Nigeria yapanga kuwarejesha raia wake wanaotaka kuondoka Afrika Kusini baada ya mashambulizi

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Nigeria inapanga kuwarejesha nyumbani raia wake walioko Afrika Kusini watakaokubali kurejea kwa hiari, huku hofu ikiongezeka kwamba mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni nchini humo yanaweza kuongezeka.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Bianca Odumegwu Ojukwu, amesema watu 130 tayari wamejiandikisha kwa mchakato huo, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.
Amesema Rais Bola Tinubu ana wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo nchini Afrika Kusini, na amelaani vurugu dhidi ya raia wa kigeni pamoja na maandamano yaliyoambatana na kile alichokiita kauli za chuki dhidi ya wageni, hotuba za chuki na matamshi ya uchochezi dhidi ya wahamiaji.
Nigeria imemuita kaimu Balozi Mkuu wa Afrika Kusini kujieleza kuhusu suala hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, nchi hiyo itawasilisha rasmi wasiwasi wake mkubwa katika mkutano utakaofanyika baadaye Jumatatu, ikisema matukio hayo yanaweza kuathiri uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Taarifa hiyo imesema mkutano huo utajikita katika maandamano ya hivi karibuni yaliyoandaliwa na makundi yanayopinga wahamiaji, pamoja na matukio yaliyoripotiwa ya raia wa Nigeria kunyanyaswa na biashara zao kushambuliwa.
Siku ya Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alisema: "Maisha ya Wanigeria na biashara nchini Afrika Kusini lazima zisiendelee kuwekwa hatarini, na tunasalia kujitolea kufanya kazi kutafuta na suluhisho la kumaliza hali hiyo.''
Ametaja pia kuuawa kwa raia wawili wa Nigeria katika matukio tofauti yaliyowahusisha maafisa wa usalama wa eneo hilo, akisema serikali ya Nigeria inadai haki itendeke.
Mwezi uliopita, Ghana pia ilimuita balozi mkuu wa Afrika Kusini baada ya kusambaa kwa video iliyomuonyesha raia wa Ghana akihojiwa kuthibitisha uhalali wa nyaraka zake za uhamiaji.
Hisia za kupinga wahamiaji ziliongezeka mapema mwaka huu baada ya taarifa kwamba kiongozi wa jamii ya Wanigeria katika mji wa bandari wa KuGompo, zamani East London, alitawazwa katika nafasi ya jadi inayoweza kufasiriwa kama mfalme, jambo lililotafsiriwa na baadhi ya raia wa Afrika Kusini kama jaribio la kujipatia ushawishi wa kisiasa.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, Afrika Kusini ina wahamiaji wapatao milioni 2.4, sawa na chini kidogo ya asilimia nne ya idadi ya watu wake, ingawa inaaminika kuwa wengine wengi wanaishi nchini humo bila vibali rasmi.
Wengi wao hutoka mataifa jirani kama Lesotho, Zimbabwe na Msumbiji, huku idadi ndogo ikitoka Nigeria.
Soma zaidi:





