Mkutano wa Delhi kuamua mustakabali wa muungano wa BRICS

Chanzo cha picha, Getty Images
Viongozi wa dunia, akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa China Xi Jinping, na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, wamekusanyika Delhi kwa ajili ya mkutano wa kilele wa BRICS.
Kundi hilo liliundwa kwa lengo la kuwa na nguvu ya usawa dhidi ya Marekani na Ulaya Magharibi, lakini vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeibua nyufa ndani yake.
Mkutano huo ni fursa kwa BRICS kudhihirisha nafasi yake kama nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayoweza kukabiliana na Magharibi, lakini pia ni jaribio kubwa kwa umoja wake.
Migogoro ya kimataifa imefichua migawanyiko mikubwa, kwa mfano, Falme za Kiarabu zimekuwa zikilengwa na mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Iran mwaka huu.
Mikutano ya BRICS katika kipindi cha miezi sita iliyopita haijazaa taarifa ya pamoja, jambo linalodaiwa kusababishwa na kutokubaliana sana kuhusu Iran na namna ya kushughulikia mizozo inayohusiana na Israel.
Suala jingine ni Donald Trump, vitisho vyake vya ushuru wa biashara vinafanya iwe muhimu zaidi kwa wanachama wa BRICS kuungana ili kuleta uwiano, lakini wakati huo huo, kukabiliana naye kunaweza kuwa na gharama kubwa.
Ikulu ya Marekani imeelezea baadhi ya mapendekezo ya BRICS kama yenye msimamo wa "kupinga Marekani," na nchi nyingi zitakuwa na tahadhari dhidi ya kumkasirisha rais huyo wa Marekani.










