Je, dunia inatawaliwa na kiumbe anayeishi kilomita 1.3 chini ya ardhi?

    • Author, Катарина Циммер
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa muda mrefu, wanasayansi waliamini kuwa viumbe wenye seli nyingi hawawezi kuishi katika kina kirefu chini ya ardhi, ambako kuna joto kali, shinikizo kubwa na oksijeni kidogo.

Lakini ugunduzi wa mdudu mdogo anayefahamika kama "devil worm" au 'minyoo ya shetani' umebadili uelewa huo. Mdudu huyo, mwenye jina la kisayansi Halicephalobus mephisto, alipatikana akiishi takriban kilomita 1.3 chini ya ardhi katika mgodi wa Beatrix nchini Afrika Kusini.

Watafiti walichuja zaidi ya lita 6,000 za maji ya chini ya ardhi kabla ya kumpata mdudu huyo mmoja tu. Katika migodi mingine miwili nchini humo, walichuja kiasi kikubwa zaidi cha maji na kugundua aina mbalimbali za minyoo, wanyama wengine wasio na uti wa mgongo, fangasi na viumbe vidogo sana.

Ugunduzi huo uliibua swali kubwa iwapo mdudu anaweza kuishi katika mazingira hayo, ni viumbe vingapi vingine ambavyo bado havijagunduliwa chini ya ardhi?

Amezoea mazingira magumu

Watafiti waligundua kuwa "devil worm" ana uwezo wa kustahimili mazingira ambayo ni magumu kwa viumbe wengi.

Katika maabara, mdudu huyo alionekana kupendelea joto la nyuzi 37 Celsius. Katika joto la kawaida la nyuzi 20, ukuaji wake hupungua na muda wake wa kuishi huwa mfupi, takriban siku nane. Lakini katika nyuzi 37, anaweza kuzaliana kila baada ya siku mbili.

Utafiti wa DNA uliofanywa mwaka 2019 ulisaidia kueleza uwezo huo. Wanasayansi waligundua kuwa mdudu huyo ana jeni nyingi zinazozalisha protini zinazosaidia kulinda protini nyingine za mwili dhidi ya madhara ya joto kali.

Katika utafiti ulioanza mwaka 2024, wanasayansi pia walichunguza molekuli iitwayo cytochrome c oxidase, ambayo ina jukumu katika matumizi ya oksijeni na uzalishaji wa nishati mwilini.

Waligundua kuwa kwa "devil worm", molekuli hiyo hufanya kazi vizuri zaidi katika joto la juu. Katika joto la kawaida, shughuli yake hupungua na hivyo uzalishaji wa nishati mwilini kupungua. Hii inaweza kueleza kwa nini mdudu huyo ana wakati mgumu kuzoea mazingira yenye baridi.

Watafiti pia wanachunguza uwezo wake wa kuzaliana bila dume. Mdudu aliyegunduliwa katika mgodi wa Beatrix alikuwa jike na aliweza kuacha mayai manane yaliyoendelea kuishi kabla hajafa.

Kwa nini wameenda chini ya ardhi?

Hili bado ni swali ambalo wanasayansi hawana jibu kamili.

Watafiti wanaamini kuwa baadhi ya minyoo huenda waliingia katika kina kirefu cha ardhi kupitia maji ya chini ya ardhi. Matukio ya matetemeko ya ardhi huenda pia zilisaidia kusafirisha viumbe hao kwenda kwenye tabaka za ndani zaidi za dunia.

Kwa mujibu wa makadirio ya watafiti, vijidudu vinavyoishi katika kina kirefu cha ardhi vinaweza kuwa asilimia 12 hadi 20 ya jumla ya viumbe vidogo duniani.

Bakteria hao huenda wana nafasi muhimu katika mfumo huo wa maisha, kwa kuwa wanaweza kuwa chanzo cha chakula na pia kiasi kidogo cha oksijeni kinachohitajika na minyoo hao.

Watafiti wamegundua pia bakteria walioko chini sana ya ardhi ambao wanafanana kinasaba licha ya kupatikana katika maeneo tofauti. Aina hiyo huenda imeishi huko tangu wakati bara kuu la Pangea lilipoanza kugawanyika, takriban miaka milioni 165 iliyopita.

Je, kuna maisha chini ya sayari nyingine?

Ugunduzi wa "devil worm" umeongeza maswali kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa maisha katika maeneo mengine nje ya Dunia.

Wataalamu wanaamini kwamba kuchunguza viumbe wanaoishi katika kina kirefu cha Dunia kunaweza kusaidia kuelewa mazingira ambayo maisha yalianzia kwenye sayari yetu na pia kusaidia katika utafutaji wa maisha katika ulimwengu.

Ikiwa kuna maisha huko, watafiti wanaona uwezekano kwamba yanaweza kuwa yamejificha chini ya uso wa sayari hiyo, ambako yanaweza kulindwa dhidi ya mazingira magumu ya juu ya uso.

Na hata kama tukio kubwa kama kugongwa kwa Dunia na sayari ya asteroidi lingeangamiza viumbe wote walio juu ya uso wa dunia na kufanya sehemu kubwa ya sayari isiwe na uwezo wa viumbe kuishi, viumbe wanaoishi chini ya ardhi huenda wakasaidia maisha kuendelea.

"Tunafikiri sisi binadamu tunaitawala dunia. Lakini kwa kweli, sivyo," anasema Esta van Heerden, mmoja wa watafiti walioshiriki katika safari iliyosaidia kugundua "devil worm".

Kwa wanasayansi, ukweli kwamba viumbe hao wameweza kuishi chini ya ardhi kwa mamilioni, au hata mabilioni ya miaka, unaonyesha jinsi maisha yalivyo na uwezo mkubwa wa kustahimili mazingira ambayo binadamu hawezi kuyaishi.