WAFCON 2026: Kenya na Tanzania kusaka heshima Morocco

Chanzo cha picha, CECAFA
Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) inaendelea leo huku macho yakielekezwa kwa timu za Afrika Mashariki, ambapo Kenya itashuka dimbani leo Alhamisi dhidi ya Senegal, wakati Tanzania itacheza kesho Ijumaa dhidi ya Burkina Faso.
Kenya itavaana na Senegal kwenye Uwanja wa Olympic mjini Rabat, ikisaka ushindi wake wa kwanza katika Kundi A baada ya kupoteza mechi ya ufunguzi 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco.
Kwa upande wa Tanzania, Twiga Stars itacheza na Burkina Faso kuanzia katika Uwanja wa Larbi Zaouli mjini Casablanca, ikiwa na lengo la kuendeleza mwanzo mzuri baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza 2-1 dhidi ya Afrika Kusini.
Mbali na mchezo wa Kenya, leo pia kutakuwa na pambano kali la Kundi A kati ya wenyeji Morocco na Algeria, litakaloanza mjini Rabat.
Katika michezo iliyochezwa Jumatano, Ghana ilianza kampeni yake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde katika Kundi D.
Nayo Cameroon iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo mwingine wa Kundi D.
Matokeo ya mechi za ufunguzi kwa Kenya na Tanzania
Ushindi wa Tanzania dhidi ya Afrika Kusini umeiweka Twiga Stars katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya hatua ya robo fainali, huku Kenya ikihitaji matokeo mazuri dhidi ya Senegal ili kujiweka katika mazingira ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.


