Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amwita Putin ‘muuaji’ baada ya Trump kumtaja kuwa ‘rafiki’ yake

Rais wa Ukraine, amemtaja Rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa ni "muuaji", akijibu matamshi ya Donald Trump aliyemtaja kiongozi huyo wa Urusi kuwa "rafiki" yake.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Gharama za Manchester United kuajiri na kufukuza makocha zakaribia pauni milioni 100

    Manchester United imekopa pauni milioni 10 siku tatu baada ya kumtangaza Mauricio Pochettino kuwa kocha wake mkuu mpya.

    Katika taarifa ya kina iliyowasilishwa kwa soko la hisa ikiambatana na matokeo ya kifedha ya robo ya kwanza ya mwaka, klabu hiyo ilisema italazimika kulipa fidia ya pauni milioni 7.5 kwa Shirikisho la Soka la Marekani ili kumpata kocha huyo kutoka Argentina.

    Manchester United ilitangaza tarehe 13 Novemba kuwa Pochettino amekubali mkataba wa miaka miwili na nusu. Siku tatu baada ya klabu hiyo kukopa pauni milioni 10.

    Mkopo huo ni miongoni mwa mikopo mitatu iliyothibitishwa baada ya tarehe 30 Septemba, na imepandisha jumla ya deni la klabu hiyo kufikia pauni milioni 240.

    Malipo ya kumwachia Pochettino kutoka kwenye mkataba wake na Marekani yamepandisha jumla ya fedha zilizotumika kuajiri na kuwafuta kazi makocha tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013 hadi pauni milioni 95.

    Hata hivyo, kiasi hicho kinatarajiwa kuzidi pauni milioni 100 baada ya kujumlisha gharama za kuajiri benchi la ufundi la Pochettino na kumfuta kazi Michael Carrick.

    Carrick alitimuliwa wiki iliyopita wakati Manchester United ilikuwa katika nafasi za kushushwa daraja, huku ikikabiliwa na mwanzo mbaya zaidi wa msimu ndani ya miaka 40.

    Pochettino ni kocha wa tisa wa kudumu kuteuliwa na Manchester United tangu Ferguson astaafu, akiwemo Ralf Rangnick aliyeteuliwa Novemba 2021.

    Manchester United imekuwa ikibadilisha makocha katikati ya misimu katika misimu yake mitatu iliyopita.

    Soma pia:

  2. Iran imesema imedungua droni ya Marekani aina ya MQ-9

    Jeshi la Iran (IRGC), limedai kuwa mfumo wake wa ulinzi wa anga umedungua droni ya Marekani aina ya MQ-9 iliyokuwa ikiruka juu ya Mlango Bahari wa Hormuz.

    Kulingana na idara ya mahusiano ya umma ya jeshi hilo, mfumo wa ulinzi wa anga uliitambua droni hiyo, ukaifuatilia na kisha kuilenga.

    Katika taarifa yake, jeshi hilo lilisema kuwa hiyo ni droni ya 58 ya Marekani aina ya MQ-9 ambayo wameilenga.

    Hata hivyo, maafisa wa Marekani bado hawajatoa tamko lolote kuhusu madai hayo, huku kukiwa hakuna uthibitisho huru kwamba droni hiyo imedunguliwa.

    Soma pia:

  3. Trump asema bei ya mafuta itashuka hivi karibuni

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema bei ya mafuta ilikuwa nafuu kabla ya kuanza kwa operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran, na kutabiri kuwa bei za mafuta zitashuka kwa kiasi kikubwa hivi karibuni.

    "Mtashuhudia bei za chini sana hivi karibuni," alisema Trump katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana.

    Rais huyo wa Marekani aliongeza kuwa bei ya mafuta kuanzia sasa itategemea jinsi Marekani itakavyotatua mizozo yake na Iran.

    Trump alisisitiza kuwa Iran inataka kufikia makubaliano na Marekani, lakini haiko tayari kukubali masharti ya Marekani.

