Lini Afrika itapata Ballon d'Or tena?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rob Stevens
- Nafasi, BBC Sport Africa
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Afrika imewahi kuwa na mshindi mmoja tu wa Ballon d'Or, na huenda ikasubiri zaidi kuona mchezaji mwingine akifuata nyayo za George Weah baada ya orodha ya mwaka huu kutangazwa.
Nahodha wa Morocco, Achraf Hakimi, na mshambuliaji wa Senegal, Sadio Mane, ndio wachezaji wawili pekee kutoka Afrika walio kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo hiyo mwaka 2026.
Wachezaji hao wawili wamewahi kumaliza katika nafasi sita bora za Ballon d'Or, lakini baada ya mwaka ambao Hispania ilitwaa Kombe la Dunia la Fifa na Kylian Mbappe kufunga mabao 10 na kuwa mfungaji bora wa muda wote katika historia ya mashindano hayo, nafasi za Hakimi au Mane kutwaa tuzo hiyo zinaonekana kuwa ndogo.
Lakini Afrika imewahi kusubiri muda mrefu kabla ya kuona nyota wake akifikia kilele cha tuzo hiyo. Je, mwaka huu unaweza kuwa mwanzo wa sura mpya?
Weah -Mwafrika pekee mwenye Ballon d'Or

Chanzo cha picha, Getty Images
Kilele cha historia ya Afrika katika Ballon d'Or kilifika mwaka 1995, wakati George Weah alipokuwa Mwafrika wa kwanza na hadi sasa pekee kutwaa tuzo hiyo.
Mshambuliaji huyo wa Liberia aliongoza kura mbele ya Mjerumani Jurgen Klinsmann na Jari Litmanen wa Finland, baada ya kufanya vizuri akiwa Paris St-Germain na AC Milan.
Mwaka 1995 ulikuwa pia wa kwanza ambapo wachezaji wanaowakilisha mataifa yasiyo ya Ulaya waliruhusiwa kuwania Ballon d'Or. Kabla ya hapo, tuzo hiyo iliyotolewa kwa mara ya kwanza na jarida la France Football mwaka 1956 ilikuwa ikihusisha wachezaji wa Ulaya pekee.
Weah ndiye Mwafrika pekee aliyewahi kwenda mpaka mwisho na kushinda tuzo hiyo.
Tangu wakati huo, nyota kadhaa wa Afrika wamekaribia, lakini hakuna aliyefanikiwa kurudia historia hiyo.
Nani alikaribia kushinda Ballon d'Or baada ya Weah?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miongoni mwa waliokaribia zaidi ni Sadio Mane, ambaye mwaka 2022 alimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya mshambuliaji wa Ufaransa Karim Benzema.
Hiyo ilikuwa nafasi bora ya pili kuwahi kufikiwa na Mwafrika tangu Weah ashinde mwaka 1995.
Mane alikuwa sehemu muhimu ya timu ya Liverpool iliyokuwa ikishindania mataji makubwa barani Ulaya na England, na pia aliiongoza Senegal kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2022.
Mafanikio hayo yalimsaidia kumaliza mbele ya wachezaji wengi wakubwa duniani, lakini Benzema alitwaa tuzo hiyo baada ya msimu bora akiwa Real Madrid.
Mane pia alimaliza wa nne mwaka 2019, wakati huo akiwa nyuma ya Lionel Messi, Virgil van Dijk na Cristiano Ronaldo. Mwaka huo ulikuwa wa kipekee kwa Afrika kwa sababu wachezaji watatu wa bara hilo waliingia 10 bora: Mane alikuwa wa nne, Mohamed Salah wa tano na Riyad Mahrez wa 10.
Salah amekuwa mmoja wa Waafrika waliofanya vizuri zaidi katika tuzo hiyo. Mwaka 2019 alimaliza wa tano, huku akiwahi pia kuingia kwenye orodha ya walioteuliwa mara sita.
Cameroon pia imekuwa na mchango mkubwa kupitia Samuel Eto'o, ambaye aliingia kwenye kinyang'anyiro mara tisa mfululizo kati ya 2003 na 2011. Nafasi yake bora ilikuwa ya tano mwaka 2009, baada ya kusaidia Barcelona kushinda Ligi ya Mabingwa kwa kufunga bao katika fainali dhidi ya Manchester United.
Kwa upande wa Ivory Coast, Didier Drogba ameteuliwa mara nane na nafasi yake bora ilikuwa ya nne mwaka 2007.
Kwa ujumla, Afrika imepata uteuzi 76 wa Ballon d'Or tangu mwaka 1995, sawa na asilimia 6.62 ya jumla ya wachezaji waliowahi kuwania tuzo hiyo.
Kwanini Hakimi na Mane wanaweza kuitoa kimasomaso Afrika mwaka huu?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mwaka huu Afrika ina wawakilishi wawili kati ya wachezaji 30 wanaowania Ballon d'Or: nahodha wa Morocco Achraf Hakimi na Sadio Mane wa Senegal.
Hakimi amekuwa na msimu mkubwa akiwa Paris St-Germain, akifunga mabao manne na kutoa pasi 17 za mabao katika mechi 49 msimu wa 2025-26. Alisaidia PSG kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligue 1, huku akitoa pasi saba za mabao katika kampeni ya Ligi ya Mabingwa.
Akiwa nahodha wa Morocco, Hakimi pia aliiongoza timu hiyo hadi robo fainali ya Kombe la Dunia 2026, ambako ilitolewa na Ufaransa kwa mabao 2-0. Katika mechi sita za mashindano hayo, alifunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao.
