Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani yaishambulia tena Iran, Trump aahidi mashambulizi makali zaidi

Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuishambulia Iran kwa "nguvu kubwa", kufuatia shambulio ambalo Tehran inadaiwa kulenga wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. WAFCON 2026: Kenya na Tanzania kusaka heshima Morocco

    Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) inaendelea leo huku macho yakielekezwa kwa timu za Afrika Mashariki, ambapo Kenya itashuka dimbani leo Alhamisi dhidi ya Senegal, wakati Tanzania itacheza kesho Ijumaa dhidi ya Burkina Faso.

    Kenya itavaana na Senegal kwenye Uwanja wa Olympic mjini Rabat, ikisaka ushindi wake wa kwanza katika Kundi A baada ya kupoteza mechi ya ufunguzi 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco.

    Kwa upande wa Tanzania, Twiga Stars itacheza na Burkina Faso kuanzia katika Uwanja wa Larbi Zaouli mjini Casablanca, ikiwa na lengo la kuendeleza mwanzo mzuri baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza 2-1 dhidi ya Afrika Kusini.

    Mbali na mchezo wa Kenya, leo pia kutakuwa na pambano kali la Kundi A kati ya wenyeji Morocco na Algeria, litakaloanza mjini Rabat.

    Katika michezo iliyochezwa Jumatano, Ghana ilianza kampeni yake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde katika Kundi D.

    Nayo Cameroon iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo mwingine wa Kundi D.

    Matokeo ya mechi za ufunguzi kwa Kenya na Tanzania

    Ushindi wa Tanzania dhidi ya Afrika Kusini umeiweka Twiga Stars katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya hatua ya robo fainali, huku Kenya ikihitaji matokeo mazuri dhidi ya Senegal ili kujiweka katika mazingira ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

  2. Liverpool yaandaa ofa ya kwanza kumsajili Barcola kutoka PSG

    Liverpool imeongeza juhudi zake za kumsajili winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, na inajiandaa kuwasilisha ofa yake ya kwanza kwa klabu hiyo ya Ufaransa.

    Barcola, mwenye umri wa miaka 23, ametajwa kuwa chaguo kuu la Liverpool katika harakati za kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Salah, aliyeondoka mwishoni mwa msimu uliopita.

    PSG inasema thamani ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ni pauni milioni 145.

    Iwapo usajili huo utakamilika kwa kiasi hicho, utavunja rekodi ya uhamisho ghali zaidi kuwahi kufanyika nchini Uingereza. Hata hivyo, viongozi wa Liverpool wana matumaini ya kufikia makubaliano kwa ada inayokaribia pauni milioni 100.

    Barcola amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na PSG, lakini inaelezwa kuwa yuko tayari kuhamia Liverpool akitafuta changamoto mpya, baada ya nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ufaransa kupungua.

    Awali, Liverpool ilikuwa ikimwania winga wa RB Leipzig Yan Diomande, lakini sasa mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na Real Madrid.

    Barcola alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichofika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2026.

  3. Marekani yashambulia tena Iran, Trump aahidi mashambulizi makali zaidi

    Jeshi la Marekani limesema limefanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran usiku wa Alhamisi, likisema ni hatua ya kujibu shambulio lililolenga wanajeshi wake walioko Mashariki ya Kati mapema wiki hii.

    Haya ni mashambulizi ya kwanza ya Marekani dhidi ya Iran katika takriban wiki moja.

    Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti milipuko karibu na Kisiwa cha Qeshm na mji wa Abadan, kusini mwa nchi hiyo.

    Shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, limemnukuu afisa wa jimbo la Hormozgan akisema kuwa vikosi vya uokoaji vinaendelea kuwatafuta watu wawili wanaodaiwa kufunikwa na vifusi baada ya kuangukiwa na nyumba katika Kisiwa cha Qeshm.

    Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuijibu Iran kwa "nguvu kubwa", kufuatia shambulio ambalo Tehran inadaiwa kulenga wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati.

    Siku ya Jumatano, jeshi la Marekani na lile la Jordan yalisema yalizuia makombora yaliyokuwa yamerushwa kuelekea Jordan, yakidai yalitoka Iran na yalilenga maeneo yenye wanajeshi wa Marekani.

    Katika taarifa yake, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo ni "jibu kali" kwa kile ilichokiita mashambulizi ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani yaliyodhibitiwa siku iliyotangulia.

    Wakati huo huo, tovuti ya habari ya Marekani Axios, ikimnukuu afisa wa Marekani ambaye haikumtaja kwa jina, ilisema Washington ilikuwa imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.

    Awali akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Trump alisema Marekani itaishambulia Iran "kwa nguvu kubwa".

    "Sasa ni zamu yetu," alisema Trump, huku akiongeza kuwa bado kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano siku zijazo, lakini akasisitiza kuwa, "tutaishambulia kwa nguvu sana."

  4. Habari na karibu kwenye habari zetu za moja kwa moja