Mwanamume asimulia alivyonusurika shambulio la simba

Chanzo cha picha, UGC
Mwanaume mmoja ameshambuliwa na simba katika kijiji cha Garajia, wilaya ya Bhavnagar, nchini India Jumatatu (Julai 6) na kujeruhiwa vibaya.
Mfugaji Kalubhai Parmar alisema kuwa shambulio hilo lilitokea wakati akiwapeleka ng'ombe wake kunywa maji.
Wakazi wa eneo hilo wanasema kuwa Kalubhai anapokea matibabu katika katika Hospitali Kuu ya Sir Takhtsinhjialikolazwa katini jiji la Bhavnagar, umbali wa kilomita 60 kutoka eneo la tukio.
Hiki ni kisa cha pili cha simba kushambulia binadamu katika wilaya ya Bhavnagar katika siku za hivi karibuni. Mnamo Juni 18, mwili wa kijana anayefahamika kama Nagjibhai Gujaria ulipatikana kwenye kichaka karibu na nyumba yake katika kijiji cha Gadha, eneo la Mahuva, karibu na eneo la Palitana.
Familia ya Nagjibhai ilidai kuwa alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika shambulio la simba.
Ni nini kilitokea?
Kulingana na Alpesh Dabhi, mwandishi wa BBC Idhaa ya Kigujarati, Kalubhai aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa mbili na nusu asubuhi ya Jumatatu akiwa nyumbani kwake.
Kalubhai alisema, "Nilikuwa nawapeleka ng'ombe wangu kunywa maji mwendo wa saa mbili na nusu asubuhi. Mara ghafla nikashambuliwa na simba aliyekuwa karibu nao. "
"Kwanza alinirukia begani na kuniangusha chini. Kisha akaning'ata mkono na kunishikilia kwa mdomo wake na kuniburza chini kwa takriban nusu saa. Baada ya muda, nilijaribu kumbana kwa mkono wangu, naye akaniachia."
Akithibitisha kisa hicho, Naibu Mhifadhi wa Misitu katika Idara ya Wanyamapori ya Shetrunji, Chirag Amin, aliambia BBC kuwa simba alimshambulia mkulima katika kijiji cha Garazia na kujeruhiwa vibaya.
Kalubhai, ambaye ana umri wa takriban miaka 50, aliongeza kusema kuwa watu walikuwa wameifahamisha idara ya misitu kuhusu simba huyo lakini aliondoka kabla ya maafisa wa idara ya misitu kufika. Idara ya misitu haikutoa maelezo kuhusiana na tukio hilo.
Katika video iliyorekodiwa wakati wa shambulio, watu waliokuwa karibu wanaonekana wakipiga kelele na kumrushia mawe simba huyo.
Alifanikiwa vipi kutoroka?
Kalubhai alisema hata vijii hawakuweza kumsaidia wakati simba alipomchukua.
Video hiyo inaonyesha kuwa simba huyo ghafla alimwachia Kalubhai na kuondoka. Kalubhai alisema kuwa simba huyo alimwacha na kuelekea upande wa ng'ombe wake.
Hata hivyo, kiongozi wa eneo hilo, Karamshibhai Chauhan, aliambia BBC kuwa simba huyo aliondoka bila kuwadhuru ng'ombe wawili wa Kalubhai.

Karamshibhai alisema, "Simba huyo alikuja kijijini na kwenda katika shamba la jirani ya Kalubhai. Lakini, alitoroka baada ya nyati wa jirani kumshinda nguvu kwa kutumia pembe zake."
"Baada ya hapo alienda kwa Kalubhai, ambako ng'ombe wawili walikuwa wamefungwa. Lakini badala ya kuwashambulia ng'ombe, alimvamia Kalubhai. Hatimaye, alimwachilia Kalubhai na kukimbia kuelekea wakokokuwa ng'ombe hao. japo aliondoka bila kuwadhuru."
Mke wa Karamshibhai, alisema, "Kalubhai alipata majeraha kwenye shingo, bega na mkono katika shambulio la simba. Awali alipelekwa hospitali ya Palitana kwa matibabu. Lakini akakimbizwa hosipitali kuu baada madaktari kushauri apelekwe Bhavnagar."
Kwa nini simba alimshambulia?
Maafisa wa idara ya misitu wa waliambia BBC kuwa milima ya Shetrunjaya ni sehemu ya eneo la hifadhi ya msitu na ni makazi ya simba na chui.
Kijiji cha Garazia kiko ndani ya eneo la Palitana la Kitengo cha Wanyamapori cha Shetrunji.
Chirag Amin aliambia BBC, "Siku moja kabla ya tukio hili, simba hao walikuwa wamemuua mtu katika kijiji cha Sonpari karibu na Garazia. Inasadikiwa kuwa simba hao watatu walikuwa wakirejea katika makazi yao lakini akulipopambazuka wakashindwa kuendelea na safari yao baada ya watu kuanza shughuli zao za siku.
"Simba hao walitatizika na vurugu na kelele za watu na kumshambulia mtu aliyekuwa akilisha mifugo wake.Video hiyo pia inaonyesha kuwa simba huyo alimjeruhi mtu huyo, na kisha akaondoka eneo hilo."
Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka idara ya misitu ilisema kuwa Kalubhai alishambuliwa na simba wakati akiwalinda mifugo yake.
Simba hao wamekuwa hapo kwa muda gani?
Hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, simba walikuwa wakipatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Gir na Eneo la Hifadhi la Gir (linalojulikana pia kama Msitu wa Gir).
Kadiri idadi ya simba ilivyoongezeka, walianza kuonekana nje ya msitu wa Gir kuanzia katikati ya miaka ya 1990. Baadaye, simba hao walionekana pia katika eneo la Paniya katika wilaya ya Amreli.
Shughuli za simba ziliongezeka kando ya kingo za mto Shetrunji. I dadi yao ilipokuwa kubwa zaidi wakahamia eneo la Liliya katika wilaya ya Amreli. Kutoka hapo, walielekea eneo la Mahuva katika wilaya ya Bhavnagar na wameishi hapo kwa miaka 10 iliyopita. Simba wamefanya milima ya Shetrunjay na maeneo yanayozunguka eneo la Palitana kuwa makaazi yao.
Mwezi uliopita, video ya simba akikimbia na begi la muumini aliyekuwa akipanda ngazi za Mlima Shetrunjaya ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Chanzo cha picha, Bipin Tankaria/BBC
Ili kuwalinda simba katika maeneo yenye watu wengi nje ya msitu wa Gir na kuzuia migogoro kati ya wanyama na binadamu, serikali ya jimbo ilianzisha Kitengo cha Wanyamapori cha Shetrunji mnamo mwaka 2019. Wafanyakazi pia waliteuliwa na Idara ya Misitu kutekeleza jukumu hilo. Ofisi ya Naibu Mhifadhi wa Misitu wa kitengo hicho iko katika mji wa Palitana.
Karamshibhai alisema, "Idadi ya simba imekuwa ikiongezeka karibu na kijiji chetu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Simba hao huwashambulia mifugo mara kwa mara. Lakini hii ni mara ya kwanza kwao kumshambulia binadamu."
Naibu Mhifadhi wa Misitu, Chirag Amin, alisema kuwa idara ya misitu imepata taarifa kuhusu mahali walipo simba hao watatu walioonekana katika kijiji cha Garazia na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa.
"Wafanyakazi wetu wapo hospitalini ambako mtu aliyejeruhiwa amelazwa na wanashirikiana na maafisa wa hospitali hiyo."