Mafanikio yake binafsi pia ni makubwa. Mwaka 2025 alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika ya CAF, akiwa raia wa kwanza wa Morocco kushinda tuzo hiyo tangu Mustapha Hadji mwaka 1998, na beki wa kwanza kutwaa tuzo hiyo tangu mwaka 1973.
Kwa upande wa Mane, hii si mara yake ya kwanza kuwa karibu na kilele. Alimaliza wa nne mwaka 2019 na wa pili mwaka 2022. Akiwa Liverpool, alikuwa sehemu ya safu hatari ya ushambuliaji pamoja na Mohamed Salah na Roberto Firmino, na akasaidia klabu hiyo kushinda Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya kuondoka Liverpool, Mane alitwaa mataji ya ligi akiwa Bayern Munich na Al-Nassr. Msimu wa 2025-26 alihusika moja kwa moja katika mabao 16 ya Al-Nassr kwenye Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Hivyo, licha ya ushindani mkubwa, Hakimi anaingia kwenye kinyang'anyiro akiwa na mafanikio ya klabu na timu ya taifa, huku Mane akiwa na uzoefu wa kufika nafasi ya pili. Wawili hao ndio matumaini makubwa ya Afrika mwaka huu ya kusogea karibu na rekodi ya George Weah.
Waafrika waliowahi kuwania Ballon d'Or mara nyingi

Chanzo cha picha, Getty Images
Samuel Eto'o (Cameroon) ndiye Mwafrika aliyeingia kwenye kinyang'anyiro cha Ballon d'Or mara nyingi zaidi. Aliteuliwa mara tisa mfululizo kati ya 2003 na 2011, huku nafasi yake bora ikiwa ya tano mwaka 2009.
Didier Drogba (Ivory Coast) anafuata akiwa na uteuzi mara nane. Alifanya vizuri zaidi mwaka 2007 alipomaliza katika nafasi ya nne.
Sadio Mane (Senegal) ameteuliwa mara tano. Nafasi yake bora ni ya pili mwaka 2022, huku pia akimaliza wa nne mwaka 2019. Uteuzi wake wa kwanza na wa sasa unatenganishwa na miaka 10.
Mohamed Salah (Misri) ameteuliwa mara sita. Mwaka 2019 alimaliza wa tano, katika mwaka ambao Afrika ilikuwa na wachezaji watatu ndani ya 10 bora.
Yaya Toure (Ivory Coast) ameteuliwa mara tano, akiwa mmoja wa wachezaji wa Afrika waliofanikiwa kuingia mara kadhaa kwenye orodha hiyo.
Riyad Mahrez (Algeria) ameteuliwa mara nne. Nafasi yake bora ilikuwa ya 10 mwaka 2019, mwaka ambao Mane na Salah pia waliingia 10 bora.
Michael Essien (Ghana) ameteuliwa mara tatu, akiwakilisha kizazi cha wachezaji wa Ghana waliofanya vizuri katika soka la Ulaya.
Mahamadou Diarra (Mali) ameteuliwa mara mbili, huku Frederic Kanoute pia akiingia kwenye orodha hiyo mara moja.
Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon) ameteuliwa mara tatu na ni mmoja wa wachezaji wa Gabon waliofikia hatua hiyo.
Achraf Hakimi (Morocco) ameteuliwa mara mbili, huku uteuzi wake wa mwaka 2026 ukiwa mmoja wa wawakilishi wawili pekee wa Afrika.
George Weah (Liberia) aliteuliwa mara mbili, lakini muhimu zaidi ni kwamba alifanikiwa kutwaa tuzo hiyo mwaka 1995 na kuwa Mwafrika wa kwanza na pekee hadi sasa kufanya hivyo.
Victor Osimhen (Nigeria) aliweka historia kwa Nigeria mwaka 2023 alipomaliza katika nafasi ya nane, ikiwa ndiyo nafasi bora zaidi kuwahi kufikiwa na mchezaji wa Nigeria.
Ademola Lookman (Nigeria) alimaliza wa 14 mwaka 2024 baada ya kufunga mabao matatu katika fainali ya Europa League akiwa na Atalanta.
Jay-Jay Okocha na Nwankwo Kanu (Nigeria) wamewahi kuingia kwenye kinyang'anyiro mara mbili kila mmoja.
Kwa jumla, Nigeria ndiyo nchi ya Afrika iliyowahi kuwa na idadi kubwa zaidi ya wachezaji walioteuliwa, ikiwa na wachezaji wanane.
Hata hivyo, Afrika bado ina safari ndefu. Nchi 39 za bara hilo bado hazijapata mchezaji wao wa kwanza kuteuliwa, huku hakuna mchezaji anayewakilisha klabu inayocheza barani Afrika ambaye amewahi kuingia kwenye orodha ya Ballon d'Or.
Kwa wanawake, hali nayo si tofauti sana. Tangu Ballon d'Or Feminin ianze mwaka 2018, ni wachezaji wanne tu kutoka Afrika waliowahi kuteuliwa: Asisat Oshoala wa Nigeria, Barbra Banda wa Zambia, pamoja na Tabitha na Temwa Chawinga wa Malawi.
Hivyo, swali bado lipo lile lile: Lini Afrika itapata Ballon d'Or tena?
Waliochangia makala haya ni Ian Williams na Yusuph Mazimu