    "Tunataka kufikia makubaliano ya kweli, si makubaliano ya uongo," alisema.

    Soma pia:

  4. Trump apiga marufuku ujenzi wa vituo vya AI nje ya Marekani

    Rais wa Marekani Donald Trump, amesema atapiga marufuku kampuni za Marekani kujenga vituo vya kuhifadhi na kuchakata data za akili unde (AI) nje ya nchi hiyo.

    Trump amesema kmapuni zitakazokiuka sera hiyo zitatozwa kodi kubwa.

    "Tutahakikisha shughuli zote hizo zinafanyika ndani ya nchi hii," alisema Trump, bila kutoa maelezo ya kina kuhusu sera hiyo inayopendekezwa.

    Vituo vya kuhifadhi na kuchakata data au data centres vilikuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa sana katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani mapema mwezi Novemba, huku wagombea wengi wa chama cha Democratic wakiahidi kuweka masharti makali zaidi kuhusu ujenzi wake.

    Kampuni kubwa za teknolojia, zikiwemo Meta na Google, tayari zimesaini mikataba ya kujenga vituo hivyo katika nchi za nje. Hata hivyo, bado haijabainika jinsi sheria hiyo itakavyotekelezwa iwapo itapitishwa.

    "Tutazizuia kampuni zetu kujenga vituo vya data nje ya nchi yetu, kwa sababu China itavichukua vyote, na hatutaruhusu hilo kutokea," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano mfupi baada ya kurejea kutoka ziara yake barani Asia.

    Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo wazo hilo litabadilika na kuwa sera rasmi.

    Soma pia:

  5. Zelensky amwita Putin kuwa ‘muuaji’ baada ya Trump kumtaja kuwa ‘rafiki’

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemtaja Rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa ni "muuaji", akijibu matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump aliyemtaja kiongozi huyo wa Urusi kuwa "rafiki" yake alipokuwa China wiki hii.

    Akizungumza na kituo cha televisheni cha CNN, Zelensky alisema kuwa "kwetu sisi,Putin ni adui kwetu sisi, yeye ni muuaji".

    Pembeni mwa mkutano wa kihistoria wa pande tatu kati ya Trump, kiongozi wa China Xi Jinping na Putin siku ya Alhamisi, Trump alimtaja Putin kuwa "rafiki" yake na kusema viongozi hao wawili wamekuwa na "uhusiano mzuri kwa miaka mingi".

    Zelensky alielezea mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi dhidi ya Ukraine kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea mwaka huu. Alisema mashambulizi hayo yalisababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia, baada ya Urusi kurusha makombora 110, yakiwemo 27 ya masafa mafupi ya balistiki, pamoja na zaidi ya droni 400.

    Saa chache baada ya mashambulizi hayo nchini Ukraine, Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba Putin "angependa kumaliza vita".

    "Wote wawili Zelensky na Putin wanataka vita vikome, na ni jambo zuri sana kwamba nina uhusiano nao," alisema Trump siku ya Ijumaa.

    Takriban watu tisa waliuawa katika mashambulizi ya Urusi yaliyolenga madaraja mjini Kyiv na vituo vya reli siku ya Ijumaa, siku chache baada ya Ukraine kuharibu vibaya Daraja la Crimea.

    Hata hivyo, Zelensky alisema licha ya msimamo wa Trump, yeye anamwona Putin kuwa "muuaji".

    "Nadhani watu wengi duniani wanamwona kuwa muuaji kwa sababu anaua watu kila siku na kila usiku," alisema.

    Mabadilishano hayo ya matamshi makali yalijiri wakati Poland, nchi jirani ya Ukraine, ilipotangaza kuwa kombora la Urusi aina ya cruise lilikuwa miongoni mwa vitu vitatu vilivyoingia katika anga yake katika eneo la kusini-mashariki mwa nchi hiyo mapema siku ya Ijumaa.

    Soma pia:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja