Wakina baba wanaofanya uamuzi mgumu wa kuwauza watoto wao ili kujikimu

Abdul Rashid Azimi anasema yuko tayari kumuuza mmoja wa mabinti zake ili aweze kuwalisha watoto wengine.

Chanzo cha picha, Imogen Anderson/BBC

Maelezo ya picha, Abdul Rashid Azimi anasema yuko tayari kumuuza mmoja wa mabinti zake ili aweze kuwalisha watoto wengine.
    • Author, Yogita Limaye
    • Nafasi, Mwandishi wa Asia Kusini na Afghanistan
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Mapambazuko yanapoanza, mamia ya wanaume hukusanyika katika uwanja wenye vumbi huko Chaghcharan, mji mkuu wa jimbo la Ghor nchini Afghanistan.

Husimama kando ya barabara wakitumaini mtu atapita na kutoa kazi yoyote ile. Hilo ndilo litaamua kama familia zao zitapata chakula siku hiyo.

Hata hivyo, nafasi ya kufanikiwa ni ndogo.

Juma Khan, mwenye umri wa miaka 45, amepata kazi ya siku tatu tu katika kipindi cha wiki sita zilizopita, akilipwa kati ya Afghani 150 hadi 200 ($2.35-$3.13) kwa siku.

"Watoto wangu walilala njaa kwa siku tatu mfululizo. Mke wangu alikuwa analia, na watoto wangu pia walikuwa wakilia. Hivyo nilimsihi jirani yangu anikopeshe fedha za kununua unga," anasema.

"Ninaishi kwa hofu kwamba watoto wangu watakufa kwa njaa."

Hadithi yake si ya kipekee hata kidogo.

Onyo: Makala haya yana maelezo yanayoweza kuumiza hisia.

Nchini Afghanistan leo, watu watatu kati ya wanne hawawezi kumudu mahitaji yao ya msingi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Ukosefu wa ajira umeenea, huduma za afya zinayumba, na misaada ambayo hapo awali ilitoa mahitaji ya msingi kwa mamilioni ya watu imepungua hadi kiwango kidogo sana kuliko ilivyokuwa zamani.

Nchi hiyo sasa inakabiliwa na viwango vya njaa ambavyo havijawahi kushuhudiwa, huku watu milioni 4.7, zaidi ya sehemu ya kumi ya wakazi wa Afghanistan, wakikadiriwa kuwa hatua moja tu kutoka kwenye baa la njaa.

Ghor ni mojawapo ya majimbo yaliyoathirika zaidi.

Wanaume wa eneo hilo wamekata tamaa.

"Nilipigiwa simu nikaambiwa watoto wangu hawajala kwa siku mbili," anasema Rabani huku sauti yake ikitetemeka kwa huzuni.

"Nilihisi kama nijiue. Lakini kisha nikafikiria, hilo litaisaidiaje familia yangu? Ndiyo maana niko hapa nikitafuta kazi."

Juma Khan (katikati), mwenye umri wa miaka 45, amepata kazi ya siku tatu tu katika kipindi cha wiki sita zilizopita.

Chanzo cha picha, Imogen Anderson/BBC

Maelezo ya picha, Juma Khan (katikati), mwenye umri wa miaka 45, amepata kazi ya siku tatu tu katika kipindi cha wiki sita zilizopita.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Khwaja Ahmad anashindwa hata kumaliza maneno machache kabla hajaanza kulia kwa kwikwi.

"Tunakufa kwa njaa. Watoto wangu wakubwa walifariki, hivyo lazima nifanye kazi ili niilishe familia yangu. Lakini mimi ni mzee, kwa hiyo hakuna anayependa kunipa kazi," anasema.

Wakati duka moja la mikate karibu na uwanja linapofunguliwa, mmiliki wake anagawa mikate mikavu kwa umati wa watu. Ndani ya sekunde chache, mikate hiyo inakatwa vipande vipande huku wanaume kadhaa waking'ang'ania vipande hivyo vya thamani.

Ghafla vurugu nyingine zinazuka. Mwanaume mmoja aliyekuwa kwenye pikipiki anafika akitaka kuajiri mfanyakazi mmoja wa kubeba matofali. Makumi ya wanaume wanamkimbilia wakijaribu kupata kazi hiyo.

Katika saa mbili tulizokuwepo hapo, ni wanaume watatu tu waliopata kazi.

Katika jamii za karibu, nyumba duni zilizo kwenye vilima vikavu vya kahawia, zikiwa chini ya vilele vyenye theluji vya safu ya milima ya Siah Koh, athari mbaya za ukosefu wa ajira zinaonekana wazi.

Abdul Rashid Azimi anatukaribisha nyumbani kwake na kuwaleta watoto wake wawili, mapacha wa miaka saba, Roqia na Rohila. Anawakumbatia huku akiwa na hamu ya kueleza kwa nini analazimika kufanya maamuzi ya kuumiza moyo.

"Niko tayari kuwauza mabinti zangu," analia. "Mimi ni maskini, nina madeni na sina msaada wowote.

