesema mashtaka hayo hayana msingi na kwamba upande wa mashtaka unafanya uchunguzi wa kubahatisha ili kutafuta ushahidi wa kuwashtaki.

    Sikota amesema kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa mapema mwakani.

    Awali, Mundubile alikanusha mashtaka hayo ya uhaini na kusema kuwa yanasukumwa na sababu za kisiasa.

    Soma pia:

  4. Marekani yaongeza vikwazo dhidi ya mtandao wa kifedha wa Iran

    Utawala wa Rais Donald Trump umeiwekea Iran vikwazo vipya, ikilenga watu na taasisi kadhaa ambazo Marekani inazituhumu kuhusishwa na mfumo wa kifedha wa siri wa Iran, unaojulikana kama “Shadow Banking System”, kulingana na taarifa iliyochapishwa hapo jana kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha ya Marekani.

    Wizara ya Fedha ya Marekani imewaongeza watu wanane wenye uhusiano na Iran pamoja na taasisi 22 zilizoko Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Uturuki na Hong Kong kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.

    Wizara hiyo imesema kuwa Mtandao wa Utekelezaji wa Uhalifu wa Kifedha (FinCEN) umebaini shughuli za kifedha zenye thamani ya takribani dola bilioni 14.7 kati ya Januari 2025 na Agosti 2026, ambazo zinaaminika kuhusishwa na mfumo huo wa kifedha wa siri wa Iran.

    Taarifa hiyo pia imesema kuwa Kituo cha Ubadilishanaji wa Fedha na Dhahabu cha Iran, kilichoanzishwa takribani miaka mitatu iliyopita kwa idhini ya Benki Kuu ya nchi hiyo, kimeongezwa kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.

    Kulingana na Wizara ya Fedha ya Marekani, mfumo wa kifedha wa siri wa Iran hutumika kuhamisha fedha zinazotokana na biashara ya kimataifa ya nchi hiyo, huku Kituo cha Ubadilishanaji wa Fedha cha Iran kikifanya kazi kama mpatanishi na kuwezesha rasilimali hizo za kifedha kufika kwenye maeneo yanayokusudiwa ndani ya Iran.

    Vikwazo hivyo vya kiuchumi vya Marekani, ambavyo vimekuwa vikiongezwa katika miezi ya hivi karibuni, ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kuitenga Iran kiuchumi, ili kudhibiti maslahi yake ya kifedha pamoja na mitandao yake ya kifedha katika mataifa mbalimbali duniani.

    Soma pia:

  5. Iran yasema haiwezi kuzuiwa kwa vikwazo vya ardhini

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa, kuizuia Iran kupitia vikwazo vya ardhini ni jambo ambalo haliwezekani kutokana na ukubwa wa nchi hiyo, pamoja na uhusiano na miingiliano iliyopo kati ya majimbo yake, miji na jamii zinazoishi katika maeneo ya mpakani.

    “Kuizuia Iran kupitia vikwazo vya ardhini ni jambo ambalo karibu haliwezekani, kutokana na ukubwa wa nchi yetu na idadi kubwa ya majimbo, ambayo kila moja lina uwezo na rasilimali tofauti. Majimbo hayo yana uhusiano mpana na majimbo jirani katika nchi zinazopakana na Iran, ikiwemo shughuli nyingi za usafiri, uhusiano wa kijamii kati ya wananchi pamoja na mizizi ya kihistoria na kitamaduni inayowaunganisha watu wa pande zote za mipaka,” alisema Araqchi.

    Aidha, Waziri huyo wa Mambo ya Kigeni alisema kuwa kwa maoni yake, Tehran inapaswa kuendelea na diplomasia itakayosaidia kupunguza vikwazo vinavyoikabili taifa hilo.

    “Njia bora ya kukabiliana na shinikizo hizi ni kuhakikisha kuwa vikwazo havifikii malengo yake, ili wanaoviweka watambue kuwa njia hiyo haifanyi kazi na haitafanya kazi.”

    Kulingana na kiongozi huyo, wanaitaka Iran iwe na uwezo wa kustahimili vikwazo vyote,ili kuiwekea Iran vikwazo isiwe na maana tena.

    “Hakuna ambaye anafaa kufikiria kuwa anaweza kuilazimisha Iran kujisalimisha kwa kuongeza shinikizo la kiuchumi na vikwazo.”

    Soma pia:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumanne ya leo