Marekani yatoa orodha ya makampuni yanayomilikiwa na Jeshi la China na kuonya

People shop at a Huawei store in Barcelona, Spain

Chanzo cha picha, Getty Images

Idara ya ulinzi nchini Marekani imebaini kwamba makampuni 20 makubwa nchini China, ikiwemo Huwawei yanamilikiwa na jeshi la China.

Orodha hiyo, ilioonekana na vyombo vya habari vya Marekani inashirikisha kampuni za video Hikvision, China Telecoms, China mobile na AVIC.

Ufichuzi huo huenda ukasababisha kuwekwa kwa vikwazo vipya vya kifedha dhidi ya kampuni hizo.

Hatua hiyo inajiri huku Marekani ikiwa imeyashinikiza mataifa mengine ikiwemo Uingereza kuipiga marufuku Huawei kwa sababu za kiusalama wa kitaifa.

BBC inaelewa kwamba orodha hiyo imechapishwa ili kuwajuza wawekezaji, washirika muhimu, kamati za bunge la Congress, wafanyabiashara wa Marekani na washirika muhimu wa kampuni za China kuhusu jukumu ambalo kampuni hizo huchukua katika kuhamisha teknolojia muhimu kwa jeshi la China.

Orodha hiyo huenda ikaongezeka.

Chini ya sheria za Marekani, Idara ya ulinzi inahitajika kuzichunguza kampuni zinazomilikiwa na jeshi la jamhuri ya China ambazo zinafanyakazi nchini Marekani

Idara ya ulinzi imekuwa chini ya shinikizo katika miezi ya hivi karibuni kutoka kwa wabunge wa Democrats na wenzao wa Republican kuchapisha na kuongeza orodha hiyo.

Mnamo mwezi Novemba, maseneta wa Marekani Tom Cotton na Chuck Schumer waliandika barua kwa waziri wa biashara Wilbur Ross, wakitaka kufahamishwa kuhusu mpango wa kubadilisha sera za Marekani ambazo ziliamrishwa na sheria za udhibiti wa mauzo ya nje mwaka 2018 na sheria ya ulinzi wa kitaifa ya Marekani 2019.

Maseneta Chuck Schumerna Tom Cotton

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maseneta Chuck Schumer na Tom Cotton wanataka idara ya biashara kuchunguza ikiwa China imekuwa ikiiba teknolojia ya Marekani kwa kutumia jeshi

Maseneta Chuck Schumer na Tom Cotton wametoa wito kwa idara ya biashara kuchunguza iwapo China imekuwa ikiiba teknolojia za Marekani kwa kutumia vifaa vya kijesh

Katika barua, maseneta walisisitiza wasiwasi wao kuhusu hatari ya kuuza teknolojia muhimu ya Marekani kwa kampuni zilizona na uhusiano na China.

Pia zilihoji kwanini idara ya biashara imekuwa ikijivuta kuweka mabadiliko ya sera ya mauzo ya nje kama ilivyoamrishwa na sheria hizo mbili.

Maseneta hao walisisitiza kwamba mabadiliko hayo yanapaswa kufanywa ili kuona iwapo chama tawala cha kikomyunisti nchini China kimekuwa kikiiba teknolojia ya Marekani kupitia vifaa vya kijeshi, pamoja na iwapo imekuwa ikiorodhesha makampuni ya China yanayotumia teknolojia ibuka kwa madhumuni ya jeshi.

Maseneta wataka mabadiliko ya sera

Je! mabadiliko haya ni ya kiwango gani na matokeo yake yatatekelezwaje? Je matokeo yake yataathiri sekta maalum za uchumi wa Marekani ambazo kampuni hizo za China zinaulenga kupitia wizi wa teknolojia, Je, matokeo ya marekebisho hayo yatawekwa wazi kwa umma, waliandika maseneta Cotton na Schumer.

"Tunawataka kufanya marekebisho hayo muhimu kwa haraka iwezekanavyo. Ahsanteni kwa muda wenu kwa suala hili lenye umuhimu mkubwa katika usalama wetu wa kitaifa.

Ikulu ya Whitehouse tayari imechukua hatua kadhaa dhidi ya Huawei na makampuni mengine ya China ikiwemo kuzuia makampuni ya Marekani kutoyauzia baadhi ya teknolojia bila ruhusa.

Utawala huo pia umesema kwamba vita vyake vya kibiashara na China , vilivyosababisha ruzuku ya mabilioni ya madola lilikuwa jibu la wizi wa njama za kibiashara za Marekani.

Taifa hilo limepokea simu kutoka kwa baadhi ya watu kuchukua hatua kali zaidi. Huawei imekana madai dhidi yake kama yasiokuwa na ushahidi. i.