Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump ‘asitisha’ mashambulizi dhidi ya Iran, Tehran ikisema mazungumzo yake na Muscat ‘yana tija’

Ripoti zinaonyesha kuwa maafisa wa Marekani wameelezea wasiwasi wao kuhusu kupungua kwa akiba ya makombora ya Patriot.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Walowezi wa Kiyahudi wachoma misikiti, magari na mashamba katika Ukingo wa Magharibi

    Maafisa wa Palestina wanasema walowezi wa Israel wamechoma moto misikiti miwili, pamoja na magari na mashamba katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu, huku mivutano katika eneo hilo ukiendelea kuongeza.

    Mashambulizi hayo ya hivi karibuni yanakuja siku mbili baada ya makabiliano kati ya walowezi na Wapalestina karibu na kijiji cha Tal, ambapo Wapalestina wanne na Waisraeli wawili walipoteza maisha.

    Pande zote mbili zilituhumiana kwa kuchochea vurugu hizo. Makabiliano hayo yamezidi kuchochea hali ya wasiwasi katika Ukingo wa Magharibi, eneo ambalo limeshuhudia ongezeko la vurugu zinazofanywa na walowezi wenye msimamo mkali dhidi ya Wapalestina, huku wakichochewa na makundi yenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia ndani ya serikali ya sasa ya Israel.

    Taarifa kutoka upande wa Palestina zinasema kuwa vijiji viwili katika Ukingo wa Magharibi vilishambuliwa na walowezi usiku kucha; magari yaliharibiwa, mali iliibwa na maandishi ya chuki yalipakwa kwenye kuta.

    Meya wa Qusra alisema kuwa walowezi walichoma moto msikiti uliokuwa katika hatua za ujenzi.

    Abdul Azim Wadi alisema kuwa walowezi walipaka maandishi ukutani mwa msikiti huo, yakiwemo neno "kisasi".

    Jeshi la Israel limesema kuwa wanajeshi walitumwa huko Qusra na kwamba polisi watafanya uchunguzi na kukusanya ushahidi.

  2. Tumeidungua ndege isiyo na rubani ya Saudi Arabia- Wahouthi

    Kundi la Houthi limedai kuangusha ndege isiyo ya na rubani ya Saudui Arabia

    Msemaji wa kundi hilo nchini lenye makao yake nchini Yemen, Yahya Saree, ameandika kwenye mtandao wa X kwamba wamefaninikiwa kuidungua ndege isiyo na rubani ya "Bajrukdar Akinci" iliyotengenezwa na Uturuki, ambayo liliitumia na jeshi la Saudi katika shambulio la angani dhidi ya mji wa Al-Jawf."

    Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa Wahouthi watajibu ukiukaji wowote wa uhuru na wana uwezo wa kufanya hivyo.

    Waasi wa Houthi wa Yemen walisema jana kuwa wamefany amashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya mafuta vya Aramco na kituo cha mafuta cha Yanbu nchini Saudi Arabia.

    Soma pia:

  3. Tumekomesha mashambulizi ya kulipiza kisasi - Msamaji wa jeshi la Iran

    Msemaji wa jeshi la Iran alisema kuwa, kwa vile mkakati wa Iran katika kipindi hiki cha vita umekuwa wa "kulipiza kisasi," na baada ya Marekani kusitisha mashambulizi yake ksiku mbili zilizopita, "sisi pia tulisitisha operesheni zetu."

    Wakati huo huo, vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Donald Trump ameamua kutoendelea na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, kwa sasa.

    Uamuzi huo, kulingana na vyombo hivyo vya habari, ulifikiwa siku ya Ijumaa baada ya maafisa kuelezea wasiwasi kuhusu kupungua kwa akiba ya mifumo ya ulinzi ya makombora ya Patriot na uwezekano wa kuwatenga washirika wa Kiarabu wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi.

    Kuhusu uwezekano wa Marekani "kutekeleza tena usitishaji wa mapigano wa upande mmoja," Mohammad Akraminia alisema kuwa "Marekani inakabiliwa na changamoto ya kufanya maamuzi ya kimkakati.

    Haina mkakati ulio wazi. Hili linaonekana katika maamuzi ya rais na utendaji wa CENTCOM."

