CCTV yafichua moto ulivyoanza katika shule ya wasichana Kenya

Chanzo cha picha, Mtandaoni
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya, imetoa video kutoka kwa CCTV ya shule ikionyesha kile kilichojiri muda mfupi kabla ya tukio la moto kuanza kwenye bweni la shule ya wasichana ambapo wanafunzi 16 wa Utumishi Academy walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Uchunguzi wa CCTV kwa ushirikiano na waalimu, timu ya uchunguzi imebaini wanafunzi saba waliohusika kwenye kitendo hicho kabla ya kutoka nje ya bweni.
Wakati uchunguzi unaendelea kubaini hasa kilichojiri, video kutoka kwa CCTV imeonyesha kuwa karibu saa 12:10 usiku, wanafunzi kadhaa walitembea kimya kimya ndani ya bweni wakati wengine wamelala fofofo.
Video iliyotolewa inaonyesha wanafunzi hao wakiingia kwenye chumba 11 kwa muda mfupi sana kabla ya kuendelea kutembea eneo lingine la bweni.
Wanafunzi wanaonekana wakifanya mienendo yao kimya kimya huku mmoja akiwa amejifunika uso.
Dakika chache baadaye, wanafunzi watatu wameonekana wakitembea kwa haraka kutoka nje ya bweni huku wawili wakisalia nyuma.
Wachunguzi wanasema wanafunzi hao walielekea sehemu nyingine ya bweni ambako magodoro yalikuwa yamepangwa na kuwasha moto wa pili.
Picha za CCTV zinaripotiwa kuwanasa wawili hao wakiwasha kibiri kabla ya kuelekea eneo la mlango wa kutoka kwenye bweni.
Wakati huu, moto ulienea kwa kasi zaidi.
Baada ya kuthibitisha kuwa moto huo umeshika kasi, wanafunzi hao wanaonekana wakitoka nje ya bweni hilo bila kuzua taharuki.
Na ndani ya dakika chache, moshi na miali ya moto vilianza kuenea katika jengo hilo.
Kufikia saa 12:13 usiku, hofu ilikuwa imezuka ndani ya bweni hilo huku wanafunzi wakiamka kutokana na moshi mwingi na miale ya moto inayozidi kuongezeka.
Wengine wanaonekana wakijaribu kuelewa kilichokuwa kikitendeka huku wengine wakihangaika kutafuta njia ya kutokea.
Na ndani ya dakika tano moto huo ulikuwa umeteketeza sehemu kubwa ya bweni huku wanafunzi waliojawa na hofu wakitafuta njia ya kutoroka.
Kati ya wanafunzi wanane waliokuwa wamezuiliwa awali, sita wamethibitishwa kupitia picha za CCTV, wa saba ni miongoni mwa walioruhusiwa kuondoka na wazazi wao hapo awali, ambaye kwa sasa hayuko kituoni lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha amepatikana na kukamatwa.
Wakati huo huo, vipimo vya DNA vya wanafunzi 16 walioaga dunia kwenye mkasa huo mbaya wa moto shuleni, matokeo yameonyesha kuwa walifariki dunia kutokana na majeraha ya moto kupita kiasi.
Soma zaidi:







