Rais wa Senegal atangaza baraza jipya la mawaziri
Rais wa Senegal Rais Bassirou Diomaye Faye ametangaza baraza jipya la mawaziri lenye wajumbe 30. Hatua hiyo imekuja wiki moja baada ya kuteuliwa kwa mwanauchumi Ahmadou Al Aminou Mohamed Lo kuwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama cha PASTEF kabla ya tangazo hilo, hakukuwa na mwanachama yeyote wa chama cha Ousmane Sonko ambaye alipaswa kujumuishwa katika baraza hilo jipya la mawaziri.
"PASTEF inatangaza kwamba haitashiriki katika serikali ijayo. Chama hicho kinataja kuwepo kwa tofauti kubwa kuhusu nafasi na jukumu la walio wengi katika mpangilio wa mamlaka ya utendaj," Taarifa hiyo ilisema.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa PASTEF hatimaye walirejeshwa serikalini, akiwemo Dkt. Alioune Dione, Waziri wa Fedha na Uchumi na Waziri wa Afya Ibrahima Sy.
Tangazo la serikali hilo la Juni Mosi, linaonekana kuwa mchanganyiko wa mwendelezo na mabadiliko, huku mawaziri kadhaa wakihifadhi nyadhifa zao kutoka serikali ya Sonko na wakati huo huo viongozi wa zamani wenye uzoefu wakirejea katika uongozi.
Senegal inapitia misukosuko ya kisiasa huku wanasiasa wake wawili maarufu zaidi – Rais Bassirou Diomaye Faye na Spika Ousmane Sonko – wakijihusisha katika mvutano mkubwa wa kisiasa.
Ousmane Sonko, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, aliondolewa katika wadhifa huo siku kumi zilizopita kisha akachaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Taifa la Senegal.
Wadhifa wa Sonko, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia Aprili mwaka 2024 hadi Mei 2026 ulichukuliwa na Ahmadou Al Aminou Mohamed Lo, Mwana Uchumi mwenye umri wa miaka 60, aliyekuwa afisa wa Benki ya Afrika Magharibi.