  4. Uganda yamteua Otunnu kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

    Serikali ya Uganda imemteua Balozi Olara Otunnu kuwania wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ikimtanguliza mwanasiasa na kiongozi mashuhuri ambaye miongo kadhaa ya utumishi wake katika diplomasia ya kimataifa.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Julai 26, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda ilitangaza kuwa imewasilisha ombi la kugombea nafasi ya juu katika Umoja wa Mataifa, huku mchakato wa kumtafuta mrithi wa António Guterres—ambaye muhula wake wa pili unafikia tamati tarehe 31 Desemba 2026—ukianza.

    Serikali ilimwelezea Otunnu kama kiongozi wa taifa anayeheshimika na mtumishi wa kimataifa mwenye uzoefu wa zaidi ya miongo minne katika nyanja za diplomasia ya kimataifa, serikali, taaluma na asasi za kiraia, ikisema kuwa historia yake pana ya uongozi inamfanya kuwa mtu mwafaka kuongoza Umoja wa Mataifa katika kipindi muhimu cha masuala ya dunia.

    ''Ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, Balozi Olum aliwahi kuhudumu kama Naibu Katibu Mkuu na Mwakilishi Maalum wa kwanza wa masuala ya watoto na migogoro ya kivita kati ya mwaka 1998 hadi 2005,'' ilisema taarifa hiyo.

    Balozi Otunnu pia aliwahi kuhudumu kama Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, pamoja na kuwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja huo; katika kipindi hicho, alianzisha mfumo wa upigaji kura wa awali (straw ballot) kwa ajili ya kumchagua Katibu Mkuu—utaratibu unaojulikana tangu wakati huo kama "Mfumo wa Otunnu" na ambao umekuwa ukiongoza uchaguzi wa aina hiyo tangu mwaka 1981.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huteuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pendekezo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kufuatia mchakato wa uteuzi wa ushindani unaohusisha nchi zote wanachama.

  5. Polisi wanamsaka mshukiwa wa shambulio dhidi ya shughuli ya LGBTQ Ujerumani

    Polisi nchini Ujerumani wanamtafuta mtu anayefahamika kama Abdul B baada ya tukio la gari kuendeshwa mbio katikati ya umati wa watu na wengine kuchomwa visu.

    Polisi mjini Berlin, wanasema mtu mmoja amefariki na wengine 15 kujeruhiwa baada ya gari kuvurumizwa kwenye umati wa watu waliokuwa wakiadhimisha gwaride la kila mwaka la kujivunia utambulisho wa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja LGBTQ, huku baadhi ya majeruhi wakiripotiwa kuwa katika hali mbaya.

    Tukio hilo lilitokea Jumamosi jioni katika bustani ya Tiergarten katikati ya jiji, karibu na Lango la Brandenburg. Polisi walisema gari hilo jeupe liliwagonga watu kadhaa kabla ya kugonga mti na kusimama.

    Polisi walisema gari hilo lilikuwa tupu wakati wahudumu wa uokoaji walipowasili, na kuanzisha operesheni ya kumtafuta mhusika au waliohusika wa tukio hilo. Gazeti la Bild lilimnukuu shahidi mmoja akisema kuwa gari hilo lilikuwa aina ya van na kwamba mwanamume mmoja alikimbia kwa miguu baada ya gari hilo kusimama.

    Maelfu ya watu walikusanyika katikati ya Berlin kwa ajili ya maadhimisho ya kila mwaka ya "Christopher Street Day," ambayo ni mojawapo ya matukio makubwa zaidi ya LGBTQ barani Ulaya. Sababu au nia ya mshambuliaji huyo bado haijajulikana.

  6. Rais Faye wa Senegal azindua chama kipya cha kisiasa

    Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, amezindua chama kipya cha kisiasa, hatua inayozidisha mgawanyiko unaoonekana wazi kati yake na mshirika wake wa zamani na aliyekuwa Waziri Mkuu, Ousmane Sonko.

    Chama hicho kipya, Kiiray (Chama cha Wazalendo wa Jamhuri), kilizinduliwa katika mji mkuu, Dakar, siku ya Jumamosi na muungano unaomuunga mkono Bw. Faye.

    Mamia ya wafuasi walihudhuria hafla hiyo ya uzinduzi.

    Wakati huo huo, Bw. Sonko alikuwa akihutubia wafuasi wake umbali wa kilomita 100 (maili 62) katika mji wa Bambey, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kitaifa inayolenga kutafuta uungwaji mkono kwa chama chake cha Pastef.

    Mapema mwezi huu, Bw. Faye alimteua mshauri mkuu Aminata Touré kuongoza kikosi kazi cha kuanzisha vuguvugu hilo jipya la kisiasa.

