Moja kwa moja, Jeshi la Marekani lasema limedungua ndege mbili zisizo na rubani za Iran katika Mlango wa Hormuz

Taarifa hiyo pia imesema kuwa vikosi vya Marekani vinaendelea kubaki katika maeneo yao ya operesheni na viko tayari kuendelea kujilinda dhidi ya kile ilichokiita uchokozi wa Iran.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Kenya yaagiza waajiri kuwalipa wafanyakazi wa nyumbani angalau dola 140 kwa mwezi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kanuni mpya za mishahara ya chini kwa wafanyakazi wa majumbani nchini Kenya zimeongeza kiwango cha chini cha mshahara wao wa kila mwezi hadi shilingi 18,047 za Kenya, sawa na takriban dola 140 za Marekani.

    Waajiri watakaokiuka masharti hayo wanakabiliwa na kifungo cha hadi miezi mitatu jela au faini ya shilingi 50,000 pesa za Kenya.

    Marekebisho hayo yanafuatia uamuzi wa hivi karibuni wa serikali wa kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kwa asilimia 12, hatua inayolenga kuwasaidia wafanyakazi kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha.

    Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, viwango hivyo vipya vinawahusu maelfu ya wafanyakazi wa majumbani, wakiwemo wasaidizi wa nyumbani, walezi wa watoto, watunza bustani na wafanyakazi wengine wa huduma za nyumbani kote nchini.

    Chini ya muundo huo mpya wa mishahara, wafanyakazi wa majumbani katika miji mikuu ikiwemo Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Eldoret sasa wanastahili kulipwa angalau shilingi 18,047 kwa mwezi.

    Ongezeko hilo ni sehemu ya mageuzi mapana ya sekta ya ajira yanayolenga kuboresha ustawi wa wafanyakazi na kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi nchini Kenya.

    Hata hivyo, wakenya wameingia mitandaoni na kueleza kutoridhishwa kwao na agizo hilo mpya.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Papa Leo aipongeza Uhispania kwa kupinga vita vinavyoendelea mashariki ya kati

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Papa Leo XIV, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, ameipongeza Uhispania kwa kile alichokitaja kuwa ni “kujitoa kwake kwa amani na umoja miongoni mwa mataifa” wakati wa ziara rasmi nchini humo siku ya Jumamosi.

    Serikali ya Uhispania imekuwa ikipinga vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza, Iran na Ukraine katika miaka ya karibuni.

    “Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa taifa lenu, ambalo daima limezingatia sheria za kimataifa na mfumo wa ushirikiano wa kimataifa wa pande nyingi. Msimamo huu unaonesha wazi kujitolea kwake kwa amani na mshikamano kati ya mataifa,” Papa alisema wakati wa hafla ya mapokezi iliyofanyika katika Kasri la Kifalme mjini Madrid.

    Kauli hiyo imekuja huku Uhispania ikiendelea kusisitiza suluhu za kidiplomasia na kuheshimu sheria za kimataifa katika kushughulikia migogoro mbalimbali ya kimataifa.

    Soma zaidi:

  3. Jeshi la Marekani lasema limedungua ndege mbili zisizo na rubani za Iran katika Mlango wa Hormuz

    g

    Chanzo cha picha, AFP VIA Getty

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika Mashariki ya Kati (CENTCOM) imedai kuwa imedungua ndege mbili zisizo na rubani ambazo ilisema zilirushwa na Iran.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, CENTCOM ilisema:

    "Vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati vilidungua ndege mbili za mashambulizi zisizo na rubani za Iran ambazo zilikuwa zikitishia usafirishaji wa kimataifa katika Mlango wa Hormuz."

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa vikosi vya Marekani vinaendelea kubaki katika maeneo yao ya operesheni na viko tayari kuendelea kujilinda dhidi ya kile ilichokitaja kuwa uchokozi wa Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 07 mwezi Juni 2026.