"Ninarudi nyumbani kutoka kazini nikiwa na midomo mikavu kwa kiu, njaa, huzuni na kuchanganyikiwa. Watoto wangu wanakuja kwangu wakisema, 'Baba, tupe mkate.' Lakini niwape nini? Kazi iko wapi?"

Anamkumbatia Rohila huku akimbusu na kulia. "Inaniumiza moyo, lakini ndiyo njia pekee ya kuwalisha watoto wangu wengine."

Vibarua hukusanyika mapema wakijaribu kupata kazi chache zinazopatikana.

Chanzo cha picha, Imogen Anderson/BBC

Maelezo ya picha, Vibarua hukusanyika mapema wakijaribu kupata kazi chache zinazopatikana.

"Chakula chetu ni mkate na maji ya moto pekee, hata chai hatuna," anasema mama yao, Kayhan.

Wanawe wawili wa kiume wenye umri wa ujana hufanya kazi ya kung'arisha viatu katikati ya mji. Mwingine hukusanya taka, ambazo Kayhan huzitumia kama kuni za kupikia.

Saeed Ahmad anatuambia kwamba tayari amelazimika kumuuza binti yake wa miaka mitano, Shaiqa, baada ya kuugua ugonjwa wa appendix na uvimbe kwenye ini lake.

"Sikuwa na fedha za kulipia gharama za matibabu. Kwa hiyo nilimuuza binti yangu kwa ndugu yangu," anasema.

Upasuaji wa Shaiqa ulifanikiwa. Fedha za matibabu hayo zilitokana na kiasi cha Afghani 200,000 ($3,200/£2,400) alichouzwa nacho.

"Kama ningechukua fedha zote wakati huo, angeondoka naye mara moja. Kwa hiyo nilimwambia anipe tu kiasi cha matibabu yake sasa, halafu ndani ya miaka mitano ijayo atanipa kilichobaki, baada ya hapo anaweza kumchukua," anaeleza Saeed.

Shaiqa anamkumbatia shingoni kwa mikono yake midogo. Uhusiano wao wa karibu unaonekana wazi, lakini baada ya miaka mitano atalazimika kuondoka kwenda kuishi nyumbani kwa huyo ndugu.

"Kama ningekuwa na pesa, kamwe nisingefanya uamuzi huu," Saeed anasema.

"Lakini nilifikiria, itakuwaje kama akifa bila kufanyiwa upasuaji? Kwa njia hii angalau ataendelea kuwa hai."

Saeed Ahmad anasema kwamba amemuuza binti yake wa miaka mitano, Shaiqa.

Chanzo cha picha, Imogen Anderson/BBC

Maelezo ya picha, Saeed Ahmad anasema kwamba amemuuza binti yake wa miaka mitano, Shaiqa.

Miaka miwili tu iliyopita, Saeed alikuwa akipata msaada fulani.

Wakati huo, yeye na familia yake, kama mamilioni ya Waafghanistan wengine, walikuwa wakipokea misaada ya chakula: unga, mafuta ya kupikia, dengu na virutubisho kwa watoto.

Lakini kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa misaada katika miaka ya hivi karibuni kumeinyima idadi kubwa ya watu msaada huu wa kuokoa maisha.

Marekani, ambayo zamani ilikuwa mfadhili mkubwa zaidi wa Afghanistan, ilipunguza karibu misaada yote kwa nchi hiyo mwaka jana. Wafadhili wengine muhimu pia wamepunguza kwa kiasi kikubwa michango yao, wakiwemo Uingereza. Takwimu za sasa za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa misaada iliyopokelewa hadi sasa mwaka huu ni pungufu kwa asilimia 70 ikilinganishwa na mwaka 2025.

Ukame mkali, ambao umeathiri zaidi ya nusu ya majimbo ya nchi hiyo, unaongeza matatizo zaidi.

"Hatukupata msaada kutoka kwa mtu yeyote, si kutoka serikalini wala mashirika yasiyo ya kiserikali," anasema mkazi Abdul Malik.

Serikali ya Taliban, iliyochukua madaraka mwaka 2021, pia inailaumu serikali iliyopita ya Afghanistan, iliyoondolewa baada ya majeshi ya kigeni kujiondoa nchini humo.

"Katika miaka 20 ya uvamizi, uchumi wa bandia uliundwa kutokana na kuingia kwa dola za Marekani," Hamdullah Fitrat, naibu msemaji wa serikali ya Taliban, anaiambia BBC.

"Baada ya uvamizi kumalizika, tulirithi umaskini, mateso, ukosefu wa ajira na matatizo mengine."

Hata hivyo, sera za Taliban zenyewe, hasa vizuizi dhidi ya wanawake, pia ni sababu kubwa inayowafanya wafadhili kujiondoa.

Walipoulizwa kuhusu hilo, serikali ya Taliban ilikataa kuwajibika kwa wafadhili kuondoka, ikisema badala yake kuwa "msaada wa kibinadamu haupaswi kuingizwa kwenye siasa."

Fitrat pia anataja mipango ya Taliban ya "kupunguza umaskini na kuunda ajira kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi," akitaja baadhi ya miradi ya miundombinu na uchimbaji madini.