    Hapo awali, Bw. Faye alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha Pastef cha Bw. Sonko, chama kilichoingia madarakani mwaka 2024 baada ya miaka mingi ya kuwa upinzani.

    Hata hivyo, uhusiano kati ya wawili hao umezorota katika miezi ya hivi karibuni, hali iliyofikia kilele wakati Bw. Faye alipomwondoa Bw. Sonko katika wadhifa wa Waziri Mkuu mwezi Mei.

    Uzinduzi wa chama hicho kipya unafanyika huku kukiwa na wimbi la wanachama kuhama chama cha Pastef na kujiunga na kambi ya rais, wakiwemo viongozi kadhaa wa ngazi ya juu wa chama hicho.

    Pastef imejitahidi kudhibiti hali ya wanachama kuhama.

    Bw. Sonko, ambaye kwa sasa ni Spika wa Bunge la Kitaifa, amekuwa mstari wa mbele kutetea marekebisho ya katiba yatakayozuia rais aliyeko madarakani kuongoza chama cha kisiasa.

    Bunge liliidhinisha mabadiliko hayo yaliyopendekezwa, lakini Bw. Faye ameamua kuyafikisha kwa wananchi kupitia kura ya maoni ya kitaifa.

    Tarehe ya kupiga kura hiyo bado haijatangazwa.

    Mgogoro huo wa kisiasa unaendelea huku Senegal ikikabiliwa na changamoto za kiuchumi kufuatia kufichuliwa kuwa deni la serikali chini ya utawala uliopita lilikuwa limeripotiwa kwa kiwango cha chini kuliko uhalisia.

    Faye na Bw. Sonko, pia wanatazamia uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika mwaka 2027, ambao unatarajiwa kuwa kipimo kikubwa cha kwanza cha uungwaji mkono wao kisiasa tangu ushirikiano wao ulipovunjika.

    Mgawanyiko kati ya wawili hao ni hatua muhimu ya mabadiliko katika siasa za Senegal.

    Wakiwa washirika wa karibu hapo awali waliofanya kampeni pamoja kwa ahadi ya kufanya marekebisho makubwa, sasa wanaongoza kambi pinzani za kisiasa zinazoshindania mustakabali wa nchi hiyo.

  7. Burnham asema hatasita kumkosoa Trump 'ikiwa ni kwa manufaa ya Uingereza'

    Waziri Mkuu Andy Burnham anasema yuko tayari kumkosoa Donald Trump kutetea "maslahi ya taifa" la Uingereza ikiwa hilo ndilo jambo sahihi la kufanya.

    Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na BBC, Burnham alisema kuwa mazungumzo yake ya awali na Trump yalikuwa mazuri, na kuongeza kuwa anamuona kuwa mtu "mchangamfu sana".

    Hata hivyo, alipoulizwa mara mbili ikiwa anamuamini rais huyo wa Marekani, hakutoa jibu la moja kwa moja, badala yake alisema: "Ni ulimwengu unaobadilika, sivyo? Na ni wazi unapaswa kushughulikia mambo kulingana na jinsi yanavyojitokeza."

    Katika mahojiano hayo, ambayo yatarushwa hewani kikamilifu siku ya Jumatatu, alisema: "Siwezi kusema wakati wowote kwamba sitakuwa na mtazamo tofauti na wake [Trump], au kwamba sitahitaji kuelezea wazo tofauti ambalo ni sahihi kwa Uingereza."

    Burnham alisema: "Nguvu yangu inatokana na kuwa karibu na watu, na hilo halitabadilika kwa sababu nimekuwa Waziri Mkuu."

    Alipoulizwa iwapo angemkosoa Trump endapo ingekuwa hatua sahihi kuchukua, alijibu "bila shaka," na kuongeza: "Lazima utetee maslahi ya taifa lako kabla ya kitu kingine chochote. Hilo ndilo linalotakiwa kufanywa ili kutekeleza wajibu huu ipasavyo."

    Burnham pia alisema alikuwa na "wasiwasi" kuhusu rais kuanzisha mzozo na Iran, na kwamba "asingesita kusema kile ninachokiona kuwa sahihi."

  8. Zaidi ya watu 300,000 wakimbia moto wa nyika Ufaransa na Uhispania

    Wazima-moto wako mbioni kudhibiti moto wa nyika uliozuka kusini-magharibi mwa Ufaransa huku upepo mkali ukisukuma miali ya moto kuelekea jiji la Bordeaux, na afisa mmoja akisema kuwa "bado wakabiliwa na kibarua kikubwa kuudhibiti moto huo."

