Unajua ukubwa wa dola trilioni moja? Mifano 7 ya utajiri 'wa kufuru' wa Elon Musk

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkurugenzi Mkuu wa SpaceX na Tesla, Elon Musk, anakaribia kuweka rekodi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya biashara duniani: kuwa mtu wa kwanza kufikia utajiri wa zaidi ya dola trilioni moja.
Kwa sasa Musk anamiliki hisa zenye thamani ya takribani dola bilioni 273 kupitia kampuni ya Tesla pekee. Lakini ikiwa thamani ya kampuni yake ya SpaceX itaendelea kupanda kama ambavyo wawekezaji wengi wanatarajia, utajiri wake unaweza kuongezeka kwa mamia ya mabilioni ya dola zaidi.
Makadirio ya baadhi ya wachambuzi yanaonesha kuwa sehemu ya umiliki wake katika kampuni ya Tesla na SpaceX kwa pamoja inaweza kufikisha thamani inayozidi dola trilioni 1.1. Hiyo ni sawa na dola bilioni 1,100 au dola milioni milioni 1.1.
Ni kiwango cha utajiri ambacho hakijawahi kufikiwa na mtu yeyote katika historia ya dunia. Lakini dola trilioni moja ni kiasi gani hasa? Ili kuelewa ukubwa wake, ni lazima kuacha kuangalia namba pekee na kuanza kuilinganisha na maisha ya watu wa kawaida, bajeti za serikali na hata uchumi wa mataifa mbalimbali.
Lakini dola trilioni moja ni kiasi gani hasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni namba kubwa kiasi kwamba ni vigumu kwa watu wengi kuielewa kwa kuangalia tarakimu pekee. Dola trilioni moja ni sawa na dola bilioni 1,000. Kwa mtu kutumia dola milioni moja kila siku, angehitaji zaidi ya miaka 2,700 kumaliza dola trilioni moja.
Njia ya pili ya kuelewa kiasi hicho ni kuigawanya kwa watu wote duniani. Idadi ya watu duniani kwa sasa inakadiriwa kufikia takribani bilioni 8.3. Kama Musk angegawa dola trilioni 1.1 kwa kila mwanaume, mwanamke na mtoto duniani, kila mtu angepata karibu dola 133.
Hiyo ni sawa na takribani shilingi za Tanzania 350,000 kwa kila mtu au karibu shilingi za Kenya 17,000 kwa kila mtu. Kwa familia ya watu watano, mgao huo ungekuwa zaidi ya shilingi milioni 1.7 za Tanzania au karibu shilingi 85,000 za Kenya.
Na kama kila mmoja angeamua kutumia shilingi 100,000 za Tanzania kwa siku, fedha hizo zingemtosha kwa zaidi ya siku tatu mfululizo bila kufanya kazi yoyote.
Kwa Mkenya anayetumia wastani wa KSh 1,700 kwa siku, kiasi kinacholingana na takribani dola 13, fedha hizo zingemtosha kwa zaidi ya siku 10.
Hata hivyo, ukubwa wa dola trilioni moja unaonekana zaidi unapolinganishwa na matumizi ya serikali na uchumi wa nchi.
Bajeti za Tanzania, Kenya na Uganda kwa karibu miaka 14

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2025/26 ni takribani shilingi trilioni 56.5, sawa na karibu dola bilioni 22.
Hii ina maana kuwa dola trilioni 1.1 zingekuwa za kutosha kufadhili bajeti nzima ya Tanzania kwa karibu miaka 50 mfululizo.
Kwa maneno mengine, mtu mwenye utajiri huo angeweza kugharamia elimu, afya, miundombinu, ulinzi na mishahara ya watumishi wa umma kwa karibu nusu karne.
Kwa upande wa Kenya, ambayo imeidhinisha bajeti ya takribani KSh trilioni 4.6 kwa mwaka wa fedha 2025/26, sawa na karibu dola bilioni 35, utajiri huo ungeweza kufadhili matumizi yote ya serikali kwa zaidi ya miaka 30.
Uganda, ambayo imepitisha bajeti ya takribani dola bilioni 20 kwa mwaka, ingeweza kufadhiliwa kwa zaidi ya miaka 55.
Lakini picha inakuwa kubwa zaidi unapozijumlisha nchi hizo tatu pamoja.
Bajeti za Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja zinafikia karibu dola bilioni 77 kwa mwaka.
Kwa kiwango hicho, dola trilioni 1.1 zingetosha kugharamia bajeti za nchi zote tatu kwa zaidi ya miaka 14 mfululizo.
Kwa maneno mengine, mtu mmoja angekuwa na utajiri unaozidi matumizi ya serikali za watu zaidi ya milioni 250 wa Afrika Mashariki kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mataifa 20 tu duniani yatamzidi Musk kwa utajiri