Lakini ingawa miradi ya muda mrefu inaweza kusaidia siku moja, ni wazi kuwa kuna mamilioni ya watu ambao hawataweza kuishi bila msaada wa haraka.

Kama Mohammad Hashem, ambaye mtoto wake wa kike mwenye miezi 14 alifariki wiki chache zilizopita.

"Mtoto wangu alikufa kwa njaa na ukosefu wa dawa... Mtoto anapokuwa mgonjwa na mwenye njaa, ni wazi atakufa," anasema.

Mzee mmoja wa eneo hilo anasema vifo vya watoto, hasa kutokana na utapiamlo, "vimeongezeka sana" katika miaka miwili iliyopita.

Hapa, hata hivyo, hakuna rekodi rasmi za vifo. Makaburi ndiyo sehemu pekee inayotoa ushahidi wa ongezeko la vifo vya watoto. Na hivyo, kama tulivyowahi kufanya hapo awali, tulihesabu makaburi madogo na makubwa tofauti. Kulikuwa na takribani makaburi madogo mara mbili zaidi ya makubwa, jambo linaloashiria kuwa watoto waliokufa walikuwa mara mbili zaidi ya watu wazima.

Muuguzi Fatima Husseini

Chanzo cha picha, Imogen Anderson/BBC

Kulikuwa na ushahidi zaidi katika hospitali kuu ya mkoa huko Chaghcharan.

Kitengo cha watoto wachanga ndicho kilichokuwa na shughuli nyingi zaidi. Kila kitanda kilikuwa kimejaa, baadhi vikiwa na watoto wawili. Wengi wao walikuwa na uzito mdogo, na idadi kubwa ilikuwa ikihangaika kupumua wenyewe.

Muuguzi mmoja analeta kitanda kidogo chenye mapacha wa kike waliozaliwa karibuni. Walizaliwa kabla ya wakati kwa miezi miwili. Mmoja ana uzito wa kilo 2, mwingine kilo 1 tu.

Walikuwa katika hali mbaya sana na waliwekwa kwenye oksijeni mara moja.

Mama yao, Shakila mwenye umri wa miaka 22, alikuwa katika wodi ya wazazi.

"Ni dhaifu kwa sababu alipokuwa na ujauzito wao hakuwa na chakula cha kutosha, mkate na chai pekee," anaeleza bibi wa mapacha hao, Gulbadan. "Ndiyo maana watoto wako katika hali hii."

Saa chache baada ya sisi kuondoka hospitalini siku hiyo, mtoto aliyekuwa na uzito mkubwa zaidi alifariki kabla hata hajapewa jina.

"Madaktari walijaribu kumsaidia lakini alifariki," anasema bibi yake mwenye huzuni siku iliyofuata.

"Nilifunga mwili wake mdogo kwa kitambaa na kumpeleka nyumbani. Mama yake alipofahamu, alizimia."

Gulbadan anamuoesha mtoto aliyebaki hai na kuongeza: "Natumaini angalau yeye ataishi."

Mapacha

Chanzo cha picha, Imogen Anderson/BBC

Maelezo ya picha,

Muuguzi Fatima Husseini anasema kuna siku ambapo watoto wachanga watatu hufariki.

"Mwanzoni ilikuwa vigumu sana kwangu kuona watoto wakifa. Lakini sasa karibu imekuwa jambo la kawaida kwetu," anasema.

Dkt. Muhammad Mosa Oldat, anayesimamia kitengo cha watoto wachanga, anasema kiwango cha vifo hupanda hadi asilimia 10, jambo ambalo "halikubaliki."

"Lakini kwa sababu ya umaskini, idadi ya wagonjwa inaongezeka kila siku," anasema. "Na hapa pia hatuna rasilimali za kutosha kuwahudumia watoto ipasavyo."

Katika kitengo cha wagonjwa mahututi kwa watoto, mtoto Zameer mwenye umri wa wiki sita anasumbuliwa na ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis) na homa ya mapafu. Magonjwa yote mawili yanaweza kutibika, lakini madaktari wanahitaji kufanya kipimo cha MRI na hawana vifaa sahihi.

Lakini jambo linaloshtua zaidi ambalo wahudumu wa afya wanatuambia ni kwamba hospitali ya umma haina dawa kwa wagonjwa wengi, hivyo familia hulazimika kununua dawa kutoka kwenye maduka ya dawa yaliyo nje ya hospitali.

"Wakati mwingine, kama kuna dawa zilizobaki kutoka kwa mtoto wa familia yenye uwezo zaidi, tunazitumia kwa watoto ambao familia zao haziwezi kumudu," anasema Fatima.

Ukosefu wa fedha unalazimisha familia nyingi kufanya maamuzi magumu.

Mjukuu wa Gulbadan aliyebaki hai alipata uzito kidogo na hali yake ya kupumua ikaimarika. Lakini siku chache baadaye, familia yake ilimrudisha nyumbani. Hawakuwa na uwezo wa kuendelea kulipia matibabu hospitalini.

Mtoto Zameer pia alipelekwa nyumbani na wazazi wake kwa sababu hiyohiyo.

Miili yao midogo sasa italazimika kupambana yenyewe katika vita ya kuendelea kuishi.