    Zaidi ya watu 300,000 nchini Ufaransa na Uhispania wamekimbia moto huo ambao umekuwa ukiwaka kwa siku kadhaa, huku upepo na viwango vya juu vya joto vikikwamisha juhudi za kuudhibiti.

    Nchini Uhispania, ambapo hali ya dharura imetangazwa, mabadiliko ya hali ya hewa yamesaidia wazima-moto nje kidogo ya Madrid.

    Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez, alikiri kuwa wanakabiliwa na "nyakati ngumu" Wakati huo huo, mamlaka mjini Valencia zimethibitisha kuwa mwananume mmoja amefariki kutokana na moto huo.

    Mwanamume huyo, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka ya 70, alikutwa na na wazima-moto akiwa amefariki ndani ya gari lake walipokuwa wakizima moto katika eneo la Salt de l'Aigua huko Manises, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya eneo hilo.

    Nchini Ufaransa, watu wengine 55,000 waliagizwa kuyahama makaazi yao Jumamosi usiku, na hivyo kufikisha takribani watu 250,000 idadi ya walioondoka katika maeneo ya kusini-magharibi ya Gironde na Landes.

    Mkuu wa wazima-moto, Nicolas Braz, aliambia shirika la habari la AFP kuwa moto huo ulikuwa ukizalisha "upepo wake wenyewe - ikiwemo vimbunga vidogo," na kuongeza kuwa ulikuwa "wa kubadilika-badilika na usiodhibitiika."

    Alisema kuwa leo inatarajiwa kuwa "usiku mwingine mgumu."

  9. Trump ‘asitisha’ mashambulizi dhidi ya Iran, Tehran ikisema mazungumzo yake na Muscat ‘yana tija’

    Ripoti nchini Marekani zinaonyesha kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameamuakutochukua hatua itakayoongeza ukubwa wa shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Iran, huku usiku mwingine ukipita bila mashambulio ya anga katika eneo hilo.

    Ripoti zinaonyesha kuwa maafisa wa Marekani wameelezea wasiwasi wao kuhusu kupungua kwa akiba ya makombora ya Patriot, pamoja na uwezekano wa kuwatenga washirika wa Kiarabu katika eneo la Ghuba—jambo ambalo linaweza kufufua matumaini ya kurejea kwenye mazungumzo baada ya karibu wiki mbili za msururu wa mashambulizi ya anga ya Marekani.

    Tangu jioni ya Ijumaa, Marekani haijafanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, bila kutoa maelezo yoyote rasmi kuhusu uamuzi huo; hata hivyo, ripoti mbalimbali za vyombo vya habari zilisema kuwa Trump aliamua siku ya Ijumaa kusitisha mashambulizi hayo ya anga.

    Axios iliripoti kuwa Pentagon iliwasilisha kwa Trump mpango wa kufanya mashambulizi ya anga, lakini alikataa kuuidhinisha, akipendelea zaidi kutafuta suluhu kupitia mazungumzo.

    Kauli pekee rasmi kuhusu suala hilo ilitoka kwa msemaji wa Ikulu ya Marekani, ambaye alisema kuwa Trump siku zote hupendelea suluhu ya kidiplomasia.

    Huku hayo yakijiri Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei, alisema kuwa hakuna kilichobadilika kuhusu usafiri wa meli kwenye Lango la Hormuz.

    Akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu mazungumzo kati ya Iran na Oman kuhusu Lango la Hormuz, Baqaei alieleza kuwa duru kadhaa za mazungumzo kati ya Iran na Oman zilifanyika siku ya Ijumaa na Jumamosi.

    Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilijadili kanuni za pamoja na taratibu za kiutendaji za kusimamia usafiri salama wa majini katika Lango la Hormuz, huku zikiheshimu mamlaka ya nchi hizo mbili zenye mwambao wa pwani.

    Ujumbe wa Oman uliondoka Tehran Jumamosi jioni, kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ambaye alisema kuwa mazungumzo hayo yamepiga hatua na kuleta matokeo chanya, huku akiongeza kuwa mashauriano ya kiufundi na kisiasa kati ya pande hizo mbili bado yanaendelea.

    Maelezo zaidi:

  10. Natumai hujambo.