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ni nchi chache sana duniani zenye uchumi unaozidi dola trilioni 1.1. Ziko nchi 20 tu zenye uchumi unaozidi $1.1 trillion, kati ya nchi 195 zinazotambuliwa duniani zikiwemo 193 chini ya Umoja wa Mataifa zina uchumi mdogo kuliko utajiri huo atakaifikia Musk.
Kwa mfano Taiwan ($977 billion), Ireland ($779 billion) Sweden ($760 billion) na Singapore ($660 billion).
Kwa Hii ina maana kuwa iwapo Musk atafikia kiwango hicho, utajiri wake binafsi utakuwa mkubwa kuliko uchumi wa kila mwaka wa mataifa mengi duniani.
Barani Afrika hakuna taifa hata moja lenye uchumi unaofikia dola trilioni moja kwa sasa.
Hata nchi zenye uchumi mkubwa zaidi kama Afrika Kusini, Misri, Algeria, Nigeria, Kenya na Ethiopia bado ziko chini ya kiwango hicho. mfano Afrika Kusini, nchi yenye uchumi wa kuigwa barani Afrika, uchumi wake ni $480 billion, Musk atakuwa nao mara mbili ya huo.
Kwa maneno mengine, mtu mmoja angeweza kuwa na utajiri unaozidi thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa kwa mwaka na mataifa mengi ya Afrika.
Angeweza kununua Zanzibar mara ngapi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Hakuna takwimu rasmi inayoweka thamani ya Zanzibar au ya mali zote zilizopo katika majiji kama Dar es Salaam, Nairobi au Mombasa.
Lakini kwa kulinganisha, thamani ya mali isiyohamishika katika miji mingi ya Afrika hupimwa kwa makumi ya mabilioni ya dola, si mamia ya mabilioni.
Kwa hiyo, hata kama mali zote za majiji makubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Tanga, Nairobi na Mombasa zingeunganishwa pamoja, bado ni vigumu kufikia dola trilioni moja.
Kwa lugha rahisi, utajiri wa kiwango hicho ungeweza kununua sehemu kubwa ya mali za miji mingi mikubwa ya Afrika Mashariki na bado kubakiza mamia ya mabilioni ya dola kununua mikoa kama Tabora, Morogoro (Tanzania) na Kaunti za Garissa, Isiolo, Taita-Taveta, Kiambu na Machakos huko Kenya.
Lakini ni utajiri wa karatasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Pamoja na ukubwa wake, ni muhimu kuelewa kuwa utajiri wa Musk hauko katika akaunti ya benki kama fedha taslimu.
Sehemu kubwa ya mali yake inatokana na thamani ya hisa zake katika kampuni mbalimbali. Ikiwa thamani ya hisa hizo itashuka, utajiri wake unaweza pia kupungua kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, kama atafikia alama ya dola trilioni moja, Musk ataingia katika eneo jipya kabisa la utajiri ambalo halijawahi kufikiwa na mwanadamu yeyote katika historia ya dunia.
Kwa wengi Afrika Mashariki, njia rahisi zaidi ya kuelewa kiasi hicho ni kufikiria hivi: dola trilioni moja si tu utajiri mkubwa. Ni kiasi kinachoweza kufadhili bajeti za nchi kadhaa kwa miongo mingi, kuzidi uchumi wa mataifa mengi, na kumpa kila mtu duniani mamia ya maelfu ya shilingi mkononi.













