Kipi kitaanza kumalizika, akiba za mafuta au vita Iran?

Chanzo cha picha, Reuters
Katika miezi mitatu ya kwanza ya vita kati ya Marekani na Iran, soko la dunia lilikumbwa na upungufu wa zaidi ya mapipa bilioni moja ya mafuta, lakini kutokana na akiba ya kimkakati hakukuwa na madhara makubwa sana, huku muda ukionekana kumuishia Rais wa Marekani Donald Trump wa kuishawishi Iran kufungua Mlango bahari wa Hormuz.
Hata hivyo, ustahimilivu wa soko unaonekana kuisha haraka, huku wachumi na mashirika ya kimataifa wakionya kuwa bila kufunguliwa kwa kizuizi kilichopo eneo la Hormuz, bei za mafuta huenda ikapanda tena mwezi Julai na Agosti, na uchumi wa dunia utaterereka vibaya
Hata vita vingemalizika leo na mafuta, gesi na bidhaa za petroli zilizokwama katika Ghuba ya Uajemi kufika katika masoko ya dunia, dunia haitakuwa tena kama ilivyokuwa hapo awali.
Itachukua miezi kadhaa kurejesha usambazaji na kujaza tena akiba zilizopungua katika hali ya awali kabla ya vita.
Vita vya Iran vilisababisha bei ya mafuta kupanda kutoka takriban dola 60 hadi zaidi ya dola 100 kwa pipa.
Baada ya Mlango Bahari wa Hormuz kufungwa, nchi za Magharibi zilianza kuuza kwa kiwango kikubwa akiba zao za kimkakati za mafuta, ikiwa ni mauzo makubwa zaidi ya akiba hizo katika historia ya kisasa.
Aidha, ilibainika kuwa makampuni binafsi pia yalikuwa na akiba kubwa ya mafuta ghafi na bidhaa za petroli zilizohifadhiwa katika matangi yao katika sehemu mbalimbali za dunia.
China ambayo ndiyo mnunuzi mkubwa zaidi wa mafuta duniani iliweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji wake wa mafuta kutoka nje.
Wataalam wameonya kwamba hatua hizi zote ni suluhisho za muda mfupi tu, na hazitoshi kutatua changamoto ya muda mrefu ya usambazaji wa nishati duniani.
Akiba inapungua
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kulingana na Fatih Birol"Unapokuwa na akiba lakini huna mapato, unaweza kuitumia kwa muda, lakini hatimaye pesa huisha. Hiyo ndiyo hali tuliyo nayo sasa," anasema
"Tatizo ni kwamba msimu wa likizo huanza mwishoni mwa Juni na mapema Julai, kipindi ambacho matumizi ya mafuta huongezeka. Kwa kuwa akiba inapungua na hakuna mafuta mapya yanayoingia sokoni kutoka Ghuba ya Uajemi, kuna hatari ya kuingia katika hali ya mgogoro mwezi Julai na Agosti," aliongeza.
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) taasisi ambayo nchi tajiri zilianzisha hasa kushughulikia hali kama hizi, imesema kuwa suluhisho pekee ni kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Mgogoro huo umefikia kiwango kikubwa kiasi kwamba mkurugenzi wa IEA Fatih Birol pamoja na taasisi zingine tatu, walitoa onyo ya pamoja na kusema kuwa
"Mauzo ya mafuta yanashuka kwa kasi isiyo ya kawaida wakati Mlango Bahari wa Hormuz ukiwa bado umefungwa," ilisoma taarifa ya pamoja ya wakuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia na WTO.
Taasisi hizo zilizema iwapo hali ya kawaida haitarejea hivi karibuni, soko la kimataifa la nishati litaathirika pakubwa.
Akiba za mafuta zitaisha lini?
Paul Horsnell mhadhiri wa masomo ya nishati katika taasisi ya Oxford anasema kuwa, makadirio kutoka Oxford Institute for Energy Studies yanaonyesha kwamba dunia ilikumbwa na upungufu wa mapipa milioni 640 ya mafuta wakati wa mgogoro wa 1978 hadi 1979, na mapipa milioni 420 wakati wa Vita vya Kwanza vya Ghuba. Lakini sasa kiwango hicho kimezidi mapipa bilioni 1.1.
"Nimewasikia baadhi ya watu wakisema kuwa hili si tukio kubwa kwa sababu soko limejirejelea viwango vya kawaida,ndiyo, soko limeendelea kufanya kazi, lakini ni kwa gharama ya kupungua kwa akiba."
Kulingana na wataalamu, akiba zitafikia kiwango cha hatari iwapo Mlango Bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa, na njia pekee ya kusawazisha mahitaji na upatikanaji itakuwa ni kupanda kwa kasi kwa bei za mafuta.
"Kadirio langu ni kwamba tuna miezi mitatu au chini zaidi kufikia hatua hiyo, na kutokana na mwenendo wa sasa, huenda ikawa muda mfupi zaidi," anasema Paul Horsnell.

Chanzo cha picha, ABEDIN TAHERKENAREH/EPA/Shutterstock
"Dunia haitakuwa kama ilivyokuwa tena"
Wataalamu wanaonya kwamba mtindo wa masoko ya nishati duniani uliokuwepo kabla ya vita umevurugika na huenda usirudi tena kama ulivyokuwa hapo awali.
Hata baada ya vita kumalizika, wanasema wazalishaji na watumiaji wa nishati wataanza kila mara kuzingatia hatari ya usumbufu mpya katika mipango yao, matumizi yao na uwekezaji wao ikiwa ni pamoja na kuongeza akiba za mafuta, kujenga njia mbadala za usafirishaji (pipelines), kuongeza uzalishaji wa ndani na kuhamia zaidi kwenye nishati mbadala.
Helen Thompson alisema kwenye Bloomberg Podcast kwamba:
"Saudi Arabia haitachukulia tena kama jambo la kawaida uwezo wa kusafirisha mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz. Vivyo hivyo, China haitachukulia tena kama jambo la kawaida uwezo wa kuagiza mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz."
Kwa ujumla, kauli hizi zinaonyesha kwamba hata kama amani itarejea, uchumi wa nishati duniani utakuwa umebadilika kwa msingi wa hofu ya usumbufu wa baadaye, hakuna uhakika wa kuendelea kama zamani.

Chanzo cha picha, Reuters
Megan O'Sullivan na Jason Bordoff, ambao ni washauri wa zamani wa Ikulu ya White House, wanaamini kwamba katika hali hii mpya ambayo imejitokeza, nafasi ya masoko huria katika mfumo wa nishati duniani itapungua, huku nafasi ya serikali ikiongezeka zaidi.
Kwa kifupi, wanaona kuwa dunia inaelekea kwenye mfumo ambapo serikali zitakuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika soko la nishati.















