Macron: Ufaransa yakamata meli ya mafuta ya Urusi iliyowekewa vikwazo
Ufaransa imekamata Tanka la Mafuta linaloshukiwa kuwa Sehemu ya meli za Urusi zinazofanya kazi zinazotumia mbinu za udanganyifu au usiri kusafirisha bidhaa zilizowekewa vikwazo
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kuwa mamlaka za Ufaransa zilikamata meli ya mafuta iliyowekewa vikwazo, inayoshukiwa kuwa sehemu ya kile kinachoitwa "shadow fleet" yaani meli inayofanya kazi kwa magendo ya Urusi, iliyokamatwa kwa msaada wa Uingereza
Maafisa wa usalama walipanda kwenye meli hiyo iitwayo Tagor katika Bahari ya Atlantiki. Mamlaka za baharini zilisema kuwa meli hiyo ilikuwa ikitumia bendera ya uwongo wakati ilipokamatwa takribani maili za baharini 400 magharibi mwa eneo la Brittany.
Macron aliandika kwenye mtandao wa X kwamba:
"Haikubaliki kwa meli kukwepa vikwazo vya kimataifa, kukiuka sheria za bahari, na kufadhili vita ambavyo Urusi imekuwa ikivifanya dhidi ya Ukraine."
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilithibitisha kuwa helikopta ya Uingereza ilitoa msaada wakati wa operesheni hiyo.
Kwa upande wake, serikali ya Urusi ililaani tukio hilo. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alisema ukamataji huo ulikuwa "haramu" na kwamba ulikuwa karibu kufanana na uharamia wa kimataifa.
Aliongeza kuwa Urusi inachukua hatua kuhakikisha usalama wa mizigo yake.
Meli ya Tagor ni meli ya nne inayoshukiwa kuwa sehemu ya kundi la meli zinazokwepa vikwazo ambayo Ufaransa imeikagua au kuikamata tangu Septemba 2025.
Unaweza kusoma;